MTWARA KUMEKUCHA: WAPIGANAJI WAVURUMUSHA KOMBORA CCM
WAPIGANAJI WAVURUMUSHA KOMBORA CCM
TAMKO LA WAPIGANAJI WA KWELI CCM
KWA AJILI YA TAIFA LETU; SASA NA BAADAYE
Uko nyuma tulishinda katika mapambano yetu kutokana na umoja wetu wa kitaifa,
usahihi wa siasa yetu na uongozi bora wa Chama. Leo na katika siku za usoni tutahitaji
umoja imara zaidi, siasa sahihi na uongozi bora wa chama.. vibepari na vibwanyenye
vya humu nchini vimeonyesha dhahiri uhasama wao dhidi ya maslahi ya wakulima na
wafanyakazi, umoja wa sasa lazima usimame juu ya misingi iliyo wazi na sahihi,
misingi ya ujamaa; kwa hiyo ni umoja wa wakulima na wafanyakazi na wale wote wanaounga
mkono kwa vitendao ujenzi wa ujamaa nchini. Mwongozo wa CCM, 1981
Imetolewa: Februari 10, 2010
SISI NI NANI
Sisi ni wananchi wa Tanzania. Sisi vile vile ni wana CCM ambao tumechoshwa na mwelekeo
wa kisiasa nchini na hasa kuhusishwa kwa baadhi ya Wana CCM na vitendo vya ufisadi
ambavyo vimekipaka matope chama lakini zaidi tumechoshwa na serikali inayoongozwa na
chama chetu kuhusishwa na ufisadi katika Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake mbalimbali.
Kama Watanzania hatuwezi tena kukaa kimya na kusubiri watu wengine waje kutuletea
mabadiliko; hatuwezi tena kukaa pembeni na kuacha raslimali za nchi yetu ziendelee
kugawanywa mikononi mwa kikundi cha watu wachache kana kwamba ni haki yao ya
kuzaliwa; hatuwezi tena kukaa kimya tukizionea haya chembechembe za ufisadi ndani ya
chama na kwenye serikali.
Kwa tamko hili tunasema imetosha! Tunataka mabadiliko kama ajenda kuu ya uchaguzi mkuu
mwaka huu. Mabadiliko ya kweli yatakaofumua fumua mtandao wa uhalifu na ufisadi nchini
na hatimaye kurejesha imani ya wananchi kwa serikali yao na kwa Chama cha Mapinduzi na
kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anayo nafasi ya kufanikiwa katika taifa lake na kuhakikisha
tunaweka misingi ya mafanikio kwa kizazi kipya cha Watanzania. Tunakataa kushiriki katika
kukilaani kizazi kijacho katika utegemezi wa fikra na vitu, uombaomba wa kudumu na
utamaduni uliokumbatiwa wa kifisadi.
Miongoni mwetu katika tamko hili ni Watanzania na wana CCM ambao ni Wabunge, Viongozi
wa Chama katika ngazingazi mbalimbali na jumuiya mbalimbali na kundi la wanachama wa
kawaida ambao nao wamechoshwa na hali ya kisiasa iliyopo ndani ya chama na hali ya
kiutawala iliyopo katika serikali.
KWANINI TUNATOA TAMKO HILI
Tunatoa tamko hili kama juhudi yetu ya wazi ya kujikosoa kama chama kwa mujibu wa Mwongozo
wa CCM wa 1981 (Ibara ya 58) ambayo sehemu yake inasema kwamba kujikosoa na
kukosoana kama njia ya kukijenga na kukiimarisha Chama na wanachama. Na vile vile
tunatekeleza haki yetu ya Kikatiba ya chama ya kuwa tayari kukosoa na kukosolewa. Tunatoa
tamko hili tukiamini ya kwamba waovu hufanikiwa pale wenye haki wanapokaa kimya.
Hatuwezi tena kukaa kimya mbele ya uovu kwani gharama yake ni kubwa mno kwa taifa na
kwa mtu mmoja mmoja.
