THE OTHER HALF
EPISODE 7
"Wengi wanaamini binadamu aliumbwa na Mungu au kiumbe kingine chenye nguvu na uwezo zaidi. Wengine wanaamini kwamba binadamu ni zao la mabadiliko ya viumbe vya kale na dunia. Vyovyote, kama tuliumbwa au tilitokea tu, kitu kikubwa zaidi ambacho kiliwekwa ndani yetu ni uhuru wa kuamua, free will.! Uwezo wako wewe binafsi kuamua kufanya utakacho na kuamua muelekeo wa maisha yako. Zawadi hii tuliyopewa licha ya kuwa adhimu, lakini pia inabeba mzigo wa jukumu linalowatesa binadamu tangu kuwepo kwa ulimwengu. Uhuru wetu wa kufanya maamuzi unaweza kutupeleka katika kuikuza mbari ya binadamu au kuipoteza kabisa. Mzigo huu pia wa jukumu unagusa mtu mmoja mmoja. Ni mara ngapi ambapo nafsini mwako, uamuzi unaotaka kufanya ni kukimbia hali iliyopo lakini moyoni unafahamu inatakiwa ubaki na kupambana? Ni mara ngapi ambapo nafsini mwako uamuzi unaotaka kufanya ni kuishi katika mstari mnyoofu lakini moyoni mwako unajua kabisa unapaswa kuvunja kanuni ili upate unachokitaka??
Uhuru wa kufanya uamuzi, free will ni Zawadi kubwa zaidi iliyowekwa ndani mwetu lakini ni mzigo mkubwa zaidi wa uwajibikaji binafsi ndani yetu na mara nyingi umekuwa ni kikwazo pale tunapotaka kusonga mbele au kupambana kutetea tunachokiamini. Mbaya zaidi ni pale tunapopambana na viumbe walio tofauti na sisi, viumbe ambao hawana hisia zetu.…. Binadamu tunajivunia ubora wa hisia, hii ni moja ya vitu ambavyo vinafanya haijalishi kutakuwa na maendeleo kiasi gani ya teknolojia, lakini kamwe roboti hawezi kufafanana na binadamu. Kwa sababu huwezi kutengeneza hisia. Hisia ni kitu tunazaliwa nacho, hakifundishwi. Hisia zote, mbaya na nzuri, hisia zote kuanzia urafiki, huruma mpaka ukatili. Ni binadamu pekee anazaliwa nazo. Lakini hisia nayo ni Zawadi na papo hapo ni kikwazo kwetu kufika tunapotaka.
Sasa je, itakuwaje pale ambapo binadamu atatakiwa kupambana na kiumbe chenye ubora kama walionao binadamu, lakini wenyewe ni bora zaidi kwa kuwa hawana hisia. Hisia pekee waliyonayo ndani yao ni Kiu ya kutaka kuishi, yaani survival.!
Binadamu, anawezaje kushinda vita pale anapotakiwa kushindana na viumbe wa ajabu, watotot wa Anabelle 1 (Maldives), waliozaliwa mwaka 1936.? Binadamu anawezaje kutetea haki yake ya kuendelea kuishi juu ya uso wa Dunia??
NDANI YA ANABELLE 27 (ULIPOKUWA MJI WA DAR ES SALAAM)
Dr. Cindy Wheaton alikuwa amemaliza kumchuna ngozi yule kiumbe pale chini na sasa alikuwa amesimama anawaangalia wenzake huku mkononi ameshikilia ngozi ya binadamu yenye manyoya mengi kama paka.
"Hii ngozi ya nini?" Kanali akauliza kwa mshangao.
"No no! Kabla hajajibu hii ngozi ya nini ni vyema kwanza atuambie anajuaje mambo mengi hivi kuhusu Anabelle na vilivyomo ndani yake?" Salim akadakia kabla Cindy hajajibu swali la Kanali.
"Salim! Huo sio muda sahihi wa kuanza kupeana mihadhara, mimi ni mtaalamu wa akiolojia kwahiyo si ajabu kujua vitu vingi." Cindy akajibu akiwa anaikunja ile ngozi bila kumuangalia Salim.
"Sikiliza Cindy… mke wangu na mtoto wangu wako humu ndani na watu wengine zaidi ya milioni nne... Mpaka sasa sijui ninachokifanya humu na nahitaji kujua unafahamu vipi taarifa zote hizi kuhusu Anabelle.?" Salim akauliza kwa hasira safari hii.
Cindy akavuta pumzi kubwa ndani na kuishusha.
"OK! Mnafahamu hili jina la Anabelle limetokea wapi?" Cindy akawauliza huku anawaangalia wenzake mmoja mmoja.
Wote wakaangaliana huku wanatikisa vichwa.
"Nadhani ndivyo zinavyoitwa… ndivyo ambavyo imezoeleka na kuripotiwa hivyo kwenye vyombo vya habari kwamba " mji fulani umegeuzwa kuwa Anabelle " Magdalena akjibu.
"Nadhani mmewahi kusikia simulizi kuhusu Pandora, si ndivyo?" Cindy akawauliza.
Wote wakaangaliana na kisha kutingisha vichwa.
Cindy akaanza kuwasimulia simulizi kuhusu Pandora kama ambavyo Mzee Caleb aliwasimulia makamu wa Rais wa Marekani David Logan na timu yake kwenye situation room. Akawaeleza kila kitu kuhusu namna ambavyo mungu wa kigiriki, Zeus alivyomuumba mwanamke wa kwanza Pandora na kumpa sanduku lenye chupa zilizojazwa udhalimu wa ulimwengu na kumpa sharti la kutofungua sanduku hilo.
Lakini hakuwaeleza chochote kuhusu mchoro wa George Washington kuhusika na sanduku hilo kwa kuwa hata yeye Cindy alikuwa haijui siri hiyo.
"Sasa! Hii simulizi ya kale inatuambia kuwa mwanamke huyu wa kwanza Pandora aliwekwa kwenye mji wa kale unaoitwa Anabelle zaidi ya miaka elfu kumi iliyopita… ndipo hapa baada ya haya matukio ya miji kutwaliwa kuanza na tulipong'amua matukio haya kuhusiana na chupa za kwenye sanduku la Pandora… tukaibatiza jina la Anabelle miji hii inayotwaliwa.!"
Cindy akanyamaza kidogo kumeza mate. Kisha akaendelea.
"Sasa huu mji wa kufikirika wa Anabelle ambao Pandora aliwekwa na Mungu Zeus, ulikuwa na visa vinavyofanana kabisa na haya yanayotokea sasa duniani… watu kupotea, wanawake kuzalishwa viumbe vya ajabu na kadhalika… kwa hiyo baada ya kutafiti sana kinachoendelea duniani kwa sasa… najaribu kuoanisha na kilichotokea kwenye Anabelle halisi ambayo Pandora aliwekwa na Mungu Zeus… na ninachoamini ni kwamba hawa viumbe wanataka kuibadili dunia nzima kuwa kama mji wa dhahania wa Anabelle ambao Mungu Zeus alimuweka Pandora baada ya kumuumba…. kwa hiyo kujibu swali lako Salim, hivyo ndivyo namna gani najua yote haya.!"
Cindy akamaliza kujieleza. Wote walikuwa wako kimya wanamuangalia tu.
Giza bado lilikuwa kama ndio linazidi kuongezeka pale walipo. Bado kwenye madirisha ndani ya nyumba kulikuwa kuna mwanga mkali kana kwamba chemli au moto umewashwa ndani. Lakini ajabu ni kwamba vile vivuli vya watu madirishani havikuwepo tena.
Cindy alikuwa amemaliza kuikunja ile ngozi ya yule kiumbe waliyemuua. Alikuwa ameikunja ngozi kama nguo na kumpa kanali aishike. Kisha akachukua ile chupa kutoka kwa Magdalena.
"Tuna Masaa machache sana mbele yetu tunatakiwa tufike katikati ya mji.!" Cindy akaongea huku anaanza kutembea kuondoka pale waliposimama.
"Tunaenda kufanya nini katikati ya mji?" Akauliza Salim.
Cindy hakujibu papo hapo. Akanyamaza kama anatafakari jambo fulani hivi namna gani amjibu Salim.
"Umemuona huyo kiumbe tuliyemuua?" Cindy akamuuliza Salim huku wanatembea kuelekea mbele.
Walikuwa wanatembea taratibu sana kwa tahadhari kubwa huku Cindy ameshikilia chupa mkononi na kuiweka mbele kama ameshika tochi.
"Nimemuona!" Salim akajibu kwa kukereka na swali hili. Kwanini amuulize kama amemuona wakati walikuwa wote tukio likiwa linatokea.
"Kama angekuwa binadamu wa kawaida unamkadiria angekuwa na miaka mingapi?" Cindy akamuuliza.
"Kwenye 28 hadi 30 hivi" Salim akajibu.
"Unakumbuka nimewaambia kuwa hawa ni watoto waliozaliwa nchini Maldives, kabla haijageuzwa kuwa Anabelle.?"
"Ongea point yako Cindy, tunakumbuka yote hayo!" Salim akang'aka huku akijitahidi sauti yake isitoke kwa nguvu.
"Nadhani kuna jambo la msingi hamlioni hapa… mnakumbuka hawa watoto walizaliwa mwaka gani kule Maldives?" Cindy akawauliza kwa msisitizo mkubwa akiata waone kile anachokitaka.
"Mungu wangu!!!" Magdalena akadakia, "walizaliwa mwaka 2036, kwa hiyo mpaka sasa walitakiwa kuwa na miaka miwili tu!" Magdalena akaongea kwa mshangao na hofu.
"Miaka miwili???" Shafii ambaye alikuwa kimya muda wote akahamaki "haya madude yanaonekana mababa mazima mnasema yana miaka miwili??"
Ikabidi wenzake watoe kicheko cha chini chini baada ya shafii kuhamaki kuwa vile viumbe ni "mababa mazima"!
" kuna jambo la muhimu sana ambalo nataka mlifahamu kuhusu Anabelle!" Cindy akaongea serious baada ya vicheko kuisha.
"Muda ndani ya Anabelle haufuati kanuni kama muda nje kwenye ulimwengu!"
"Una maanisha nini?" Kanali akauliza.
"Nadhani anamaanisha muda ndani ya Anabelle unaenda kwa kasi zaidi tofauti na muda nje huko ulomwenguni.!" Salim akajibu akiwa serious pia.
"Uko sahihi kabisa" Cindy akaongea, "muda ndani ya Anabelle unaenda kasi zaidi tofauti na ulimwenguni… ndio maana unaona hawa viumbe wana miaka miwili pekee lakini wanaonekana ni watu wazima kabisa wa miaka 30!! Na hii ndio sababu kwanini mji ukishatwaliwa unaonekana umechakaa kana kwamba haujawahi kukaliwa na watu kwa karne kadhaa.. Yote hii ni athari ya muda... Unakuwa unaenda kasi zaidi ndani ya Anabelle tofauti na duniani.!"
Cindy aliongea huku amegeuka kuwatazama wenzake. Wote walikuwa wamesimama wanamuangalia.
"Kwa hiyo basi... Unataka kusema kwamba huu muda ambao tumekaa humu ambao nakadiria ni kama masaa mawili pekee inawezekana kabisa tumekuwa humu kwa muda zaidi ya huo?" Kanali akauliza.
"Kabisa… hilo sio swali… hiyo ndiyo hali halisi… sisi tunahisi timekuwa humu kwa muda mchache lakini labda mwasaa mawili… lakini uhalisia ni kwamba… muda humu upo kasi zaidi kwahiyo inawezekana pengine tuko humu kwa wiki kadhaa tayari.!" Cindy aliongea huku ametoa tabasamu la huzuni.
"Umesema kwamba ni muhimu tufahamu hili? Unaweza kuwa mahususi zaidi kutueleza kwanini tunapaswa kuzingatia tofauti ya kasi ya muda tukiwa humu ndani?" Salim akaukiza.
"Nadhani anamaanisha kuwa tutazeeka haraka!" Shafii akatoa jibu la kijinga tena.
Kutokana na msongo waliokuwa nao kutokana na taarifa hii hata vicheko havikuwatoka.
"Ni bora hata tungekuwa tunazeeka haraka pekee.. Lakini ubaya ni kwamba ubongo wetu unaweza kuchanganyikiwa katika kung'amua uhalisia wa muda kiasi kwamba unaweza kupata shinikizo na kitu kibaya zaidi kikatokea.!" Cindy akajibu huku anageuka na kuanza kutembea.
Na wenzake nao wakamfuata.
"Kitu kibaya?? Kama kipi?" Kanali akauliza.
Magdalena akadakia na kujibu.
"Kanali, nadhani wote tunafahamu kuwa muda ni tofauti, yaani interval baina ya matukio mawili… na ubongo wetu una uwezo wa kuhisi hii interval na pia hii inaathiri fiziolojia ya mwili na mfumo… kwa kuwa tumezaliwa kwenye Dunia ya kawaida ubongo wetu tayari umeweka namna ambayo unahisi interval hizi na kuoanisha na fiziolljia na mabadilikk ya mfumo wa mwili… kwahiyo tukiwa humu kwa kuwa muda unaenda kasi zaidi maana yake pia kutakuwa na mabadiliko ya kimwili ya kasi zaidi, mfano kuzeeka… lakini ubongo wetu haujawahi kuhisi interval za humu kwa kuwa hatunazaliwa humu… hii unaweza kusababisha ubongo kupata msongo na shinikizo kwa kutumia oksojeni nyingi zaidi na glucose nyingi zaidi ili kuhimili hali hii mpya ya intervals na mabadiliko ya fiziolojia… sasa hii ndio itatuletea balaaa… ubongo unaweza kufeli muda wowote.!"
Magdalena akaawaeleza wenzake kitaalamu kabisa na kwa umahiri wa hali ya juu. Cindy akaitikia kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubali maelezo aliyoyatoa.
“kwa hiyo tunatakiwa tufanye tulichokuja kukifanya haraka sana.” Cindy akaongea huku anazidi kutembea kwa haraka wenzake wakimfuata.
“na haujatuambia mpaka sasa ni nini hasa tunatakiwa kukifanya humu?” Salim akauliza.
“kitu cha kwanza kabisa tunatakiwa kutafuta mlango wa kikundi cha cha watu wanaojiita The 46.!” Cindy akaongea kwa kifupi.
“ndio kina nani hao?” Salim akauliza kwa shauku.
INAENDELEA POST INAYOFUATA…