THE OTHER HALF
EPISODE 6
"…upo muda ambao ukiutazama ulimwengu, ukiitazama dunia na historia yake… unajiuliza kama tumejifunza kitu chochote kutokana na yaliyotokea.! Jambo la msingi na lenye ukweli zaidi, ni kwamba japo tunapita katika magumu yaleyale yanayofanana, lakini unapofikia muda wa kuondoka hapa duniani kila mtu anakufa peke yake. Kila mmoja anaondoka katika hali ya upweke…. Lakini…. Kama yuko mtu hata mmoja tu ambaye ana maana kubwa katika maisha yako, kama yuko mtu umewahi kumuinua, kama yuko mtu walau hata mmoja ambaye atakukumbuka kila siku baada ya wewe kuondoka.… huwezi kufa kamwe…. Hata utakapoondoka duniani…. Utaendelea kuishi milele…"
EPISODE 5
Ndani ya Anabelle 27 (uliokuwa mji wa Dar es Salaam)
Wote watano, Cindy, Salim, Kanali, Magdalena na Shafii walikuwa wamesimama wakiangalia vile vivuli vya watu vilivyokuwa kwenye zile nyumba ndani ya Anabelle.
Baridi lilikuwa ni kali kweli kweli, na giza lilikuwa nene haswa, hii ilifanya ule mwanga ndani ya zile nyumba kuonekana kwa uzuri zaidi na kuvifanya vivuli vya watu madirishani kuwa dhahiri kabisa.
Ule muungurumo wa sauti ya taratibu kama simba ulizidi kuwasogelea kadiri muda ulivyoenda.
"Cindy!" Salim akaita kwa sauti ya chini ya woga. "Cindy, tutapotezwa sasa hivi!"
"Ssssshhhh! Nyamaza.!" Cindy ananong'ona.
"Msisogee hata hatua moja.!"
Cindy akaongea huku akimvuta Magdalena pembeni, kwahiyo yeye na Magdalena wakawa wesimama kando kama hatua tano hivi pembeni ya Kanali, Shafii na Salim.
"Msisogee hata hatua moja" Cindy akawasisitiza tena Salim, Shafii na Kanali.
Ile sauti kama simba anayeunguruma taratibu ilizidi kusogea karibu. Ilifika karibu kiasi kwamba ilikuwa kama vile inatoka hatua tatu tu kutoka pale waliposimama akina Salim.
Walikuwa wanatetemeka kiasi kwamba jasho lilikuwa linakaribia kuwatoka licha ya baridi kali lililopo ndani ya Anabelle.
Walikuwa wanatamani kama vile mwanga utokee, giza liondoke waone hicho kinachounguruma karibu yao.
Muungurumo wa hicho kiumbe ulikuwa kama simba kabisa, lakini ulikuwa unatoka katika sauti fulani ya chini sana hali iliyofanya kuogofya zaidi maana ilikuwa kana kwamba kiumbe hicho kimekasirika kweli kweli na lilikuwa kinajitahidi kuzuia hasira zake.
Salim akakata jicho pembeni kumwangalia Cindy na Magdalena pale ambapo walikuwa wamesimama. Akagundua kwamba Magdalena alikuwa ameificha ile taa aliyoishika mkononi ambayo ilikuwa imegeuka rangi ya bluu. Alikuwa ameificha chupa ndani ya jaketi lake na haionekani.
Mawazo kadhaa yakapita ndani ya kichwa cha Salim. Cindy ana mpango gani? Kwanini ameficha ile chupa? Kwanini amejitenga pembeni yeye na Magdalena?
Ile sauti ya muungurumo sasa ilikuwa imefika miguuni mwao kabisa. Kwa jinsi ambavyo walikuwa na woga Mkuu ndani yao, walikuwa wanahofu hata kutazama chini. Lakini hata hivyo pia giza nene ambalo lilikuwa limetawala wasingeweza kuona pale chini walipokanyaga hata kama wangeliangalia.
Kanali, Salim na Shafii walikuwa wameganda kama masanamu.
Shafii kutokana na uoga kumzidia kuliko kiwango, akafanya kosa moja kubwa… akainamisha kichwa na kutazama chini.
Akakutana macho kwa macho na macho makali kama ya paka yanavyong'aa gizani.