UTANGULIZI
Taifa letu liko katika kipindi kigumu zaidi cha historia yake; kipindi ambacho kila Mtanzania
anatakiwa kupima mwelekeo wa taifa letu na vile vile anaitwa na historia kufanya maamuzi.
Tunaamini kama kila mmoja wetu ataamua kujipima yeye mwenyewe na kufanya maamuzi
ambayo anajua ni muhimu kwa taifa, nchi yetu itaweza kutoka katika hali iliyopo sasa ambayo
ni kuridhika na mfumo wetu wa kiutawala ambao ndio umekuwa mwamba wa utendaji wa
kifisadi kuanzia ngazi za chini za utawala wa taifa letu hadi ngazi za juu kabisa.
Tunaamini kuwa ili kuweza kuleta mwelekeo mpya wa taifa letu hatuna budi kubadilisha fikra
zetu na mtazamo wetu wa utawala na kuamua kuchukua maamuzi ya kubadili mwelekeo wa
taifa letu ili sisi na watoto wetu pamoja na uzao wa watoto wetu tuweze kushiriki katika ujenzi
wa taifa jipya la kisasa na la Kitanzania.
Katika hili tunaamini Chama cha Mapinduzi kina nafasi ya pekee katika uongozi wa taifa letu,
nafasi ambayo kila mwana CCM anaitwa kuiangalia na kuilinda. Chama cha Mapinduzi kina
sera, mtazamo na vyombo ambavyo vinaweza kabisa kuchochea mabadiliko tunayoyataka
kama taifa. Chama chetu kina watu wenye uwezo kuleta mabadiliko hayo.
Hata hivyo mtazamo huu chanya unakabiliwa na ukweli mwingine ulio dhahiri; matatizo na
changamoto tunazoziona katika taifa letu leo hii na hasa katika utendaji wa serikali yetu vyote
vimetokea wakati Chama chetu ndiyo kimeshika hatamu ya uongozi wa taifa letu, bara na
visiwani. Hatuwezi kamwe katika dhamira safi kubebesha lawama watu au chombo kingine
chochote isipokuwa kulegalega na kumomonyoka kwa maadili ya uongozi wa Chama ambako
moja kwa moja kunaonekana katika kulegalega na kumomonyoka kwa maadili ya utendaji
kazi serikalini.
Kama Watanzania wenye mapenzi mema kwa taifa letu na kama wana CCM ambao
tunakitakia chama chetu ushindi katika mwaka huu wa Uamuzi na Uchaguzi Mkuu hatuwezi
kamwe kukaa kimya na kuombea mabadiliko yatokee bila ya sisi wenyewe kuwa sehemu ya
mabadiliko hayo. Tunaamini, kama wana na mabinti wa Tanzania na kama wana CCM
mabadiliko tunayoyataka kwenye taifa letu hayawezi kamwe kutokea kwa kusubiri wengine
wafanye au wengine watende; mabadiliko yote tunayoyataka ni sisi wenyewe tutayaleta na
kuyasimamia.
Hivyo basi,
TUKITAMBUA:
Kwamba, Watanzania wote wenye vyama mbalimbali, itikadi mbalimbali, na mirengo
mbalimbali ya kisiasa wamechoshwa na vitendo vya kifisadi vilivyokubuhu na utendaji duni
wa mara kwa mara na wa kusikitisha wa vyombo mbalimbali vya serikali yao;
Kwamba, kuchoshwa kwao huko kumewafanya baadhi yao kuwa na hali ya kutokujali
(apathy) ya mambo yanayohusu nchi yao na hivyo kila mmoja kujali zaidi mambo yake binafsi
na maslahi ya familia yake na siyo yale ya jamii nzima;
Kwamba, katika kutokujali huko baadhi yao wameanza kushiriki katika vitendo mbalimbali
vya kifisadi kwani wanajua hakuna mtu anayejali tena na kila mtu na lwake na hivyo
kuanzisha maadili potofu kabisa na ya hatari kwa taifa lolote lile. Maadili haya potofu ndiyo
yameendeleza na yasipobomolewa yataendeleza uwepo wa ufisadi na utendaji kazi wa
mifumo ya kihalifu (criminal syndicates) na mitandao ya kihalifu (organized crimes) katika taifa
letu; mifumo ambayo imepenya hadi kwenye taasisi zetu nyeti.
