SoC03 Tazama namna Mahakama na Serikali zinavyoshirikiana kuminya haki ya Mtumishi wa Umma kusuluhishwa migogoro ya kazi

Stories of Change - 2023 Competition

sajo

JF-Expert Member
Nov 8, 2010
3,029
5,259
Tarehe 28 Machi 2022, Mahakama ya Rufani Tanzania (CAT) kupitia hukumu ya kesi ya Rufaa ya TANZANIA POSTS CORPORATION dhidi ya DOMINIC A. KALANGI (Rufaa ya Madai Na. 12 ya 2022) [2022] inapatikana hapa iliamua kuwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) haina mamlaka ya kusikiliza na kutatua migogoro ya kazi inayohusisha wafanyakazi wa Serikali.

Katika hukumu hiyo, Mahakama ilielekeza migogoro inayohusu watumishi wa umma, kupelekwa mbele ya Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) bila kuzingatia kuwa PSC haina mamlaka ya awali ya kisheria ya kupokea na kusikiliza migogoro ya watumishi wa umma isipokuwa ina mamlaka ya kirufani tu ya kusikiliza Rufaa za watumishi wa umma dhidi ya maamuzi ya mamlaka zao za nidhamu. Mahakama ilisema kuwa imekitafsiri kifungu cha 32A cha Sheria ya Utumishi wa Umma na kufikia uamuzi huo.

PSA 32A.png

Kifungu cha 32A cha Sheria ya Utumishi wa Umma.

Maneno makali ya Mahakama yalikuwa katika aya ya mwisho ya ukurasa wa 9 kati ya 10 wa hukumu hiyo, ambapo mahakama iliamua ifuatavyo;

Kalangi extract.png

Tafsiri ya Kiswahili isiyo Rasmi ni hii;
Kwa maneno ya kifungu hicho tulichokinakili, haina shaka kuwa mashauri yote ya kinidhamu au migogoro yote ya kazi inayohusisha watumishi wa umma inaangukia katika mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Umma ambapo maamuzi yake tume hiyo yanaweza kukatiwa rufaa kwa Rais. Kama ilivyosemwa kwa usahihi na Bi. Kinyasi na tulivyoiona hapo juu, CMA haina mamlaka ya kusikiliza migogoro hiyo.

Matokeo ya Hukumu
Kisheria, Hukumu hiyo ilibadilisha vifungu mbalimbali vya sheria za kazi na kuvifanya visiwe na maana iliyokusudiwa na Bunge au kwa kuondoa maana iliyopo katika vifungu hivyo. Sheria zilizoathirika ni zifuatazo:

Sheria ya Taasisi za Kazi Sura ya 300 Marejeo ya 2019, iliathiriwa kifungu cha 14 (1 ) kwa kuondoa uwezo na mamlaka ya CMA kusikiliza migogoro ya kazi ya wafanyakazi wote chini ya sheria yoyote. Kwa sasa inabidi kirekebishwe na kueleza kuwa CMA inasikiliza migogoro ya kazi ya watumishi wa sekta binafsi tu na kwa sheria zisizohusu watumishi wa umma;

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura ya 366 Marejeo ya 2019, iliathiriwa kifungu cha 2 (1) kinachosema kuwa Sheria hiyo itatumika na wafanyakazi wote nchini ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma, kwa sasa inabidi kirekebishwe na kusomeka kuwa Sheria itatumika kwa wafanyakazi wa sekta binafsi tu. Pia ikaathiriwa kifungu cha 4 (a) kinachotoa tafsiri ya neno mgogoro kuwa ni mgogoro wowote unaohusisha suala la kazi kati ya mwajiri yoyote kwa upande mmoja na mwajiriwa yoyote kwa upande wa pili. Kwa sasa kinabidi kurekebishwa na kieleze kuwa mgogoro ni ule unaohusisha ajira kwa sekta binafsi tu. Izingatiwe kuwa kwenye Sheria ya Utumishi wa Umma, sio tu hakuna maana ya neno mgogoro bali hata neno mgogoro lenyewe halipo katika Sheria hiyo;

Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 Marejeo ya 2019, iliathiriwa katika Kifungu cha 10 (1) ambacho kinaeleza mamlaka na uwezo wa Tume ya Utumishi wa Umma. Hakuna sehemu Sheria inapoeleza kuwa PSC itakuwa na uwezo wa kusikiliza na kutatua migogoro ya wafanyakazi wa umma bali kifungu namba 10 (1) (d) kinaipa PSC mamlaka ya kupokea na kusikiliza Rufaa za watumishi wa umma dhidi ya mamlaka zao za kinidhamu. Kwa sasa inabidi kurekebishwa kwa kuongeza kifungu kitachoipa PSC uwezo wa kupokea malalamiko na migogoro na kuitatua, pia inabidi iongezwe tafsiri ya neno mgogoro na inabidi kutungwa kanuni za uendeshaji wa migogoro katika tume hiyo ambazo kwa sasa hazipo.

