Taxi - (130)
ILIPOISHIA
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam walikuwa wamezipokea habari zile kwa kitu zaidi ya mshangao, hofu kubwa. Hofu ilipenya katika fikra zao kwa kule kusikia kwamba haikuwepo fununu yoyote juu ya kupatikana kwa watu waliofanya tukio lile ambalo lilionekana ni zaidi ya uhalifu wa kawaida, lilikuwa limefikia kiwango cha kuitwa ugaidi. Kila mtu alimtazama mwenziwe kwa macho yaliyoitangaza hofu iliyojificha moyoni mwake.
Siku hiyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Ramon Mamboleo alikuwa na hasira kali na alikuwa katika uso wa kusawajika kidogo. Hakuna kitu kilichomkasirisha kama wahalifu. Mhalifu alimchukulia kama shetani mwenyewe na alikuwa tayari kumsaka kwa ari zote ili ampate na kumpeleka gerezani alikokuita jehanamu.
Ilikuwa saa tisa alasiri alipowasili kituo kikuu cha polisi akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukuta watu wa habari: waandishi wa magazeti, redio na televisheni wakimsubiri. Muda wote alikuwa akipokea ujumbe mfupi wa simu na kupigiwa simu toka kwa wakuu wake wa kazi na watu wengine waliotaka kujua jeshi la polisi lilikuwa limefikia wapi katika uchunguzi wake ili kuwabaini waliofanya uhalifu huo.
ENDELEA...
Hakutaka kuongea na mwanahabari yeyote kwa muda ule, kwani hakuwa amepokea taarifa yoyote toka kwa wasaidizi wake. Aliposhuka garini alielekea moja kwa moja ofisini kwake. Ilikuwa ofisi pana na sakafuni ilifunikwa kwa zulia maridadi jekundu na katikati ya lile zulia likiwa na nembo kubwa ya Jeshi la Polisi la Tanzania.
Ndani ya ofisi ile kulikuwa na meza ndefu ya mikutano iliyozungukwa na viti kumi na mbili. Viti vitano upande wa kushoto, viti vingine vitano upande wa kulia, kiti kimoja mwanzoni mwa ile meza na kiti kimoja kilikuwa mwisho wa meza.
Naibu Kamishna Mamboleo aliketi juu ya kiti chake kikubwa chenye foronya laini cha kuzunguka na chenye magurudumu yaliyokiruhusu kusogea, kiti kile kilikuwa nyuma ya meza kubwa ya ofisini yenye majalada mengi juu yake. Bendera ndogo mbili zilionekana juu ya ile meza, moja ikiwa bendera za Taifa na nyingine ya Jeshi la Polisi. Vitabu kadhaa vikiwemo vya Sheria na Katiba ya Tanzania, kidau cha wino, mhuri na kichupa kidogo chenye wino mweupe wa kufutia maandishi.
Pembeni ya ile meza ya ofisini kulikuwa na mashine ndogo ya kidijitali ya kurudufu, mashine maalumu ya kuchapa barua na nyraka mbalimbali za kiofisi, mashine ya picha na mashine moja ya nukushi. Naibu Kamishna Mamboleo alishusha pumzi ndefu.
“Majaribo mawili ya mauaji katika familia moja ndani ya saa kumi na nne!” Naibu Kamishna Mamboleo alijikuta akiropoka. “Mke kwa risasi na mume kwa bomu! Ni nani hawa waliofanya hivi? Na kwa nini wafanye hivi kwa familia hii? Je, familia hii ina adui yeyote?” Naibu Kamishna Mamboleo alijiuliza.
Hata hivyo, hakutarajia kupata majibu haraka kiasi hicho kwani alikuwa anasubiri uchunguzi uliokuwa ukifanywa na vijana wake machachari wakiongozwa na Inspekta Abel wa mkoa wa kipolisi wa Ilala. Hata hivyo, kama kuna kitu kilikuwa kinamsumbua sana Naibu Kamishna Mamboleo ni kusubiri. Subira ni jambo lililokuwa likimtesa mno kama adhabu. Alihisi kila dakika aliyoendelea kusubiri ilikuwa ikimjeruhi moyo wake na kuutia jeraha. Kiti alichokalia alikihisi kilikuwa kinawaka moto.
Wazo kuu lilikuwa moja tu, awapate vipi wahalifu hao wasio na hata chembe ya huruma, wahalifu wenye kutaka kuichafua amani ya nchi hii na kufurahia kumwaga damu isiyo na hatia? Angepeda sana kuwapata wahalifu hao haraka iwezekanavyo. Tatizo lilikuwa angewapataje haraka kiasi hicho? Jiji la Dar es Salaam lilifurika watu wote: wema kwa waovu, wenye hatia kwa wasio na hatia. Ni vipi awapate watu wachache wenye hatia miongoni mwa mamilioni wasio na hatia kwa muda mfupi?
Kila alivyojiuliza alijikuta akipata jibu moja tu, jibu lililozidi kumjeruhi moyo wake, hakuwa na budi ya kusubiri taarifa ya uchunguzi! Alitakiwa asubiri hadi hapo wasaidizi wake wamalize uchunguzi wao na kukusanya taarifa zote muhimu za kiitelijensia ambazo zingewaongoza hadi mbele ya wahalifu hao.
Taarifa hizo zilitegemea sana kuifahamu mienendo ya Sammy katika siku za karibuni na watu aliokuwa anakutana nao, wapi alikokuwa usiku wa siku ambayo mkewe alipigwa risasi, alikopita kabla ya kufika nyumbani, watu gani waliokutana nao siku hiyo au alioongea nao kwenye simu na mambo gani waliyoongea.
Ni hayo ambayo yangetengeneza njia ya kuwapeleka polisi kwa wahalifu hao, lakini ilihitajika subira. Kusubiri kulimtisha zaidi Naibu Kamishna Mamboleo kuliko hata wahalifu wenyewe. Hakupenda kuketi ofisini akisubiri kwa sababu hakujua wahalifu hao walikuwa wanapanga nini katika kipindi hicho, pengine walikuwa wanajiandaa kushambulia watu wengine wasio na hatia au hata kutoroka nchi!
Sababu nyingine iliyomfanya ashindwe kusubiri ni kwamba raia wema jijini Dar es Salaam walikuwa wamejawa hofu kubwa na usalama wao, ni yeye Naibu Kamishna Mamboleo aliyekabidhiwa jukumu la kuhakikisha raia na mali zao ndani ya jiji la Dar es Salaam wanakuwa salama.
Hakupendezwa kabisa na hali ile, kama mlinzi wa amani katika jiji la Dar es Salaam, aliyepewa dhamana hiyo na taifa, asingeweza kukaa kwa amani ofisini kwake akishuhudia amani hiyo ikitoweka na hata kuwafanya raia wema kuanza kuichukia serikali yao.
Hadi muda huo jeshi la polisi lilikwisha wahoji watu wengi wakiwemo majirani wa Sammy, marafiki, jamaa wa karibu na hata wafanyakazi wa Udzungwa Beach Resort alikokuwa akifanya kazi Sammy kabla hajaacha. Katika mahojiano na msako mkali uliofanywa, wapo wengi waliokamatwa na kushikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi baada ya kushukiwa kuhusika, lakini bado kulikuwapo maswali mengi ya kukanganya yaliyotakiwa kupatiwa majibu ili kuwaongoza polisi mbele ya wahalifu hao.
Hata hivyo, kulikuwa na mtu mmoja tu katika jiji zima la Dar es Salaam ambaye alikuwa na majibu yote ya maswali hayo. Mtu huyo, msichana mrembo, mrefu, maji ya kunde na mwenye umbo matata lenye kuweza kuitaabisha vibaya nafsi ya mwanamume yeyote, alikuwa na sura ya duara, macho malegevu, pua ndefu na midomo yenye kingo pana.
Mtu huyo machoni kwa jamii isiyoelewa kazi yake alionekana binti mrembo aliyepaswa kuolewa na mwanamume mwenye fedha zake akatulia ndani, azae na kumhudumia mume basi. Lakini kwa magaidi na wahalifu wa kimataifa, binti huyo aliogopwa sana kwani alikuwa na uwezo mkubwa na mbinu nyingi za kumfikia adui na oparesheni alizowahi kuzifanya ziliwafanya wengi kuhisi pengine hakuwa binadamu wa kawaida.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko Jackal kuku mweus mtugani wa wapi huyo
NB:
Litro 👩