Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (81)

ILIPOISHIA

Mr. Oduya alichukua simu yake na kutafuta namba za Dk. Masanja, meneja mkuu wa hoteli ya Udzungwa Beach Resort na kupiga ili kupata uhakika. Majibu aliyopewa yalimfanya ajihisi kukanganyikiwa, akili yake ilijaribu kukataa kabisa kukubaliana na taarifa ile na kile alichokishuhudia kwenye katika nyaraka zile za ununuzi wa gari.

Alijitahidi kuwa makini zaidi na akiishirikisha akili yake kikamilifu katika kumletea taarifa za kuaminika, kwani mambo yale hayakuwa yanamwingia kichwani kabisa! Ni vipi Sammy ameendelea kujitokeza katika harakati zake za kuusaka urais wa Tanzania na kugeuka kuwa kitisho?

Aliinua uso wake na kutazama juu akionekana kuwaza mbali. Wakati huo Spoiler na Dulla Mcomoro walikuwa kimya kabisa wakimtazama kwa wasiwasi. Akiwa katika hali ile mara hisia mbaya zikamjia na hapo mapigo ya moyo wake yakaanza kwenda kasi isivyo kawaida, hasa alipowaza kuwa huwenda wapinzani wake kisiasa walikuwa na fununu fulani kuhusiana na lile gari na wangeweza kulitumia kummaliza.

SASA ENDELEA...

Akiwa amezama kwenye tafakuri ile, akili yake ikaenda mbele zaidi katika kuunda hoja kichwani. Akaanza kuwaorodhesha washindani wake wakuu wa kisiasa bila kujali vyama walivyotokea, akianzia na wapinzani wake wakuu ndani ya Chama Cha Ukombozi, Benard Tumbo, Dk. Hussein Abbas na Anuary Kamba. Kisha akawafikiria wa kutoka vyama vingine walioonekana kukubalika zaidi, Zingo Kabwela na Tindua Luis.

Alipomaliza akaanza kutathmini vizuri nguvu na hali ya mahusiano yake kisiasa na viongozi wa nchi ikiwemo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama. Tathmini yake ikamweleza kuwa mahusiano ya nyanja zote baina yake na viongozi wa nchi na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama bado yalikuwa mazuri ingawa kulikuwa na misuguano ya kawaida ya hapa na pale kati yake na baadhi ya viongozi hao kutokana na tofauti za kimitazamo.

Alipotafakari kwa kina juu ya misuguano hiyo akajaribu kuwaza kama kulikuwepo mmojawapo wa wapinzani wake kisiasa au kiongozi ambaye angeweza kuwa na ukaribu na Sammy, bado haikuweza kumridhisha kuwa hata kama kusingekuwa na yeyote kati yao mwenye ukaribu na Sammy bado isingeweza kuwa sababu toshelevu ya kumfanya asichukue tahadhari.

Baada ya kimya cha kitambo fulani Mr. Oduya aliinua uso wake uliosawajika na kumtazama Spoiler. “Unamfahamu Samuel John Kambona?” alumuuliza kwa sauti tulivu.

“Sina hakika, lakini nadhani ni yule bwege aliyekuwa anafanya kazi hoteli ya Udzungwa Beach Resort,” Spoiler alisema baada ya kitambo kifupi cha kuvuta kumbukumbu. Mr. Oduya alibetua kichwa chake kukubali.

“Bado ni kizungumkuti kwani sina hakika kama hadi wakati huu hakuna yeyote kati ya wapinzani wangu kisiasa anayefahamu kuhusu hilo gari. Nimeshtuka sana kuona kuwa ni Sammy huyu huyu ndiye mmiliki wa gari ambalo siku zote nilidhani lilishateketezwa. Kwa kweli hizi ni taarifa za kustaajabisha na kuogofya sana,” Mr. Oduya alisema katika hali ya kukanganyikiwa huku taratibu akiviminyaminya vidole vyake vya mikononi katika hali ya kuupisha utulivu kichwani mwamke.

Kilipita tena kitambo fulani cha ukimya kila mmoja akijaribu kutafakari, kisha Mr. Oduya alishtuka akionekana kukumbuka jambo.

