Pamoja ya kuwa nii article ni ya mda mrefu ila nimependa kuiweka hapa kutokana na vitimbi visivyoisha vya huyu mzeee wa kimachame asiyeamua kurudi kwake akapumzike na kutafuta kufia jukwaani..
Kuna baadhi ya maneno yamenichekesha kwani ni mtu ambaye akisimama jukwaani hana tofauti na ZE KOMEDI kwa anayoongea...
CHAMA cha Tanzania Labour(TLP) ndicho kilichokuwa kikishikilia jimbo la Biharamulo Magharibi, baada ya kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Mgombea ubunge wa TLP katika uchaguzi huo, Phares Kabuye, ambaye kwa sasa ni marehemu, alipata kura 24,206.
Kabuye alikuwa ni mtu wa watu na muelewa na hasa katika masuala ya kisiasa. Kitaaluma alikuwa ni Mwalimu. Alifundisha kwa miaka mingi shule kadhaa za msingi. Kutokana na ukarimu wake, uchapa kazi wake na kupendwa na watu wa rika zote, wananchi waliamua kuunganisha nguvu zao mwaka 2005 na kumpatia ushindi huo.
Ni uwazi na ukweli usiopingika kwamba ushindi wa Kabuye katika jimbo hilo, ulikuja kutokana na msuguano uliokuwepo wakati huo ndani ya CCM wakati huo, ambapo waliteua mtu ambaye wananchi wengi hawakumtaka, hiyo ni baada ya kukaa bungeni kutoka mwaka 2000-2005.
Hivyo, kutokana na kifo chake, ilikuwa ni lazima TLP imsimamishe mgombea kwa vile ndicho chama kilichokuwa kikiliongoza jimbo hilo. Endapo sheria za nchi, zingekuwa kama za wenzetu wa nchi za nje, baada ya Kabuye kufariki dunia, TLP ndiyo ingelifanya uteuzi wa mwanachama wake mwingine kuziba nafasi hiyo.
Hata hivyo, mtu anaweza kusema kwamba Kabuye alizikwa na TLP nyumbani kwake, hii ni kutokana na kura ambazo chama hicho kilipata kwenye uchaguzi huo, licha ya kampeni zake kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, Augustine Mrema.
Wakati mwaka 2005 TLP ilipata jumla ya kura 24,206, safari hii kwenye uchaguzi huo mdogo, imeambulia kura 198 tu, ambazo unaweza kuita ni aibu kubwa kwa chama ambacho kilikuwa kikiongoza jimbo hilo.
Ni aibu kwa sababu kuna chama hakikumsimamisha mgombea kwenye uchaguzi mkuu wa 2005, ambacho safari hii kimeshika nafasi ya pili na kupata kura zaidi ya 10,000. Jibu rahisi hapa unaweza kusema TLP imemzika rasmi Kabuye na TLP yake jimboni humo na kwamba huo ndio mwisho wa safari ya chama hicho katika siasa za jimbo hilo. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa walioipigia kura TLP mwaka 2005, walikuwa ni wanachama wa CCM baada ya kutokubaliana na mgombea aliyesimamishwa na chama hicho.
Pamoja na wanaCCM hao kukipatia kura chama hicho mwaka 2005, imejidhihirisha kwenye uchaguzi huu mdogo, kuwa wengi walioamua kurudi CCM kutoka TLP mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2005. Pamoja na Mrema kuomba kura za huruma katika kampeni ili kumuenzi Kabuye, lakini wananchi wa jimbo hilo walionekana kutokitambua chama hicho na kuamua kukizika rasmi kwa kukinyima kura.
Katika kampeni zake, mara nyingi Mrema alikuwa akiituhumu CHADEMA kucheza rafu; na kuna wakati alikwenda mbali zaidi na kupiga magoti chini kumuomba Mwenyezi Mungu awalaani viongozi wa CHADEMA kwa rafu zao. Eee Mwenyezi Mungu sikia kilio changu hiki
.hebu waone hawa mafisadi wakubwa CHADEMA uwalaani. Hili jimbo lilikuwa ni la TLP, lakini kwa uroho wao wa madaraka wanangangania eti na wao wanalitaka.
Mungu wangu pamoja na kwamba wewe ni Mungu wa wote, lakini kwa hili, naomba unipendelee mimi Mrema na TLP yangu. Uwalaani hawa CHADEMA,alisema Mrema katika mkutano wake kwenye uwanja wa mpira wa wilaya hiyo. Mrema alikuwa ni kivutio kikubwa katika kampeni hizo. Mara nyingi alichelewa kuanza mikutano ya kampeni, kutokana na kupiga nyimbo za injili kwenye gari lake la matangazo.
Wakati mwingine alikilaani pia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutokuwa na huruma na kulingangania jimbo hilo moja tu. Hata hawa CCM, Mungu wangu nao waangalie kwa jicho lako, kwa sababu pamoja na kwamba wanamiliki majimbo 274, lakini bado wanakangangania haka kangu kamoja, alisema Mrema na kumuomba DJ kuweka wimbo wa Nibebe wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili, Rose Muhando, na kisha yeye kuanza kucheza jukwaani.
