Taxi - (127)
ILIPOISHIA
Wakati wakikaribia kwenye fremu za maduka yanayozunguka Kanisa la Anglikana, Tunu alitoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi na kuzirushia mbele kwa dereva, “Ukifika mtaa wa Moshi kunja kulia na kuufuata mtaa huo, kisha punguza kidogo mwendo, nishuke halafu wewe ongeza mwendo ili kuwapoteza, sawa?”
Yule dereva aliitikia kwa kichwa huku akilitupia jicho lile gari lililokuwa nyuma yao. Akakunja kuingia kulia akiufuata mtaa wa Moshi huku akimkwepa mtoto mmoja aliyekuwa anakatiza barabara. Muda ule ule Tunu aliufungua mlango akashuka haraka na kuusukuma ule mlango, ukajibamiza. Akachepuka na kujibanza nyuma ya mti mmoja mkubwa wa kivuli jirani ya nyumba moja ya wageni.
Lile gari lililokuwa nyuma yao pia liliingia barabara ile lakini kwa kuchelewa kidogo likaongeza mwendo kuifuata ile taxi. Dereva wa taxi aliufikia mtaa wa Arusha na kuuvuka, akaendelea mbele akiifuata barabara ile ya vumbi. Sasa alikusudia kuwafanya wale watu waamini kuwa yule dada alikuwa bado yumo ndani ya ile taxi.
* * * * *
Kwa mara ya kwanza tangu alipoanza harakati zake za kutaka kuingia ikulu, Mr. Oduya alijikuta katika hali ya wasiwasi na mashaka makubwa. Kwa mbali hofu ilikuwa ikitishia kuutawala moyo wake, hasa kwa hisia zilizokuwa zikimnong’oneza kuwa mambo yameanza kumwendea mrama. Alikuwa amekanganyikiwa akiwa ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka ofisini kwake.
ENDELEA...
Mambo hayo hayakuwa yakimwingia kichwani kwake kabisa, alikuwa anajiuliza ni vipi Tunu akafanikiwa kuwatoroka watu wote waliowekwa kumfuatilia? Tena watu wenye ufanisi mkubwa katika kazi hiyo na wenye silaha? Kidogo akawa amejifunza ni mtu wa aina gani alikuwa anasumbuka naye ndiyo maana baadaye aliamua kuwatuma watu maalumu kwa kazi moja tu, kuua. Watu hao walitakiwa kumuua Tunu popote ambapo wangemwona.
Mr. Oduya aliamini kuwa Tunu hakuwa mtu wa kawaida kama alivyokuwa anamchukulia mwanzo, mbaya zaidi, hata yule dereva teksi Tom ambaye walimtegemea kwa shughuli za kuchukua watu wake na kuwakimbiza huku na kule pia alikuwa amejiunga na Tunu!
Sasa Mr. Oduya alianza kujiuliza iwapo aachane na ndoto ile ya urais kisha atoroke nchi na kukimbilia nchini Canada ambako alikuwa amewekeza kwa kiasi kikubwa, akaishi kwa raha mustarehe na mpenzi wake Zainabu, akitumia utajiri wake mkubwa. Hata hivyo, wazo hilo alilipinga kwa kuona kuwa hiyo ilikuwa dalili ya mtu mwoga. Yeye hakuwa mwoga, hivyo alipaswa kupambana hadi dakika ya mwisho.
Kichwa chake kilikuwa kimechemka utadhani ubongo wake uligeuka kuwa
volcano iliyotishia kulipuka wakati wowote, aliuhisi ubongo wake ukiwaka moto na muda wowote kichwa kingelipuka na kusambaratika. Hadi muda huo hakuwa ameambua japo lepe la usingizi, kwa siku mbili mfululizo tangu alipogundua kuwa lile gari aina ya
Cadillac DeVille lenye muundo wa kizamani lilionekana Mzizima TV na sasa lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine.
Kwa kuiamini timu yake iliyoongozwa na Spoiler, Mr. Oduya alitegemea suala la kumpata mmiliki mpya wa lile gari na kuliteketeza lile gari lingekuwa rahisi na kuchukua muda mfupi, lakini tangu kuibuka kwa yule binti, Tunu, ambaye alionekana waziwazi kuanzisha vita ili kumkwamisha, mambo yakaanza kwenda mrama.
Timu yote aliyoitegemea kuifanya kazi hiyo ilionekana kuzidiwa akili na yule binti. Mr. Oduya hakujua Tunu alikuwa ana nini hasa? Ni mara ngapi amejaribu kwa uwezo wake wote kutaka kumtia mkononi lakini binti huyo amekuwa akiikwepa mitego yote na kuwapotea katika mazingira ya utata?
