THE OTHER HALF
EPISODE 5
"…kila tendo ambalo tunalifanya, linatuma mawimbi ya mwitikio katika Dunia. Haijalishi tendo hili tunalolifanya ni dogo kwa kiasi gani. Pia kila neno tunalotamka lina uwezo wa kuleta athari chanya ama hasi kwa wale wanaotuzunguka. Kwa mujibu wa tafiti za saikolojia zinasema kwamba, leo hii mwanaume wa kawaida ataongea si chini ya maneno elfu saba kwa siku na mwanamke ataongea si chini ya maneno elfu ishirini. Lakini ni neno moja tu, au sentesi moja tu ina uwezo wa kubadili mwelekeo wa Dunia.!"
Maeneo fulani nchini Tanzania karibu na palipokuwa na mji wa Dar es Salaam
Timi ya wataalamu iliyokuwa inaongozwa na Salim, pamoja na kikosi maalumu cha jeshi walikuwa wamesafiri zaidi ya masaa kumi kutoka katika wilaya ya Ruangwa mpaka kufika Morogoro na baadae kuelekea maeneo karibu kabisa na Chalinze.
Kuanzia Morogoro walikopita mpaka hapa Chalinze, idadi ya watu ilikuwa ni kubwa kweli kweli na mvurugano ulikuwa mkubwa sana. Kulikuwa na purukushani nyingi sana kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wamekimbia mji wa Dar baada ya kutolewa taarifa ya mji huo kuonyesha dalili kuwa unaelekea kutwaliwa.
Mji mzima wa Morogoro na vitongoji vyake ulokiwa umetawaliwa na purukushani na msongamano wa watu kama vile sokoni. Kelele zilitapakaa kwenye anga lote, kila kona watu walikuwa wanahaha na mabegi ya nguo na vyombo vya majumbani. Taharuki ilikuwa ni kubwa mno, kila kona unayotazama watu walikuwa wanakimbia au kutembea kwa haraka kuelekea mbali wawezavyo na mji wa Dar.
Salim na timu ya wataalamu wenzake walikuwa wameendesha magari moja kwa moja kuelekea karibu na Chalinze ambako kulikuwa na kituo maalumu kilichokuwa kinaandikisha watu walikuwa wamefanikiwa kutoka ndani ya jiji la Dar kukimbilia Morogoro. Mpaka muda huu ambao ulikuwa unapata saa kumi na moja jioni tayari jiji la Dar lilikuwa limeshatwaliwa na kufanywa Anabelle 27. Pia Ruangwa nayo waliyokuwa wameikimbia masaa machache yaliyopita tayari nayo ilikuwa imegeuzwa Anabelle 29. Kulikuwa na mji mwingine nchini Nigeria nao ulikuwa umegeuzwa kuwa Anabelle 28.
Lengo la Salim na wenzake kuja mpaka huku Chalinze kwenye kituo cha kuandikisha waliofanikiwa kukimbia Dar kabla ya kutwaliwa ni ili waweze kujua idadi ya watu waliobakia ndani ya Dar, lakini kwa Salim yeye hasa alikuja hapa ili kujua kama familia yake, mkewe kipenzi Khadija na roho yake, binti yake kipenzi Basrat walifanikiwa kukimbia Dar kabla haijatwaliwa.
Kituo chenyewe ambacho kilikuwa kinaandikisha watu, kilikuwa kimewekwa kwenye jengo fulani hivi la muda lililotengenezwa kwa mahema ya kijeshi. Alafu barabarani ukawekwa uzio wa geti dogo la mlingoti wa chuma ambao ulikuwa unafunguka kwenda juu na chini ili kuruhusu watu kupita.
Uandikishaji uliokuwa unafanyika haukuwa na kuandikisha kwenye daftari. Teknolojia ilikuwa imekua haswa mwaka huu 2038, watu walikuwa wanaandikishwa kwa mfumo wa teknohama ya kibaiolojia.
