CCM yatema mawaziri wanane kuwania NEC
2007-08-02 10:27:47
Na Mary Edward, PST Dodoma
Wakati Chama cha Mapinduzi kimeshikwana kigugumizi kuwataja wagombea waliotemwa na waliopitishwa kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, imebainika kuwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri wanane, wametupwa nje ya kinyang`anyiro hicho.
Mawaziri hao, wametemwa kwenye kikao cha mchujo cha siku mbili cha NEC kilichokutana mjini hapa juzi na jana.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu mbalimbali vimewataja baadhi ya vigogo walioenguliwa kuwania nafasi hiyo nyeti ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Salome Mbatia na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Rita Mlaki.
Hali kadhalika, vyanzo hivyo vya habari, vimewataja Bw. Kisyeri Chambiri na Chacha Mwita Gachuma kuwa ni miongoni mwa watu mashuhuri ndani ya chama hicho ambao safari hii wametupwa nje kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara.
Vigogo wengine wa CCM ambao wametemwa kwenye mchujo huo ni pamoja na Bw. Didas Masaburi na Chacha Nyamoyo Wambura? aliyekuwa akigombea ujumbe wa NEC kupitia Umoja wa Wazazi Tanzania.
Taarifa zaidi zilidai kuwa, mwenyekiti wa sasa wa Mkoa wa Mtwara aliyekuwa akigombea ujumbe wa NEC, alianguka na kupoteza fahamu kikaoni baada ya jina lake kuondolewa katika mchujo huo.