Wakati CCM na CHADEMA vilikuwa vikifanya mikutano minne hadi sita kwa siku moja katika maeneo mbalimbali, TLP kilikuwa kikifanya mikutano miwili kwa siku, huku Mrema akilalamika mbele ya wananchi kwamba yeye hana fedha za bangi na dawa za kulevya wala za kifisadi. Hakufafanua mbele ya mikutano yake, maana ya maneno yake hayo.
Hapa wamesema sana kwamba TLP haitasimamisha mgombea wake kwenye jimbo hilo wakidai kwamba Mrema amefulia. Mimi nataka niwaambie kwamba Mrema ni msafi sana, kwa sababu sina pesa za bangi na dawa za kulevya, wala pesa za ufisadi.
Mrema ni mtu safi katika inji hii na ndiyo maana hata Mbunge wenu Kabuye alipofariki Rais Kikwete ndiye aliyetupatia sisi TLP ndege ya kumleta hapa. Kwa kweli namshukuru sana Kikwete, ni mtu mzuri sana katika inji hii, alisema Mrema.
Aliongeza, mimi nataka niwaambie na kuwaonya hao CHADEMA na Baba yao CCM, kwamba hili jimbo ni la TLP na Mrema wake. Kwanza nashangaa, aliyefiwa ni TLP, lakini wanaongangania urithi ni watu wengine kutoka nje ya TLP. Hivi kama si uhuni, ni nini ndugu zangu?.
Katika hatua nyingine, Mrema alimtuhumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kuwa amekuwa akijitahidi kila mara kufanya vitendo vya makusudi kwa ajili ya kuihujumu TLP.
Mrema alitoa tuhuma hizo siku alipofungua matawi ya TLP katika eneo la Majengo A na Soko la zamani mjini Biharamulo, ambako alidai kukamata kadi kadhaa za CHADEMA zilizopelekwa katika matawi ya TLP, kwa lengo la kuwarubuni wanachama wake wajiunge na CHADEMA.
Ndugu zangu huyu Mbowe ni mtu hatari, kule Tarime alitangaza rasmi kuvunjika kwa ndoa ya wapinzani. Leo amefika hapa Biharamulo na ameanza kucheza rafu, anasema eti TLP tunamuunga mkono mgombea wao. Ni muongo. Ni CHADEMA hawa hawa walioshirikiana na CCM kumhujumu Kabuye kwa kumfungulia mashitaka ya uongo.
Wamekuja hapa na makadi yao ya CHADEMA, wameyapeleka katika matawi yetu ya TLP, wamejaribu kushawishi wanachama wetu waikimbie TLP na wajiunge na CHADEMA. Nasema huu ni ujambazi. Mbowe wewe ni ndugu yangu, tunatoka mkoa mmoja. Niachie haka kajimbo kamoja, mbona mimi Tarime sikuja huko? alilalamika Mrema.
Hata hivyo, Mrema alisema pamoja na njama hizo, yeye kama mwenye nyumba amefanikiwa kuwarejesha ndani ya chama chake wanachama wote wa TLP walioasi na kuhamia CHADEMA, ambapo siku hiyo alifunga tawi moja la CHADEMA la Majengo A eneo la soko jipya mjini Biharamulo.
Katika hatua nyingine ambayo ilionekana kuwafurahisha watu, Mrema aliiagiza CHADEMA kushusha bendera za chama chake mara moja kwenye magari yao, vinginevyo kingechukuliwa hatua za kisheria. Hatua hiyo ya Mrema, ilitokana na CHADEMA kutangaza katika mikutano yake ya kampeni katika jimbo hilo kwamba vyama vya TLP, CUF na NCCR-Mageuzi, vimeamua kuiunga mkono katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Biharamulo Magharibi.
Hata siku mojaa TLP kama TLP haiwezi kufanya mchezo wa kitoto kama huo
jimbo hili la Biharamulo Magharibi lilikuwa likiongozwa na TLP, sasa iweje leo sisi TLP tuseme kwamba hatusimamishi mgombea kwa ajili ya kulitetea jimbo ambalo mbunge wake amefariki dunia, anasema.
Anasema, mimi nashindwa kuwaelewa hawa CHADEMA, wao walifiwa kule Tarime, tukwaunga mkono, wala hatukumsimamisha mgombea wetu, lakini leo wao wamekuja hapa na kila aina ya kimbelembele, eti wanataka kuchukuwa jimbo hili, huo ni wizi mtupu, wala hawana jipya.
Hata hivyo, mwisho wa siku ni TLP ambayo ilikuwa ikiongoza jimbo hilo, ndiyo iliyoshika nafasi ya mwisho kwenye uchaguzi huo, tena kwa kupata kura za aibu, ambazo hazikufikia 200. Je, huu ndiyo mwisho wa TLP katika jimbo la Biharamulo Magharibi; ama ni mwanzo mzuri wa kujipanga upya?.