Athari nyingine ni kufutwa kwa kesi mbalimbali za kazi zilizokuwa zikiendelea CMA na Mahakama Kuu ya Tanzania zikihusisha watumishi wa umma.

Ni kwa Namna gani mahakama na Serikali vimeshirikiana?
Serikali ndiyo iliyoleta hoja mahakamani kuwa CMA haina mamlaka ya kusikiliza migogoro inayohusisha watumishi wa umma. Mahakama ikakubaliana na hoja ya Serikali kwa kumsifu wakili wa serikali (Ms Kinyasi) kuwa alichokisema ni sahihi kabisa, ikatoa uamuzi wa kuzuia migogoro hiyo isiende CMA bali iende PSC.Haikutoa maagizo ya marekebisho ya Sheria.

Mara baada ya hukumu hiyo, Serikali ilitakiwa kwa hati ya dharula kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria za kazi ili kukidhi maamuzi yaliyofanywa na mahakama, lakini mpaka leo, takribani miezi 15 sasa hakijafanyika.

Ninaamini kuwa kwa namna fulani Serikali inanufaika na kutokuwapo kwa marekebisho hayo ya sheria kisheria na hivyo kwa makusudi kabisa imeamua kutopeleka muswada bungeni. Matokeo yake ni kuwa mfanyakazi wa serikali ameporwa haki ya kutatuliwa migogoro kwa kuwa hawezi tena kufika CMA na pia hataweza kupeleka PSC kwa kuwa nao hawana mamlaka ya awali kusikiliza mgogoro wa kikazi.

Tunajua kuwa kazi ya Bunge ni kutunga sheria na kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria. Suala la uwezo wa kisheria wa mahakama kusikiliza kesi huwa linawekwa na Bunge wakati wa utungaji wa Sheria na haliwezi kuwekwa na Mahakama wakati ikiandika hukumu kwa kuwa kama mahakama itafanya hivyo maana yake itakuwa imeingilia muhimili wa bunge.

Sasa je, Serikali haikosei kwa watumishi wake?
Kama walivyo waajiri wengine, Serikali nayo huwa inakosea na hivyo inastahili kushtakiwa na kuwajibika kwa makosa iliyoyafanya dhidi ya watumishi wake.
Mfano, Serikali ikiamua kwa makusudi kutowalipa mishahara wafanyakazi wake, huo ni uvunjifu wa mkataba wa ajira, je watalalamika wapi? Kabla ya tarehe 28 Machi 2022 watumishi hawa walikuwa na uwezo wa kulalamika CMA lakini sasa hawawezi kwenda hata kidogo.

Nini kifanyike?
Mahakama (CAT) ifanye mapitio ya hukumu hiyo (suo motu) na kubatilisha uamuzi ilioutoa kwa kuwa haukuwa sahihi, haikutafsiri vyema sheria na ulizidi mipaka ya Mahakama. Tuitwe marafiki wa Mahakama kuiongoza kufika tafsiri sahihi.

Vivyo hivyo, Serikali ipeleke haraka bungeni muswada wa kurekebisha vifungu vya sheria vilivyobadilishwa na hukumu ili wafanyakazi wa serikali wapate haki yao iliyoporwa.

Moja ya misingi ya Utawala Bora ni hali ya uwepo wa utawala wa sheria ambapo watu binafsi na serikali huwa na hadhi sawa mbele ya sheria. Kupitia hukumu hiyo, heshima kwa utawala wa sheria ilivunjwa na mihimili hii miwili, yaani Mahakama na Serikali iliposhirikiana kunyang'anya haki ya mtumishi wa umma kutatuliwa migogoro yake ya kazi na hivyo, mahakama na serikali zimejiweka juu ya sheria kuliko wafanyakazi wa umma. Mahakama ilijivua jukumu lake la msingi la kuwa chombo pekee cha kutoa haki, ikashiriki kupora haki ya watumishi wa serikali.​
 
Back
Top Bottom