THE OTHER HALF
SEASON 1 - LEGEND OF ANABELLE
"…mara zote linapotokea jambo ulimwenguni au katika maisha binafsi, watu wanatulia na kusibiri. Kusubiri muda sahihi wa kufanya maamuzi, muda sahihi wa kuipata fursa, muda sahihi wa kutatua changamoto… lakini uhalisia ni kwamba hakuna muda sahihi katika maisha, hakuna muda sahihi ambao fursa itajitokeza, hakuna muda sahihi ambao utafaa kufanya maamuzi. Unatakiwa kuutengeneza muda sahihi, kutengeneza muda sahihi na kuitengeneza fursa, kutengeneza muda sahihi na kuchukua maamuzi. Huu ndio mtazamo na fikra za watu walioubadilisha ulimwengu zilivyokuwa. Hawasubiri fursa, hawasubiri muda sahihi. Wanatengeneza muda sahihi. Wanatengeneza fursa. Wanafanya maamuzi, hata pale ambapo dalili zote zinashawishi wasifanye maamuzi.!
…hii ndio sababu kwanini unatakiwa kutokuridhika na kung'ang'ania kile tu unachokijua… ukiendelea kujua kile tu unachokijua, ufahamu wako haupanuki. Ukiendelea kufanya pekee kile ulicho na ustadi nacho, maarifa yako hayaongezeki. Ili tuwe na ulimwengu ulio bora, kila siku tunapaswa kufanya gunduzi na kujifunza vitu vipya. Kuna maarifa ambayo kwa sasa ulimwengu unaweza kudhani hauyahitaji, lakini ipo siku ndiyo yatakayo kuwa na tija ya kuuokoa ulimwengu.
Ulimwengu, na watu wote tuliomo ndani yake. Tunatakiwa kuwa tayari muda wowote.
Ipo siku ambayo tutaiona si muda sahihi, siku ambayo haina fursa dhahiri, na ndiyo siku hii ambayo maarifa haya yatatuinua kutengeneza fursa, kutengeneza muda sahihi na kuukokoa ulimwengu kutoka mikononi mwa watoto wa Anabelle 1 (Maldives)..."
EPISOSE 9
Book of Codes
ROME, VATICAN CITY
Giza kinene kilichoshiba hasa kilikuwa kinaashiria labda tayari ilikuwa ni saa Tisa usiku.
Watu sita waliokuwa wamevalia majoho meusi walikuwa wamesimama katikati ya eneo la wazi la mji wa Vatican linalojulikana kama Saint Peter's Square.
Namna walivyokuwa wamevaa, ilikuwa ni katika namna ambayo ilifanana kabisa na wale watu wa Rabat, Morocco.
Majoho meusi, miguuni wako pekupeku wakionekana wazi kabisa kuwa wametembea umbali mrefu sana. Pia shingoni walikuwa na tatoo iliyosomeka "SANCTA CEDES".
Tofauti na wale watu wa Rabat, Morocco hawa hawakuwa wamebeba sanduku, walikuwa mikono mitupu japokuwa mmoja wao alionekana amebeba kitu mikononi alichokivingirisha na kitambaa cheusi.
Kwa idadi pia walikuwa sawa kabisa na wale wa Morocco, nao hawa walikuwa watu sita.
Pembeni yao pale waliposimama zilikuwa zimelezwa maiti nne za askari wa ulinzi wa hapa Vatican wakiwa wanaonekana wamekatwa shingo kwa kisu.
Watu hawa sita wenye majoho meusi walikuwa wamesimama katika namna ambayo kama walikuwa wanatafakari ni wapi waelekee japokuwa walikuwa kimya hawajadili chochote kile.
Sehemu hii ilikuwa katika namna ambayo, ukifika katikati kabisa ya mji wa Vatican, unakuwa upo eneo hili linaitwa Saint Peter's Square. Hilo eneo ni kama 'round about' kubwa sana ambayo unaweza hata kufanyika mkutano wa hadhara. Kutoka hapa unaweza kuelekea kulia ambako unakitana na mageti makubwa yanayo kupeleka ndani ya ofisi za Papa pamoja na kanisa kuu la hapa maarufu kama Basilica (Saint Peter's Basilica). Alafu upande wa pili kunaakazi yenyewe (apartments) ambazo ndimo Papa anaishi.
Lakini pia kutoka hapa Saint Peter's Square unaweza kuelekea barabara ya mkono wa kushoto ambayo inakupeleka moja kwa moja kwenye maktaba na makumbusho maalumu ya Vatican yanayojulikana kama '16 Chapel'.
Huku ndiko hasa ambako walikuwa wanataka kuelekea.
Yule mmoja wao hawa watu sita ambaye alibeba kitu alicbokifunika kwa kitambaa akaanza kutembea kuelekea huku mkono wa kushoto njia inayoelekea 16 chapel ambako kuna maktaba na makumbusho.
Baada ya yeye kuongoza kuelekea njia hii na wenzake wote nao wakamfuata kuelekea huko.
Giza lilikuwa nene hasa kutokana na huu usiku wa manane. Lakini watu hawa walitembea kwa ufasaha kana kwamba maisha yao yote wamekuwa wakiishi kwenye giza totoro la namna hii.
