Mwananchi Communications Limited
Serikali ya Tanzania imejipanga kwelikweli katika kubeba jukumu la uenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 itakayoshirikiana na nchi za Kenya na Uganda.
Mara baada ya nchi kutambua kuwa inataka uenyeji wa fainali hizo zitakazokuwa za 36 tangu michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 1957, tayari mipango ilianza mapema ya kuhakikisha inakuwa na miundombinu rafiki kwa wageni watakaoshiriki fainali hizo zinazoandaliwa kwa mara ya kwanza na nchi za Afrika Mashariki (EAC).
Mbali na miundombinu, pia Tanzania ilishajipanga kujenga uwanja mpya wa kisasa katika jiji la kitalii la Arusha utakaokuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 30,000 watakaokaa na wenye huduma zote kwa uwanja wa kisasa kama huo ambao utafahamika kama The Hexagon Arusha Stadium.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Ally Mayay, uwanja huo utajengwa pembezoni mwa jiji la Arusha katika Kata ya Olmoti na tayari michoro ipo tayari na kwa sasa mainjinia wapo kazini kwa ajili ya ujenzi huo utakaochukua muda wa miezi 18 (mwaka na nusu) hadi kukamilika.
Mbali na uwanja huo, pia Benjamin Mkapa na Amaan Zanzibar ambavyo kwa sasa vyote vipo kwenye ukarabati navyo vinatarajiwa kutumiwa kwa fainali hizo zinazokuwa za sita kwa Ukanda wa Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) baada ya awali Sudan na Ethiopia kuandaa mara tano tofauti hadi kati ya 1957 na 1976 iliyokuwa mara ya mwisho kwa nchi za ukanda huo.
Pichani ni muonekano wa mchoro ya uwanja huo utakaofanana kwa kiasi flani na ule wa Allianz Arena unaomilikiwa na Bayern Munich ya Ujerumani na ule wa Taifa wa Senegal.