Kwamba sasa afisa wa TAKUKURU Bhoke Ryoba ameuawa na "watu wasiojulikana" mbele ya kadamnasi ya watu inaendeleza kile ambacho wengine tumekisema kwa miaka sita sasa - kuna tatizo la msingi la muundo na utendaji katika Usalama wa Taifa.
Ninakumbushia tu.
Ofisa wa TAKUKURU amuua mwenzake Dar
mtanzania, Jumatatu, Desemba 24, 2012 03:43 Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
*Walikuwa kwenye sherehe, akamtwanga risasi jichoni
*Alipomaliza kuua, akajisalimisha kituo cha polisi
OFISA wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Makao Makuu jijini Dar es Salaam, Mussa John (34), amemuua kwa risasi ofisa mwenzake, Bhoke Ryoba (32).
Tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati wafanyakazi hao pamoja na wenzao, walipokuwa katika sherehe za kuuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2013.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema mauaji hayo yalitokea juzi saa 1.30 usiku, katika ufukwe wa Hoteli ya Sourthen Beach iliyopo Kigamboni, Temeke Dar es Salaam.
Watumishi hao walikodi gari ndogo na kwenda kwenye ufukwe huo, kwa ajili ya kupata vinywaji na chakula. Wakati walipokuwa wakifurahia, ghafla inasemekana John alichukua bastola kisha akampiga Bhoke kwa risasi iliyompata jichoni.
Tukio hilo lilisababisha Bhoke atokwe damu nyingi na wenzake walipoona hivyo, wakaanza kutimua mbio huku na kule.
Baadaye walimchukua majeruhi na kumkimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akiwa katika hali mbaya na alifariki dunia usiku wa kumkia jana, wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Kutokana na tukio hilo, mtuhumiwa John alijisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi Changombe Temeke, ambako bado anashikiliwa huku uchunguzi zaidi wa tukio hilo ukiendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa hapo hapo Muhimbili.
Bado tunaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hili, ili tuweze kujiridhisha na mazingira halisi ya tukio zima kwani wakati linatokea, hapakuwa na ugomvi wowote.
Kwa hiyo, tukio linahitaji uchunguzi wa kina tujue namna bastola hiyo ilivyotumika kumpiga marehemu na sherehe hizo zilikuwa zinahusu nini kwani waliohusika ni baadhi tu ya watumishi wa TAKUKURU, alisema Kamanda Kiondo.
Wakati Kamanda Kiondo akitoa taarifa hiyo, Ofisa Habari wa TAKUKURU, Doreen Kapwani, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
Katika taarifa hiyo, Dorren hakueleza kwa undani juu ya tukio hilo, licha ya kusema kuwa uchunguzi zaidi unafanywa na Jeshi la Polisi.
Tumekuwa tukipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali, wakihitaji kufahamu ukweli kuhusu tukio la kupigwa risasi kwa mtumishi wa TAKUKURU, Bhoke Ryoba.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, anapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tukio hili, kwamba ni kweli mtumishi Bhoke Ryoba, amefariki dunia Jumamosi usiku baada ya kupigwa risasi. Uchunguzi wa polisi kuhusu chanzo cha tukio hilo bado unaendelea, alisema Doreen kwa kifupi katika taarifa yake hiyo.