Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (133)

ILIPOISHIA

Alimtazama kwa makini kwa kumkazia macho. Tunu alimsalimia kisha akajieleza kuwa yeye ni rafiki wa familia ya Elli na alifika hapo kuonana na Victoria. Baada ya maswali mawili matatu hatimaye Victoria aliulizwa na kuwataka wale walinzi wamruhusu Tunu aingie.

Tunu aliruhusiwa kuingia ndani ya ule uzio alikowakuta walinzi wengine wawili. Akapokelelwa na Victoria aliyemshangaa baada ya kuona akiwa hana gari. Tunu alimwabia kuwa alilazimika kuliacha kule kwenye mgahawa wa Elli’s kwa sababu za kiusalama, wakaongozana na kuingia sebuleni alikomkuta Winifrida akiwa amejikuyata kwa huzuni huku akilia kilio cha kwikwi. Winifrida alipomwona Tunu akaanza kulia kwa uchungu mkubwa na kwa sauti ya juu, mwili wote ulikuwa unamtetemeka.

“Winnie!” Tunu aliita huku akimshika Winifrida mikono, akamwinua na kumkumbatia lakini miguu ya Tunu haikuwa na nguvu hata za kusimama. Tunu akamketisha kwenye sofa huku akiketi kando yake na kuanza kumpetipeti mgongoni katika hali ya kumfariji. Winifrida alikuwa amepata taarifa za shambulizi lililomlaza kitandani kaka yake Sammy.

ENDELEA...

Ni kama vile simanzi ilikuwa imezidi baada ya Winifrida kumwona Tunu, hata pale Tunu alipojaribu kumbembeleza na kumfariji bado Winifrida alionekana hakuwa akijiweza kabisa. Kilio chake kilimshtua sana Victoria na kumfanya kuanza kumtilia shaka, alihisi labda lilikuwepo jambo fulani kati yao lililozidisha simanzi ila alikuwa hataki kusema.

Akajiuliza, ni nini ambacho kingeweza kumfanya Winifrida kulia kiasi kile, hasa baada ya kumwona Tunu? Kwa mtazamo wa kawaida, yeyote asingeshindwa kubaini kuwa kulikuwepo na jambo au siri kubwa sana moyoni mwa Winifrida. Mara kwa mara Winifrida alionekana kutaka kumweleza Tunu kitu fulani kilichokuwa moyoni mwake, alifungua mdomo wake kutaka kusema lakini maneno hayakutoka.

Kila alipotaka kusema alihisi donge fulani la uchungu likizidi kumkaba kooni na kumsononesha sana. Victoria aliwatazama kwa makini jinsi walivyokuwa wakifarijiana kama mama na mwanawe.

“Winnie, kwani kuna tatizo gani? Maana naona umebadilika ghafla!” Victoria aliuliza kwa mshangao lakini akashangaa kumwona Winifrida akiinuka na kukimbilia nje, akazunguka kueleka nyuma ya nyumba huku akiendelea kulia kilio cha kwikwi.

Wote wakapigwa na butwaa, walimtazama Winifrida kwa mshangao, kisha wakaangaliana katika hali ya kujaribu kuulizana kitu.

“Kuna nini, mbona sielewi!” Tunu aliuliza kwa mshangao. Victoria akanyanyua mabega yake juu na kuyashusha huku akibetua midomo yake. Kisha akaondoka kumfuata Winifrida kule nyuma ya nyumba.

“Winnie, kuna nini? Hivi unajua jinsi unavyolia hivi utamfanya hata Pendo ahisi labda kuna jambo baya zaidi limewatokea wazazi wake,” Victoria alimwambia Winifrida huku akipapasa kichwani.

Winifrida alitaka kusema neno lakini maneno hayakuweza kutoka, donge la uchungu lilizidi kumkaba kooni na kumfanya azidi kutokwa na machozi, kwa kweli alishindwa kuvumilia, akalia kwa uchungu.

“Winnie, naomba nisikilize mdogo wangu, kuendelea kulia hivi hakutaweza kuwasaidia kaka yako na wifi yako wapate nafuu, sanasana ni kuwachulia tu…” Victoria alisema kwa upole huku akijaribu kumfuta machozi yaliyokuwa yanachuruzika kwenye mashavu yake. “Cha msingi ni kuzidi kuwaombea kwa Mungu ili waweze kupona na, sawa?”

