Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,243
- 34,899
Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi. Kuna dhana inajengwa kwamba viongozi wa Chama chetu hawataki kupigania uwepo wa Tume Huru.
Kwamba tumeridhika na viubunge na viudiwani tunavyopata every five years, etc. Kwamba ili tuweze kushinda na kuchukua dola lazima tuache kushiriki uchaguzi hadi hapo tutakapopata Tume Huru, etc.
Hoja hii ni potofu.
Tume Huru ya Uchaguzi haipatikani nje ya mapambano mapana ya kutafuta demokrasia katika nchi yetu. Tume Huru ni sehemu tu ya tatizo la msingi la nchi yetu: tatizo la ukosefu wa demokrasia.
Tume ya Uchaguzi imeundwa kwa mujibu wa Katiba iliyopo. Inafanya kazi, by and large, kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizopo.
Kupigania Tume Huru maana yake ni kupigania Katiba Mpya; au angalau marekebisho ya Katiba iliyopo. Haiwezekani kupigania Tume Huru au marekebisho ya Katiba ya sasa in vacuo; inapiganiwa katika mazingira halisi ya kisiasa, kikatiba/kisheria na kitaasisi tunamoishi.
Kwa maneno mengine, ili upiganie Tume Huru lazima uwe na jukwaa la kusimamia. Iwe Bunge, au vyombo vya habari au mikutano ya hadhara, au kuchukua silaha na kwenda 'msituni', etc. Yote hayo ni majukwaa.
Sasa hoja ni je, tutumie jukwaa gani ili kupata Tume Huru??? Tukiacha kushiriki uchaguzi, tunabakia na jukwaa gani la kudai Tume Huru??? Mazingira ya vyombo vya habari, kama jukwaa la mapambano, ni rafiki na wezeshi kiasi gani??? Mikutano ya hadhara, jukwaa lingine muhimu, ni rafiki na wezeshi kiasi gani???
Ukiachia hii miaka ya Magufuli, je, mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani imekuwa mirahisi kiasi gani siku za nyuma kama majukwaa ya kudai demokrasia na Tume Huru???
Ukiachia wakati huu, vyombo vya habari vimekuwa rahisi kiasi gani kama majukwaa ya kidemokrasia??? Vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa rafiki na wezeshi kiasi gani katika madai yetu ya demokrasia na Tume Huru???
Ukweli ni kwamba maeneo yote haya yamekuwa na matatizo. Lakini hatujaacha kutumia fursa kidogo zilizokuwapo kudai demokrasia zaidi.
Hatuna uhuru wa vyombo vya habari sasa kuliko ilivyokuwa kabla ya Magufuli. Kuna matatizo mengi kwenye eneo hili kuliko zamani.
Lakini hakuna mtu anayedai vyombo vyetu vya habari viache kukusanya, kuandika na kusambaza habari hadi hapo tutakapopata uhuru kamili wa habari. Vyombo hivyo vinaendelea kufanya kazi zao katika mazingira halisi yaliyopo huku vikiendelea kudai uhuru wa habari.
Vivyo hivyo na sisi tunapaswa kuendelea kudai Tume Huru katika mazingira halisi ya kiuchaguzi yaliyopo.
Hatuwezi kususia jukwaa muhimu kama Bunge, licha ya matatizo yake mengi yaliyopo, unless jukwaa hilo lifungwe kabisa. Hatuwezi kususia uchaguzi, unless jukwaa la uchaguzi lifungwe kabisa, kama ilivyotokea majuzi kwenye uchaguzi wa mitaa na vijiji.
Mjadala huu unanikumbusha mjadala wa 'Mageuzi au Mapinduzi' ('Reform or Revolution') kati ya wanamapinduzi wa kijamaa wa Ulaya zaidi ya miaka mia moja iliyopita.
Wenye 'msimamo mkali' wa kimapinduzi walikuwa wanadai hakuna kushiriki harakati za kimageuzi kama vile mapambano ya kibunge; tufanye mapinduzi kwanza, etc.
Wengine wenye 'msimamo vuguvugu' wakidai kilele cha mapinduzi kinafikiwa kwa njia ya mageuzi ya kiuchaguzi, etc. Lenin aliwatuhumu wenye msimamo mkali kuwa wanasumbuliwa na 'ugonjwa wa utoto' ('an infantile disorder'!!!)
Na sisi pia hatutakiwi kuwa na ugonjwa huo. Kila jukwaa la mapambano ya kidemokrasia ni muhimu litumike. Kutumia njia mojawapo tu haitaleta matunda. Tunahitaji kutumia fursa zote zilizopo.