Taxi - (136)
Akiwa bado amezama kwenye lindi la fikra nzito alishtushwa toka kwenye mawazo yake baada ya mlango wa ofisi yake kugongwa mara moja na kisha kufunguliwa, askari wake wawili machachari wakaingia. Hawa walikuwa Inspekta Abel na Sajenti Mapunda ambao walipoingia walisimama mbele ya meza yake kwa ukakamavu na kupiga saluti.
“Vipi, umepata kitu?” Naibu Kamishna Ramon Mamboleo aliuliza mara baada ya kujibu ile salamu huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Inspekta Abel. Muda huo alikuwa amesimama kandokando ya meza yake akiwa ameshika kiuno. Uso wake ulikuwa bado umemezwa na fikra na sononeko.
“Ndiyo, afande!” Inspekta Abel aliitikia kwa ukakamavu huku akinyoosha mkono wake kumkabidhi Naibu Kamishna Ramon Mamboleo faili dogo lenye taarifa za uchunguzi alilokuwa amelishika mkononi.
Naibu Kamishna Ramon Mamboleo alilipokea lile faili kisha akaketi kwenye kiti chake huku akiwaashiria wale askari waketi. Wote wakaketi kwenye viti vilivyokuwa vinatazamana vikiwa mbele ya meza ya Naibu Kamishna Ramon Mamboleo.
Mamboleo alilifungua lile faili, akajiegemeza kwenye kiti chake na kupitia harakaharaka lakini kwa umakini mkubwa ile taarifa kisha akaziangalia nyaraka zingine kutoka kampuni ya mawasiliano iliyoonesha namba zote za simu alizopigiwa Sammy na ujumbe mfupi aliotumiwa, kisha akaziangalia picha kadhaa zilizokuwa zimeambatanishwa na taarifa ile na kuachia tabasamu. Ingalau sasa alikuwa amepata cha kuelezea, na pia mahali pazuri pa kuanzia. Ilikuwa ni kheri kwake, askari ambao aliwapa kazi ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo walipata kitu cha ziada ndani ya muda mfupi.
Baada ya kuipitia taarifa ile kwa takriban dakika ishirini, Naibu Kamishna Ramon Mamboleo alitulia kwa dakika zipatazo mbili, akavuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.
“Ingalau tumepata pa kuanzia, hata hivyo, bado nawahitaji sasa mchimbue zaidi, hawa wote waliohusishwa humu nataka wahojiwe na wale mtakaohisi kuhusika muwatie ndani,” Naibu Kamishna Ramon Mamboleo alisema huku akilifunga lile faili.
“Sawa, afande!” Inspekta Abel aliitikia kwa sauti ya ukakamavu.
Naibu Kamishna Ramon Mamboleo aliinuka na hapo hapo Inspekta Abel na Sajenti Mapunda nao wakainuka na kusimama kwa ukakamavu. Wakapeana mikono na kuagana.
* * * * *
“Vyote ni shilingi laki moja na elfu thetathini na tano tu,” mhudumu mmoja wa kike alisema akimtazama Tom kwa makini. Hayo yalitokea ndani ya ‘
supermarket’ kubwa iliyopo kwenye majengo ya
Mlimani City eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo Tom alikwenda kujipatia mahitaji muhimu kwa ajili yake na Tunu.
Baada ya kutajiwa kiasi, Tom alizama mfukoni na kutoa
wallet yake, akahesabu kiasi hicho cha fedha na kumkabidhi yule mhudumu na kupewa risiti yake, akaaga na kuanza kupiga hatua kutoka huku akisukuma torori dogo lililojaa bidhaa mbalimbali ambazo zilikuwa zimefungashwa ndani ya mifuko yenye chapa ya jina la ‘supermarket’ hiyo. Tom alikuwa bado amevalia suti nyeusi, kofia na miwani myeusi ya jua.
Wakati akitoka kulifuata gari lake lililokuwa limeegeshwa katika viunga vya maegesho ya magari ndani ya uzio wenye ulinzi wa Mlimani City, aliyazungusha macho yake kutazama pande zote kabla hajajivuta taratibu kuelekea kilipo chombo chake cha usafiri. Muda huohuo simu yake ya mkononi ikaanza kuita, Tom aliiangalia kwa makini na kuliona jina la Tunu, akashusha pumzi na kuipokea.
“Hello!”
“Tom, usije tena, nimewasiliana na Bob Chopa na tumekubaliana kuwa kwa sababu za kiusalama yeye ndiye atanifuata huku, halafu wewe tutakutana Kinyerezi. Sijui wewe umefikia wapi?” Tunu aliuliza kwa sauti iliyoonesha furaha isiyo kifani.
“Nimefanikiwa, sasa ndo natoka hapa Mlimani City,” Tom alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.
“Una uhakika kila kitu kiko sawa? Hakuna shaka yoyote?” Tunu aliuliza kwa shauku.
“
Yeah, hali ni shwari ila kama kitatokea chochote nitakujulisha,” Tom alisema huku akiyazungusha macho yake pembe zote kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote aliyemtilia shaka.
“Basi nitakukuta huko kuanzia saa mbili usiku, itanibidi kwanza nipitie nyumbani kwangu Sinza nika...” Tunu alijibu.
“Kuwa makini sana, kuna watu wamewekwa huko kukusubiria,” Tom alimuasa Tunu.
“Usihofu, Tom, ninajua... huu ni mchezo mdogo sana kwangu, wenyewe watashangaa na roho zao,” Tunu alisema huku akiangua kicheko hafifu.
“Na vipi kuhusu gari?”
“Wacha likae palepale Elli’s, lipo mahali salama.”
“
Okay, see you later,” Tom alisema huku akilifikia gari lake aina ya
Toyota Rav4 L jeupe, akazungusha tena macho yake pembe zote kuangalia kama kulikuwa na mtu yeyote aliyekuwa akimfuatilia, hakumwona.
“
See you,” Tunu alisema na kukata simu.
Tom akafungua kwanza mlango wa nyuma wa gari na kutia mizigo yake huko kisha akaelekea kwenye mlango wa dereva na kuufungua akaingia na kuketi halafu akatia gari moto. Alitokea kwenye geti la upande wa kaskazini kwenye barabara ya Survey, kisha akaingia upande wa kulia akiifuata barabara ya Survey. Ikapita kama sekunde tano tu, gari lingine aina ya
Toyota Hilux double cabin la rangi ya bluu lililokuwa na namba bandia ambalo pia lilikuwapo kwenye viunga vya maegesho ya Mlimani City, nalo likatoka kumfuata.
Tom pasipo kujua akaendelea na safari yake, aliufikia mzunguko wa barabara za Sam Nujoma na ile ya Survey na kuingia kulia akiifuata barabara ya Sam Nujoma. Alipoifikia barabara ya Igesa iliyokuwa inakwenda kutokea Sinza akaburini, Tom akaamua kupima upepo ili aone kama kulikuwa na gari lolote lililokuwa limemuungia mkia nyuma, hivyo akakunja kushoto kuifuata barabara ile.
Lile gari aina ya
Toyota Hilux double cabin la rangi ya bluu lililokuwa nyuma yake likiyaacha magari matatu katikati yao nalo likakunja kuelekea barabara ile, Tom akaanza kupata shaka kwamba huenda alikuwa anafuatiliwa. Kwa kutazama vioo saidizi vya pembeni vya gari lake alipata kuliona gari lile vizuri, akakumbuka kuwa alikuwa ameliona pale kwenye viunga vya maegesho ya Mlimani City.
Akaamua kuongeza kasi ya gari lake ili kuona kama na wao wangeweza kuongeza mwendo. Alipotazama tena kwenye vioo saidizi vya pembeni akaliona lile gari nalo likiongeza mwendo huku likijaribu kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake. Sasa Tom hakuwa na shaka kuwa alikuwa anafatwa. Akaona afanye jambo ili kuwapoteza.
Inaendelea...
NB:
Litro 👩