Muro aongeza utata
•
Awasilisha risiti za pingu alizokamatwa nazo
na Martin Malera
SAKATA la mwandishi wa habari za uchunguzi, Jerry Muro, limeingia katika hatua mpya baada ya kubainika kuwa ana risiti za pingu ambazo polisi walimkamata nazo.
Umiliki huo wa pingu unaongeza utata katika sakata zima linalomhusisha na utapeli, ingawa linajibu swali la Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyetilia shaka zilikotoka pingu hizo.
Juzi alikaririwa akimtaka Muro awapelekee polisi risiti, akisema si rahisi kupata pingu kwa kuwa "haziuzwi hovyo kama njugu."
Kamanda Kova alisema ni marufuku kwa raia kumiliki pingu, na kwamba kupatikana nazo ni kosa la jinai.
Alisisitiza kuwa pingu ni mali ya polisi, magereza na jeshi; hivyo mtu wa kawaida kukutwa nazo ni kosa la jinai. Na alidai kwamba Muro asingeweza kupata risiti.
"Pamoja na kumwambia atuletee risiti, tunajua hatafanikiwa kuzipata kwa kuwa pingu haziuzwi ovyo kwani mwenye mamlaka ya kumuweka nguvuni mtu ni polisi pekee," alisema Kamanda Kova.
Hata hivyo, jana Muro alilithibitishia Tanzania Daima kwamba anamiliki kihalali pingu na bastola aina ya CZ 97B namba A6466 iliyotengenezwa nchini Czechoslovakia.
Risiti hiyo inaonyesha Muro alinunua pingu hizo Mei 20 (mwaka umefutikafutika) katika duka la silaha la Mzinga Corporation lililoko Upanga, jijini Dar es Salaam, akapewa risiti namba 34357310.
Kwa mujibu wa risiti hiyo iliyoandikwa jina kamili la Muro, pingu hizo zilinunuliwa kwa sh 25,000.
Tanzania Daima ilipowasiliana na duka hilo la silaha, mmoja wa wafanyakazi wake ambaye hakutaka kutaja jina, alikataa kuzungumzia risiti hiyo kwa madai kuwa si msemaji.
Mfanyakazi huyo alilitaka Tanzania Daima kuwasiliana na Meneja Mkuu wa Mzinga Corporation, lakini hakupatikana. Ilidaiwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Muro anayekabiliwa na tuhuma za kudai rushwa kwa vitisho pamoja na kukutwa na pingu isivyo halali, amekuwa gumzo tangu kuanza kwa sakata hili kutokana na utata wa taarifa zinazomhusu, hasa zinolewazo na polisi.
Mwanahabari huyo ambaye yuko nje kwa dhamana, anakabiliwa na tuhuma za kukusudia kutaka kuomba rushwa na kujifanya ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).
Juzi, Kamanda Kova alimwingiza Muro katika mtandao wa matapeli sugu.
Kwa mujibu wa Kova, Muro na matapeli wengine wawili, wanadaiwa kushirikiana katika mpango wa kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage kati ya Januari 28 na 31 mwaka huu.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Deogratius Mgassa (35) na Edmund Kapama (52).
Walimhusisha Wage na kashfa ya ufisadi na umiliki wa majumba na hoteli za kifahari mjini Morogoro, wakataka awape pesa ili "wasimlipue".
Kwa mujibu wa maelezo ya mlalamikaji huyo, watuhumiwa hao walijitambulisha kama maofisa wa Takukuru, wenye vyeo tofauti.
Inadaiwa kwamba mmoja wao alijitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru Dar es Salaam, mwingine akajifanya ofisa wa kawaida kutoka taasisi hiyo, wa tatu alijitambulisha kama mwanajeshi wa nyota tatu na ofisa wa Takukuru Kitengo cha Habari.
Muro alikamatwa mwishoni mwa wiki, majira ya saa 5 asubuhi katika Hoteli ya City Garden katikati ya Jiji la Dar es Salaam baada kuwekewa mtego na Jeshi la Polisi.
Tayari Baraza la Habari Tanzania (MCT) limetoa taarifa kuelezea kusikitishwa kwake na tukio hilo na kulitaka Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi, kutomnyanyasa na kuhakikisha haki inatendeka ili umma ujue kilichomtokea mshindi huyo wa tuzo ya uandishi bora wa mwaka 2009, katika uchunguzi wa habari za rushwa.
Umma umegawanyika kuhusu sakata la Muro, huku baadhi ya wananchi, wakiwamo wabunge, wakionyesha kumtetea kwa madai kuwa amebambikiwa tuhuma hizo kwa sababu ya kazi zake za kufichua rushwa ya polisi wa usalama barabarani.
Source Tanzania Daima, Feb 4, 2010