“Katika kufuatilia taarifa hizi mmehakikisha hamjaacha kielelezo?” Mr. Oduya alimuuliza Spoiler huku akimkazia macho.

“Hapana, hatujaacha kitu, tulichukua tahadhari zote, tulihakikisha tumebadili muonekano wetu, tukitumia gari lenye namba bandia na kuvaa glavu laini mikononi ambazo haikuwa rahisi mtu kutushtukia,” Spoiler alisema kwa uhakika.

“Silas, usichukulie kirahisi hivyo, kumbukeni kuwa hii ni vita. Mkifanya chochote hakikisheni hamuachi kitu tusije tukavuruga na kujipa kesi nyingine. Sawa?”

“Usijali, mkuu,” Spoiler na Dulla Mcomoro wakasema kwa pamoja.

“Okay, sasa mna kazi nyingine. Hakikisheni usiku huu huu huyu mtu anayeitwa Samuel John Kambona anapatikana kisha mpelekeni kwenye nyumba ya Kinondoni Makaburini na gari lake liteketezwe kabisa. Amenitafuta muda mrefu na sasa amenipata, I think he derseves to die,” Mr. Oduya alisema kwa sauti ya kitetemeshi kutokana na ghadhabu aliyokuwa nayo.

Spoiler na Dulla Mcomoro walikubali kwa kubetua kichwa, kisha wakanyanyuka na kuanza kuondoka wakifahamu kuwa kauli ile iliashiria kuwa maongezi kati yao mle ndani na Mr. Oduya yalikuwa yamefika tamati. Spoiler ndiye alikuwa wa kwanza kusimama sekunde chache kabla Dulla Mcomoro hajafanya hivyo.

“Tambueni kuwa nimewapa jukumu hili kwa sababu bado nawaamini sana, hivyo hakikisheni hamfanyi makosa,” Mr. Oduya aliongea kwa sauti tulivu ya kusihi na katika sauti yake kulikuwa na hali ya hofu iliyokuwa imejificha nafsini mwake. Alilazimisha tabasamu usoni mwake ingawa tabasamu hilo lilikataa kabisa kuumbika.

Spoiler na Dulla Mcomoro walibetua vichwa huku wakisimama kwa ukakamavu kama wanajeshi kisha wakaanza kuzitupa hatua zao taratibu kuondoka kwenye ofisi ile na kuufikia mlango, Spoiler aliufungua huku akiwa na hakika kuwa macho ya Mr. Oduya yalikuwa nyuma yao yakiwasindikiza.

Alipoufungua ule mlango akageuka na kumtazama tena Mr. Oduya aliyekuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti chake, alichokiona usoni kwa Mr. Oduya lilikuwa ni tabasamu lililohanikiza kila aina ya unyama. Bila kupoteza muda Spoiler akamtupia tabasamu la kuonesha kuwa alikuwa tayari kwa lolote, kisha wakatoka nje ya ofisi ile na kufunga mlango.

* * * * *

Saa mbili kasorobo usiku nyumbani kwa Sammy, Winifrida alikuwa anakatakata nyanya za kachumbari huku akimtupia jicho la wizi Joyce, ambaye muda huo alikuwa kafungua milango ya jokofu kubwa lililokuwa katika ukumbi wa chakula ila alionekana kuzama kwenye lindi la mawazo wala asichukue kitu alichokusudia.

Joyce alikuwa amesimama huku aking’ong’ona kucha zake, alikuwa amezama katika lindi la mawazo yaliyomfanya kuiona dunia yote ikiwa imemwelemea na kumkalia kichwani. Alijaribu kuwaza hili na lile katika namna ya kutafuta ni jinsi gani angeweza kuirejesha faraja na furaha iliyotoweka ghafla kwenye ndoa yake.

Donge la uchungu lilikuwa limemkaba kooni, alishindwa kuuzuia uchungu aliouhisi ukipenya moyoni mwake kutokana na mzozo uliokuwa umezuka kati yake na Sammy mchana wa siku ile. Tangu Sammy aliporudi nyumbani saa tano na ushee asubuhi hadi alipoondoka saa kumi na mbili jioni hawakuwa katika hali ya maelewano.

