SoC03 Tutumie maji chini ya ardhi kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji

Stories of Change - 2023 Competition

Kidaya

Member
Dec 20, 2011
55
49
Tunahitaji maji katika shughuli za kila siku za kibinadamu (kunywa, upishi na usafi), kiuchumi (kilimo na ufugaji, uvuvi, ujenzi, kuzalisha nishati, utalii, viwandani n.k) na mazingira. Katika kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa mijini na vijijini, Serikali inatekeleza miradi ya maji inayogharimu fedha nyingi kutokana na sababu za kijiografia, wingi wa watu na mtawanyiko wa watu. Pamoja na jitihada hizo, Serikali, wadau na wananchi tunaweza kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa maeneo yasiyo na huduma ya maji na yenye matumizi makubwa ya maji kwa kutumia maji chini ya ardhi. Maji chini ya ardhi yanapatikana kwa kuchimba visima vifupi kwa mikono (kina kisichozidi mita 20) au visima viferu (kina cha mita 30 hadi 250). Kwa ujumla, maji chini ya ardhi ni nafuu kuyapata na salama zaidi kutokana na kutokuwa rahisi kuathiriwa na shughuli za kibinadamu na mazingira japo usambazaji wake una ufanisi kwa watu wachache ukilinganisha na maji juu ya ardhi.

Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2023/24, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa mwezi Desemba, 2022 ni 88% kwa mijini na 77% kwa vijijini. Maji yanayopatikana kila mwaka nchini ni wastani wa mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka (maji juu ya ardhi - mita za ujazo bilioni 105 na maji chini ya ardhi - mita za ujazo bilioni 21). Kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,105 kwa idadi ya watu milioni 59.8 wa Tanzania Bara. Kiasi hicho kipo juu ya kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa cha wastani wa mita za ujazo 1,700. Taarifa za Wizara ya Maji zinaonesha kuwa ni 12% tuu ya maji chini ya ardhi yanayotumika katika nchi yetu. Takwimu hizi zinaonesha kuwa kwa nchi yetu hatuna uhaba wa maji bali changamoto ni kuyafikisha kwa watumiaji.

Hatua zifuatazo zinaweza kutumika kuongeza utumiaji wa maji chini ya ardhi;

1. Kufungamanisha ujenzi wa miradi itakayokuwa na matumizi makubwa ya maji na uchimbaji wa visima virefu

Miradi ya ujenzi wa shule, vyuo, vituo vya afya, masoko na vituo vya kibiashara, vituo vya usafiri (stendi za mabasi, viwanja vya ndege), viwanja vya mpira, mahoteli, viwanda n.k. inapokamilika huhudumia idadi kubwa ya watu inayoendana na matumizi makubwa ya maji. Miradi hii inapotumia maji yaliyo kwenye mtandao mmoja na wananchi huweza kusababisha uhaba wa maji kunakochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi au kuharibika kwa miundo mbinu ya mtandao wa maji. Lakini endapo ujenzi wa maeneo yanayokusanya watu wengi na yenye matumizi makubwa ya maji ungehusisha na kuchimba kisima kirefu cha maji, changamoto za uhaba au ukosefu wa maji kweye maeneo hayo ingekuwa imetatuliwa kwa kiasi kikubwa.

2. Kuwa na visima virefu kwa maeneo ambayo kijiografia au kibajeti yapo mbali kufikiwa na mtandao wa maji.
Niliwahi kuishi kwenye nyumba za Watumsihi Housing Company zilizopo Kisesa - Mwanza, ambazo zinapata maji kutoka kwenye kisima chao kinachotumia pampu ya umeme kupandisha maji kwenye tenki linalosambaza maji kwenye nyumba zote 59 kwa nguvu ya mvutano (gravitational force). Kila nyumba imefungwa mita ya maji ambapo mpangaji hulipia kwa kadri ya matumizi yake ili kupata fedha za kununulia umeme wa kuendeshea pampu. Wazo hili linafaa kutumika katika maeneo mengine kwa kuwa na visima virefu kama chanzo cha maji kwenye makazi ya watu, na wananchi kulipia gharama za uendeshaji.

WHC Kisesa Housing.jpg

Nyumba za WHC-Kisesa zinazopata maji yake kutoka kwenye kisima kirefu. (Picha kutoka tovuti ya Watumishi Housing Investiments)

3. Kuwaunganisha wananchi wenye uwezo wa kuchimba visima vifupi ili kuchimba kisima kirefu.
Katika maeneo mengi yenye shida ya maji, ni kawaida kuona mwananchi mmoja mmoja kajiongeza kwa kuchimba kisima kifupi kwenye eneo lake kinachogharimu takribani Tsh 2,000,000 ikijumuisha gharama za uchimbaji wa mkono, kutengeneza na kuweka ringi za zege, kufunga pampu na kuweka tenki la maji. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Mtaa au Kijiji inawezekana isiwe rahisi kwa mamlaka kuwa na fedha za kuchimba kisima kirefu kwa ajili ya wananchi wengi lakini endapo wananchi kadhaa wenye uwezo na mipango ya kuchimba visima vifupi wangeunganishwa na mamlaka ya Kijiji au Mtaa husika, inawezekana wakachangia fedha takribani Tsh. 10,000,000 za kuchimba kisima kirefu ambacho kitatoa huduma ya maji kwa watu wengi zaidi kwenye mtaa au kijiji hicho. Wananchi wengine wakawekewa utaratibu wa kulipia gharama za kuunganishiwa maji na za uendeshaji.

4. Serikali kupunguza au kufuta gharama za kibali na ada za kila mwaka kwa wenye visima.
Kuna gharama za kulipia unapotaka kutumia maji chini ya ardhi. Kwa mfano, kwa Mamlaka ya Bonde la Mto Wami/Ruvu gharama za kuchimba kisima zinaanzia Tsh. 60,000 kwa matumizi madogo ya nyumbani na Tsh. 150,000 kwa matumizi makubwa na ada ya kila mwaka ya Sh100,000 na Sh150,000 mtawalia. Uwepo wa gharama hizi unavunja moyo wenye lengo la kuchimba visima ili kusaidiana na Serikali kufikia lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji. Kwa kuwa tayari kuna kodi ya umiliki wa ardhi na kodi ya majengo, kumtoza fedha mwananchi anaechimba kisima kwenye ardhi yake kwa gharama zake na kwa matumizi yasiyo ya kibiashara nadhani sio sawa sana, badala yake mwananchi huyu angehamasishwa kwa kuwekewa miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi wengine wanaomzunguka ambao watalipia maji kadri wanavyotumia ili mamlaka zipate mapato.

Maji chini ya ardhi yanaweza kutumika kukidhi mahitaji ya maji kwenye jamii, shughuli za kiuchumi na mazingira. Utumiaji wa maji haya una faida nyingi kama chanzo cha kudumu na cha uhakika endapo maji yatatumika vizuri na kutunzwa yasichafuliwe na shughuli za kibinadamu. Ili kufaidika vizuri na maji chini ya ardhi, uwajibikaji katika matumizi ya maji, udhibiti wa mara kwa mara na kupima usalama wa maji ni muhimu katika kuhakikisha matumizi endelevu na yaliyo salama.​
 
Grarama za maji ukiwa umbali wa mita mia ni zaidi ya 1 m lakini ukichimba kisima kwa njia ya kawaida na unapata maji ya uhakika hyo milioni haiwezi isha. Uchimbaji wa maji yaliyo chini ya ardhi ni rahisi haswa kwa matumizi ya nyumbani. na zaidi ya hayo pia ukiwa na maji yako hutalipia bili kila siku za dawasa/ au mwawasa. nk.
 
Nawashukuru sana wote mliosoma na kunipigia kura. Kipeekee niwashukuru Jamii Forums wakiongozwa na Mkurugenzi wao Mr. M. Melo kwa shindano hili linalotupa fursa ya kutoa mawazo yetu chanya ya kuchochea mabadiliko tunayotaka kuyaona kwenye jamii yetu. Niwashukuru pia washiriki wenzangu wote. Lets keep on advocating for changes.
 
Back
Top Bottom