Winifrida alibetua kichwa chake huku akishusha pumzi ndefu na baada ya kitambo kirefu hatimaye alinyamaza na dakika tano zilizofuata waliongozwa kuelekea sebuleni. Hapo sebuleni walimkuta Tunu akiwa anaongeza na simu huku akionekana kuwa na wasiwasi kidogo. Alipowaona alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akijiweka sawa pale kwenye sofa.

“Ndiyo Tom, kwa upande wangu mimi niko poa kabisa, sijui wewe?” Tunu alisema huku akikunja sura yake kama aliyekuwa anatafakari sana.

“Nilikuwa na wasiwasi sana baada ya kuona umenipotea katika mazingira yasiyoeleweka, nikawa na wasiwasi huenda wale watu walikupata.”

“Wapi?” Tunu aliuliza huku akishtuka kidogo.

“Kule Ilala...”

“Uliniona? Wewe ulikuwa wapi?” Tunu aliuliza kwa wasiwasi huku picha ya lile tukio la kufuatwa na wale wanaume watatu kule hospitali ya Amana ikijiumba akilini kwake.

“Nilikuwa nakufuatilia nyuma nyuma ili kama wakikupata na kulianzisha balaa niweze kukulinda.”

“Kwani wewe ulikuwa umevaaje? Maana kuna mtu nilimwona lakini sikumwelewa kabisa!” Tunu aliuliza kwa mshangao huku akijaribu kuvuta picha ya tukio la kule Ilala.

“Nilivaa suti nyeusi, kofia nyeusi na miwani myeusi…”

“Ooh! Ni wewe! Unajua niliona mtu akinifuatilia kwa nyuma lakini sikuweza kutambua kama ni wewe. Nilidhani ni miongoni mwa wale watu wa jamaa yetu na kuna wakati nilipogeuka nikashangaa kutokukuona, ndiyo maana nikaamua kufanya tukio lililowaacha watu mdomo wazi wakati mimi nikiingia mitini.”

“Nilitamani sana nikuite lakini sikutaka jamaa wanishtukie hivyo nikaacha kukufuatilia mara baada ya kuwaona wakiwa nyuma yangu. Nilikuwa natumia njia za mkato kukufuatilia, hivyo nilikwenda kutokea mtaa wa pili lakini sikukuona tena, nikawa na wasiwasi.”

Okay!” Tunu alisema kwa mshangao kisha akaongeza, “Kwani ulijuaje kama nilikuwa maeneo yale?”

“Wala sikuwa najua chochote, ilitokea tu muda huo nilikuwa kwa jamaa yangu mmoja ambaye mara nyingi huwa namtumia kama informer, ana ofisi yake mtaa wa Uhuru na Kigoma, jirani na vibanda vya wasusi wa Kimasai mara nikakuona ukipita mbiombio na kabla sijajua cha kufanya nikawaona jamaa wawili wakikufuata nyuma, kwa jinsi walivyokuwa nikajua kimenuka,” Tom alisema na kumfanya Tunu acheke.

Baada ya kile kicheko Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha kikatokea kitambo kifupi cha ukimya. “Basi nitakupigia simu baadaye kidogo, nipo sehemu najaribu kupata taarifa fulanifulani, si unajua tena hatuna muda.”

Okay, nipigie mara tu utakapomaliza mambo yako!” Tom alisema na mara simu ikakatwa. Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani huku akiwatazama Winifrida na Victoria. Baada ya hapo kikatokea kitambo fulani cha ukimya. Kila mmoja alionekana akitafakari jambo.

“Nilishindwa kurudi tena kule hospitali baada ya tukio la bomu nyumbani kwa Sammy, vipi kuna taarifa gani kuhusu hali za wapendwa wetu?” Tunu alimuuliza Victoria akiuvunja ule ukimya wa ghafla uliojitokeza.

“Joyce anaendelea vizuri, ameweza kuamka na...” Victoria alisema na kusita kidogo, akamtupia jicho Winifrida. “Winnie, hebu kamletee mgeni kinywaji. Sijui utatumia nini mgeni wetu?” alisema huku akimtazama Tunu.

“Chochote kitanifaa.”