Siku nzima Sammy alikuwa akimpiga vijembe Joyce. Joyce hakuamini, alizoea utani wa mumewe lakini kila alipomtazama machoni hakuona dalili yoyote ya utani. Hakutaka kuamini kuwa ingetokea siku mumewe angemkasirikia kiasi kile. Ilifikia hatua alijiuliza kama yote hayo yalitokana na yeye kumweleza ukweli kuhusu kilichojitokeza kati yake na mwanamuziki Dynamo Plus au kulikuwa na jambo jingine lililojificha katikati.

Inaendelea...

CC the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple
 
Taxi - (82)

“Nimekukosea nini kiasi hicho, mume wangu? Nilidhani yameisha kumbe bado unayo moyoni. Kwa hiyo uungwana wangu niliokuonesha kwa kukueleza ukweli ndiyo umeamua kuutumia kuniumiza?” Joyce alimuuliza Sammy kwa uchungu baada ya kuona hali ikizidi kuwa mbaya.

Sammy hakumjibu, alimtazama kama kinyago tu. Joyce alikuna kichwa aanzie wapi kusawazisha mambo. Hakuamini kama ile hasira ya mumewe ilikuwa imekuja ghafla tu. Bila shaka ilifugwa kwa muda mrefu na sasa ilikuwa imekomaa vya kutosha. Ilisubiri tu ipate mwanya ianze kujitawala badala ya kufugwa tu. Mwanya umeshapatikana, hasira imetoka na inaonesha makucha.

Joyce aliwaza kuwa hakupaswa kupuuzia, alitakiwa atafute njia ya kuidhibiti, aiangamize na kuitowesha kabisa kungali bado mapema. Kwa vipi sasa?

Muda huo Sammy alikuwa amekaa juu ya sofa, Joyce naye alikaa kwenye sofa lile lile ila hawakukaribiana. Kwa kitambo kirefu kimya kilitawala kati yao ingawa hali haikuwa tulivu katika vichwa vyao. Joyce alikohoa kidogo kutakasa koo lake kisha akaanza, “Mume wangu, naomba…” alisita baada ya kumwona Sammy akiinuka na kuondoka.

Kilikuwa kitendo cha dharau sana, Sammy alipotoka aliwasha gari lake na kuondoka zake bila hata kuaga alikuwa akienda wapi na hakuwa amerejea hadi muda ule, hivyo kichwa cha Joyce kilionekana kuzidiwa na uzito usiosemeka wa mawazo. Ni yeye tu labda na Mungu wake ndiye aliyejua kilichokuwa kikipita akilini mwake muda huo.

Mawazo juu ya mustakabali wa ndoa yao. Mawazo juu ya taaluma yake ya ubunifu wa mavazi na ndoto yake ya kutaka kuwa mbunifu bora barani Afrika. Mawazo juu ya wasiwasi wa kumpoteza mwanamume ampendaye, mwanamume wa aina na kariba yake ambaye ndiye chaguo la moyo wake. Mawazo juu ya… ah! Mambo yalikuwa mengi kichwani kiasi kwamba alijihisi kutaka kuchanganyikiwa.

Siku hiyo ilikuwa ndefu sana kwa Joyce kuliko kawaida, hadi muda ule hakuwa ameweka chochote tumboni na wala hakuhisi njaa kabisa. Ingawa amewahi kuwa na misuguano ya hapa na pale na Sammy lakini ilikuwa ya kawaida na mara nyingi iliisha kwa mazungumzo tu. Lakini lile lilikuwa jambo geni kabisa! Kwa miaka takriban nane waliyoishi hapakuwa na hata siku moja ya namna hiyo… Hata moja!

“Wifi, naona leo hauko sawa! Kwani kuna nini?” sauti ya Winifrida ilimzindua Joyce kutoka kwenye lindi la mawazo, alimtazama Winifrida kwa kitambo kidogo bila kusema neno, kisha akatabasamu kwa mbali na kushusha pumzi. Akanyanyua mabega yake juu na kuyashusha halafu akageuka tena, akafunga taratibu milango ya jokofu.

