Laiti Ningejua! 4
Mtunzi Bishop Hiluka
“It’s been a year now since I came back,” (Ni mwaka sasa tangu nirudi) alisema Adnan na kuendelea, “Si unajua Mzee Fahad alifariki dunia? Kwa hiyo familia ikanitaka nirudi ili kusimamia miradi aliyoiacha.”
“C’mon, man, don’t tell me!” (Wacha wee, usiniambie!) nilimaka kwa mshtuko mkubwa sana huku nikimkazia macho Adnan. “Mzee Fahad amefariki dunia! Lini?” niliuliza nikiwa bado nina mshtuko mkubwa.
Endelea...
“Mbona umeshapita mwaka na ushee sasa tangu alipofariki dunia! Tulizika na tayari tumekwisha sahau…” alinijibu Adnan kisha kama aliyekumbuka jambo akanitupia swali. “Why are you here, what are you doing here, Bilali?” (Mbona uko hapa, unafanya nini hapa, Bilali?)
“Naelekea Dar es Salaam, lakini nimekwama hapa kwa takriban saa nne sasa sababu ya mgomo wa madereva wa mabasi nchi nzima,” nilimwambia Adnan kwa huzuni
“Daah… Pole sana ndugu yangu, bahati mbaya na mimi naishia Kibiti. Lakini kama hutajali, naweza kukusogeza hadi hapo Kibiti najua ukifika hapo huwezi kukosa namna ya kufika jijini,” aliniambia Adnan huku akiniashiria nizunguke upande wa pili niingie kwenye gari.
Nami sikujivunga nilizunguka upande wa pili wa lile gari nikafungua mlango wa nyuma wa abiria na kupanda ndani ya gari.
Ndani ya gari lile kulikuwa na watu wengine watatu, mwanadada mmoja mrembo wa Kiarabu ambaye sikuweza kumtambua alikuwa ameketi kwenye siti ya mbele kushoto kwa dereva, na kwa mwonekano wa haraka tu ungeweza kubaini kuwa ki umri hakuwa amezidi miaka ishirini na nane.
Kwenye siti mbili za nyuma kulikuwa na kijana mdogo wa kiume ambaye nilipomtazama mara moja tu niliweza kuhisi kuwa alikuwa ni mtoto wa Adnan kwa kuwa walifanana sana.
Alikuwa na umri wa kukadiria wa miaka mitano hivi na alikuwa ameketi kwenye siti ya katikati na kando yake aliketi mwanadada mwingine mrembo wa Kiarabu ambaye nilipomuona tu nikamtambua mara moja kuwa alikuwa ni dada wa Adnan aliyeitwa Jameela.
Jamila alikuwa mdogo kwa Adnan, japokuwa wakati ule mimi na Adnan tulipokuwa tunasoma pale Benjamin Mkapa High School Jameela alikuwa bado yupo shule ya msingi, lakini sura yake haikuwa imebadilika, hivyo niliweza kumtambua mara moja.
Wakati naingia na kuketi kule nyuma, Jameela alikuwa akinitazama kwa tabasamu la bashasha, akanisalimu kwa bashasha zote huku akionekana kubabaika kidogo na utanashati wangu. Niseme tu kuwa nilikuwa miongoni mwa vijana wachache sana waliokuwa na mvuto wa hali ya juu kwa wasichana warembo wa sampuli ile ya Jameela.
Nami niliitikia ile salamu yake kwa bashasha na kumuuliza habari za siku nyingi lakini Jameela alinijibu kwa kifupi huku akionesha kuwa na uoga fulani hivi, mara kwa mara alikuwa akimtupia jicho la wizi Adnan, jicho lililokuwa limebeba hofu fulani.
Baada ya kusalimiana na Jameela niligeuza shingo yangu kumtazama yule mwanadada mwingine aliyekuwa ameketi kule mbele kushoto kwa dereva, nikamsalimia pia kwa bashasha ili isionekane kuwa nilikuwa nabagua. Wakati wote huo nikiwasalimia wale wasichana Adnan alikuwa kimya akinitazama kwa makini.
Nilipomaliza salamu Adnan akanitambulisha kwa yule mwanadada aliyekuwa ameketi kwenye ile siti ya abiria ya mbele kushoto kwake kuwa alikuwa ni mke wake, Ada Abdulaziz, na yule mtoto aliyekuwa ameketi kule kwenye siti ya nyuma alikuwa mtoto wao na alikuwa amempa jina la baba yake, Fahad.
Alipomaliza utambulisho ule akaniuliza kama na mimi nilikuwa nina mke na watoto. Swali lile likanifanya nitabasamu kidogo huku nikimtupia jicho la wizi Jameela ambaye wakati wote huo alikuwa anatabasamu tu huku akiviminyaminya vidole vya mikono yake kama mtoto aliyekuwa anadeka.
Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani kisha nikamjibu Adnan kuwa nilikuwa bado sijaoa na wala sikuwa na mchumba. Jameela akaonesha mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha na kuniuliza swali kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa nilikuwa sijaoa na sikuwa na mchumba?
Nilimjibu kuwa nilikuwa bado natafuta mwenza wangu kwa kuwa niliamini kuwa mke mwema hupatikana kwa subira na muda ukifika hakuna kitu ambacho kingenizuia kuoa. Nilisema na kuangua kicheko hafifu.
Wakati nilipokuwa nikiongea maneno yale niligundua jambo moja, ilionekana wazi kuwa swali la Jameela halikuwa limemfurahisha kabisa Adnan, kwani aligeuka na kumkata jicho lililoashiria kuchukizwa. Kwa swali lile ilionekana kana kwamba Jameela alikuwa amefanya dhambi fulani kubwa ambayo ilimshangaza hata shetani.
