SoC02 Tufahamu wabantu na Lugha zao(Lugha za kibantu)

Stories of Change - 2022 Competition

GoJeVa

Member
Sep 15, 2021
41
59
TUWAFAHAMU WABANTU NA LUGHA ZAO(LUGHA ZA KIBANTU).

MFANO WA LUGHA ZA KIBANTU.


Kiswahili na lahaja zake
: Tanzania, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Komori, Mayotte, Msumbiji, Somalia.

Kinyarwanda: Rwanda.

Kirundi: Burundi.

Lingala:Angola, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon.

Chichewa : Malawi.

Kizulu: Afrika Kusini.

Kisukuma : Tanzania.

Kishona: Msumbiji, Zambia, Zimbabwe.

Gikuyu/Kikuyu: Kenya.

Kikongo :Angola, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Chiluba: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Angola.

Utangulizi.

Lengo la makala hii ni kutaka watu wafahamu lugha za kibantu ni zipi, na wabantu ni wakina nani. Hivyo basi ungana na mimi ili tujue mengi yaliyomo katika makala hii maalumu.

Kwanza kabisa inabidi tujue maana ya istilahi za muhimu kutoka katika kichwa cha mada yetu kuu kama vile; maana ya wabantu na maana ya lugha.

Lugha ni sauti za nasibu zilizokubalika katika jamii ya watu fulani ili zitumike kama njia yao ya mawasiliano.

Wabantu ni watu wenye asili ya afrika, watu hawa ni wale walio wazawa wa nchi zilimo ndani ya bara la afrika mfano wa baadhi za nchi ambamo wabantu hupatikana ni kama vile; Tanzani,Rwanda,Afrika kusini, Kameruni,Kenya,Nigeria,Jamuhuri ya watu wa Kongo na zinginezo nyingi.

Kibantu ni lugha za kikabila au makabila mbalimbali ndani ya bara la afrika mashariki, ikumbukwe ndani ya bara la afrika kuna makabila mengi sana na lugha za hayo makabila ndio huitwa lugha za kibantu. Mfano wa hizo lugha za kibantu ni kama vile; Chichewa ambacho huzungumzwa na kabila la wachewa nchini Malawi, Kizulu ambacho huzungumzwa na kabila la wazulu nchini afrika kusini, Kinyakyusa ambacho huzungumzwa na kabila la wanyakyusa nchini Tanzania, Kisukuma ambacho huzungumzwa na wasukuma nchini Tanzania, Kishona ambacho huzungumzwa na kabila la washona linalopatikana Zimbabwe pamoja nchi jirani. Hiyo ni mifano michache ya lugha za kibantu.

ZINGATIO MUHIMU: Baadhi ya lugha za kibantu zimefikia hatua ya kurasimishwa na kusanifishwa, na hii imepelekea lugha hizo kuwa rasmi katika baadhi ya nchi, mfano wa lugha hizo ni kama vile; Kinyarwanda ambacho ni lugha rasmi nchi Rwanda na huzungumzwa kwa kiasi kikubwa na raia wa nchi hiyo, Kirundi hii ni lugha ya kibantu ambayo imekuwa rasmi nchini Burundi, Kiswahili hii pia lugha ya kibantu ambayo ni lugha ya taifa nchini Tanzania pia huzungumzwa eneo kubwa la afrika mashariki, Kilingala hii ni lugha ya kibantu ambayo imekuwa rasmi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Kongo, hiyo ni mifano michache ya lugha za kibantu zilizorasimishwa katika baadhi ya nchi.

UBANTU WA KISWAHILI.
Kiswahili kinajidhihirisha kuwa ni kibantu katika namna mbili; namna ya kwanza ule uwepo wa kiswahili kabla ya ujio wa wageni(ushahidi huu unathibitishwa wazi na wageni wa kwanza kufika pwani ya afrika mashariki, kama vile; Ali idris(1100-1166), Al-Masudi(915.BK), Marco polo. Wageni hawa walithibitisha wazi kuwa walipofika pwani ya afrika mashariki walikuta wenyeji wana lugha yao, ambayo inasadikika ni Kiswahili). Namna ya pili ni kwamba Kiswahili kina uhusiano mkubwa na lugha za Kibantu(ushahidi huu unathibitishwa na mfanano mkubwa wa lugha ya Kiswahili na lugha zingine za kibantu kama vile kisukuma,kihehe,kibena, kindali,kihaya).


