SoC03 Teknolojia tatu muhimu zinazoweza kutusaidia katika kutatua changamoto na kutuletea maendeleo

Stories of Change - 2023 Competition

cilla

JF-Expert Member
Jul 15, 2011
369
296
TEKNOLOJIA TATU MUHIMU ZINAZOWEZA KUTUSAIDIA KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO NA KUTULETEA MAENDELEO.


TEKNOLOJIA NI NINI?
Neno Teknolojia au kwa kiingereza technology ni neno ambalo limetokana na lugha ya kigiriki “technología“ lenye maana ya maarifa ya ujuzi, sanaa na ufundi yaliyowekwa katika matumizi ya vitu, uundaji na utumiaji wa njia za kiufundi na uhusiano wao na maisha, jamii, na mazingira.Leo hii kuna mapinduzi makubwa sana katika elimu, afya, kilimo, miundombinu,utawala na kadhalika kwa sababu ya kuwepo kwa teknolojia.

Katika Ulimwengu wa sasa teknolojia ni zaidi ya jeshi, pesa au ujasusi.Dunia ya leo mwenye teknolojia ndio mwenye kila kitu.Tukiwekeza katika teknolojia vizuri inaweza kutuletea maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali nchini.

TEKNOLOJIA TATU MUHIMU ZINAZOWEZA KULETA MAPINDUZI KATIKA ELIMU NA UTAWALA .

1.KUMBI ZA KISASA ZA MIKUTANO KWA NJIA YA VIDEO (Video conferencing large boardroom).
Hii ni moja ya njia ya kisasa sana inayotumiwa duniania kwa ajili ya mikutano na semina mbalimbali ya mubashara ambayo kwa wakati mmoja mzungumzaji anaweza kuongea na mamia au maelfu ya watu pasipo watu hao kusafiri na kwenda kukusanyikia mahali pamoja.Kumbi hizi zinakuwa ni za kisasa zilizofungiwa vifaa maalumu(Monitors and audiovisual installations) vinavyowezesha wafuatiliaji kuona na kusikia vizuri lakini pia anaweza kuchangia mawazo yake pale inapohitajika.


Njia hii ya matumizi ya teknolojia ya kumbi za kisasa inaweza wezakutafaa sana endapo zitakuwepo angalau kila wilaya nchini kwaajili yakuwajengea uwezo watumishi wetu wa umma.

Teknolojia hii itasaidia sana kuwepo kwa semina mbalimbali mara kwa mara za kuwajengea uwezo watumishi wa umma katika sekta mbalimbali kwa wakati mmoja.Kama kumbi za namna hii zikiwepo angalau kila wilaya nchini itasaidia sana kuokoa muda na gharama za usafiri kwa watumishi,wakufunzi,walimu na wawezeshaji. Wakati mwingine serikali kwasababu ya gharama na bajeti ndogo,inashindwa kuwa na semina na mafunzo ya mambo mtambuka katika sekta zetu mbalimbali ambayo yanahitaji watumishi na viongozi wetu kujengewa uwezo kila mara ili kuendana na wakati na mazingira yaliopo kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili waweze kukabiliana nayo vizuri.

Ukumbi huu unaweza kutumiwa na sekta ya polisi,afya, mahakama, ualimu, watendaji, maafisa kilimo n.k

2.MFUMO IGIZI (SIMULATOR PROGRAMU).
Mfumo igizi au kwa kimombo simulator program ni teknolojia iliyoundwa kwa kuiga mfanano wa kitu halisi ambapo mtumiaji anaweza kutumia na akijihisi yupo katika mazingira yake halisi. Mfano mwanafunzi katika chuo cha uuguzi anaweza kuanza kufanya mazoezi katika kitu au mdoli wenye mfanano wa karibu na binadamu.Au rubani kabla ya kurusha ndege halisi(airplane) analazimika kutumia kifaa igizi(Flight Simulators) kwaajili ya mazoezi yenye mfanano wa kila kitu katika chumba cha urubani mithili ya ndege yenyewe halisi kabla ya kwenda kurusha ndege yenyewe.

Mfumo igizi upo wa aina mbalimbali kwa matumizi mbalimbali kama burudani, ujifunzaji ,mazoezi nk.

Sisi kama nchi kutokana na upungufu wa maabara za kujifunzia na gharama za ununuzi wa vifaa na kemikali Ili kuweza kuwajengea wanafunzi wetu uelewa katika masomo ya sayansi ni vizuri kama tutafikiria kuwa na Mfumo Igizi wa maabara (Lab Simulator) wakujifunzia.Mfumo huu unamsaidia mwanafunzi kujifunza kwa urahisi na kurudia rudi pasipo kwenda maabara halisi.Mfano wa maabara igizi za kemia ,zinamuwezesha mwanafunzi kuchanganya kemikali katika programu igizi mara nyingi zaidi awezavyo bila kuwa na wasiwasi wakudhurika au upotevu wa kemikali.

Mfumo huu unasaidia kuokoa gharama za manunuzi ya kemikali nyingi kwaajili ya mwanafunzi kujifunzia.Pia inampa mwanafunzi uwezo wa kurudia mara nyingi tofauti na akitumia kemikali halisi kwasababu ni gharama.Kwa vyuo vya ufundi pia wanaweza kuwa na simulator au mfumo Igizi kwenye kozi mbalimbali kama za udereva ambapo mtu anaweza kujifunza kuendesha gari katika chumba cha darasa kabla ya kuingia barabarani.

3.VIDEO ZA MAFUNZO(video tuitorial)
Tunakumbuka kipindi cha korona wakati shule zilipokuwa zimefungwa ambavyo vipindi mbalimbali vya elimu kwenye runinga zetu jinsi ilivyokuwa msaada kwa wanafunzi wengi waliokuwa wamesalia majumbani.

Kulingana na upungufu wa walimu wa sayansi hasa kwa shule za sekondari, serikali inaweza kuwekeza kwenye utengenezaji wa picha mjongeo(video) kwa masomo mbalimbali ili zitumike kwaajili ya wanafunzi wa sekondari nchini wenye upungufu wa walimu.Sio tu kwamba zitasaidia wanafunzi lakini pia zitakuwa msaada mkubwa sana kwa walimu kwasababu hata wao wanaweza kuzitumia katika kujikumbusha maeneo yanayomtatiza katika somo lake.

Faida ya kujifunza kwa njia hii pia ni kwamba inakupa nafasi ya kurudia rudia tena na tena sehemu ambayo haikueleweka kwa wanafunzi.Changamoto inaweza ikawa ni umeme kwa baadhi ya shule lakini umeme ni jambo ambalo serikali ikiamua inaweza kufikisha umeme katika shule zote nchini.

Mwisho

Teknolojia ipo kwaajili yakutatua changamoto na kurahisisha kazi tuitumie vizuri kwa maendeleo yetu

 
Back
Top Bottom