Yaani kulikuwa na wanajeshi pale kwenye kituo cha uandishaji waliobeba vifaa fulani hivi vyenye umbo kama linalokaribia kufanana na bastola lakini kifaa chenyewe kina vikolombwezo vingi zaidi. Kifaa hiki walikiita B-punch (au B-gun).
Chenyewe kilifanya kazi katika mtindo ambao mtu anayepita anampa mkono afisa wa jeshi mwenye kifaa hiki, kisha afisa huyo anaelekeza mdogo wa kifaa kama sindano hivi kwenye mkono wa muhusika kisha anamchoma kumpandikizia kidude kidogo kinaitwa MMA B-Chip (Miniaturized Microarrays Biological Chip).
Kitu hiki (MMA B-chip) ambacho kinapandikizwa kwa muhusika ni kidogo mno labda chenye ukubwa wa punje mbili za mchanga. Lakini kifaa hiki kinasoma taarifa za kiafya na 'identity' ya muhusika na kutuma taarifa hizo kwenye system ya taarifa za serikali.
Zoezi hili la kupandikiza kidude hiki linadumu kwa kama sekunde tano tu, kwa hiyo kwa dakika moja afisa wa jeshi anaweza kuandikisha zaidi ya watu ishirini kwa mfumo huu.
Baada ya Salim na wenzake kufika eneo hili walipaki magari yao mahali fulani karibu na kituo hiki na kisha Salim na Kanali wa kile kikosi cha kijeshi kinacjowalinda wakaongozana kuelekea kile kituo kilipo.
Wakaelekea moja kwa moja mpaka kwenye upande wa ofisi za kituo hiki cha uandikishaji na walipofika kanali akaomba aelekezwe aonane na afisa Mkuu wa kijeshi aliyepo kituoni hapo kama kiongozi wa hawa wanajeshi wote wanaoandikisha watu.
Wakapelekwa moja kwa moja kwenye hema fulani kubwa lililojitenga pambeni na kuingia ndani. Humu palikuwa pameangiliwa kama ofisi ya kabisa na kulikuwa na afisa wa kijeshi Brigedia Jenerali Samson Mwambusi ambaye alikuwa anaongoza zoezi hili la kijeshi kuandikisha raia waliofanikiwa kuondoka ndani ya jiji LA Dar es Salaam.
Baada ya kuingia ndani ya hema lake hili LA ofisi na kupeana salamu zao za kijeshi na kisha kuketi wakaanza mazungumzo.
"Mkuu mimi ni Kanali Robert Shamte, kiongozi wa Team 5C inayowalinda wataalamu wanaofanya tafiti katika maeneo yaliyotwaliwa… huyu mwenzangu anaitwa Salim Kawambwa ni kutoka Idara ya Usalama wa Taifa na ndiye kiongozi wa timu hiyo ya wataalamu.!"
Kanali akajitambulisha na kumtambulisha Salim.
"Nafahamu taarifa zenu kanali, tena kuna maagizo yenu hapa.!" Meja Mwambusi akaongea.
"Maagizo gani mkuu?" Kanali akauliza.
"Naomba niwasikilize kwanza nyinyi.!" Meja akajibu.
"Mkuu, sisi tulikuwa na masuala machache tu kwanza kama hutojali utupe mihtasari wa zoezi zima la evacuation.!" Salim akauliza.
"Mpaka sasa ni watu milioni tatu pekee ndio tunahakika wametoka ndani ya Dar es Salaam kabla haijatwaliwa… hii ina maana kwamba watu milioni nne waliosalia wamepotea ndani ya jiji baada ta kutwaliwa… pia nusu ya baraza la mawaziri nao wamepotea ndani ya mji… kabla jiji halijatwaliwa tulifanikiwa kumuondoa Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na nusu ya baraza la mawaziri… wamehifadhiwa Kwenye kambi ya jeshi hapo Kizuka, Ngerengere.."
Meja akawaeleza kwa ufupi. Ukapita ukimya kama wa dakika mbili hivi.
"Nilikuwa na ombi kidogo Meja.!" Salim akaongea kwa unyonge.
"Ndio?"