Kiumbe huyo akaachia ule mlio wake wa kuunguruma aliokuwa anaubana muda wote, akaachia muungurumo huo mkali kama simba na kuruka kwa kasi ya ajabu kumvamia Shafii.
Muda huo huo kwa kasi kubwa pia ya ajabu, Cindi akatoa ile Chupa aliyoificha ndani ya koti na kumrushia yule kiumbe aliyekuwa amemrukia na kumvamia Shafii.
Chupa ile ilipotua kwa kiumbe huyo, ghafala akamuachai Shafii na kuanza kugala gala chini na kupaparika kama vile ana kifafa.
Cindy akakimbia na kuikota ile chupa na kuishika kwa kuining'iniza juu ya yule kiumbe.
Chupa bado ilikuwa inang'aa kwa rangi ya bluu kwa hiyo hii ilitoa mwanga hafifu uliowasaidia kumuona kwa uzuri yule kiumbe pale chini.
Umbo lake alikuwa ni binadamu kabisa… kama vile binadamu mwenye miaka 28 au 30.
Lakini binadamu huyu mwili wake wote ulikuwa na manyoya ya paka. Mwili mzima mpaka usoni na viganja vya mikono alikuwa amefunikwa kwa manyoya ya paka.
Macho yake pia yalikuwa ni ya bluu yenye kungaa kama alivyo paka. Lakini mwili wote alikuwa ni binadamu tena wa jinsia ya kiume.
Pale chini kiumbe huyu alipokuwa amelala na kugala gala huku Cindy bado akiwa ameishikilia ile chupa juu ya huyu kiumbe, taratibu alikuwa anaanza kuvimba kwa kutumumuka na ile hali ya kupaparika ikawa inapungua kana kwamba alikuwa anakaribia kukata roho.
"Shikilia hii chupa hivi hivi" Cindy akamkabidhi Chupa Magdalena ambaye aliishika vile vile juu ya yule kiumbe kama ambavyo Cindy alikuwa ameishika.
"Kanali naomba kisu" Cindy akaongea na Kanali.
Kanali alikuwa amemokodolea macho tu akionekana kama vile haelewi anachoambiwa.
Wote watatu, Kanali, Shafii na Kanali bado walikuwa wako kwenye bumbuwazi kutokana na kile kilichotokea pale.
"Kanali.!!" Cindy akaita kwa nguvu zaidi.
"Naam!" Kanali akashtuka kutokana kwenye bumbuwazi na msahangao.
"Nipe kisu!" Cindy akaongea.
Kanali akatoa kisu kichokuwa kwenye 'holder' kiunoni mwake kwenye mkanda wa kombati zake za kijeshi.
Cindi akapokea kile kisu, kisha akatoa kutoka ndani ya jaketi lake kikopo fulani chenye ukubwa wa kama robo lita. Alafu akapiga magoti na kutoboa yule kiumbe pale chini aliyekuwa ametutumka haswa mwili wake.
Akamtoboa na kuanza kukinga damu yake kwenye kikopo. Damu iliyokuwa inatoka kwa kiumbe huyu ilikuwa ni nyekundu lakini ni nyekundu iliyopauka sana kupitiliza.
Wenzake wote walikuwa bado wako kwenye mshangao mkubwa kwa hiyo walishindwa hata kuuliza swali ni nini kilikuwa kinaendelea hapo.
Kikopo kikajaa na Cindy akakifunga na kukirudisha kwenye mfuko wa jaketi lake.
"Cindy!" Salim hatimaye alitamka kutoka kwenye mshangao.
Cindy hakuitika, akainua tu kichwa kutazama Salim. Japokuwa walikuwa kwenye kiza totoro, lakini aliweza kuona 'kuchanganyikiwa' kwa Salim kuliko jionyesha dhahiri usoni mwake.
"Cindy! Nini kinaendelea hapa?" Salim aliongea huku anahema.
"Ulikiwa ni mtego?" Cindy akaongea huku kama anatabasamu kwa mbali.
"Mtego?? Na sisi ndio tulikuwa chambo wako?? Si ndio?" Salim akaongea kwa hasira huku bado sauti yake ikiwa na woga.
"Usikarike sana! Tumefanikiwa, si unaona?" Cindy akatabasamu huku anaonyesha kidole kwa yule kiumbe pale chini ambaye sasa alionekana hana uhai.
"Na hiki ni nini?" Salim akauliza akimnhooshea kidole yule kiumbe aliyelala chini.
"Sijui nimuiteje… labda nimuite mkazi wa Anabelle. Yes, huyu ni moja ya wakazi wa Anabelle.!" Cindy akaongea huku anatimia kisu kumkata ngozi yule kiumbe pale chini lakini katika namna ambayo kama vile anamchuna ngozi.
"Unataka kusema watu wote karibia milioni nne walishindwa kutoka ndani ya dar ndio wamegeuka kuwa namna hii?" Kanali akauliza kwa mshangao.
"Hapana… well, labda walau mimi nadhani hapana.!"
"Unaaana gani? Huyu ametoka wapi sasa?" Kanali akauliza tena.
"Huyu ni moja kati ya wale watoto elfu waliozaliwa kimazingira nchini Maldives mwaka Juzi 2036! Mnakumbuka ile stori niliwaambia jinsi hii chupa ilivyolkotwa na wavuvi na kisha watoto wachanga kuzaliwa wakiwa na manyoya ya paka na baadae kupotea? Sasa huyu naamini ni moja wapo wa watoto wale!" Cindy akaongea huku anaendelea kumchuna ngozi yule kiumbe pale chini.
Akina Salim wote wakajikuta wamegonganisha macho kwa kuangaliana kwa mshangao.
"Amefikaje Tanzania huyu kiumbe?" Salim akauliza.
"Hilo ndilo swala ambalo limenifanya nijitoe muhanga kuingia humu… kama wewe pia na mimi nahitaji kifahami wamewezaje kufika hapa Tanzania… na si hapa tu Tanzania… kila sehemu ambayo mji unatwaliwa naamini lazima kuna hawa viumbe… na najiuliza wanawezaje kuenea duniani kote kutokea Maldives!" Cindy akaongea huku bado anamchuna ngozi yule kiumbe.
"Kabla hujaongea maneno mengine ya kutuchanganya zaidi… kwa hiyo watu wote ambao walibaki kwenye Anabelle wako wapi?" Shafii akauliza.
"Hitaji lao kuu la kwanza ni wanaume… ndio maana nilipomsikia anaunguruma mimi na Maw tukajitenga pembeni.!"
"Wanataka nini kwa wanaume?" Salim akauliza.
"Mji ukishatwaliwa na kuwa Anabelle waliobaki ndani yake wanagawanywa sehemu mbili… sehemu moja wanaume na nyingine wanawake… wanaume wanapelekwa mahali… sehemu maalumu… naomba niite hii sehemu zizini… kwa hiyo wanapelekwa zizini kwa ajili ya shughuli maalumu!"
"Shughuli gani?" Salim akauliza tena.
"Wanakamuliwa damu mpaka wanakufa… nadhani umeona damu ya hawa viumbe ilivyo! Haina haemoglobin ya kutosha… kwa hiyo wanahitaji kunywa damu ili kupata haemoglobin katika damu yao waendelee kuishi.!" Cindy akaacha kidogo kumchuna ngozi yule kiumbe na kuwaangalia akina Salim, akijua fika kabisa Salim anataka kuuliza swali gani.
"Kabla haujanijibu unafahamu vipi yote haya, naomba unieleze kuhusu wanawake… umesema watu wanaobakia kwenye Anabelle wanagawanywa sehemu mbili, wanawake na wanaume… wanaume umesema wanakamuliwa damu mpaka kufa… wanawake ni nini kinawakuta??" Salim akauliza kwa uchungu akiwambuka mkewe Khadija na mtoto wake Basrat.
"Wanawake wanaishi… wanapelekwa kwenye zizi lingine! Na huko kazi yao ni kuzalishwa kila baada ya miezi sita… wanazalishwa viumbe vinavyofanana na hiki… wanazalishwa maisha yao yote mpaka watakapofariki.!"
Cindy akajibu na kisha kuinama chini kuendelea kumchuna ngozi yule kiumbe.
Wenzake wote walishikwa na bumbuwazi. Walitamani kuongea kitu lakini maneno yalikuwa hayatoki.
"Unayajuaje yote haya?" Salim akauliza kwa uchungu huku chozi linatiririka shavuni mwake.
Cindy akainua kichwa na kuwatazama.
ITAENDELEA JUMANNE..