SoC03 Tusimame kwenye nafasi zetu katika malezi ya watoto, ajira kwa watoto ni ukiukwaji wa haki za watoto

Stories of Change - 2023 Competition

Harold Sanja

New Member
Jun 2, 2023
3
3
UTANGULIZI.
Licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali, wazazi, jamii, Asasi za kiraia, wadau wa Elimu, na taasisi za kidini katika kuhakikisha suala la malezi linakuwa jukumu la kila mtu katika jamii, suala hili la malezi ya watoto bado limekuwa na changamoto kubwa sana kutokana na usasa na ubinafsi unaomfanya kila mzazi kuwa macho na malezi ya watoto wake pekee na kufanya suala la malezi kuwa la mtu binafsi na sio jamii nzima.

Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, suala la Malezi ya watoto lilikuwa ni jukumu la mzazi na jamii kwa ujumla, ilipotokea watoto wamefanya kosa mbele za watu, kabla suala halijafika kwa wazazi, wanajamii walikuwa na jukumu la kuwasahihisha na hata kuwaonya ili watoto wakue kwa kufuata miiko na maadili ya jamii husika, siku hizi suala la "Mtoto wa mwenzio ni wako" limebaki katika vinywa na si katika matendo hii ni kwasababu Wazazi, Walezi, Serikali na jamii kwa ujumla imekuwa haisimami kwenye nafasi yake katika maelezi ya watoto jambo ambalo linasababisha kuwa na watoto wasiofata miiko na maadili ya jamii zetu.

SUALA LA AJIRA KWA WATOTO.
Sote tunajua kuwa kila mtoto anayohaki ya kupendwa na kupatiwa mahitaji yote ya msingi , zaidi ya yote kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule anayohaki ya kupelekwa shule na kupata Elimu. Mara nyingi huwa najiuliza, ukiukwaji wa haki za watoto unatokana na kutokujua sheria au makusudi tu?

Mwaka 2022 nilipata bahati ya kuwa Karani wa Sensa ya watu na makazi, ambapo jukumu langu lilikuwa ni kuisaidia serikali kupata taarifa za Kijamii na kiuchumi za wananchi, katika zoezi hili niligundua kuwa kuna idadi kubwa ya watoto walio chini ya miaka 18 ambao wananyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu kwasababu ya kufanya kazi kama waajiriwa (Ajira kwa watoto).

Nilishangaa zaidi kuona watumishi wa umma ambao licha ya kuwa wameelimika lakini bado walikuwa wakiishi na mabinti wa chini ya miaka 18 kama wafanyakazi wa ndani, wakati kwa kawaida watoto wa miaka 12, 13, 14 na 15 wapo katika umri wa kuwa shule. Kwa kuwa hilo la ajira kwa watoto halikuwa limenipeleka basi nilifanya kazi niliyotumwa na serikali ya kuchukua taarifa za watu na makazi.

TAKWIMU ZINADHIHIRISHA UWEPO WA TATIZO HILI LA AJIRA KWA WATOTO.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kazi duniani(ILO) ya Mwaka 2007 (ILO Global report on Child Labour) Duniani kuna zaidi ya watoto Milioni 151 wenye umri wa miaka 5 hadi 17 ambao wanafanya kazi Kama waajiriwa(Child Labour). Lakini pia "Analytical Report of Tanzania National Child Labour Survey" (NBS: 2016) inaripoti kuwa, inakadiriwa kuwa nchini Tanzania kuna watoto Milioni 4.2 wenye umri wa miaka 5 hadi 17 ambao wanafanya kazi kama waajiriwa ni sawa na asilimia 28.8% ya watoto wote waliopo nchini. .

SHERIA ZILIZOPO ZINAFUATWA?
Kwa mujibu wa Sheria ya ajira na Mahusiano ya kazi namba 6 ya Mwaka 2004, inakataza watoto chini ya miaka 18 kuajiriwa au kufanya kazi kwenye mazingira hatarishi, pia sheria hii inataja adhabu zitakazotolewa kwa wote watakaokwenda kinyume na sheria hii.

Pia sheria ya elimu namba 49 ya Mwaka 2002 inasema ni wajibu wa mzazi kuhakikisha kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule anaandikishwa kuanza masomo lakini pia mzazi ahakikishe mtoto anahudhuria shuleni hadi atakapohitimu Elimu ya msingi.

Kwa mujibu wa sheria hizi, ni Wajibu wa Wazazi, Serikali na Jamii kuhakikisha wanasimama kwenye nafasi zao katika suala la malezi ya watoto kiasi cha kupinga na kutokomeza tatizo hili la ajira kwa watoto.

Inasikitisha sana kukuta mtoto chini ya miaka 18 ameajiriwa kwenye kilimo, kazi za nyumbani, migodini, kwenye madanguro ya wanaojiuza, kwenye vyombo vya Usafirishaji Kama Kondakta na wapiga debe, na maeneo mengine mengi ambayo ni hatarishi kwa usalama wa watoto.

