Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Part (TLP) Augustino Mrema, amesema watu wanaosema Rais Jakaya Kikwete amezungukwa na wezi ni wachochezi na wanahatarisha usalama wa taifa.
Mrema aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akichambua kauli za baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao pia ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walizozitoa mwezi uliopita kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF).
Wanasiasa hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Joseph Butiku, walidai kuwa Rais Kikwete amezungukwa na wezi katika serikali yake na hivyo kumwia vigumu kuchukua maamuzi yoyote magumu kwa mustakabali wa nchi.
Alisema watu wa aina hiyo ni wachochezi na kwamba kauli zao zinatakiwa kukemewa na wananchi wote kwa madai kuwa Rais Kikwete amechaguliwa kwa mujibu wa katiba ya nchi. Wakati Mrema akiwakemea wanasiasa hao, yeye pia aliwahi kutoa kauli kama hizo walizotoa wenzake katika vipindi mbalimbali katika harakati zake za kisiasa hapa nchini mpaka akafikishwa mahakamani ili kuthibitisha kauli yake.
Kati ya madai aliyowahi kuyatoa, kwa mfano, ni pamoja na kusema Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, na mawaziri waandamizi katika serikali yake walihongwa Sh. milioni 900.
Mkutano huo wa Mrema na waandishi wa habari ulisimamiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Clement Mshana.
Aidha, Mrema aliongozana na viongozi wa chama chake akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TLP, Hamad Tao. Katika kongamano la Mwalimu Nyerere, makada wa CCM na viongozi wa vyama vya upinzani walipata fursa ya kutoa maoni yao ambapo kikubwa walimtaka kujitenga na baadhi ya mafisadi ambao wanatumia nafasi zao kujinufaisha.
Miongoni mwa makada wa CCM walioshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafu, Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, Joseph Butiku na yeye Mrema alialikwa na alishiriki.
Alipoulizwa ni kwa nini hakutumia nafasi aliyoalikwa katika kongamano hilo kuwaambia makada hao waache kutoa lugha za uchochezi kwa Rais Kikwete, Mrema alikataa kujibu swali hilo na badala yake akamwachia Naibu Katibu Mkuu wake, Tao, ili ajibu.
Tao aliwajibu waandishi wa habari kuwa, Mrema aliomba nafasi ya kuwajibu kwa kunyoosha kidole juu mara tatu lakini mwenyekiti aliyekuwa akiongoza mjadala huo akakataa kumpa nafasi.
Alipoulizwa kuhusu kusema Mkapa alipokea rushwa ya jiwe la dhahabu na kama hiyo haikuwa lugha ya uchochezi inayohatarisha usalama wa nchi, Mrema pia alikataa kujibu swali hilo na kumpa tena Tao alijibu.
Hata hivyo, Tao hakutoa majibu kama swali lilivyotaka isipokuwa alizunguka na kusema kuwa mtu akipewa zawadi inayopitiliza, hiyo inahesabiwa kama rushwa.
Mrema alipobanwa maswali na waandishi wa habari aeleze kama kuna kitu amepewa ili azungumze hayo aliyoyasema alisema yeye hatarajii chochote kutoka kwa Kikwete wala hana mpango wa kutaka kurudi CCM.
"Mimi mwakani naenda kugombea ubunge katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro na najua nitapata tena bila nguvu ya mtu yoyote, hivyo sijikombi kwa Kikwete," alisema.
CHANZO: NIPASHE