TUKIZINGATIA:
Kwamba, endapo Chama cha Mapinduzi hakitafanya mabadiliko makubwa, ya haraka na
yanayohitajika katika juhudi za kujisahihisha, basi Watanzania wataendelea kukata tamaa na
uongozi uliopo na hivyo kufungua mlango wa kuibuka kwa harakati zenye mirengo ya siasa
kali za mabadiliko ambazo zitawavutia wananchi. Sehemu nyingi duniani ambazo
zimetawaliwa kwa muda mrefu na chama kimoja zimeshuhudia mwelekeo huo wa wananchi
wake;
Kwamba, mabadiliko ya kweli yanaweza kuletwa na Watanzania wote na ya kwamba chama
chetu hakina ukiritimba wa uongozi na kwamba Mtanzania yeyote mwenye mawazo yenye
kujenga taifa, yenye kuendeleza uwazi, na yenye kutetea raslimali zetu ni rafiki yetu na
kamwe hawezi kuwa adui; Haijalishi Mtanzania huyo yuko wapi, ni wa chama gani na ana
nafasi gani ya kijamii. Kila mzalendo wa kweli mwenye kutakia mafanikio taifa letu ni
mwenzetu;
Kwamba, pasipo maamuzi yenye kuzingatia mustakabali wa taifa, yenye kujali kile
kinachotokea katika taifa letu leo hii Tanzania itaendelea kuwa shamba la wageni na
wananchi wakiendelea kuwa vibarua tu kwenye shamba hilo. Tunaamini kama Watanzania na
kama wana CCM ni lazima tufanye maamuzi yenye kuonesha ukweli kwamba tunajali kile
kinachotokea katika taifa letu.
Kwamba, Chama cha Mapinduzi kikiirudia misingi yake ya ujamaa na kujitegemea pasipo
kulazimika kumwomba radhi yeyote; kikirudia mwelekeo wa ujenzi wa taifa ambao
tuliutangaza mara baada ya Uhuru, Mapinduzi na Muungano; tukikumbatia miiko ya uongozi
kama ilivyoanishwa katika Azimio la Arusha huku tukilitafsiri katika hali halisi ya leo bila
kulizimua kwa nadharia zilizoshindwa, basi wananchi watakua na haki na sababu ya
kuendelea kukichagua chama hiki na kukubali kuongozwa nacho.
Kwamba, kama wana CCM tutashindwa kujichunguza, kujisahihisha na kujibadilisha ili kutoa
uongozi safi, bora, wenye kuthubutu na wenye maadili na maono, basi Watanzania wanayo
haki na kwa hakika wanao wajibu wa kutukataa na kukumbatia chama kingine chochote
ambacho kinaonesha uwezo na mwelekeo wa kutimiza njozi yao ya ujenzi wa taifa la kisasa.
Kutokana na ukweli huu, tunaamini kuwa katika dhamira safi kabisa hatuwezi kukaa kimya na
kuombea mabadiliko yatokee au yaongozwe na watu wengine. Hatuko tayari kuiachia hatima
ya taifa letu mikononi mwa kikundi cha watu wachache wenye kuendeleza na kulinda maslahi
yao na familia zao. Tukiamini kuwa CCM bado kina nafasi moja ya kusimamia mabadiliko ya
kweli ya uongozi wa taifa lakini kwanza ni lazima kama chama tujisafishe kwanza kama
ilivyokuwa desturi yetu miaka mingi iliyopita.
Hivyo basi;
TUNATANGAZA:
Kwamba, Chama cha Mapinduzi hakiwezi na hakipaswi kusimama kuomba kura tena kwa
wananchi isipokuwa baada ya ushahidi wa wazi wa vitendo wenye kung'oa chembechembe
zote zenye kuendeleza vitendo vya rushwa na hongo, uzembe, kutokuwajibika, ubadhirifu,
ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka kwa ajili ya manufaa binafsi ya
watu wafanyao hayo yaani Ufisadi;
Kwamba, bila ya kushughulikia mambo hayo yote ambayo kwa ujumla wake hujulikana kama
ufisadi Chama cha Mapinduzi kinajiweka katika mazingira mabaya ya uchaguzi na kuendelea
kuwa sehemu ya shuku kwa wale wasiokitakia mema. Mazingira haya yanafanya ushindi
wowote wa wana CCM kugubikwa na wingu la kutokuaminika;
Kwamba, kama wana CCM tuliokolea itikadi ya chama na makada wazuri na waaminifu wa
siasa za Chama chetu tunakataa mara moja, daima na milele kuwa na ushirika wowote na
wana CCM wengine ambao wanatuhumiwa, kutajwa, kushukiwa na hata kuhusishwa na
kashfa zote kubwa ambazo zimeligubika taifa kwa karibu miongo miwili sasa.
Kwamba, hakuna uwezekano wowote wa mapatano, mshikamano, umoja, au kwa namna
yoyote ile usuluhishi kati ya pande mbili zinazopingana ndani ya chama hususan kwenye
masuala yanayohusiana na ufisadi. Tunaamini njia pekee ya kurejesha nidhamu na umoja wa
kweli ni kuondolewa mara moja kwa chembe zote zenye kuharibu jina la chama na ambao
wamelidhulumu taifa letu utajiri wake.
Kutokana na ukweli huo;
TUNAAZIMIA YAFUATAVYO:
1. Tunakataa mpango wowote, juhudi zozote na mchakato wowote utakaolenga kutafuta
umoja na upatanishi kati ya chembe za ufisadi ndani ya chama Tunaamini hakuna
umoja na ushirika wa kweli unaoweza kupatikana na mafisadi au na wale wanufaikaji
wa vitendo vya ufisadi. Chama cha Mapinduzi hakina nafasi kwao au makuwadi wao.
2. Tunakataa juhudi zozote za kujaribu kuwaondoa wanachama wenye uwezo wa
kuongoza na walioonesha uwezo huo kwa vitendo kwa kisingizio cha umri ili
kuwapisha vijana. Tunaamini kama Taifa tutafanya kosa kubwa sana kuamua mara
moja kuliachia taifa mikononi mwa vijana kwa sababu ya umri tu. Tunaamini kila
mwana CCM mwenye uwezo wa kuongoza na anayekubalika kwa wananchi wake
asinyimwe nafasi ya kuongoza kwa kisingizio cha umri. Tunawaunga mkono wana
CCM ambao ya kuwa na uwezo wa kuongoza wameamua kukaa pembeni ili kuruhusu
wanachama wengine kuingia katika safu ya uongozi. Uamuzi huu usionekane kuwa ni
udhaifu au ni njia ya kuwalazimisha wengine kuufuata. Kustaafu nafasi ya uongozi
kunaweza kufanywa na mtu yeyote pasipo kujali umri wake.
