Taxi (145)
“Ofisa, kama umekuja hapa kwa sababu ya hilo basi jua sina chochote cha kukusaidia,” Mr. Oduya alisema huku akimtazama Inspekta Abel kwa makini na kuyatuliza macho yake kwenye uso wake.
“Waweza kuniambia, inakuwaje wafanyakazi watatu wa kampuni zako wakauawa kwa risasi katika usiku mmoja, wawili wakiwa ndani ya nyumba moja, tena nyumba ya mmojawao? Je, walikuwa na ugomvi na mtu yeyote?” Inspekta Abel aliuliza huku akiwa ameyatuliza macho yake usoni kwa Mr. Oduya.
Mr. Oduya alimtazama Inspekta Abel kwa kitambo kidogo kisha akatingisha kichwa chake kulia na kushoto taratibu, “Hayo siwezi kuyafahamu. Walikuwa na maisha yao binafsi nje ya kazi, mimi siwezi kujua, samahani kwa hilo.”
Inspekta Abel aliachia tabasamu kisha akakohoa kidogo kusafisha koo lake kabla hajauliza, “Mr. Oduya, unaweza kuniambia hadi sasa umechukua hatua zipi, hata kuomba uchunguzi baada ya kupokea taarifa za vifo vyao? Kumbuka ndugu wa marehemu wanataka uchunguzi ufanyike...”
“Bwana Inspekta, mimi ni Mwenyekiti Mtendaji wa
The Splendid Group, kampuni hii ina kampuni kubwa ishirini chini yake na zote zina wakurugenzi watendaji na mameneja, siyo jukumu langu kuchukua hatua za moja kwa moja kwa wafanyazi kwani sina ‘
link’ ya moja kwa moja na wao. Mimi ni mmiliki lakini wao wana viongozi wao,” Mr. Oduya alisema kwa sauti tulivu na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Ni kweli wana viongozi wao ambao ni waajiriwa wako, kwani wewe ndiye mmiliki... kumbuka wana ndugu na wategemezi wao ambao walikuwa wanawategemea!” Inspekta Abel alisema, kisha kukawa na ukimya wa kitambo fulani kabla ya Inspekta Abel kuuvunja ule ukimya, “Na vipi kuhusu tetesi kwamba kampuni yako inawatenga ndugu wa marehemu?”
“Sijapokea malalamiko kama hayo, sijui wewe umeyapata wapi?” Mr. Oduya aliuliza huku akimtazama Inspekta Abel kwa mshangao.
“Wenyewe wanasema kuwa wanatengwa...” Inspekta Abel alisema na kuongeza, “
anyway... tuyaache hayo, pia kuna mwanamume mmoja anaitwa Casmir Njoroge ambaye amejeruhiwa kwenye ajali ya taxi iliyogonga nyumba usiku wa kuamkia leo huko Sinza Mori na baadaye kukimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala. Je. Unamfahamu vipi huyu bwana?”
“Hadi sasa sifahamu chochote kuhusu mtu anayeitwa Casmir Njoroge aliyejeruhiwa kwenye ajali ya taxi, labda yeye amekwambia chochote kuhusu mimi?” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti tulivu huku akijitahidi kuifanya sauti yake iwe ya kawaida.
“Hapana, kusema ukweli Casmir hakutwambia chochote kuhusu wewe kwani yupo chumba cha wagonjwa mahututi na hawezi kuongea, ila kuna watu wawili wamemtambua kuwa walimwona akifika na kuingia kwenye kichochoro cha nyumba ya Sammy kule Tabata Chang’ombe dakika tano tu kabla hajatoka na bomu kulipuka,” Inspekta Abel alisema huku akiilamba midomo yake.
“Sasa, labda mimi nahusikaje na mtu huyu anayehusishwa na ugaidi?” Mr. Oduya aliuliza kwa sauti iliyoonesha kuwa alikwisha anza kushindwa kuidhibiti hasira yake.
“Katika uchunguzi wetu tumegundua kuwa Casmir Njoroge anatokea nchi jirani ya Kenya na anao uhusiano wa karibu sana na mfanyakazi wako Silas Potela, kwani wote wanatoka Kenya na waliwahi kuhusishwa na vikundi vya uhalifu nchini humo, hasa kikundi cha Mungiki,” Inspekta Abel alisema huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.
“Bado sijaelewa, inspekta, mimi nahusikaje hapo? Silas Potela ni mfanyakazi wangu, historia yake ya yote aliyoyafanya Kenya enzi hizo hayanihusu kwa kuwa hapa kwangu anafanya kazi vizuri na ana tabia njema, pia sina uwezo wa kumzuia mfanyakazi wangu yeyote kuwa na uhusiano na mtu mwingine hata kama mtu huyo ana historia ya uhalifu huko alikotoka. Sidhani kama ni sahihi kunituhumu kwa jambo hili, bwana inspekta!” Mr. Oduya alisema kwa msisitizo huku macho yake yakiwaka kwa hasira.
“Wala hakuna mtu anayekutuhumu, bwana mkubwa... nilidhani ipo haja ya kukuona ili nipate maelezo yako juu ya kuhusishwa kwa vijana wako na matukio ya hivi karibuni ya uhalifu...” Inspekta Abel alisema na kunyamaza kidogo, akameza mate kutowesha koo lake.
“Tumegundua kuwa kwa siku za karibuni yamekuwepo mawasiliano ya simu kati ya Casmir Njoroge na wafanyakazi wako wawili, Silas Potela na dereva wako Madjid Chege, ambaye pia ana asili ya Kenya! Mawasiliano hayo yamemhusisha pia mtu mwingine kutoka Kenya, Robert Kamau, na tunadhani pia yumo humu nchini,” Inspekta Abel aliongeza huku akimtazama Mr. Oduya kwa makini.
“Inspekta, naona sasa unaanza kuvuka mipaka! Nimeshakwambia sihusiki na chochote kuhusu maisha binafsi ya wafanyakazi wangu lakini hutaki kunielewa!” Mr. Oduya alisema kwa kufoka. Kama sauti yake ilivyobadilika, sura yake pia ilikuwa imebadilika.
Kitambo cha sekunde kadhaa za ukimya kilipita, walibaki wakitumbuliana macho kwa namna ya kusomana mawazo yao. Kisha, taratibu tabasamu jipya lilianza kuchanua usoni kwa Mr. Oduya. Halikuwa tabasamu lile ambalo Inspekta Abel alilizoea. Hili lilikuwa tabasamu jembamba, lisilopendeza hata kidogo, tabasamu ambalo lilifuatiwa na swali, “Bado tu unataka maelezo zaidi, bwana inspekta?”
“Vifo vya watu watatu wanaokuhusu vimetokea, mmoja wao ametambuliwa kuhusika na uvamizi kwenye nyumba ya Sammy. Mwingine tena anayehusishwa na watu wako anapata ajali ya kutatanisha, pia amehusishwa kulipua nyumba ya Sammy. Kama unadhani utaweza kuwa na jambo la kuniambia, basi utanitafuta,” Inspekta Abel alisema na kunyanyuka.
Alisimama akamtazama Mr. Oduya kwa kitambo na kuachia tabasamu, “Natumai kupata msaada toka kwako, mzee wangu.” Akasema na kuanza kupiga hatua kuondoka huku akimwacha Mr. Oduya ameketi kimya akimsindikiza kwa macho makali wakati akitoka nje ya ofisi yake.
Mambo bado ni 🔥🔥🔥. Kule Tunu huku Inspekta Abel. Je, Mr. Oduya atafanyaje ili kujinasua? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua...
NB:
Litro 👩