SoC02 Tutakufa ila Utanzania wetu utadumu milele

Stories of Change - 2022 Competition

Chifumoses

New Member
Aug 30, 2022
1
0
Wengi watanzania tumekua ni watu wa kulalamika, kuhuzunika, kunyanyasika, kunyanyasana na kubaguana wenyewe kwa wenyewe kwasababu za kiuchumi, elimu, nyadhifa, makabila, ujinga/upumbavu, imani zetu tulizonazo na pengine kutokana na mapungufu ya kibinadamu.

Watanzania tuliowengi tunapitia matatizo sana ya afya, umaskini, hofu, madeni hata furaha kwenye maisha yetu ya kila siku imekua ni nadra sana. Binafsi naamini tunao utulivu wa kutosha ila hatuna amani ndani ya mioyo na akili zetu.

Tuliowengi tunaishi kwa kubahatisha, kusaidiwa, kutegemea zaidi kusubiria kuletewa bila kujua wakati mwingine tunasubiria nini na tunamsubiria nani atuletee hayo maendeleo tunayoyahitaji na kuyaota.

Hadi hivi sasa tunajivunia vitu vilivyotengenezwa na wakoloni, hadi leo uhuru wa kutoa maoni umekua ni mgumu pale tu unapojaribu kuzungumza ukweli na hali halisi iliyokuwepo ni utakimbizwa na msemo wa Mchochezi. Hivi ni lini tutaweza kuzitumia rasilimali zetu vizuri kwa ajili ya Taifa letu na vizazi vyetu vijazo?

Au labda tuseme ni mapungufu tu ya kibinadamu sisi watanzania yanatusumbua zaidi na ndio yamepelekea tufike hapa.

Au labda tuendelee tu kuimba kwa sauti ya juu sana nyimbo yetu ya Taifa kuna miujiza fulani labda itatokea. Au sisi tuliowengi hatutambui na hatutaki kutambua chochote zaidi ya matumbo yetu.

Tuache kumtafuta mchawi watanzania wenzangu, wachawi ni sisi wenyewe. Hizi Au Au kiukweli haziwezi kuisha pasipo umoja, kuungana na kushirikiana.

Ni wangapi kati yetu sisi watanzania tunaelewa msemo wetu pendwa "Tii Sheria Bila Shuruti" Je, ni kweli sisi watanzania kwa idadi yetu, ni wangapi tunazijua izo sheria? Je, ni kweli huwa shuruti haitokei kwa watu wote pale tunapotii Sheria?

Au ndio mpaka mtanzania mwenzetu adhurike na arekodiwe anavyoteseka kutokana na uzembe, upumbavu na majivuno ya wachache wanaotumia vyombo vya dola vibaya kwa masilahi yao binafsi ndio wachache wanaokumbuka wapaze sauti, hii tabia ya kusubiria litokee tujifunze tutaiacha lini?

Hii tabia ya kujikuta uwe na ushahidi majanga yanapokutokea ndio utetewe tena ushahidi upate bahati uzagae sehemu za mitandao ndio Usaidiwe, hiki kitabia tutakiacha lini? Watanzania sisi jamani Tujaribu kupunguza unafiki na tusaidiane kujitathimini.

Watanzania tuliowengi tunapaswa kubadilika, tuache kuishi kwa mazoea na tuwe kitu kimoja kwenye yanayotuumiza sisi na kizazi chetu ikiwemo mfumo mzima wa Elimu, Afya, Miundombinu, Kilimo, Ufugaji na Ajira na vyote vitusumbuavyo kila mara.

Kulifanikisha hili, Kila Mtanzania anapaswa kujichunguza, kujirekebisha na kujitambua linapokuja suala la kuyatafakari Maendeleo. Maendeleo ni kupevuka pia kiakili, kimtazamo, kifalsafa kwenye kila kitu tunachopitia ili kupata ufumbuzi yakinifu, salama, uliobora na wa kudumu.

Njia rahisi ya kubadilisha fikra za sisi Watanzania kwa pamoja ni kujaribu kubadilika kwanza mtanzania mimi na wewe katika kujifunza, kukumbushana, kusikilizana na kujenga hoja ili tuwe na mlengo mmoja wa kudumu kwenye yale ambayo yataleta maendeleo kwenye masirahi mapana ya taifa letu la sasa na vizazi vijazo.

Kwenye kila sehemu kama vile Kanisani, Misikitini na Kwenye Ofisi zetu lazima kuna muongozo unaozingatia taratibu, kanuni, sheria na haki za kila kitu cha pale.

Mfano, dini zetu na vitabu vyake. Timu zetu na katiba zake. Watanzania sisi tuliowengi ni imara kwenye kufatilia yasiyo na maana sana kuliko yaliyo na maana zaidi. Hatubezani ila sio sawa kutegemea imani na kumuachia Mungu mambo ya muhimu na ya msingi zaidi ila mambo mengine ikiwemo mpira tumekua ni washabiki wazuri sana.

Ni dhahiri tunahangamia sana sisi vijana kwa uzembe na kujiendekeza kwenye mapuuzi mengi tuliyoyaendekeza.Vijana tumeendekeza zaidi mihemko ya starehe, lawama na kusubiri kusaidiwa. Vijana wengi tumekua na kitabia ya kujiona tunajua kila kitu,utaratibu wa kufikiria kwa weledi umekua ni adimu kwa sisi vijana wengi. Vijana ndio ngao ya Taifa letu, ni Taifa la kesho si ndio misemo yetu.

Tunaibadilisha vipi Tanzania ikiwa hatujui na hatutambui umuhimu wa Katiba?

Wangapi tunajua hata maana ya Katiba?

Hivi historia ya Katiba yetu, tunaijua?

Ni watanzania wangapi tunaijua katiba kama vile tujuavyo vitabu vya imani zetu. Tungeweza kuijua katiba yetu, sisi sote tunaojua kusoma na kuandika tungekuwa tumepunguza changamoto na matatizo mengi sana.

Maendeleo kwa sisi watanzania kwenye uchumi, siasa, michezo, afya, miundombinu na elimu sio suala la utani. Sio suala la kubeza kabisa kama tunavofanya. Sidhani kama ni la kumuachia Mungu tu, kama Nyimbo ya Taifa tunavyoiimba kimazoea na kiitifaki tu, kwa kuimba tu bila kuamua kwa sauti moja tutawezaje watanzania wenzangu, Kubalikiwa? Tuache unafiki na kila siku Tujitathimini.

Mbona michezo wakati mwingine aswa mpira tunaweza kukusanyika kwa pamoja furaha tena kwa utulivu, kusherehekea, kuhoji, kulalamika na hata maamuzi kutolewa kwa haraka kutokana na nguvu ya sauti ya wananchi.

Nguvu ya wananchi inatokana na ushirikiano, umoja, uwepo wetu kwenye kila linalochochea maendeleo ya taifa sasa na wakati ujao.

Tumekua ni wepesi sana kushirikiana yanapotokea majanga, sherehe za kuhitimu na ushindi wa michezo yetu bila vurugu na hata kwenye usalama wetu tumekuwa na umoja wa hali ya juu.

Mfano, Hali ya kumpiga mwizi baada ya aliyeibiwa kupaza sauti mbona Watanzania wenzangu tumekuwa wepesi kukusanyika, umoja huohuo tuamue kuuleta kirahisi kuhoji yale ya msingi yanayoleta maendeleo ya tija ndani ya Tanzania letu.

Ni wajibu wetu kwa pamoja kuhakikisha kwa umoja tunayaleta maendeleo kwa misingi ya kusoma kwa ufasaha kabisa Katiba ya Nchi yetu.

Tunapaswa kujenga mazoea ya kuijadili zaidi na zaidi Katiba yetu ili tuzijue sheria, kanuni, na haki zetu.

Tukiwa tunahakika tulio wengi tunaijua, tukitengeneza misingi ya kuweza kuijua Katiba tutakua tumeanza taratibu nzuri zaidi ya kuuthamini, kuutambua na kuuheshimu Utanzania wetu.

Tutaweza kubadilisha mapungufu ya Katiba yetu baada ya tuliowengi kuanza kuifahamu, kuielewa, kuitambua inatambua na kulinda na kusimamia vipi mapana ya sheria, kanuni na haki zetu.

Mapungufu ya mifumo yetu yatarekebishika kwa urahisi zaidi tutakapoamua kuijua kwa wengi wetu Katiba kwanza.

Katiba ni kama msahafu au Bibilia ya nchi yetu. Tunaposoma Katiba tunajitengenezea mazingira mazuri ya kuwa na Maarifa. Taarifa inapojichua kwenye vichwa vyetu maarifa hupatikana.

Tujitathimini! Tusije kuacha Kujitathimini, Hakuna namna ya mimi au wewe kudumu lazima Tutakufa ila Utanzania wetu utadumu milele.

Watanzania wenzangu Tuwajibike kwa kusoma Katiba Yetu.

Ahsanteni.
 
Back
Top Bottom