UPEKEE WA LUGHA ZETU ZA KIBANTU.
Ni jambo la adili kujivunia lugha zetu za kiafrika, kwa sababu lugha hizi ambazo kwa jina lingine tunaweza ziita lugha za kibantu zina upekee mkubwa sana, upekee huo ndio hufanya lugha zetu za kibantu kuwa na umaridhawa pale tunapozitumia. Hebu tuone upekee huo katika maeneo yafuatayo;

1. Miishio ya irabu katika vitenzi vingi kwenye lugha za kibantu.

Lugha nyingi za kibantu kama vile; kizulu, Chichewa, kinyakyusa, Kiswahili zina miishio ya irabu katika vitenzi vyake. Hii inaleta upekee katika lugha zetu za kiafrika, kwa mfano;

KizuluChichewaKiswahiliKinyakyusa
UyadlaamadyaAnakulaIkulya
UyaculaamaimbaAnaimbaIkwimba
UyezaakubweraAnakujaIkwisa
UyahlekaamasekaAnachekaIkuseka
*Ukiangalia vitenzi vyote hapo juu vimeishia na irabu na huo ndio upekee wa lugha zetu za kiafrika.

2. Mpangilio wa Kiima na Kiarifu katika sentensi za lugha za kibantu.

Katika kujenga tungo ndani ya lugha za kibantu, huwa kuna ngazi nne ambazo ni neno, kirai, kishazi na sentensi. Katika ngazi ya mwisho ambapo tunapata sentesi, sentensi hiyo inaweza kuwekwa au kugawanywa katika sehemu mbili ambazo ni kiima na kiarifu. Mgawanyo huo wa sentensi katika kiima na kiarifu pia hutokea kwa kiasi kikubwa katika lugha nyingi za kibantu, kwa mfano;

kiimaKiarifu
KiswahiliMtotoAnakula
KizuluinganeUyadla
KinyakyusaUmwanaIkulya
ChichewamwanaAmadya
*Mpangilio wa sentensi hizo, wote umebeba viima na viarifu, hii ni kwa sababu lugha hizi zina asili sawa na zote ni lugha za wabantu.

3.Mgawanyo wa vipashio katika vitenzi vya lugha za kibantu.

Vitenzi vya lugha za kibantu huweza kugawanyika katika viambishi vidogo vidogo kama vile; viambishi vya nafsi, viambishi vya njeo(wakati), viambishi vya umoja na uwingi na vinginevyo vingi. Kitu cha upekee ni kuwa lugha nyingi za kiafrika zina ruhusu mgawanyo huu wa viambishi, kwa mfano;

Kiambishi cha nafsi(nafsi ya tatu umoja).Kiambishi cha wakati/njeo(wakati ulipo).Mzizi wa nenoKiambishi tamati
Kiswahilia--na--kul--a.
Chichewaa--ma--dy--a.
Kizuluu--ya--dl--a.
Kinyakyusai--ku--ly--a.
*Hivyo, pia katika mfano huu inaonesha wazi lugha za kibantu zinawiana kwa kiasi kikubwa na kuwa na upekee wake.

IKUMBUKWE.

Licha ya lugha zetu za kibantu kuwa na upekee mkubwa, bado haindoi ukweli kuwa katika dunia yetu hakuna lugha bora kuzidi nyingine, lugha zote zina hadhi sawa. Pia, lugha zina tabia ya kuathiriana yaani lugha moja inaweza kuchukua msamiati katika lugha nyingine na kuutumia. Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi ambayo yametoholewa kutoka kwenye lugha zingine kama vile, kutoka kwenye lugha ya kiarabu, kutoka kwenye lugha ya kingereza pia na katika lugha zingine. Vile vile lugha kama ya kingereza pia imetohoa msamiati mwingi kutoka katika lugha zingine, kama vile; kutoka kwenye lugha ya kigiriki, kilatini na lugha zingine pia.

AHSANTENI.

MAREJEO

1.Introduction to the Phonology of the Bantu Languages. By Carl Meinhof. Translated, revised, and enlarged in collaboration with the author and Dr Alice Werner, by N. J. v. Warmelo. pp. 248, 1 map. Berlin: Dietrich Reimer (Ernst Vohsen). London: Williams & Norgate, Ltd., 1932.

2. Wikipedia, kamusi huru. www.wikipedia.org.
 
Umechambua vizuri, ila makala yako ni ya elimu, uchumi, utawala, kilimo au afya? Ni swali tyu!
Hii ni makala inayohusu elimu, kwa sababu dhana ya elimu inasema...
."Elimu ni njia ambayo hutumiwa na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine." Kwa hiyo hayo ni maarifa ambayo nimeyafikisha kwa hadhira ili ambao walikuwa hawayafahamu wayafahamu.
 
Back
Top Bottom