Ripoti ya Tume ya Takwimu ya taifa ya mwaka 2016 inaweka wazi kuwa, kwa maeneo ya mjini wasichana ni waathirika zaidi wa tatizo la ajira kwa watoto ukilinganisha na wavulana, huku kwa maeneo ya vijijini kukiwa na idadi sawa ya waathirika wa ajira kwa watoto kati ya wavulana na wasichana.

CHANZO CHA TATIZO LA AJIRA KWA WATOTO.
Kwa tafiti nilizozifanya kwa maeneo mengi niliyowahi kuishi na kusoma, nimegundua kuwa tatizo la ajira kwa watoto kwa kiasi kikubwa linasababishwa na Wazazi, Jamii na Serikali kutosimama kwenye nafasi zao(Kutotimiza wajibu) katika malezi ya watoto, kuhakikisha kila mtoto anapata haki zake za msingi na kupinga unyanyasaji na ukatili wanaofanyiwa watoto kutokana na tatizo la ajira kwa watoto.

Wazazi hawasimami kwenye nafasi zao(hawatimizi wajibu wao) kama wazazi katika suala zima la malezi ya watoto kwa kuwapa watoto mahitaji yao ya msingi kama vile chakula na mavazi, hivyobasi kutokana na wazazi kushindwa kuwapa watoto wao mahitaji yao kinachotokea ni watoto kwenda kufanya kazi kwa watu wengine ili kupata mahitaji yao na hapo ndipo tatizo la ajira kwa watoto linapoanzia.

Jamii haitimizi wajibu katika malezi ya watoto kwasababu jamii imekuwa ikiyafumbia macho baadhi ya matendo ya ukiukwaji wa haki za watoto, pia jamii haichukui hatua stahiki kwa watoto wanaokwenda kinyume na miiko na maadili ya jamii zao na hapo ndipo tatizo la ajira kwa watoto lipoanza kuota mizizi katika ngazi ya jamii hadi Wilaya na Mkoa.

Serikali imeweka sheria ambazo haizisimamii kwa ufasaha katika malezi ya watoto hasa katika suala zima la ajira kwa watoto ambapo hakuna juhudi za wazi au oparesheni za wazi zinazofanywa na serikali katika kutokomeza tatizo hili hivyo wafanyakazi wa serikali hawatimizi wajibu wao katika kuhakikisha Kuna kuwa na ustawi wa jamii na utawala bora kwa kutatua tatizo hili la ajira kwa watoto.

MADHARA YATOKANAYO NA AJIRA KWA WATOTO.
Nimekuwa shuhuda wa madhara mengi yanayotokana na ajira kwa watoto ambayo madhara hayo yanawaathiri watoto wenyewe, jamii na taifa kwa ujumla. Baadhi ya madhara hayo ni, Watoto kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu hivyo kusababisha ongezeko la ujinga katika jamii, watoto wanapata matatizo ya kisaikolojia kutokana na ukatili na unyanyasaji wanaofanyiwa na Waajiri wao, na ukatili huo husababisha Mimba za utotoni na maambukizi ya magongwa kama vile UKIMWI, kwa namna nyingine ajira kwa watoto husababisha kuzuka kwa watoto wa mitaani , makundi ya watumaiji wa madawa ya kulevya na wahalifu kama majambazi na waporaji.

NINI KIFANYIKE KUTOKOMEZA TATIZO LA AJIRA KWA WATOTO?
Kwanza,ni lazima WATU WASIMAME KWENYE NAFASI ZAO(Watimize Wajibu wao) kama Wazazi, Walezi, Jamii na viongozi wa serikali katika malezi ya watoto lakini pia kuwe na ushirikiano baina yao katika kutokomeza tatizo la ajira kwa watoto, kwa kufanya hivyo kwa kisasi kikubwa tutakuwa tumeweza kutatua tatizo hili.

Pili, Taasisi za kidini, Wadau wa Elimu na Asasi zisizo za kiserikali zishirikishwe katika mapambano dhidi ya ajira kwa watoto na malezi ya watoto kwa ujumla wake, hii ifanyike kwa kutunga sera mbalimbali Kama vile "Ajira kwa watoto ni ukiukwaji wa haki za watoto tushirikiane kupigania haki za watoto" na kuanzisha program za utoaji wa Elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari kama vile magazeti, redio na televisheni.

Mwisho, Hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wazazi ambao hawatimizi wajibu wao katika malezi ya watoto na watu wote wanao waajiri watoto kwenye shughuli mbalimbali za nyumbani, kwenye maduka, mashambani, kwenye migodi na barabarani. Kwa kufanya hivyo, ni imani yangu kuwa tatizo la ajira kwa watoto litakwisha na kufanya nchi yetu kuwa na vizazi bora vijavyo, vizazi vya watu waliopata Elimu, Wazalendo, Wachapakazi na Waadilifu. Lakini kwa upande mwingine tusipofanya hivyo, tusiposimama kwenye nafasi zetu na kutimiza wajibu wetu tutakuwa na Kizazi cha ajabu sana siku za usoni.
 
Back
Top Bottom