Nilibaki kimya na muda ule ule Adnan aliliondoa gari na safari ya kuelekea Kibiti ikaanza. Kuanzia hapo hakukuwa na stori tena, tulisafiri tukiwa kimya kabisa kwa kitambo kirefu hadi pale nilipoamua kuanzisha maongezi kwa kumuuliza Adnan ni wapi walikokuwa wakitoka.
“Tunatoka Lindi kwenye shughuli ya harusi ya mdogo wake waifu, tulienda juzi na ndoa ilikuwa jana,” Adnan aliniambia.
“Okay… na Kibiti kuna nini tena?” nilimsaili Adnan katika namna ya kutaka kuwachangamsha baada ya kuhisi hali fulani ya ukimya ndani ya lile gari.
“Ooh, hivi sijakwambia? Kabla mzee Fahad hajafariki dunia alikuwa kahamishia makazi yake Kibiti ambako alifungua miradi mbalimbali, ile nyumba ya Ilala aliamua kuipangisha,” alisema Adnan na kunifanya nishangae kidogo.
“Ooh, kumbe! Bahati mbaya tangu ulipoondoka kwenda South Africa nilifika mara moja au mbili tu pale nyumbani Ilala halafu nikakata mguu, hivyo nikawa sijui kinachoendelea,” nilimwambia Adnan.
“Kuna siku moja tu, nadhani ilikuwa mwaka juzi, nilikutana na kaka yako Feisal nikiwa katika mishemishe zangu, akaniambia kuwa bado uko South Africa,” nikaongeza.
“Kama ni mwaka juzi kweli nilikuwa South Africa. Hata hivvyo, mbona sikuondoka moja kwa moja, nilikuwa narudi nyumbani nakaa siku mbili tatu kisha kuondoka! Si unajua tena unapokuwa na mke hutakiwi kuwa mbali kipindi kirefu, utashangaa siku unarudi home unakuta mkeo ameolewa,” alisema Adnan huku akigeuza shingo yake kumtazama mkewe na kuachia kicheko hafifu.
Wote tukajikuta tukiangua kicheko. Lakini muda wote wa mazungumzo yetu Jameela alikuwa mkimya sana na sasa alikuwa ameegemeza vizuri kichwa chake kwenye siti huku akinitupia jicho la wizi mara kwa mara. Nilivyomchunguza niligundua kuwa alikuwa akitamani sana kuchangia maongezi lakini ni wazi alikuwa akimuogopa sana kaka yake.
Kutokana na hali ile hisia fulani hivi ndani yangu zikaanza kunipata na kunifanya nihisi hali isiyokuwa ya kawaida kukaa karibu na Jameela, ingawa hiyo haikuwa mara yangu ya kwanza kukaa karibu na Jameela, kwani alipokuwa akisoma Sekondari ya Kisutu, Adnan aliniomba niwe namfundisha hesabu kwa kuwa nilikuwa bingwa wa hesabu darasani.
Na kipindi chote hicho nilikuwa nikimchukulia kama dada yangu wa tumbo moja na yeye aliniona kama kaka yake, sawa na alivyokuwa akimchukulia Adnan, na sikuwahi hata siku moja kufikiria kama ningeweza kuanzisha uhusiano wowote wa kimapenzi na binti yule.
Hivyo nilianza kujiuliza kwa nini Jameela alikuwa akinitazama kwa jicho la aina ile tena kwa wizi kana kwamba alikuwa ameniona kwa mara ya kwanza! Hata hivyo, sikutaka kumnyima nafasi ile ya kunitazama, hivyo mara kwa mara nikawa nikizuga kutazama nje ya gari lile kupitia kioo kisafi cha dirisha.
Niligundua kuwa jicho la Jameela lilipokuwa likiniangalia kwa namna moja au nyingine lilikuwa linazidi kuamsha hisia zangu na kuyaruhusu mawazo mengi kuanza kupitia kichwani kwangu, nilianza kujiuliza maswali mengi pasipo kupata majibu: kwanza kwa nini alishangaa sana na kuonesha furaha pale aliposikia kuwa nilikuwa sijaoa na wala sikuwa na mchumba?
Je, swali lake kuwa iliwezekanaje kwa mwanaume mzuri kama mimi kusema kuwa sijaoa na sina mchumba liliashiria nini kwa mtazamo wake, kwamba sikupaswa kusema vile au ilikuwa ni dhambi kwangu kutokuwa na mke wala mchumba?
Maswali hayo na mengine mengi yalizidi kupita kichwani kwangu, hata hivyo, sikutaka kuyapa sana nafasi maana sikujua Jameela alikuwa anawaza nini juu yangu. Huenda aliniona kama kijana mhuni fulani asiyeweza kuishi na mwanamke au pengine nilikuwa mtu fulani asiye na mbele wala nyuma!
“Vipi hivi mnakabilianaje na hali hii mbaya ya kiusalama hapo Kibiti?” nilimuuliza Adnan baada ya kitambo kirefu cha ukimya ndani ya lile gari..
“Kwa kweli hali ni mbaya, hata hivyo serikali inajitahidi sana kudumisha usalama ingawa kuna kitu wengi hawakijui kuhusu haya mauaji yanayoendelea,” alisema Adnan na kunifanya nikae vizuri kusikia mambo niliyokuwa siyajui juu ya yale mauaji yale yaliyojumuisha maeneo yote ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji .
Itaendelea...