* * * * *

Kwenye jumba moja la kifahari la ghorofa moja lililojengwa katika eneo la Kinondoni Makaburini, Spoiler na Dulla Mcomoro walikuwa wanajiandaa ili kwenda kuifanya kazi waliyoagizwa na Mr. Oduya. Walikuwa wamefika hapo kujiandaa baada ya kutoka ofisini kwa Mr. Oduya.

Lilikuwa jumba la vyumba vitano vya kulala vilivyosheheni samani zote muhimu, sebule mbili kubwa chini na juu, ukumbi wa chakula, ofisi na maktaba ya siri, na chumba cha siri cha mateso. Hata hivyo, jumba lile lilikuwa halikaliwi na mtu yeyote, Mr. Oduya na watu wake waalifika kwenye jumba hilo pale walipokuwa na mission maalumu.

Spoiler aliandaa nguo maalumu na vifaa vya kazi. Nguo nyeusi, buti na barakoa. Akachukua bastola moja aina ya FNX 45 Tactical yenye kiwambo cha kuzuia sauti na kumpatia Dulla Mcomoro, kisha akachukua visu viwili vikubwa, kimoja akakiweka kwenye nyonga na kingine nyuma ya mguu kikifunikwa na suruali.

Alipomaliza alichukua chupa ya kemikali aina ya Chloroform inayotumika kumlegeza au kumzimisha mtu kiasi kwamba kushindwa kujitambua na kuhisi chochote na wahalifu wakafanya chochote wanachoweza kwa muda wa kutosha. Aliitazama kwa kitambo na kumpa Dulla Mcomoro ambaye aliitazama na kuachia tabasamu kisha akaiweka kwenye begi lake dogo aliloliweka mgongoni.

Walipoona kila kitu kipo sawa Spoiler alitoa simu na kupiga namba fulani, akaongea na mtu mmoja na kutoa maagizo kisha akakata simu na kumpa ishara Dulla Mcomoro amfuate. Walitoka na kujipaki kwenye pikipiki aina ya Boxer BM 150 na kuanza safari ya kuelekea kwenye mission yao.

* * * * *

Saa mbili na nusu usiku, katika mgahawa wa kisasa wa ELLI’S kulikuwa na pilikapilika za aina yake za kujistarehesha. Ndani ya ukumbi mkubwa wa chakula na vinywaji wa mgahawa ule wa kisasa sauti ya muziki laini wa taratibu ilikuwa ikisikika kutoka katika spika zilizokuwa sehemu fulani na kuzikonga nyoyo za watu waliofika kwa ajili ya chakula na vinywaji usiku ule.

Hakika usiku wa mjini haukuujua usiku kwa kuwa ulikuwa umejaa kila aina ya starehe na anasa. Giza lililozoeleka kutawala usiku maeneo ya vijijini na miji midogo halikuwa na nguvu wala uwezo katika maeneo ya starehe yasiyo na idadi jijini Dar es Salaam. Nuru za rangi mbalimbali toka katika majumba na taa za barabarani zilikuwa zikilidhihaki giza hilo kiasi cha kuufanya usiku kuwa mchana wa aina yake.

Katika ukumbi ule mkubwa wa chakula wa mgahawa wa kisasa wa ELLI’S, mwanadada Tunu alikuwa ameketi kwa utulivu kwenye kiti kifupi chenye foronya laini. Aliketi kwenye meza moja iliyokuwa imejitenga kwenye kona moja ya ukumbi ule akiwa mtulivu sana, mbele yake kulikuwa na chupa kubwa na bilauri ya mvinyo mwekundu aina ya Dodoma Wine na alikuwa akizungusha kidole chake cha shahada kwenye ile bilauri huku akitafakari na kuzungusha macho yake kuwachunguza watu walioketi mle ukumbini.

Itaendelea...
 