Alikuwa ameketi pale kwenye kiti chake kwa takriban dakika arobaini na tano akiwa hajui afanye nini, hiyo ilikuwa ni baada ya kuongea na vijana wake aliowafokea sana kuhusiana na kitendo cha wao kuendelea kuzidiwa akili na Tunu.
“Ninaomba maelezo mafupi sasa hivi, kwa nini mmeshindwa kumnasa huyo binti?” Mr. Oduya aliwauliza Spoiler, Victor na Job waliokuwa wameketi mbele yake huku wamejiinamia.
Spoiler, Victor na Job waliinua nyuso zao, wakatazamana na Spoiler akawa wa kwanza kusema. “Nadhani, bosi hatutakuwa na maelezo ya kukuridhisha kwa nini hatujafanikiwa kumtia mbaroni hadi sasa, kwa sababu…”
“Ni wazembe tu!” Mr. Oduya alimkatiza Spoiler kwa kufoka, uso kaukunja na kutengeneza ndita usoni. “Au mna sababu nyingine?”
Spoiler aliwatupia jicho Victor na Job mara moja kisha akaketi vema kitini. Alishaanza kuingiwa na hofu iliyochanganyika na woga. Alikuwa na kila sababu ya kujisikia vile. Mr. Oduya alikuwa mtu katili sana asiyeruhusu makosa ya kipumbavu yaliyoashiria uzembe yatokee kwenye kazi zake, ingawa machoni kwa watu alionekana mnyenyekevu na mwenye kusaidia jamii lakini ukweli ni kwamba alikuwa hana tofauti na mnyama yeyote wa porini.
“Siyo wazembe bosi,” Spoiler alisema kwa sauti ya chini.
“Kumbe nini?” Mr. Oduya aliuliza huku akimtolea macho. “Mlishajua kuwa Tunu tayari amekutana na Sammy na kisha akagundua kuwa gari lake limewekwa
GPS device. Hakukuwa tena na sababu ya kuendelea kumwacha akiwa hai, mlikuwa mnasubiri nini, pingu? Sasa amefanikiwa kuwatoroka, mnataka kusema nini? Ni uzembe tu!” Mr. Oduya alifoka.
Victor alishusha pumzi, akawageukia akina Spoiler na Job waliokuwa wanamtumbulia macho Mr. Oduya kwa wasiwasi.
“Inawezekana kweli kuwa ni uzembe wetu, mzee,” Victor alijikakamua na kusema, “lakini hapa tunamzungumzia Tunu Michael, shushushu mbobezi aliyepata mafunzo maalumu ya kijeshi na mwenye shahada ya umahiri ya ujasusi wa mambo ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi, isitoshe ni ninja na kama ilivyo kwa maninja wote ni kama wanatumia nguvu za mizimu…”
“Upumbavu!” Mr. Oduya alisema huku akishusha ngumi nzito mezani iliyowashtua watu wote. “Hatuzungumzii nguvu ya mizimu katika kazi kama hizi, Victor… wewe na Job pia ni mashushushu. Wewe umekaa miaka mitatu nchini Cuba ukijifunza upelelezi wa kisasa na bado unazungumzia nguvu ya mizimu…” Mr. Oduya alikuwa amefura kwelikweli, sasa alikuwa anaongea kama anayetaka kupiga kelele. “Au mlitakaje? Tuwachanje kwanza chale mwilini ndipo mumkamate Tunu?”
Victor alimlaani sana Mr. Oduya kimoyomoyo, alitamani kumtukana kisha ainuke na kuondoka zake lakini akaogopa, kwani yule mzee hakuwa tajiri tu wa kawaida, alikuwa na nguvu kubwa sana serikalini na ndani ya vyombo vya usalama akiaminiwa na watu wengi kama bilionea anayesaidia jamii.
“Hatuhitaji kuchanjwa chale, mzee, hilo tunalijua. Lakini Tunu, si kama unavyomjua… huyu ni shushushu hatari sana aliyepata mafunzo ambayo katika nchi hii wapo wawili tu, mafunzo hayo ndiyo humsaidia kung’amua jambo lolote hatari kabla halijatokea. Sisi si wazembe, kama unavyotutuhumu. Tumefanya kazi ngapi kubwa na za hatari, mzee?” Victor alisema kwa sauti kakamavu iliyoficha hasira ndani yake.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal kuku mweus
NB:
Litro 👩