"Naona uwaambie vijana wako waangalie kwenye orodha ya watu waliofanikiwa kutoka kwenye jiji… waangalie kama kuna Khadija Kawambwa na Basrat Kawambwa..!" Salim akaongea kwa huzuni.
"Ni familia yako hii?" Meja akauliza.
"Ndio mkuu.!"
Kisha Meja akanyanyua simu ya upepo iliyopo pale mezani na kuanza kumpa maagizo afisa anayehusika na kumbukumbu kuangalia taafifa hizo za hayo majina.
Akasubiri kwenye simu kama dakika Tatu hivi kisha akaiweka chini.
"Salim! Pole sana... Hatuna hayo majina kwenye orodha… kuna uwezekano hawakufanikiwa kutoka ndani ya jiji kabla ya kutwaliwa.!" Meja akaongea kwa sauti ya huzuni.
Salim hakujibu chochote. Akajiinamia tu chini kwa uchungu.
"Mkuu umeeleza pia kuna maagizo yetu hapa!" Kanali akahamisha maongezi na kukumbushia suala aliloongea Meja mwanzoni mwa Mazungumzo yao.
"Ndio! Kuna maagizo yenu hapa… ni kuhusu Dr. Cindy Wheaton.!" Meja akaongea.
Wote wakamuangalia kwa mshtuko. Hata Salim aliyekuwa amejiinamia akainua uso.
"Amefanyaje?" Salim akauliza huku bado akiwa na sauti ya huzuni kama analia.
"Kuna taarifa kutoka nchini kwake Marekani, kuna ndege ya kijeshi inakuja kumchukua ndani ya masaa machache yajayo.. Tunatakiwa kumsafirisha muda huu mpaka uwanja wa ndege wa kijeshi Morogoro..!"
Meja akaongea kwa udadisi kuona akina Salim watasemaje.
"Wamewaeleza kwanini wanataka kumrudisha haraka hivyo?" Salim akauliza.
"Hapana hawajasema… ndio maana bosi wako wa Mkurugenzi wa Usalama anahitaji uhakikishe kabla hajaondoka ufahamu kwanini wanataka kumrudisha kwa haraka namna hiyo!"
Kuna hisia Fulani mbaya na hasira Salim akaanza kuzipata. Akajikita anainuka kutoka kwenye kiti na kuanza kutoka nje kwa hasira.
Hasira hizi zilikuwa zinampanda baada ya kukumbuka kauli ya Magdalena walipokuwa wanatoka Ruangwa, "nahisi kuna kitu Cindy anakijua ila anatuficha."
Hasira zilimpanda zaidi akifikiria kuwa familia yake, kitu pekee chanye thamani kubwa kwenye maisha yake, mkewe Khadija na mtoto wake Basrat wamebaki na kupotea ndani ya Dar baada ya kutwaliwa, lakini kuna mwenzao inawezekana anaijua siri fulani na hataki kuwaambia na sasa nchi hake wanataka kumrudisha kwao kwa dharura kiasi hiki.
Hasira zilimpanda haswa.
"Yuko wapi?" Salim akauliza kwa hasira mara tu baada ya yeye na kanali kurejea pale walipopaki magari na kuwaacha wenzao wengine.
"Nani?" Magdalena akamuuliza.
"Cindy! Yuko wapi?" Akauliza tena kwa hasira huku anatetemeka.
"Oooohh no!! Nini kinaendelea tena? Umepata taarifa kuhusu Khadija na Basrat?" Magdalena akauliza swali lingine baada ya kujibu swali.
"Nimeuliza Cindy yuko wapi?" Salim akauliza kwa sauti kubwa ya hasira.
"Amechukua gari moja ameelekea Dar?" Magdalena akajibu kwa uoga.
"Mnasemaje? Ameenda dar?? Mmemruhusu vipi? Haumjui kuwa dar imeshageuzwa kuwa Anabelle?? Huyu Cindy amechanganyikiwa?" Salim akaongea kwa kufoka huku anampa ishara Kanali wapande kwenye gari.