“Nasikitika kuwa hatuna chochote ila tunazo soda, juisi, bia, wine, chai na maji!” Victoria alisema kwa utani huku akiangua kicheko hafifu na kumfanya Tunu naye aangue kicheko.

“Basi naomba wine, kama ipo red wine yoyote nitafurahi zaidi,” Tunu alisema bila wasiwasi wowote huku akijiweka vizuri pale kwenye sofa.

Winifrida aliinuka huku anashusha pumzi na kuelekea kwenye ukumbi wa chakula kulikokuwa na jokofu kubwa la vinywaji, huku macho yote yakimsindikiza.

“Sikutaka asikie. Kwa kweli hali ya shemeji Sammy ni tata sana, hata madaktari wanakiri kuwa hawana uhakika kama ataweza kuamka tena,” Victoria alisema kwa huzuni huku akizuia machozi yaliyokuwa yanamlengalenga machoni.

Inaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami WISDOM SEEDS mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal kuku mweus mtugani wa wapi huyo

NB: Litro 👩
 
Taxi - (134)

Tunu alihisi mwili wake ukizizima kwa hofu na kuishiwa nguvu. Kikatokea kitambo fulani cha ukimya, alipotaka kusema neno akasita baada ya kumwona Winifrida akirudi akiwa amebeba trei ndogo yenye chupa kubwa ya mvinyo aina ya Pinot Noir na bilauri ndefu, aliiweka ile trei mezani. “Karibu,” alimkaribisha Tunu kwa heshima zote huku akishusha pumzi.

“Ahsante, mdogo wangu,” Tunu alimshukuru Winifrida, akaifungua ile chupa na kumimina mvinyo kwenye bilauri kisha akanyanyua ile bilauri na kupiga funda moja kubwa kisha akairudisha bilauri ile mezani, na hapo wakabaki wakitazamana kwa kitambo. Winifrida alikuwa ameketi kwenye sofa akiwa jirani kabisa na Tunu huku akimtazama kwa namna ambayo hakuna aliyeelewa nini kilikuwa moyoni mwake.

Victoria alimwangalia Winifrida kwa makini kisha akayahamishia macho yake kwa Tunu, wakaangaliana. Macho yao yaliweza kuongea mengi. Victoria akashusha pumzi na kuinuka.

“Utanisamehe kidogo, Tunu, ninakuacha na Winnie, kuna kitu nakwenda kufanya na nitarejea baada ya kama dakika kumi hivi. Jisikie huru,” Victoria alimwambia Tunu na kusimama huku akimtazama kwa makini akionekana kusubiri ruhusa yake.

“Usihofu, dada, maadam nipo na Winnie basi unaruhusiwa kiroho safi,” Tunu alimwambia Victoria huku akiachia kicheko hafifu. Victoria akaondoka akiwaacha Tunu na Winifrida.

* * * * *

“Tunu amefanikiwa kuwatoroka tena!” Mr. Oduya alimaka kwa mshangao uliochanganyika na hasira kwenye simu huku akiyakodoa macho yake mbele kwa hasira kana kwamba kulikuwa na mtu mbele yake aliyekuwa akiongea naye.

Alikuwa akiitazama picha yake mwenyewe iliyokuwa imetundikwa ukutani. Ilikuwa picha kubwa iliyotundikwa jirani na picha ya Rais wa Tanzania, Dk. Yohana Funguo. Mr. Oduya alibaki akiwa kimya ameyakodoa macho yake kwenye ile picha huku akiwa hajui aseme nini. Kwa kadiri alivyomfahamu Tunu, alijua kuwa bila ya kumdhibiti mapema basi angesababisha matatizo makubwa.

Kwa mara nyingine tena katika harakati zake Tunu alikuwa amesababisha hofu katika moyo wake, akahisi jasho jembamba likimtoka usoni. Hakujua afanye nini, kwani aliamini kuwa Tunu alipenda sana kufanya harakati za kimya kimya kwa hadhari na uangalifu zaidi.

Hata hivyo, alifarijika kiasi fulani alipojikumbusha kuwa pamoja na ujanja wote wa Tunu lakini asingeweza kuwakwepa watu wote aliowaweka kumfuatilia, Mr. Oduya aliwaamini sana watu wake aliowaweka sehemu mbalimbali za mji walizoamini kuwa Tunu angeweza kufika au kupita, watu hao walikuwa kikazi na hawakuwa na mzaha kabisa.

