Mwanahalisi wamefulia tuu
SERIKALI YAUZA TBC KINYEMELA
SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC) limeingia ubia na kampuni ya China bila ya kushirikisha Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), imefahamika.
Aidha, taarifa ambazo gazeti hili limepata zinasema si serikali wala menejimenti ya TBC aliyetangaza zabuni (
Expression of Interest) ili makampuni mengine yaweze kupeleka maombi ya kushirikiana na shirika hilo katika mfumo mpya wa utangazaji.
Hivyo kupatikana kwa mbia wa TBC katika maombi ya kusimamia masafa ya kitaifa, kunaelekea kuvunja Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 inayoshurutisha utangazaji wa tenda ili kila anayetaka ashiriki.
TBC imeungana na kampuni ya Star Communication Network Technology Co. Ltd ya China na kuanzisha kinachoitwa sasa Star Media (Tanzania) Company Limited, kwa kuipatia hisa 6,500 huku yenyewe ikibaki na 3,500.
Kila hisa kati ya hizo ina thamani ya dola 100. Star Media imesajiliwa Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA) 26 Juni 2009 na kupewa hati Na. 71639. Imedhaminiwa kwa dola 1 milioni.
Kaimu Mkurugenzi wa PPRA, Ayubu Kasuwi amesema mamlaka yake haijashiriki kwa namna yoyote katika hatua za kuwezesha TBC kuuza hisa zake kwa kampuni hiyo.
TBC inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na hatua ya kuingia ubia sharti ifuate mlolongo wa taratibu za kisheria, ikiwa ni pamoja na kutangaza tenda.
Kasuwi alisema ofisi yake haina taarifa za kuuzwa kwa hisa asilimia 65 za TBC na kwamba imeanza kufuatilia taarifa hizo.
TBC iko katika mchakato wa kubadilisha mfumo wa utangazaji kutoka analogi (
analogue) unaotumika sasa kuingia digito (
digital).
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Hazina, ambaye alitambulishwa na Katibu Muhtasi wake kwa jina moja la Mbelwa, alisema hana taarifa za kuuzwa kwa hisa za TBC.
Hata hivyo, Mbelwa hakuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, badala yake alishauri aulizwe Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBC, Wilfred Nyachia.
Nyachia ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kushika wadhifa huo, hakupatikana ofisini kwake wala kwa simu yake ya mkononi.
Katika hali ya kawaida, Msajili wa Hazina ndiye mwenye jukumu la kutunza kama mwakilishi wa serikali kumbukumbu za mali na huduma za serikali, mashirika, wakala na makampuni.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBC, Tido Mhando alisema mamlaka zote zinazotakiwa kufahamu mchakato huo, zimejulishwa.
Mhando alisema, Yeyote anayetaka kujua suala lolote kuhusu ubia wa TBC na kampuni ya kichina, aende kwenye mamlaka hizo.
Aliponganganizwa kueleza anachokijua, Mhando alingaka, Kwani wewe unataka kujua nini hasa? Kama unataka kufahamu jinsi tulivyoungana na kampuni hiyo nenda kwenye mamlaka zinazohusika. Zote zina taarifa
nenda TCRA, BRELA, utaelezwa.
Taarifa za ndani ya serikali zinasema, kampuni hiyo ya Kichina iliwahi kuomba kuwekeza katika sekta ya habari katika nchi za Uganda na Kenya, lakini ilikataliwa.
Kama wewe ni mwandishi wa habari kwa nini unafanya kazi kwa kutumia maneno ya mitaani? Tafuta ushahidi ndipo uulize. Kwa taarifa yako ninafahamu kuwa muda si mrefu mwekezaji huyu ataanza kufanya kazi na KBC (Shirika la Utangazaji la Kenya), alieleza Mhando.
Mhando aligoma kuelezea utaratibu uliotumiwa kumtafuta mbia, badala yake akasisitiza zifuatwe mamlaka zinazowajibika kusimamia masuala hayo.
Kwa taarifa yako, hivi karibuni tulikuwa na mkutano Dodoma kujadili suala hilo. Mwenyekiti alikuwa Waziri Mkuu
Nakueleza hayo ili ufahamu kuwa yametekelezwa kwa level (kiwango) hiyo, alisema.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, maombi ya Star Media ya kumiliki masafa ya digito, kati ya asilimia 100 ambazo imeomba kutoka serikalini kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), asilimia 65 zitakuwa za kampuni ya Kichina wakati asilimia 35 ndizo zitakuwa na TBC.
Kwa kadri mambo yalivyo, kampuni hizi mbili tayari zimejihakikishia kupewa masafa kwa pamoja.
Muungano wa Mawasiliano ya Kimataifa (International Telecommunication Union-ITU) unataka kila taifa mwanachama kuhakikisha matangazo yote ya televisheni na redio yanakuwa katika viwango vya digito ifikapo mwaka 2012.
TCRA imewataka wananchi wanaopinga mgawo wa masafa, wapeleke hoja zao kwa Mkurugenzi Mkuu katika siku 14 tangu kutolewa kwa matangazo haya.
Serikali, kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetenga nafasi tatu tu za kampuni zitakazopewa leseni ya kuendeshea mitambo ya kurushia matangazo ya televisheni kwa viwango vya digito (Digital Television Multiplex Services).
Mpango wa kuhakikisha matangazo yote yanatolewa kwa njia ya digito ulianza kwa kufanya vikao na watangazaji wote mwaka 2005.
Kutokana na mchakato huo, TCRA imegawa leseni za kuendesha mitambo hiyo katika maeneo matatu: Serikali, sekta ya biashara na madhehebu ya dini.
Taarifa nyingine kutoka BRELA zinasema kampuni ya Star Media hisa zake zimesajiliwa kwa mfumo wa dola badala ya shilingi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kaimu Mtendaji mkuu wa BRELA, Noel Shani alikiri kwamba Star Media imesajiliwa kwa kutumia dola badala ya shilingi, jambo ambalo amekiri kuwa ni kinyume cha taratibu.
Ni kweli, lakini tutawajulisha ili waweze kuja kubadilisha, amesema.
Taarifa zinasema kampuni waliyoingia nayo haikufanyiwa tathmini (due diligence). Mkataba wake haujachunguzwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala hakuna Baraka za Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo, TCRA inasema haina jukumu la kufuata taratibu za ndani za TBC katika kuunda kampuni au kuingia ubia na kampuni nyingine ya kigeni au ya ndani.
Hata hivyo, kwa TBC kubakiwa na asilimia 35 na kuachia asilimia 65 kwa wageni kumeelezwa kupingana na mapendekezo ya serikali katika sera mpya ya habari, ambayo kama ikipitishwa, wageni hawataruhusiwa kuwa na hisa kubwa katika sekta ya habari kuliko watu wa ndani.
Katika maombi yao ya awali, TBC waliomba peke yao, lakini baadaye wakaingiza wageni hao walioingia nao ubia.
http://www.mwanahalisi.co.tz/index.php?id=622