Wote wakapanda kwenye magari na kwa kasi wakaanza kuelekea barabara inayoenda Dar es salaam kumuwahi Cindy wajue mpango wake kabla hajafanya kitu cha ajabu na kisha wamkamate kumpeleka Morogoro na ambako ndege ya jeshi la Marekani ilikuwa inakuja kumchukua.
"Vipi kuhusu Khadija na Basrat?" Magdalena akamuuliza Salim kwa Upole wakiwa wanakaribia kabisa kupiga Mlandizi.
"Hawakufanikiwa kutoka!" Salim akajibu kwa mkato akiwa serious kuzuia hisia zake asilie mbele za watu.
Magdalena akashindwa kusema chochote kumfariji, akamuwekea tu mkono begani na kumpapasa kwa ukarimu wa kumfariji.
Ukaribu ambao Magdalena aliujenga kwa Salim na jinsi alivyokuwa anamjali, ilitoa hisia kwa wengine labda Magdalena ana hisia fulani za kimapenzi kwa Salim. Alikuwa anamjali kupitiliza kuzidi namna ambavyo rafiki anapaswa kumjali rafiki yake.
Dakika kumi na tano baadae walikuwa wamepita Kibaha maili moja, na kwa mbali wakaanza kuiona gari ambayo Cindy aliitumia kuondoka nayo.
Wakaendesha mpaka pale ambapo gari ya Cindy ilikuwa imepaki. Wakashuka wote.
"Cindy! Unafanya nini hapa?" Salim akaongea kwa hasira kuelekea aliposimama Cindy.
"Nataka kuingia ndani ya Anabelle!" Cindy akajibu bila kumuangalia Salim.
Akikuwa anafunga zipu ya jaketi zito alilokuwa wamemkuta analivaa.
"Umechanganyikiwa au? Unajua kuwa ukiingia humo ndio umepotea na hautotoka kamwe?" Salim akafoka.
"Najua!" Cindy akajibu kwa ufupi.
"Cindy ni vyema utueleze kilichomo kichwani mwako ambacho hatukijui?"
"Nadhani nimefahamu masuala machache ya msingi kuhusu Anabelle namna gani ya kuingia na kutoka ukiwa hai... Sina hakika na ninachokiwaza lakini nataka kujaribu.!" Cindy akaongea akiwa emaliza kufunga zipu ya jaketi na kiwaangalia.
"Umegundua nini?" Salim akauliza kwa shauku.
"Siwezi kukuambia labda ukiongozana na mimi kuingia!"
"Siwezi kufanya ujinga wa kiasi hicho!" Salim akafoka.
"Salim nikuulize kitu? Mke wako na mwanao walifanikiwa kutoka?"
"Hapana!" Salim akajibu kwa uchungu.
"Hiyo inamaana kwamba wako mle ndani… unaweza ukajaribu kuwasaidia au unaweza kuendelea kuwa muoga kama kunguru!" Cindy akaongea huku anaonyesha kidole kuelekea muelekea ulipo jiji la Dar, Anabelle mpya kutwaliwa.
Mita chache kutoka waliposimama kulikuwa na ufa ardhini ulioashiria mpaka wa Anabelle na ulimwengu.
"Cindy Siwezi kukuruhusu uingie humo… nina amari ya kukurejesha Morogoro ili upelekwe kwenu Marekani.!" Kanali akaingilia maongezi.
Cindy akainama chini kwenye mkoba wake wa mgongoni na kutoa Chupa. Chupa ile ambayo aliichukua kutoka Chuo Kikuu cha Stanford.
"Hiki ndicho wanachohitaji… hii chupa! Kanali unaweza kunipiga risasi, lakini Siwezi kurudi wala kukukabidhi hii chupa… naingia sasa ndani ya Anabelle, Salim nadhani ni vyema ukiongozana nami… nadhani nafahamu ni namna gani tunaweza kutoka Salama… sina uhakika… lakini ni vyema kujaribu kuelewa kinachoendelea ndani ya hizi Anabelle baada ya saa kumi kupita kuliko kukaa tu na kushuhudia ulimwengu mzima unateketea kwa kutwaliwa mbele ya macho yetu…"
Cindy akaongea huku anageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye ule Ufa ardhini kutenganisha Anabelle na ulimwengu.
"Shit!" Salimu akaongea kwa hasira na kuanza kutembea kumfuata Cindy.
"Salim unafanya nini?" Magdalena akahamaki na kumshika mkono.
"Magdalena, familia yangu iko humo ndani… kama kuna lolote naweza kufanya kuwaokoa niko tayari hata kama inahatarisha maisha yangu.!"
"Na mimi nakuja!" Magdalena akaongea kwa hofu karibu machozi yadondoke.
"Hakuna ulazima wa wewe kuja Magdalena!"
"Salim! Kama unaingia humo kwenye Anabelle na mimi nakuja… na huwezi kunizuia! Nakuja" Magdalena akaongea kwa hisia huku anahema kwa hofu.
"Yeyote anayekuja achukue jaketi zito la Baridi!" Cindy akaongea akiwa amesimama pembeni mwa ufa pale ardhini.
Magdalena na Salim wakafungua milango ya gari na kuchukua majaketi mazito ya baridi.
Wakashangaa kumuona kanali na Shafii yule mtaalamu wa Vinasaba nao wanachukua majaketi.
Salim hakuongea chochote. Akatikisa kichwa tu.
Wote wanne wakatembea mpaka pale Cindy aliposimama.
Aliyebaki alikuwa ni Goodluck, yule afisa polisi na wanajeshi wengine waliosalia wa Team 5C.
"Wakuu, sisi tunaingia ndani ya Anabelle… mkiona siku zinapita na tuko kimya nadhani nadhani mnafahamu nini ambacho kitakuwa kimetupata… tuombeeni kheri! Kwaherini.!"
Kanali akaongea na Goodluck na wanajeshi amabo walikuwa wanabakia.
Hii ilikuwa tayari inakaribia kabisa majira ya saa moja jioni. Muda huu ulimaanisha kwamba "wakazi" wa Anabelle watakuwa wameshaamka... Kwasababu muda Salama wa kuingia ndani ya Anabelle kwa binadamu ni saa kumi jioni.
Kwahiyo, majira haya ya saa moja jioni, Cindy, Salim, Magdalena, Shafii na Kanali walivuka ule ufa wa mpaka ardhini na kuingia ndani ya Anabelle.
Walitembea kwa takribani nusu saa nzima mpaka wakaanza kufika mwanzoni mwa mitaa na majumba ya hii Anabelle ambayo masaa machache yaliyopota ilikuwa ni jiji la Dar Es salaam.
Kadiri walivyokuwa wanaingia ndani ya Anabelle ndivyo ambavyo baridi lilikuwa linaobgezeka.
Majengo yote yalikuwa makuu kuu kama vile ni mji uliotelekezwa karne nyingi zilizopita. Giza lilikuwa ni kubwa mno kiasi kwamba walikuwa hawaoni hata barabara wanayokanyaga. Pia ukimya nao ulikuwa ni mkubwa na wa kutisha.
Nyumba zilikuwa na mwanga fulani madirishani kana kwamba ndani kuna taa za chemli au moto umewashwa.
Pia kadiri walivyokuwa wanaenda ndani ndani mwa mitaa ya Anabelle, ndivyo ambavyo chupa yenye karatasi ambayo Cindy aliishika mkononi ilikuwa inabadilika na kuwa rangi ya blue iliyoiva sana.
Ghafla ule ublue wa chupa ukakolea zaidi na moshi ukaanza kutoka kwenye chupa.
Katika zile ngumba kuu kuu za mitaa ya Anabelle, madirishani vikaanza kuonekana kwamba vivuli vya watu na sauti kama simba wengi wanaunguruma taratibu kwa sauti ya chini.
Cindy, Salim na wenzao wakasimama ghafla kwa woga wakitazama huku na huo sauti zile za muungurumo zinapotokea.
"Cindy, nadhani huu ndio muda sasa utueleze hizo siri zako kabla hivyo viumbe vinavyo unguruma havijatufikia.!"
Magdalena akaongea kwa sauti ya kutetemeka kwa woga mkubwa.
Itaendelea Jumamosi..