Kama Tunu angethubutu kurudi tena hospitali au kulifuata gari lake aliloliacha kule kwenye mgahawa wa Elli’s angekufa kama kuku. Na kama angekuwa mpumbavu kiasi cha kujitokeza ili kupambana na watu wake angekufa pia. Mr. Oduya alitamani kumpata Tunu akiwa hai ili amfundishe adabu, alitamani yeye mwenyewe aitumie bastola yake, kwa dhamira moja tu, kumuua.

Mawazo yakiwa bado yanapita kichwani kwake, alikumbuka kuwa simu ilikuwa bado ipo hewani na upande wa pili wa simu kulikuwa na watu waliokuwa wanasubiri kusikia neno lake. “Tunu ametoroka!” Mr. Oduya aliongea tena, safari hii aliongea kwa sauti ya kunong’ona kana kwamba alikuwa akimnong’oneza mtu aliyekuwa ameketi jirani yake.

“Sikieni, hakikisheni anapatikana haraka kwa gharama yoyote ile, akiwa hai au maiti. Jipangeni maeneo yote kama tulivyokubaliana na msisahau kufuatilia Sinza nyumbani kwake na Sharif Shamba, nyumbani kwa Tom. Ila kuweni makini sana maana ana hila nyingi, msikubali awababaishe,” alisema na kukata simu.

Aliketi kwenye kiti chake kikubwa cha kuzunguka kilichokuwa na magurudumu yaliyokiwezesha kusogea kisha akashusha pumzi za ndani kwa ndani huku akimhurumia Tunu kwa kuwa alikuwa anajihangaisha, kwani asingeweza kufika mbali wala kupata ushahidi wowote wa kumtia Oduya hatiani kuhusiana na suala la Sammy na mkewe.

* * * * *

Baada ya Victoria kuondoka na kuwaacha Tunu na Winifrida wakiwa peke yao, kilizuka tena kitambo kirefu cha ukimya. Katika kipindi kile cha ukimya Tunu alikuwa anatafakari sana kuhusu kazi iliyo mbele yake na jinsi ya kupata ushahidi wa kumtia hatiani Mr. Oduya na genge lake, kama si kwa suala la Sammy na familia yake basi kwa kile alichokifanya hapo kabla.

Alinyakua tena bilauri ya mvinyo aina ya Pinot Noir na kupiga mafunda mawili na kuirudisha bilauri ile mezani, akamtazama Winifrida kwa makini akijaribu kuyasoma mawazo yake. Kuna jambo alikuwa ameligundua usoni kwa Winifrida, jambo hilo likamfanya aachie tabasamu pana. Winifrida alikuwa ametahayari sana na hakujua aseme nini.

“Pole sana, Winnie, nafahamu ni majonzi kiasi gani uliyo nayo baada
ya mkasa huu uliowakumba kaka’ako na wifi yako. Mimi pia nimesikitika sana ndiyo maana unaniona narudi hapa mara mbilimbili,” Tunu alimwambia Winifrida huku huzuni ikiwa imemshika.

Winifrida alikuwa ameinamisha uso wake akitazama sakafuni huku anamsikiliza Tunu kwa makini halafu akashusha pumzi kwa mkupuo huku akiwa kama anayefikiria jambo fulani, kisha akainua uso wake kumwangalia Tunu huku machozi yakimlenga lenga machoni, akayafuta na kuinamisha tena uso wake kutazama chini.

“Ninaamini kuwa vyombo vya dola vinafanya kazi kikamilifu kuwasaka watu wote waliohusika, hata hivyo sina hakika sana kama watafanikiwa kwani waliofanya hivyo ni watu makini waliojipanga na wanaozifahamu vyema nyendo za maafisa wa usalama wa serikali hii, hali inayowapa mwanya rahisi wa kutopatikana. Mimi na wewe tunawafahamu wahusika, na kwa kupitia ile memory card tungeweza kuwafanya waozee gerezani lakini tatizo ndiyo imespotea baada ya nyumba kulipuliwa na bomu...” Tunu alisema kwa huzuni huku akimkazia macho Winifrida.

