Taxi - (126)
“Oh! kumbe umebadili mawazo, ungeniambia ni wapi tunapoelekea sasa badala ya kusema tu ingia kulia!” yule dereva alisema kwa jazba kidogo. Wakati huo ile taxi ilikuwa inafika mwisho wa ile barabara, dereva akaingia kulia.
“Wewe fuata maelekezo yangu, suala la fedha siyo tatizo,” Tunu alimjibu kwa sauti tulivu lakini akionekana kukerwa kidogo.
“Sawa basi usijali bosi wangu, wewe kwangu siyo mfalme tu, hata ukitaka urais nakupa. Wewe sema popote nitakupeleka,” yule dereva alisema huku uso wake ukitengeneza tabasamu la kirafiki.
“Ingia upande wa kulia hapo kama unaifuata barabara ya Uhuru kisha uingie kushoto kuufuata mtaa wa Tukuyu,” Tunu alimwambia yule dereva wakati wakiifikia ile barabara ya Uhuru iliyokuwa na msongamano wa magari muda huo.
Dereva akafanya kama alivyoagizwa. Aliliingiza gari lake katika barabara ya Uhuru kama aliyekuwa anaeleka Buguruni kisha akachepuka na kuufuata ule mtaa wa Tukuyu huku gari likikosakosa kugongana na daladala linalofanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Banana. Pasipo kujali matusi ya dereva na abiria wa lile daladala, yule dereva aliongeza mwendo wakapita mtaa ule uliokatiza katikati ya makazi ya watu hadi walipoufikia mtaa wa Kasulu.
Walipokuwa mwishoni mwa mtaa ule wa Tukuyu kabla hawajaufikia mtaa wa Kasulu Tunu akageuka tena nyuma kulitazama lile gari lililokuwa limewafungia mkia kwa nyuma. Bado lilikuwa likiwafuatilia na sasa lilikuwa likiufuata mtaa ule wa Tukuyu likiwa katika mwendo wa kasi. Ilionekana wazi kabisa kuwa watu waty hawakuonekana kuwapa mwanya wa kuwatoroka.
Kengele ya hatari ikalia kichwani kwa Tunu, sasa alihisi kuwa wale watu walikuwa wamedhamiria kufanya jambo baya zaidi, pengine walidhamiria kuua. Hakuona tena sababu ya kuendelea kumficha dereva wake, kwani kumficha kungemfanya kuwa na wakati mgumu sana wa kuwapoteza wale watu.
“Naomba nisikilie, sina sababu ya kukuficha kwa sababu nakuamini. Kuna gari nyuma yetu linatufuata tangu tulipotoka kule Elli’s, fanya namna yoyote ya kuhakikisha unawapoteza kwani sitaki kabisa wajue naenda wapi, sawa?” Tunu alimwambia yule dereva kwa sauti ya kuamuru.
Yule dereva akaangalia nyuma na kuliona lile gari aina ya Toyota Wish likizidi kuwasogelea, akaonekana kushtuka sana na kumtupia Tunu jicho huku wasiwasi ukijengeka usoni kwake. “Kwa nini wakufuatilie, kwani umewafanya nini, dada?” yule dereva aliuliza huku akihisi jasho likimtoka mwilini.
“Yule ni mume wangu, nimemtoroka nyumbani. Naomba fanya nilivyokwambia mambo mengine nitakueleza tukishawapoteza,” Tunu alisema huku akigeuza shingo yake kutazama nyuma. Dereva akamwelewa na kuchepuka kuufuata mtaa wa Kasulu upande wa kushoto. Muda huo Tunu aligeuka tena kutazama nyuma akaliona lile gari likizidi kuwasogelea, akatabasamu huku akijisemea moyoni, “Nyie subirini tu, dawa yenu ipo jikoni.”
Sasa dereva wa taxi alianza kuendesha gari kama aliyepandwa na kichaa, alipoufikia mtaa wa Arusha akakunja kushoto akiufuata ule mtaa kisha akakunja kuingia kulia na kuufuata mtaa wa Pangani kisha akakunja tena kuingia kulia akiufuata mtaa wa Mwanza. Mtaa ule ulikuwa mfupi, akakunja kuingia kulia kwake akiufuata mtaa wa Tanga, akawa anarudi nyuma kwenda kutokea tena mtaa wa Arusha.
Walipoingia tena kwenye barabara ya mtaa wa Arusha Tunu akageuka tena kulitazama lile gari kwa nyuma, akafarijika kutoliona likiwa nyuma yao na hapo akageuka tena mbele kumtazama dereva ambaye alikuwa anatabasamu. Katika mtaa ule wa Arusha dereva aliingia kushoto na walipofika
Pangan Water, Ilala Depot akaingia kulia kuufuata mtaa mmoja wa barabara ya vumbi hadi alipoufikia tena mtaa Tukuyu.
Walipokuwa wanaingia katika mtaa ule wa Tukuyu Tunu alipogeuka tena kutazama nyuma, na hapo moyo wake ukapiga kite kwa nguvu kama aliyepigwa konde zito la kushtukiza kichwani. Lile gari aina ya Toyota Wish lilikuwepo nyuma yao. Akashtuka sana. Hata yule dereva pia alishtuka sana. Tunu alimwona yule dereva akibabaika kidogo.
“Usijali, wewe nyoosha moja kwa moja, nitakwambia cha kufanya,” Tunu alimwambia yule dereva huku akipeleka mkono wake kiunoni, akaishika bastola yake akiwa tayari kwa lolote. Dereva wa taxi aliongeza mwendo. Wakati huo akili ya Tunu ilikuwa inafanya kazi haraka sana ili aweze kujinasua kutoka kwenye mawindo ya wale watu walioonekana kuwa na uchu wa kuutoa uhai wake.
Wakati wakikaribia kwenye fremu za maduka yanayozunguka Kanisa la Anglikana, Tunu alitoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi na kuzirushia mbele kwa dereva, “Ukifika mtaa wa Moshi kunja kulia na kuufuata mtaa huo, kisha punguza kidogo mwendo, nishuke halafu wewe ongeza mwendo ili kuwapoteza, sawa?”
Yule dereva aliitikia kwa kichwa huku akilitupia jicho lile gari lililokuwa nyuma yao. Akakunja kuingia kulia akiufuata mtaa wa Moshi huku akimkwepa mtoto mmoja aliyekuwa anakatiza barabara. Muda ule ule Tunu aliufungua mlango akashuka haraka na kuusukuma ule mlango, ukajibamiza. Akachepuka na kujibanza nyuma ya mti mmoja mkubwa wa kivuli jirani ya nyumba moja ya wageni.
Lile gari lililokuwa nyuma yao pia liliingia barabara ile lakini kwa kuchelewa kidogo likaongeza mwendo kuifuata ile taxi. Dereva wa taxi aliufikia mtaa wa Arusha na kuuvuka, akaendelea mbele akiifuata barabara ile ya vumbi. Sasa alikusudia kuwafanya wale watu waamini kuwa yule dada alikuwa bado yumo ndani ya ile taxi.
* * * * *
Kwa mara ya kwanza tangu alipoanza harakati zake za kutaka kuingia ikulu, Mr. Oduya alijikuta katika hali ya wasiwasi na mashaka makubwa. Kwa mbali hofu ilikuwa ikitishia kuutawala moyo wake, hasa kwa hisia zilizokuwa zikimnong’oneza kuwa mambo yameanza kumwendea mrama. Alikuwa amekanganyikiwa akiwa ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka ofisini kwake.
Itaendelea...
NB:
Litro 👩