Taasisi ya MOI yasema inatoa msamaha wa Tsh. Bilioni 3 kila mwaka kwa wagonjwa wanaokosa gharama za matibabu

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kupitia Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Prof. Charles Mkony wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwapunguzia deni ambalo wanadaiwa kutokana na msamaha wa gharama za matibabu kwa baadhi ya wagonjwa ambao wamepatiwa huduma na kushindwa kulipia.
photo_2023-11-28_18-19-02.jpg
Akizunguza Novemba 28, 2023 katika hafla ya uzinduzi miradi mbalimbali ya utoaji wa huduma, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya MOI, Prof. Charles Mkony amesema kuwa taasisi hiyo kwa mwaka imekuwa na wastani wa kiasi cha Shilingi Bilioni tatu ambacho deni la msamaha wa gharama za matibabu kwa wagonjwa wanaoishi maisha duni, lakini amedai kuwa kumekuwepo na msahama hata kwa ambao wapo nje ya vigezo.
photo_2023-11-28_18-19-03.jpg
"Katika kutoa huduma hapa MOI tunaendelea kukabiliwa na changamoto ya misamaha ya gharama za matibabu kwa wagonjwa, wakiwemo wasio kuwa na vigezo vya kupewa msamaha jambo ambalo linasababisha madeni kwa taasisi, kwa kuwa matibabu mengi yanahitajika upandikizi na dawa ambavyo ni gharama kubwa na wadhabuni wanaotuuzia vifaa hivyo wanaendelea kutudai, wagonjwa wengi wanaoomba msamaha ni wagonjwa wananchi wenye kipato duni," amesema Prof. Charles.

Amesema "Kwa taarifa zilizopo kiasi cha msamaha kinachotolewa kwa mwaka ni wastani wa Bilioni tatu. Tunaomba Mh. Waziri (Ummy Mwalimu) utusaidie kuona uwezekano wa Serikali kuipunguzia taasisi hii mzigo wa deni kwa msamaha wa gharama za matibabu."

Amesema kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikiwahudumia wananchi wa aina zote katika jamii ikiwemo watu wanaopata ajali mbalimbali ikiwemo bodaboda.
photo_2023-11-28_18-19-05 (2).jpg

photo_2023-11-28_18-19-05.jpg
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi huo amesema suala hilo linaelekea kupata utatuzi kwa kuwa tayari Serikali inaelekea kutekeleza suala la Bima ya Afya kwa wote ambalo tayari limepitishwa na Bunge.

Aidha, Waziri Ummy amewataka wananchi kuamini na kutumia Taasisi ya MOI kupata matibabu ambayo awali walikuwa wanaweza kutumia gharama kubwa kuyafuata nje ya Nchi.

Amesema huduma ya kimataifa na watu maalum ambayo wameiziduliwa MOI ni jawabu kwa baadhi ya watu ambao walikuwa wanatamani kupata huduma hiyo kwa uharaka na katika mazingira rafiki zaidi.

Mradi wa kliniki mpya ya wagonjwa maalumu wa kimataifa (premier and international service) umezinduliwa na Ummy, ambaye ametoa wito kwa wadau mbalimbali ikiwemo wabunge, wafanyabiashara wenye uhitaji wa huduma kutumia kliniki hiyo.
photo_2023-11-28_18-19-04.jpg
Amepongeza kuanzishwa kwa kliniki hiyo ambayo amedai itakuwa na tija kwa wananchi ndani na nje ya Nchi hususani Ukanda wa Afrika Mashariki.

"Niwapongeze MOI kwa kliniki hii na wagonjwa maalum na wagonjwa wa kimataifa itakuwa kliniki ya mfano ambayo itavutia wagonjwa kutoka Nchi mbalimbali, pia itavutia Watanzania wengi ambao wanataka huduma za haraka mtu ana shughuli zake ndani ya masaa matatu anataka atoke," amesema.

Hata hivyo, amewahasa watendaji MOI wakiongozwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Prof. Abel Makubi kujikita kwenye huduma ya ubobezi badala yake huduma nyingine mfano za mapokezi waziendeshe kwa ubia na wadau mfano kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa wanaokuja kupata tiba wakitokea nje ya Nchi.

"Tunataka mgonjwa apokelewe vizuri kutokea uwanja wa ndege sio kazi yenu MOI mnaweza kuingia ubia na wadau nyie mkabaki na huduma ya ubobezi."

Pia Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Prof. Paschal Rugajo amepongeza jitihada za Serikali kuifanya MOI kuendelea kutoa huduma kwa vifaa vya kisasa, ambapo amesema kuwa kwa sasa jukumu lilopo ni kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Pia, Abbas Tarimba Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Ilala, ambaye ni Naibu Spika Mussa Azzan Zungu amepongeza jitihada zinazofanywa na MOI kupitia Mkurugenzi wake, Prof. Makubi, watendaji wengine pamoja na Wizara ya Afya inayoongozwa na Waziri Ummy Mwalimu kwa kutekeleza mambo ambayo amedai ni alama.

Tarimba amesema "Tanzania yawezekana kabisa tuna tatizo la kuchagua aina ya watu wa kuongoza taasisi kiasi kwamba wakafanya mambo wakayaweka na kizazi kingine kikaja kuyaona mambo mazuri."

Amesisitiza huduma zinazotolewa MOI ni huduma bora ambazo hata wataalam wa nje wamekuwa wakipongeza, hivyo ametoa rai kwa Serikali na wadau kuendelea kuinga mkono MOI ili iendelee kutoa huduma katika ubora zaidi kupitia wataalamu wenye uweledi na vifaa vya kisasa.

Miradi na miundombinu mipya iliyozinduliwa na kukaguliwa na Waziri Ummy ni mradi wa kliniki mpya ya wagonjwa maalumu wa kimataifa (premier and international service), eneo la wateja kusubiria huduma katika eneo la EMD (MOI Clients' lounge), Uzinduzi wa Mashine mpya za MRI, uzinduzi wa Mashine mpya za CT SCAN , uzinduzi wa miongozo standard operating procedures (SOPS) na MOI Hospital Formula.

Prof. Makubi ambaye ana kipindi cha kisichozidi miezi sita tangu ateuliwe katika nafasi yake, amesema vifaa hiyo vina ubora wa kimataifa na kuwa vitaongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa huduma kwa uharaka na ubora zaidi.
 
Back
Top Bottom