“Nimerudi tena kwako nikitaka kujua, pengine uliamua kunificha au sasa unakumbuka uliiweka sehemu gani. Kama uliiacha kule kule nijue sehemu, naweza kuwatumia watu wangu wa karibu wajaribu kupekua kama wataweza kuiona,” Tunu alimaliza kuongea kisha akainyakua tena ile bilauri ya mvinyo iliyokuwa mezani na kuvuta funda moja kubwa na kuirudisha tena mezani huku akiendelea kumtazama Winifrida.

“Da, Tunu, hata sijui nisemeje sasa!” Winifrida alisema kwa sauti ya chini ya kukata tamaa kama ambaye hakutaka watu wengine zaidi ya Tunu wasikie maongezi yao. Mara hii Tunu aliweza kuhisi kuwa Winifrida alikuwa mwingi wa wasiwasi na alikuwa akiongea kwa woga. Hali hiyo ikamshtua ingawaje alijitahidi sana kuuzuia mshtuko wake.

“Nafahamu kuwa pengine ikawa si rahisi sana kwako kufahamu kaka yako yupo kwenye hatari kwa kiwango gani, ila naamini kuwa ukitulia vizuri na kufikiria unaweza kuwa na hisia ya jambo fulani ambalo huenda likawa msaada mkubwa wa kuniwezesha kuwanasa wote waliohusika,” Tunu alizungumza kwa sauti ya chini huku pia akikwepa maongezi yao yasisikike na watu wengine.

Tunu alifikiria sana na kushusha pumzi, alikuwa anatazama kule alikokuwa ameelekea Victoria katika namna ya kuibia ibia, ingawa alijitahidi sana kuificha hali ile. Tunu aliona, hali hiyo ilikuwa ni ishara nyingine muhimu aliyoweza kuishtukia haraka, hivyo hakuwa na mashaka tena kuwa Winifrida alikuwa na jambo ambalo alitamani sana kulisema ila hakutaka mtu mwingine asikie.

“Ni kweli kuwa nilikuwemo ndani wakati wale majambazi wanaingia lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya mimi kufahamu yaliyokuwa yanaendelea kwa kuwa nilikuwa nimejificha ndani ya kabati,” Winifrida alimjibu Tunu kwa msisitizo.

“Sawa! lakini hebu kumbuka vizuri ulipoihifadhi memory card, naamini kabisa kuwa itakuwa pamoja na simu yako. Je, simu ipo wapi, au nayo uliiacha kule kule nyumbani?” Tunu aimuuliza Winifrida kwa sauti tulivu ya kubembeleza huku moyoni akijyapima maneno yake kama yalikuwa na ukweli wowote.

“Kwa kweli sikumbuki,” Winifrida alijibu na kumfanya Tunu asitishe mohojiano, alibaki akimtazama kwa makini ingawa Winifrida aliendelea kuyakwepesha macho yake pembeni yasikutane na ya Tunu, na kwa hali ile Tunu akajua kuwa Winifrida alikuwa akimficha jambo fulani ambalo asingeweza kumlazimisha aliweke bayana kwa wakati ule.

“Sawa kama hujisikii kuniambia, inawezekana pengine huniamini au ni kweli hujui. Lakini elewa kuwa mimi pia nimeumizwa sana na matukio haya ya kaka yako na wifi yako, nisingeweza kustahimili kuacha kazi zangu zote na kufuatilia suala hili moja tu,” Tunu alisema huku akijinyoosha.

“Basi niitie wifi yako nimuage niondoke zangu, nitaendelea kuwepo hapa jijini kwa muda wa siku kadhaa, hivyo siku ukijisikia kuniambia chochote namba zangu hizi hapa, wewe nibip tu,” Tunu alimwambia Winifrida huku akisimama na kunyoosha mkono wake kumpa business card yenye namba zake za simu.

Winifrida alionekana kusita kidogo, aliitazama ile kadi kwa wasiwasi kisha macho yake yakahamia kwenye uso wa Tunu, “Basi kaa, n’takwambia ukweli...” alisema huku akimeza mate kutowesha koo lake lililokauka. Tunu alimtazama kwa makini na kuketi tena juu ya sofa.

Mambo yanazidi kunoga. Je, Winifrida anataka kumwambia nini Tunu? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kusisimua...

NB: Litro 👩
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom