Posted Date::11/5/2007
Mtuhumiwa kashfa ya rada afikishwa kizimbani Dar
Na Festo Polea
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Takukuru), imekamilisha upelelezi wa tuhuma za rushwa kuhusina na utata wa ununuzi wa rada na mmoja wa watuhumiwa katika kashfa hiyo, Shailesh Pragji Vithlani, amefunguliwa mashitaka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar salaam, ili kujibu tuhuma zinazomkabili.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za taasisi hiyo, Mkurugunzi wa Idara ya Elimu kwa Umma wa Takukuru, Mary Mosha, alisema mshitakiwa huyo alibainika kushiriki katika mlolongo wa ununuzi wa rada kutokana na uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo.
Alisema taasisi hiyo imeshafungua kesi namba 1474/2007 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya mtuhumiwa huyo, itakayokuwa chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi.
Kwa sasa natangaza rasmi kuwa mshitakiwa popote alipo duniani anatafutwa kwa ajili ya kujibu mashitaka yanayomkabili na asipofanya hivyo tutamkamata kwa vile hati ya kumkamata imeshatolewa na mahakama? alisisitiza Mosha
Mosha alisema Mshitakiwa huyo anayetafutwa ana uraia wa Tanzania na Uingereza, hivyo wamewasiliana na Polisi wa Kimataifa (Interpol), ili popote alipo duniani aweze kukamatwa na kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo alipotakiwa kuwataja watuhumiwa wengine waliobainika kuhusika na ununuzi huo wa rada, alikataa kwa madai kuwa taasisi hiyo imeanza kumfungulia mashitaka mtuhumiwa mmoja kwa kufuata taratibu na sheria za Takukuru na kwamba baadaye wataendelea kuwashughulikia wengine.