Taxi - (83)

Alikuwa anakunywa taratibu akishushia baada ya mlo mtamu aliomaliza kula muda mfupi kabla. Aliitazama saa yake na kugundua kuwa zilikuwa zimepita takriban dakika arobaini tangu alipoketi mle ukumbini, aliyekuwa amemfuata bado hajamtia machoni. Je, amedanganywa? Hapana, hawezi kuwa amekosea!

Wakati alipoingia katika mgahawa ule alikumbuka kuulizia na akahakikishia kuwa mtu aliyekuwa akimtafuta alikuwepo pale jioni hiyo na alitoka muda mfupi kabla yeye hajaingia na angerudi kwa kuwa kuna mizigo yake aliiacha na kuahidi kuifuata. Hivyo, Tunu hakuwa na shaka yoyote kuwa mtu huyo angerejea.

Hadi wakati ule alikuwa bado amevaa gauni la kitenge cha wax lililoshonwa kwa mtindo wa ‘Ankara midi tube dress’ likiishia juu kidogo ya magoti yake, likaushika vyema mwili wake na kulichora umbo lake maridhawa na viatu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio. Miwani yake myeusi ya jua alikuwa ameiweka juu ya kichwa chake na mkoba wake mzuri wa kike ulikuwa juu ya meza.

Akiwa ameketi kwenye ile meza aliwatazama wateja wengine waliokuwa wameketi katika meza mbalimbali, kila mmoja alikuwa katika hali ya utulivu kama ambaye hakuwa na wasiwasi wowote duniani. Katika uchunguzi wake macho yake yalianza kutua kwenye meza moja mbele yake iliyokuwa na watu watatu, mwanamume mmoja wa kizungu aliyeonekana kubabaishwa na wasichana wawili wa Kibantu.

Wasichana wale walikuwa warembo kwelikweli wenye mavazi ya kileo yaliyowabana na kuonesha maungo yao yalivyoumbika, meza yao ilikuwa imechafuka kwa nyama choma na vinywaji vya bei mbaya, wao wakitoa oda kwa mhudumu na mzungu analipa. Walikuwa wanamchezea mapaja, kifua na kidevu kwa mahaba na yeye alikuwa anacheka, anaridhika.

Macho ya Tunu yakaiacha meza ile na kuhamia kwa watu wawili waliokuwa wameketi kwenye meza ya tatu tu kutoka pale alipoketi, kulikuwa na wanaume wawili walioonekana kumwangalia Tunu kwa matamanio. Wanaume hao walikuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40 na walikuwa wanakunywa pombe kali aina ya Grant’s Blended Scotch Whisky, muda wote walikuwa wanamchombeza Tunu kwa maneno haya na yale lakini hakuonekana kuwajali.

Mmoja alikuwa mfupi kiumbo lakini mkakamavu akiwa na mwili uliojengeka kwa mazoezi na sura yake ilionesha unyenyekevu mkubwa. Alivalia fulana nyeusi iliyombana na kulionesha vyema umbo lake lililojengeka kwa misuli na suruali nyeusi ya jeans, miguuni alivaa buti ngumu za ngozi. Alijulika kwa jina la Bob Chopa na hakuna aliyelijua jina lake halisi.

Mwanamume wa pili alikuwa mrefu aliyepanda hewani kisawasawa na mwenye mwili ulioshiba, alikuwa mweupe kiasi na kichwa chake kilikuwa kinang’ara kwa upara mpana, uso wake ulikuwa mpana na macho yake yalikuwa makubwa. Alivaa suti maridadi ya kijivu na viatu vyeusi vya ngozi.

Aliyaondoa macho yake kutoka kwa wale wanaume na kuyatembeza kuwaangalia watu wengine. Meza nyingine zilikuwa na watu ambao hawakumshawishi sana kuwatazama. Hakupata taabu kugundua kuwa waliokuwa wameketi katika meza hizo ni mtu na mkewe. Wengine wachumba na wale ni mtu na mchepuko wake mpya, kwa jinsi walivyokuwa wamekaa.

Meza mbili tatu zilikuwa zimekaliwa na wafanyabiashara wakubwa na viongozi wa kiserikali, wengine walionekana wazi kuwa ni mafisadi au wapiga dili na hapo walikuwa wanapanga harakati zao kwa sauti ya mnong’ono.

Kisha macho ya Tunu yakaangukia kwenye meza moja iliyokuwa jirani na mlango wa kuelekea maliwato, ambapo alikuwa ameketi mwanadada mmoja, peke yake kama yeye, alikuwa akinywa bia aina ya Heineken taratibu bila haraka. Tunu alishindwa kuyaondosha macho yake kutoka kwa yule mrembo, hakukumbuka ni wapi na lini aliwahi kumwona.

Alikuwa mrefu, mpana na alivaa sketi fupi nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi nyeupe ya mikono mirefu na viatu vya flati. Mkononi alikuwa amevaa saa ghali ya kike na alipakata mkoba mzuri wa nguo ya pundamilia uliomgharimu fedha nyingi. Alionekana mtulivu sana akisubiri kitu au mtu muhimu sana, kwani mara kwa mara alikuwa akiitupia jicho saa yake ya mkononi na kukunja sura yake.

Kwa taabu sana Tunu aliyaondosha macho yake toka kumtazama yule mwanadada na kumgeukia mhudumu mmoja aliyekuwa anapita jirani na meza yake, akamwita, “Samahani, anti…”

Yule mhudumu alisimama na kumsogelea Tunu huku akimtazama kwa makini.

“Hivi, yule bwana anayeendesha lile gari la kizamani aina ya Cadillac DeVille atarudi kweli, maana nilikuwa nahitaji huduma yake lakini nashangaa hadi sasa sijamwona!” Tunu alimuuliza yule mhudumu huku akipitisha ulimi wake kulamba midomo yake.

“Sina uhakika, kwani huna namba yake ya simu umpigie?” yule mhudumu aliuliza huku akiyatupa macho yake kutazama kwenye meza aliyoketi mzungu na wanawake wawili wa kibantu waliokuwa wakimwita.

“Ningekuwa nayo wala nisingehangaika kukuuliza,” Tunu aliuliza ma kuminya midomo yake.

“Basi endelea kusubiri, maana subira yavuta heri,” yule mhudumu alisema na kuanza kupiga hatua kwenda kwenye ile meza alikoitwa. Tunu alishusha pumzi na kujiegemeza kwenye kiti chake na kuyatupa tena macho yake kwa yule mwanadada aliyeketi peke yake ambaye hakulijua jina lake.

Alimwona akiinamisha kichwa chake kama aliyeona kitu katika bilauri yake ya bia, alitazama ndani ya ile bilauri kwa kitambo kisha aliinua uso wake taratibu kwa madaha kana kwamba alikuwa anaigiza filamu, mara macho yao yakakutana. Kwa dakika nzima macho yao yalitulia yakitizamana kama ambao walikuwa wakisomana fikra zao, kisha yule mwanadada aliyahamisha macho yake na kutazama kando.

Mambo yanazidi kunoga ndani ya Bandari Salama, ingawa jiji hili si salama kama lilivyo jina lake. Nani ni nani katika jiji hili? Na nani anajua nani anafanya nini? Endelea kuifuatilia stori hii ya kusisimu ambayo kisa chake hakijapata kusimuliwa ili ujue hatma yake...
 
Nashukuru kwa maoni yako lakini hiyo ndiyo style yangu ya uandishi, na-enjoy kuelezea kile ninachokiona kwenye akili yangu. Kama hupendi sina namna nyingine ya kukulazimisha...
Kaka hilo wazo kifanyie kazi.Maelezo yanamchosha msomaji inabidi upunguze.usikatae ushauri uko na mantiki.usifanye kwa mazoea fanya kwa ufanisi
 
Hayo majina ya viongozi wa vyama vya upinzani sio ya mchezo
 
Mkorogano mtupu, ahsante Bishop, ila Sam bwege kweli ameshindwaje kumsamehe Joy???
Ila wanaume ndio walivyo kaambiwa ukweli hataki kumsamehe angekuwa yeye apo angeshasamehewa
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom