Doctor Mama Amon
Platinum Member
- Mar 30, 2018
- 2,311
- 3,490
John Mrema (Kushoto) Freeman Mbowe (Kulia)
I. Utangulizi
Kundi la watiania 55 ndani ya Chadema, wakiongozwa na John Mrema, limethibitisha kwamba hoja za kikambi zilizoibuka wakati wa uchaguzi ndani ya Chadema bado zinaendelezwa na Timu Mbowe.
Hoja mojawapo ilikuwa kwamba Lissu hafai kuwa Mwenyekiti kwa kuwa hana fedha ya kuongoza Chadema. Hii ilikuwa ni hoja ya Kambi ya Freeman Mbowe.
Sasa John Mrema na wenzake wanaendeleza hoja hii. Wanadai kuwa mkakati wa "Bila Mabadiliko Hakuna Uchaguzi" utainyima Chadema rasilimali fedha kutoka kwa wagombea ambazo zingesaidia katika ujenzi wa Chadema.
Kwa miaka kadhaa, John Mrema, akiwa Kiongozi wa Kitaifa na wakati mwingine Mkurugenzi wa Uchaguzi, ametekeleza sera hii ya "Mwenye fedha ndiye mwenye haki ya kugombea."
Mrema alifikia hatua anawaita watia nia makao makuu ili wakichangie chama. Hakuna senti inapelekwa majimboni. Na mtiania asiyechanga jina lake lilikatwa.
Lakini kina Mrema wanasahau kuwa kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani zinafanyika kwa siku 70 pekee, kati ya siku 1,825 za kujenga chama, sawa na 4% ya muda wa miaka mitano .
Wanasahau kwamba mtaji wa kujenga chama ni buku buku za wapiga kura wanaotarajiwa kuleta ushindi, wakiwa wanachangia chama kwa kutumia kanuni ya "tone tone."
Wanasahau kuwa mgombea ubunge anabeba mzigo mkubwa jimboni ikiwemo kuwabeba wagombea udiwani. Bado wanamfyonza fedha tu!
Na wanasahau kwamba, ndani ya siku 70 za uchaguzi kigezo cha kifedha cha ufanisi wa kampeni za uchaguzi (financial performance indicator) ni kiasi cha dola zitakazotumika kwa kila mpiga kura mtarajiwa (dollar per registered voter).
Mfano, katika jimbo lenye wapiga kura laki moja na nusu (150,000), kama wastani wa bajeti ya uchaguzi kwa kila mpiga kura ni dola moja, basi, zinahitajika dola 150,000 sawa na TZS 405,000,000.
Hii ni fedha ambayo haiwezi kutoka mfukoni kwa mtu mmoja pekee, yaani mgombea ubunge.
Bahati nzuri, sasa Tundu Lissu amepiga marufuku sera hizi za "wanasiasa wabenzi."
Lissu ameshinda uenyekiti kutokana na kura za "wabangaizaji" wenzake waliomchangia kwa kutumia kanuni ya "tone tone" na anasema kuwa ataendesha chama kutokana na kanuni hiyo.
Zama za siasa za wabenzi ndani ya Chadema zimekufa siku Mbowe alipokabidhi Chama. Mwenye masikio na asikie.
Ukweli ni kwamba hoja zao zimeshajibiwa kwa ukamilifu na kubomolewa kabisa. Majibu ya Mwenyekiti Tundu Lissu kwa kelele za kina John Mrema yako hapa chini.
II. Sababu za Kina Mrema kuunga mkono uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025
Kina Mrema wanadai kwamba wanapinga mpango wa Chadema wa kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 kabla ya mabadiliko ya kimfumo kwa sababu zifuatazo:
- Ajenda ya "No Reforms, No Elections" iliyoasisiwa na vikao vya Chadema haijumuishi kipengele cha kuzuia uchaguzi mkuu, bali inalenga kutengeneza shinikizo la kisiasa bila kudhamiria kuzuia au kususia uchaguzi.;
- Chadema haina uwezo kuzuia uchaguzi wakati iko nje ya mchakato wa uchaguzi;
- Tumekwishafeli kuzuia uchaguzi maana tayari mchakato wa kutekeleza uchaguzi umeshaanza na uandikishaji wapiga kura pamoja na kugawanya majimbo;
- Mpaka sasa vyama vyote vya siasa, madhehebu makubwa ya dini na asasi za kiraia hawaungi mkono ajenda yetu ya kuzuia uchaguzi mkuu; na
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi ni mkakati ulio kinyume cha katiba ya Chadema na unapingana na kanuni zake.
- Kususia uchaguzi kutaifanya Chadema kukosa ruzuku, ambao ni mkakati wa uhakika wa kuinua mapato ya chama kuliko ulivyo mkakati wa tone tone, na hivyo chama kushindwa kujiendesha.
- Mazingira ya uchaguzi yasiyo rafiki kwa vyama vya upizani, yaliyopo sasa hivi, yanaweza kutumiwa na Chadema kuishinda CCM katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
- Mkakati wa "No Reform No Election" utainyima Chadema fedha kutoka kwa baadhi ya wagombea ambazo zingetumika kujenga chama wakati wa uchaguzi, maana watia nia watakata tamaa ya kuwekeza kwenye chama.
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi ni mkakati ulio kinyume cha katiba ya nchi na unapingana na sheria za Tanzania.
- Hakuna uwezekano wa kutekeleza ajenda hii kwa ufanisi katika muda mfupi uliobaki kabla ya Oktoba 2025.
- Kwa ajili ya kulinda uhai wa Chadema, mabadiliko yanao umuhimu lakini hayana uharaka, wakati uchaguzi unao umuhimu na uharaka, kwa maana kwamba Chadema inapaswa kutekeleza mkakati wa "Ama Kupigania Mabadiliko au Uchaguzi" lakini sio kutekeleza mikakati yote miwili kwa mpigo.
- Japo lengo kuu la Chadema ni kushiriki uchaguzi ili kuitoa CCM madarakani bado tunapaswa kuwa tayari kushiriki uchaguzi ili kupigania hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Mabarza ya Madiwani.
III. Majibu ya Lissu kwa hoja za Kina Mrema
Hoja zote za Kina Mrema tayari zimeshajibiwa na Lissu, hasa kupitia mkutano na watia nia uliofanyika makao makuu ya Chadema tarehe 03 Aprili 2025. Majibu ya Lissu yako hivi:
- Ajenda ya "No Reforms, No Elections" iliyoasisiwa na vikao vya Chadema inajumuishi kipengele cha kuzuia uchaguzi mkuu, kwani maneno "no elections" yanamaanisha "hakuna uchaguzi" na ili uchaguzi usiwepo inabidi uzuiwe;
- Chadema inao uwezo kuzuia uchaguzi wakati iko nje ya mchakato wa uchaguzi kwa sababu ipo ndani ya Tanzania mahali ambako uchaguzi unapaswa kufanyika;
- Ni kweli hatujazuia uandikishaji wapiga kura wala kugawanywa kwa majimbo lakini bado tunayo nafasi ya kuziia hatua za mchakato wa uchaguzi zinazofuata;
- Mpaka sasa Chadema tunaendelea na mkakati wa public engagement kwa njia ya mikutano ya nje na ndani tukivilenga vyama vyote vya siasa, madhehebu makubwa ya dini na asasi za kiraia, na hivyo sio sahihi kwa sasa kusema makundi haya hayaungi mkono ajenda yetu ya kuzuia uchaguzi mkuu; na ushahid wa kuungwa mkono unaanza kuibuka, mfano ni chapisho katika gazeti la Pambazuko (Toleo la JUmatatu, 7 Aprili 2025) lisemalo "Bunge Lisifungwe."
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi sio mkakati ulio kinyume cha katiba ya Chadema na haupingani na kanuni zake kwani kusogeza mbele ratiba ya uchaguzi kutatoa fursa bora zaidi ya kutekeleza katiba ya Chadema.
- Ni kweli kwamba kususia na/au kuzuia uchaguzi kutaifanya Chadema kukosa ruzuku, lakini sio kweli kwamba kwa sasa ruzuku ni mkakati wa uhakika wa kuinua mapato ya chama kuliko ulivyo mkakati wetu wa tone tone, maana yamkini ya kushinda uchaguzi katika mazingira ya sasa ni karibu na zero.
- Kwa mujibu wa ushahidi kutokana na uchaguzi wa 2015, 2019, 2020 na 2024, mazingira ya uchaguzi yasiyo rafiki kwa vyama vya upizani, yaliyopo sasa hivi, hayawezi kutumiwa na Chadema kuishinda CCM katika uchaguzi wa Oktoba 2025.
- Kweli, Mkakati wa "No Reform No Election" utainyima Chadema fedha kutoka kwa baadhi ya wagombea ambazo zingetumika kujenga chama wakati wa uchaguzi, lakini chama hakijengwi kwa siku 70 za uchaguzi, wala sio sera ya chama kwamba tutatumia fedha za wagombea kujenga chama, maana kazi ya mgombea ni kunadi sera jukwaani.
- Mkakati wa "No reform, No elections" kwa ajili ya kushinikiza kutokufanyika kwa uchaguzi sio mkakati ulio kinyume cha katiba ya nchi na unapingana na sheria za Tanzania, kwani mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, kuwasiliana na wadau, na hatua kama hizo zinakubalika kikatiba na kisheria.
- Ni kweli hakuna uwezekano wa kutekeleza ajenda hii kwa ufanisi katika muda mfupi uliobaki kabla ya Oktoba 2025, lakini kanuni za uendeshaji wa mradi wa ujasiriadola zinaonyesha kwamba kuna uwezekano wa kusogeza mbele ratiba ya uchaguzi;
- Kwa ajili ya kulinda uhai wa Chadema, mabadiliko yanao umuhimu na yanao uharaka, kama ambavyo uchaguzi unao umuhimu na uharaka, kwa maana kwamba Chadema inapaswa kutekeleza mkakati wa "Kupigania Mabadiliko Pamoja na Uchaguzi" wa mpigo.
- Japo lengo kuu la Chadema ni kushiriki uchaguzi ili kuitoa CCM madarakani bado tunaweza kuamua kuwa tayari kushiriki uchaguzi ili kupigania hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Mabarza ya Madiwani, lakini mfumo wa sasa hauturuhusu hata kupata hadhi hiyo.
Kwa ujumla, njia bora ya kuonyesha ubovu wa hoja ya akina Mrema ni kufafanua majibu ya Tundu Lissu katika matamko namba 9, 10, 11 na 12 hapo juu.
Utetezi wa tamko namba 09: Kuna tofauti kati ya uchochezi haramu na uchochezi halali
Ukweli ni kwamba kampeni hii ni uchochezi halali kwa ajili ya kuleta mabadiliko halali kwa mujibu wa katiba na sheria za Tanzania.
Kwa mujibu wa Katiba (1977), kila raia anayo haki ya kukusanyika, kuandamana, kufanya mikutano ya ndani na nje, na kufanya mawasiliano na wenzake kadiri anavyo taka.
Kwa usahihi, mikutano ya hadhara na maandamano ni haki ya kikatiba kama ilivyobainishwa chini ya kifungu cha 20 cha Katiba ya 1977 na kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya siasa sura ya 258 Toleo la 2019. Uhuru wa mawasiliano pia umetamkwa kwenye ibara ya 18 ya Katiba yetu.
Na Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 16, Toleo la 2019, inatofautisha kati ya "uasi halali" na "uasi haramu" katika ibara ya 55.
Kuhusu "uasi haramu," yaani "uchochezi haramu," kifungu cha 51(1)(b) kinasema kwamba:
"Nia ya kufanya uchochezi (haramu) ni nia ya: ... kuwatia hamasa wakazi wowote wa Jamhuri ya Muungano ili kuleta mageuzi, kwa njia nyingine isiyo ya halali kuhusu jambo lolote katika Jamhuri ya Muungano lililowekwa na sheria"
Na kuhusu "uasi halali" yaani "uchochezi halali" kifungu cha 51(2)(b) kinasema kwamba:
"Kitendo, hotuba au tangazo halitahesabiwa kuwa ni la uchochezi (haramu) kwa sababu tu linalenga katika: ... kuonyesha makosa au mapungufu katika serikali au Katiba ya Jamhuri ya Muungano au kama ilivyowekwa na sheria, au katika usimamiaji utoaji wa haki kwa lengo kurekebisha makosa hayo au upungufu huo"
Kwa sababu ya vifungu hivi vya kikatiba na kisheria, kampeni ya "No refrorm No Election" ni halali mpaka hapo itakapothibitika vinginevyo.
Utetezi wa tamko namba 10: Mantiki ya kusogeza mbele uchaguzi
Kuhusu tamko la Lissu namba 10 hapo juu, Lissu anaona kuwa kanuni za uendeshaji wa mradi wa ujasiriadola zinaonyesha kwamba kuna uwezekano wa kusogeza mbele ratiba ya uchaguzi. Nafafanua kanuni anazozirejea.
Kwa mujibu wa kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi (project management triangle) kuna vitu vinne ambavyo meneja wa mradi anapaswa kuvisimamia muda wote, Yaani ubora, muda, bajeti na ukubwa wa vipaumbele vya mradi. Kwa Kimombo tunasema "quality, time, budget, and scope."
Kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi
Kwa mujibu wa kanuni ya pembetatu ya usimamizi wa mradi , misingi mine inahusika katika kusimamia mradi wowote, ukiwemo mradi wa kuendesha nchi.
- Mosi, ubora wa mradi ni kitu kimoja kisichopaswa kubadilika (constant);
- Pili, muda, bajeti na ukubwa wa vipaumbele vya mradi ni vitu vitatu vinavyoweza kubadilika (variables) kulingana na matakwa ya meneja wa mradi.
- Tatu, ubora wa mradi unategemea kupatikana kwa fedha ya bajeti iliyopangwa, kupatikana kwa muda wa kutosha kutekeleza mradi na ukubwa wa vipaumbele unaoendana na bajeti na muda.
- Na nne, kwa lengo la kulinda ubora wa mradi, mabadiliko yoyote katika kigezo kimojawapo kati vigezo vitatu vya muda, bajeti na ukubwa wa vipaumbele yanapaswa kuambatana na mabadiliko katika vigezo vingine viwili vilivyobaki.
Kwa mfano, utekelezaji wa mradi utakamilika mapema ama kwa kuongeza bajeti au kupunguza ukubwa wa vipaumbele vya mradi.
Vivyo hivyo, kuongeza ukubwa wa vipaumbele vya mradi kunahitaji ongezeko la bajeti na/au muda. Na kupunguza bajeti bila kuongeza muda wa kutekeleza mradi kunapunguza ubora wa mradi.
Kwa hiyo, kama “Kufanya Mabadiliko ya Mifumo ya uchaguzi” sio kipaumbele katika Mradi wa kuendesha nchi unaotekelezwa na serikali, kama serikali itakibeba kipaumbele hiki, maana yake ni kwamba inapaswa kubadilisha bajeti yake na/au ratiba ya utendaji wa kazi za serikali. Uamuzi wa aina hii utategemea uharaka wa kipaumbele hiki.
Rais Samia anasema kuwa haoni uharaka wa kubadilisha vipaumbele vyake vya sasa kwa kuongeza kipaumbele cha “Kufanya Mabadiliko ya Mifumo ya uchaguzi.” Kina John Mrema wanakubaliana naye.
Lakini Chadema ya Lissu wanasema kwamba “Kufanya Mabadiliko ya Mifumo ya uchaguzi" ni kipaumbele ambacho kina umuhimu na uharaka unaohalalisha mabadiliko kwenye bajeti na ratiba ya mradi wa kuendesha nchi, na kwamba serikali inayo mamlaka ya kurekebisha ratiba ya uchaguzi.
Nakubaliana na kina Lissu kwa sababu nitakazozitaja kwenye hoja inayofuata hapa chini.
Utetezi wa tamko namba 11: Umuhimu na uharaka wa mabadiliko
Kuhusu tamko namba 11 hapo juu, ni maoni yangu kwamba, Wanachojaribu kufanya kina Mrema ni kukataa "kanuni ya umuhimu na uharaka" katika kufanya menejimenti ya muda. Yaani, "importance and urgency principle".
Mara nyingi, kazi zenye umuhimu na uharaka mkubwa ni zile zinazohitajika ili kumwezesha meneja wa mradi kufanikisha malengo aliyonayo kwa mujibu wa mipango wa mradi wenye kuonyesha kazi gani ifanyike lini, nani aifanye, na kwa vipi.
Na mara nyingi, kazi zenye umuhimu na uharaka mdogo ni zile ambazo ziko nje ya mpango wa mradi wenye kuonyesha kazi gani ifanyike lini, nani aifanye, na kwa vipi. Kazi hizi zinaletwa na mtu baki kwa utaratibu wa dharula.
Jedwali la kanuni ya umuhimu na uharaka lifuatalo linaonyesha mahusiano kati ya mambo haya manne:
- Umuhimu mkubwa,
- Umuhimu mdogo,
- Uharaka mkubwa, na
- Uharaka mdogo.
Kutokana na jedwali hili, ni wazi kuwa, kazi zote zinazofanyika hapa duniani zinaweza kugawanywa katika kundi mojawapo kati ya makundi manne yafuatayo bila kubaki, yaani:
- Kazi yenye umuhimu na uharaka, au
- Kazi yenye umuhimu lakini haina uharaka, au
- Kazi isiyo na umuhimu lakini ina uharaka, au
- Kazi isiyo na umuhimu wala uharaka.
Kwa hiyo, kwa upande mmoja, Rais Samia na Lissu wanakubaliana kuhusu kauli kwamba: kazi ya kazi ya kufanya "Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi" ni yenye umuhimu."
Na kwa upande mwingine, Rais Samia na Lissu wanatofautiana kuhusu kauli kwamba: kazi ya kufanya "Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi" inao uharaka kuliko vipaumbele vingine vya serikaili.
Hivyo, hapa kuna majukumu mawili mbele ya Timu Lissu wanaotaka "Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi", kinyume na anavyofikiri Rais Samia:
- Mosi, Timu Lissu wanapaswa kuonyesha kwa nini kauli ifuatayo, kama inavyotolewa na kina Lissu, ni ya kweli:
- "Kwamba kazi ya kufanya Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi ina uharaka mkubwa kuliko vipaumbele vingine vya serikali."
- Na pili, wanapaswa kuonyesha kwa nini kauli ifuatayo, kama ilivyotolewa na Rais Samia, sio ya kweli,
- "Kwamba, vipaumbele baki vya serikali vina uharaka mkubwa kuliko kazi ya kufanya Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi."
- Bila mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi hakuna uchaguzi wa haki unaoweza kufanyika;
- Pasipo uchaguzi wa haki Tanzania itaendelea kuongozwa na serikali haramu, kwa maana ya serikali inayotokana na mchakato haramu;
- Lakini, Tanzania haipaswi kuendelea kuongozwa na serikali haramu hata kwa siku moja;
- Kwa hiyo, ajenda ya kufanya mabadiliko ya kimfumo kabla ya uchaguzi ni yenye umuhimu na uharaka.
Na kuhusu tamko namba 12 hapo juu, katika muktadha wa vigezo muhimu vya uchaguzi unaoweza kuleta ushindi kwa vyama vya upinzani.
Tunafahamu kuwa, uwezekano wa kushinda uchaguzi hutegemea vigezo (determinants) sita, yaani: (1) mgombea bora, (2) ajenda bora, (3) mtandao wa rasilimali watu wenye kuongea lugha moja kabla na wakati wa kampeni, (4) rasilimali fedha za kutosheleza mahitaji ya kibajeti, (5) wapiga kura wenye kiu ya haki na amani na (6) mfumo wa uchaguzi ulio rafiki kwa wadai wote.
Vigezo hivi sita, vinayo michango yenye uzito tofauti katika kufanikisha ushindi.
Kwa mujibu wa tunayoyajua kuhusu chaguzi za Tanzania tangu 2015 hadi 2024, michango hiyo, katika asilimia zilizo kwenye mabano, ni kama ifuatavyo:
Mgombea bora (5%), ajenda bora (5%), mtandao mpana wa rasilimali watu wenye kuongea lugha moja kabla na wakati wa kampeni (5%), rasilimali fedha na rasilimali vitu za kutosheleza bajeti ya kampeni ya angalau dola moja kwa kila mpiga kura (5%), wapiga kura wenye kiu ya haki na amani (5%), na mfumo wa uchaguzi rafiki (75%).
V. Hitimisho
Kutokana na yaliyosemwa hapo juu, ni hitimisho langu:
- Kwamba, kwa ajili ya kulinda uhai wa Chadema, mabadiliko yanao umuhimu na yanao uharaka, kama ambavyo uchaguzi unao umuhimu na uharaka, kwa maana kwamba Chadema inapaswa kutekeleza mkakati wa "Kupigania Mabadiliko Pamoja na Uchaguzi" wa mpigo.
- Na kwamba, japo lengo kuu la Chadema ni kushiriki uchaguzi ili kuitoa CCM madarakani bado tunaweza kuamua kuwa tayari kushiriki uchaguzi ili kupigania hadhi ya kuwa chama kikuu cha upinzani katika vikao vya maamuzi kama vile Bunge na Mabarza ya Madiwani, lakini mfumo wa sasa hauturuhusu hata kupata hadhi hiyo.