3. Kutetea raslimali za taifa letu na utajiri wa nchi yetu kwa kukusudia kuzuia mikataba
na mipango yoyote yenye kurundika utajiri wetu mikononi mwa wafanyabiashara
wakubwa bila kujali maslahi ya leo ya taifa au yale ya kizazi kijacho. Tunachukua
msimamo huo tukiamini kuwa kama viongozi wa CCM tunalojukumu la kichama
kueneza matunda ya Uhuru kwa wananchi wote kwa ajili ya manufaa yao na
maendeleo ya Taifa kwa jumla. Ibara ya 17:2 ya Katiba ya CCM. Jukumu hili siyo la
wapinzani au wafadhili wa kigeni; ni jukumu letu kama Watanzania na kama wana
CCM
4. Kupigania haki ya kila Mtanzania kugombania nafasi ya uongozi pasipo
kulazimishwa kujiunga na chama cha siasa. Kama Watanzania kwanza na kama wana
CCM, tunaamini haki ya kuchaguliwa isiunganishwe na ulazima wa kujiunga na chama
cha siasa kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunavunja Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na vile vile kupingana na Tamko la Haki za Binadamu la 1948
ambalo Tanzania imeliridhia. Chama cha Mapinduzi na Wana CCM hatuogopi
wagombea binafsi kwani tunaamini Chama chetu kinakubalika, kina uwezo wa
kuongoza bila kujali wagombea wengine wanatoka wapi au wanapatikana vipi.
5. Kuhakikisha mfumo bora wa kuwajibika na kuwajibishana unakuwepo katika
serikali kwa kupendekeza mabadiliko ya Katiba na Sheria mbalimbali ili hatimaye
mfumo ambao umefungua milango ya kifisadi unakosolewa, kubomolewa na
kubadilishwa na mfumo ambao hautatoa nafasi kwa watu na vikundi vya watu
kuneemeka kwa kutumia mbinu za kifisadi. Bila ya kuubadili mfumo huu tunaamini
mafisadi wataendelea kuibuka kati yetu na kama taifa tutaendelea kupiga kambi
kwenye hili bonde la ufisadi miaka nenda rudi. Ni lazima tuubadili mfumo huu
tukizingatia vile vile malengo ya MKUKUTA II.
MTAZAMO MPYA WA UWAJIBIKAJI
Kwa muda mrefu mchakato wa nidhamu ya chama umekuwa ukitumika kuchelewesha
uwajibikaji wa wanachama wetu. Tumeendelea kutumia miundo mbinu mibaya ya nidhamu
kiasi kwamba Chama kimeonekana kulea uzembe na kubeba viongozi muflisi.
Katika juhudi za kujisahihisha na kujikosoa tunapendekeza kuanzia sasa kiongozi yeyote
wa chama anayekabiliwa na tuhuma nzito ziwe za kisiasa, kihalifu au kiuwajibikaji serikalini
atatakiwa kujiuzulu mara moja ili kuondoa mtazamo ambao Mwongozo Mtukufu wa
Chama wa mwaka 1981 iliukataa pale unaposema Mara nyingi tumependelea kuteteana,
kufichiana makosa na hata kutafuta visingizio visivyo na msingi. Neno kuleana, kwetu sisi
(ingawa kuna malezi mema na mabaya) limechukua nafasi ya kukosoana.
Haiwezekani kama Watanzania na kama wana CCM tukavumuiia kiongozi anayetuhumiwa
katika makosa ya kihalifu au kashfa kubwa na ambaye mbele ya jamii tayari amekwishachafuka.
Kiongozi huyo ambaye ameshindwa kujieleza na kukabiliana na tuhuma
dhidi yake mbele ya mahakama ya hadhara anakipaka chama matope na ni vizuri yeye
mwenyewe awajibike au alazimishwe kuwajibika.
Mtindo huu wa kuwajibishana ndani ya chama na kuheshimu hadhara ya wananchi hutumiwa
karibu na nchi zote ambazo zimeamua kufuata utawala wa demokrasia. Kiongozi
ambaye ameandamwa na tuhuma mbalimbali hastahili kuwa kiongozi.
Kwa hiyo,
1. Viongozi wafuatao wasimamishwe mara moja katika uongozi wa chama kwa mujibu
wa Ibara ya 8.2.4 ya Kanuni za Maadili ya Chama na kwa vile tayari wameshachafuka
kutokana na uzito wa tuhuma mbalimbali (wengine hadi za kihalifu) hawastahili kuwa
viongozi katika nafasi yoyote ndani ya Chama. Tunataka viongozi hawa waamue
wenyewe kuachia nafasi zao au Chama kiwawajibishe mara moja. Kundi hili
limekipaka chama matope.
- Edward Lowassa MB
- Daniel Yona
- Rostam Aziz MB
- Andrew Chenge MB
- Basil Mramba MB
- Nazir Karamagi MB
- Makongoro Mahanga MB
- Felix Mrema MB
- Sofia Simba MB
- Kingunge Ngombale MwiruMB
- Robert Mboma (Gen. Mstaafu)
- Apson Mwangonda
- Stephen Wassira MB
- Johnson Mwanyika
- Gray S Mgonja
- Nimrod Mkono MB
-
Viongozi wengine wa chama nao washughulikiwe kwa mujibu wa kanuni na taratibu za
chama bila ya kuwaonea haya, kuwavumilia, kuwabeba au kwa namna yoyote ile kuwatafutia
udhuru wa kwanini wasishughulikiwa.
2. Wahusika wakuu wa kashfa hizi zifuatazo washughulikiwe kichama na kiserikali
ikiwemo ni pamoja na kufikishwa mahakamini chini ya sheria ya Mitandao ya Kihalifu
na Uhujumu Uchumi ya 1984. Tunatambua baadhi yao ni wale ambao
tumependekeza hapo juu wawajibike wenyewe kwa kuachilia nafasi za uongozi ndani
ya chama.
· Kashfa ya Loliondo ambapo urithi wa watoto wetu uliuzwa na umeendelea kuuzwa
kwa wageni.
· Kashfa ya IPTL -
· Kashfa ya Commodity Import Support
· Kashfa ya Mgodi wa Kiwira
· Kashfa ya Akaunti ya EPA
· Kashfa ya Meremeta Ltd, Mwananchi Gold, Deep Green Finance, na Tangold
· Kashfa ya Rada
· Kashfa ya Ununuzi wa Airbus
· Kashfa ya Ununuzi wa Gulfstream 500 (ndege ya Rais)
· Kashfa ya Richmond
· Kashfa ya Dowans
· Kashfa ya magari, silaha na helikopta za JWTZ
· Kashfa ya silaha haramu
· Kashfa za madawa ya kulevya
· Kashfa ya uuzwaji wa maeneo wazi
· Kashfa ya misamaha ya kodi ya Alex Stewart
· Kashfa ya Ujenzi wa Minara miwiliya Benki Kuu
· Kashfa ya uuzaji wa maeneo ya ufukwe Dar
Kashfa hizo zote zimetutia aibu kama Watanzania na zaidi pia kama wana CCM ambao
Chama chetu ndiyo kimeunda serikali inayotawala. Hatuwezi kamwe kukubali kwa namna
yoyote ile kuendelea kukaa na wahusika wa kashfa hizo kwa kisingizio au sababu
yoyote ile. Endapo Chama chetu kitaamua kuwavumilia na kuwasafisha wahusika wa
kashfa hizi mbalimbali kwa kisingizio cha kutafuta umoja, mshikamano, na utulivu basi
watakuwa wamepiga kura ya kukimega chama.
Tukinyambua maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere alipoongoza taifa letu kuwa
katika kikundi kimoja na serikali ya Kibaguzi ya Afrika ya Kusini kwenye Jumuiya ya
MadolaMwalimu kupiga kura kuwakubali hawa, ni kupiga kura kutufukuza sisi nasi vile vile
tunatangaza kuwa kuwakubali mafisadi ndani ya chama, ni kufukuza waadilifu
3. Kwa vile kashfa zote hizo na nyingine ambazo hatujazihusisha zinahusiana moja kwa
moja na uchumi wetu tunatoa wito kwa Serikali kuhamishia kesi zote zilizopo sasa
zinazohusiana na hili kwa Mahakama ya Makosa ya Uchumi kwa mujibu wa sheria
hiyo ya 1984. Yaani, Mahakama Kuu ikae kama Mahakama ya Makosa ya Uchumi
kusikiliza kesi hizo. Hatuelewi ni kwanini kesi hizi zote zinashughulikiwa kwa kiasi
kikubwa nje ya sheria hiyo yenye lengo la kudhibiti mitandao ya kihalifu (organized
crime) na uhujumu uchumi (economic sabotage).
4. Tunatoa wito kwa Serikali yetu kurejesha nchini fedha zote ambazo zimehifadhiwa nje
ya nchi na viongozi wa umma wanaobanwa na sheria ya maadili ya 1998. Tunatoa wito
kwa serikali kuomba msaada wa nchi za Uswisi, Costa Rica, UAE na serikali za Isle of
Man, Jersey na sehemu nyingine zinazojulikana kwa kuficha taarifa za kodi (tax
heavens) ili kuweza kutambua Watanzania ambao kutokana na nafasi zao za utumishi
wa umma wamejirundikia mabilioni ya fedha zetu huko ugenini katika jitihada za
kukwepa kulipia kodi hapa nchini au kuelezea vyanzo vya mapato hayo.
5. Mkutano Mkuu wa Chama baadaye mwaka huu pamoja na ajenda nyingine
uendelezea mabadiliko katika namna ya kupata viongozi hususan katika nafasi ya
Urais. Kwa miaka kadhaa sasa tumeona mizengwe ikifanyika na kutumika katika
nafasi hiyo. Tukitambua na kuheshimu mabadiliko ya namna ya kuwapata wagombea
wa Ubunge tunaamini mabadiliko hayo hayatoshi pasipo kufanya mabadiliko vile vile
katika namna ya kumpata mgombea wa nafasi ya Urais.
Hivyo basi, tunapendekeza mfumo wa wagombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya
chama chetu kushindanishwa kwa ajenda zao mbele ya wanachama katika kura
mbalimbali za maoni mikoani na hatimaye wale ambao watakuwa wanaonekana
kukubalika katika mfumo ambao unaweza kubuniwa ndio watapigiwa kura na mkutano
mkuu kugombea nafasi hiyo.
Mtindo wa kuachia Halmashauri Kuu na Kamati Kuu kuamua jina la nani liletwe
kwenye mkutano mkuu umepitwa na wakati. Tutengeneze mfumo ambao utawachuja
wagombea pamoja na wagombea wenza katika ngazi za chini na hatimaye Mkutano
Mkuu ndio utachagua timu ya wagombea wake kwa kuangalia ajenda zao kwa taifa.
Timu ya wagombea ambao ajenda yao inakubalika na kuchaguliwa kuwa wagombea
kwa niaba ya Chama chetu basi ajenda yao ndiyo inaunda Ilani ya Uchaguzi. Mtindo
kama huu ndio unatumika nchini Marekani na kwenye nchi nyingine nyingi zenye
kufuata demokrasia ya kweli.
Kwa kufanya hivi tunaamini tutafungua nafasi kubwa ya mawazo, mipango, na hoja
nzuri zaidi na kutoa nafasi hata kwa wana CCM ambao hawana majina makubwa lakini
wenye mawazo bora zaidi na yanayofaa katika kuongoza mabadiliko. Tunaamini kuwa
bila ya kubadilisha namna ambayo mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama chetu
anapatikana hatuwezi kwa kiasi kikubwa kuondoa mwonekano wa kubebwa na
kupendelewa unaoweza kutokea au mbinu chafu kutumika.
Mwisho.
Tunaona yatupasa turudie tena maneno yale ya hekima kutoka katika Azimio la Arusha:
Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha
kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka
mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena.
Hatutaki kuonewa tena, hatutaki kunyonywa tena, na hatutaki kupuuzwa tena. Tunataka
mabadiliko, mabadiliko ambayo Watanzania wenyewe wanayastahili na watayaongoza
kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010 na baadaye. Mabadiliko ambayo yatafungua ukurasa mpya
wa mafanikio kwa kizazi cha sasa cha Watanzania na kizazi cha baadaye.
Wapiganaji CCM
Wapiganajiccm@yahoo.com