Walipofika kwenye geti lenye kuruhusu kuingia '16 Chapel' yule aliyebeba kitu alichokivingirisha akagonga geti mara tatu, kisha akatulia. Akarudia kugonga tena mara tatu, akatulia, kisha akagonga tena mara tatu kwa awu nyingine ya tatu na kisha akaacha kugonga geti.
Akasimama kimya kabisa na wenzake kama maroboti walisubiri. Wakasubiri kama dakika mbili hivi na mara kidirisha kidogo sana kwenye geti chenye ukubwa wa kama kiganja cha mkono na umbo la mraba kikafunguliwa.
"Wageni wa nani?" Sauti kutoka kwenye kile kidirisha ikauliza.
"Father Ricardo.!" Mmoja wa wale watu akajibu.
Geti likafunguliwa haraka haraka na kwa tahadhari kana kwamba mfunguaji hakutaka kusikika kama anafungua geti.
Baada ya geti kufunguliwa wale watu wakaingia.
"Father Ricardo!" Yule aliyefungua geti akajitambulisha huku ananyoosha mkono wa salamu. Alikuwa ni mtu mzima wa kupata umri kama miaka 54 hadi 56 hivi, na muonekano wake na lafudhi yake ilionyesha alikuwa ni mtu wa Hispania.
"Sancta Cedes!" Mmoja wa wale watu akajibu kwa kujitambulisha pasipo kushikana mkono wa salamu ulionyooshwa na father Ricardo.
Father Ricardo hakutaka kupoteza muda zaidi, haraka sana na kwa tahadhari kubwa akawaongoza kuingia ndani ya Makumbusho ya '16 Chapel' kwa kupitia mlango wa nyuma wa Makumbusho.
Huu ulikuwa ni usiku wa manane, kupata saa tisa usiku, kwa hiyo makumbusho yalikuwa tupu kabisa. Watu pekee ambao walikuwa humu kwa sasa alikuwa ni Father Ricardo na hawa watu sita.
"Nadhani tukabidhiane haraka kabla sijaanza kutafutwa!" Father Ricardo akaongea kwa sauti ya chini.
Ndani ya makumbusho kulikuwa na kama taa moja tu imewashwa upande Fulani, kwahiyo kulikuwa na mwanga hafifu lakini ulitosha kuona vyema.
Mmoja wa wale watu sita, yule ambaye alikuwa amebeba kitu alichokivingirisha na kitambaa cheusi akapiga goti moja sakafunu na kuweka chini kile kitu alichokuwa amekishika mikononi na kuanza kufungua kitambaa alichokivingirisha.
Akafungua kile kitambaa cheusi chote, na ndani yake kulikuwa na kitabu chenye ukubwa wa saizi ya kati, kama ukubwa wa laptop.
Kulikuwa kitabu kinene, kikiwa na ukurasa mgumu wa nje kama gome. Juu ya kurasa ya nje ya kitabu hiki kilikuwa kinamaandishi yameandikwa kwa herufi kubwa kwa mwandiko aina ya 'gothic' na maandishi haya yalisomeka,
"BOOK OF CODES"
Father Ricardo akaweka mkono kifuani kwake kana kwamba ahamini kile alichokuwa anakiona. Akaipiga ishara ya msalaba kama mara tatu hivi. Akapiga mgoti chini na kunyoosha mikono kama anataka kukiinua kile kitabu.
"Tafadhali" Father Ricardo akamuambia yule mtu ambaye alikuwa amepiga goti moja sakafuni.
Yule mtu akasimama. Father Ricardo akakainuua kitabu na kukikumbatia kifuani kana kwamba mtoto anayempenda mno. Akakibusu kitabu mara kadhaa kisha akainuka.
Haraka akatembea kuelekea upande wa pili wa Jengo ambako kulikuwa na 'shelves' za vitabu.
Akatumia takribani dakika kumi kutafuta tafuta kutoka shelve moja kwenda nyingine kana kwamba kuna sehemu anaitafuta kwenye ile shelves.
Alipoiona akachomeka kitabu hiki katikati ya vitabu vingine na kisha kurejea upande ambao walikuwa wamesimama wale.
"Kipo sahihi!" Mmoja wa wale watu akamuuliza Father Ricardo.
"Sahihi kabisa… mbarikiwe sana wanangu!" Father Ricardo akawashukuru.
"Sasa nadhani utukabidhi mzigo wetu!" Yule mtu akaongea tena.
"Bila shaka!" Father Ricardo akajibu na kuanza kuwaongoza kutoka ndani ya makumbusho kupitia mlango wa nyuma kama walivyoingia.
Lakini kabla hawajatoka kabisa. Pembeni ya ukuta kulikuwa na simu ya mezani. Father Ricardo akainua simu na kubofya. Kisha akaweka sikioni.
"Nipe taarifa!" Father Ricardo akaongea.
"Papa amelala bando!" Sauti ikaongea upande wa pili wa simu.
"Nakuja nao Basilica… sitaki usumbufu wa walinzi!"
"Usiwe na shaka kuhusu hilo." Sauti upande wa pili ikajibu.
Baada ya hapo wakatoka makumbusho ya '16 chapel' na kwa umakini mkubwa Father Ricardo akafungua geti lisipige kelele na wakatoka na kuanza kuifuata njia inayoelekea Saint Peter's Square.
Itaendelea Jumatatu