Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

Stori ya kijasusi - HEKAHEKA!

Bishop hii kitu ni balaa aisee, hivi ulishawahi kutoa vitabu kweli? Hii ni shida, sijawahi kuona sehemu ukiandika hivi vitu kabisa, na sijui jina lako halisi ni nani ila upo vizuri sana big up sana mkuu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Bishop hii kitu ni balaa aisee, hivi ulishawahi kutoa vitabu kweli? Hii ni shida, sijawahi kuona sehemu ukiandika hivi vitu kabisa, na sijui jina lako halisi ni nani ila upo vizuri sana big up sana mkuu

Sent using Jamii Forums mobile app
Hilo ndilo jina langu mkuu, popie kwani huoni kuwa mimi ni 'Verified Member', yaani mwanachama ambaye amethibitishwa kuwa jina analotumia humu ni lake, wala si jina bandia. Ninazo hadithi nyingi sana nilizotunga na kuzitoa kwenye magazeti, ila kwa sasa nafikiria kutoa vitabu...
 
HEKAHEKA! 26

Na Bishop Hiluka

“Chukua hivi vidonge vya kutuliza maumivu, ukimeza utapata nafuu kabisa,” aliniambia huku akinipa vidonge viwili vya kutuliza maumivu na bilauri ya maji.

Wakati nikivichukua vile vidonge na kuvitupia mdomoni niliitupia jicho saa yake aliyokuwa ameivaa mkononi na kugundua kuwa ilikuwa inasomeka saa tatu na robo.

Muda ule miale ya jua la saa tatu asubuhi ilikuwa imepenya dirishani na kutuama chumbani na kuenea hadi pale kwenye kitanda nilipolala. Ni dhahiri kuwa joto la miale ile ya jua la saa tatu asubuhi lilikuwa limeamsha homa hafifu mwilini mwangu.

Endelea...

Niligida mafunda kadhaa ya maji yaliyokuwa kwenye ile bilauri nikivisukumia ndani vidonge vile kisha nilimrudishia yule daktari ile bilauri huku nikimtazama kwa utulivu.

“Pole sana…” yule daktari aliniambia huku akiachia tabasamu la kirafiki. Kisha alitoa mashine ndogo ya kupimia shinikizo la damu na mapigo ya moyo.

“Samahani, nataka niangalie mwenendo wa presha na mapigo ya moyo wako…” alisema yule daktari.

Aliifunga ile mashine kwenye mkono wangu wa kushoto kisha akaanza kuipampu kwa muda na mara presha [pressure gauge] ikaanza kupanda juu.

Niliyafumba macho yangu huku nikibana pumzi kutokana na ile mashine kuanza kubana kwenye mkono wangu na kusababisha maumivu kidogo.

Baada ya kitambo fulani yule daktari alianza kulegeza taratibu kifungo fulani kidogo kilichokuwa pembeni, mara nikasikika sauti ya ‘hisssiii’ huku pressure gauge ikishuka taratibu, na wakati huo namba zilikuwa zikijiandika kwenye kioo kidogo juu ya ile mashine.

Nilikuwa makini kutazama pale kwenye namba lakini niliishia kuona maandishi SYS 110 na chini yake kukiwa na maandishi DIA 60, huku chini zaidi kukiwa na maandishi PULSE 72. Hata hivyo, sikujua maana yake ila nilihisi kuwa zile namba zilimaanisha presha ya damu yangu na mapigo ya moyo.

Nikamuona akiweka rekodi kwenye faili alilokuja nalo na kunitazama.

“Naona presha yako inaanza kuimarika, una 110 juu ya 60 ambayo siyo mbaya na moyo wako unapiga mara 72 kwa dakika,” alisema na kuchukua vifaa vyake kisha akaanza kupiga hatua zake haraka kuondoka, sikutaka aondoke bila kunitegulia kitendawili changu, hivyo nikamtupia swali.

“Samahani dokta, hapa nipo wapi?” nikamuuliza huku hofu ikinitambaa taratibu.

Yule daktari aligeuza shingo yake na kunitazama kwa kitambo kisha nikamuona akishusha pumzi za ndani kwa ndani. Hata hivyo sikuweza kuona tashwishwi yoyote usoni kwake.

“Usijali, utafahamu baadaye kidogo, ila upo kwenye mikono salama,” alijibu na kuanza kuondoka haraka lakini nikamwita tena kitendo kilichomfanya ageuke tena kunitazama huku akionesha uso wa mashaka kidogo.

“Nini kilitokea na hapa ni wapi?” nilimuuliza tena yule daktari huku nikiyapuuza maneno yake na kumkazia macho, na hapo nikamuona akiyakwepa macho yangu na kutazama kando huku akishusha pumzi ndefu.

“Kwani tatizo lako nini? Nimekwambia uko kwenye mikono salama,” aliongea kwa ukali kidogo yule daktari huku akionekana kuanza kukerwa na maswali yangu, kisha aliyapeleka macho yake kutazama dirishani kama mtu aliyekuwa anawaza jambo fulani.

“Nisamehe, sikupaswa kukujibu kwa ukali,” alisema yule daktari huku akijipiga kofi dogo kwenye paji lake la uso kisha akapandisha mabega yake juu na kushusha pumzi ndefu.

“Kwani nimelazwa hapa tangu lini?” nilimuuliza tena huku nikiendelea kuyapuuza maneno yake na kumkazia macho.

“Leo ni siku ya nne tangu uletwe hapa,” yule daktari alinijibu huku akishika kitasa cha mlango na kukinyonga. Kabla hajatoka kabisa nikaongea neno lililomfanya ageuke tena kunitazama.

“Dokta nasikia njaa.”

“Usijali utaletewa chakula sasa hivi,” alisema yule daktari na kutoka nje haraka, ilionekana kama vile hakupenda kuulizwa maswali.

Mara tu yule daktari alipoondoka mle chumbani ile hali ya upweke ikanirudia tena pale kitandani huku nikiupisha utulivu kichwani mwangu.

Nilibaki nikiwa nautazama ule mlango huku nikizidi kuhisi kuchanganyikiwa kidogo kutokana na tabia ya yule daktari ya kuonesha kuyakwepa maswali yangu na kutotaka kuongea na mimi.

Na hapo fikra zangu zikahamia kutafakari juu ya Madame Pamela na wale makomandoo waliokuwa wakinitesa kwa kuwa nilionekana gaidi mwenye taarifa nyeti ambazo serikali ilizihitaji kwa gharama yoyote. Je, Madame Pamela aliwezaje kuniacha hai?

Kisha likanijia swali, je, ni nani wale walioingia ndani ya kile chumba na kumtaka Madame Pamela asitishe mateso wakati nilipokuwa nateswa kwa kupigwa shoti ya umeme ndani ya lile tangi la maji? Kwanini walimtaka Madame Pamela asitishe kunitesa?

Nilizidi kushangaa, sikusita kujiuliza ni nani aliyelipia gharama zote za matibabu yangu kwa kipindi chote cha siku nne tangu niletwe pale!

Nilishusha pumzi za ndani kwa ndani huku moyo wangu ukiendelea kupoteza utulivu, hasa nilipokumbuka kauli ya Madame Pamela aliponiambia kuwa ‘hatajali kuhusu kifo changu, ikiwa sitaki kusema ukweli ni lazima ningekufa tu’!

Hata hivyo akili yangu ilianza kugoma kuamini kama nilikuwa hai nikihudumiwa kwenye chumba kilichokuwa na mifumo ya kisasa kabisa ya uchunguzi kwa mgonjwa. Nikajikuta nikibaki kwenye mkanganyiko usioelezeka, huku akili yangu ikianza kuniambia kuwa huenda pale nilikuwa ndotoni.

Ili kuhakikisha kama kweli sikuwa naota nikajifinya kidogo kwenye shavu langu la kushoto ili nione kama sikuwa naota. Finya yangu ya mashaka ilinifanya nitumie nguvu kubwa na hivyo nilipata maumivu makali sana.

“Ooh shit!” nikang’aka kwa sababu ya maumivu makali niliyoyahisi.

Ni kweli sikuwa naota na nilikuwa hai lakini swali lililoendelea kunisumbua lilikuwa, niliokokaje kutoka kwenye kifo kilichotokana na mateso makali na hata kuteswa kwenye kiti cha umeme kabla sijatumbukizwa kwenye tangi lililojazwa maji lililounganishwa na mfumo wa umeme? Jambo hilo likabaki kuwa kitendawili!

Hali ile ikasababisha jasho jepesi lianze kunitoka sehemu mbalimbali za mwili wangu japo mle ndani hakukuwa na joto, aina fulani ya joto la woga wa aina yake lilinitambaa mwilini na mapigo ya moyo wangu yakaanza kwenda mbio isivyo kawaida!

Kila nilipomfikiria Madame Pamela nilijikuta nikikosa amani, nikahisi kuwa japo nilikuwa hai lakini hicho kisingekuwa kigezo tosha cha kunifanya niamini kuwa nilikuwa katika mikono salama. Kwa hiyo nikajionya kuwa makini zaidi.

Hata hivyo, sikuwa na namna yoyote ya kufanya kwani chochote ambacho kingeweza kutokea nilipaswa kukabiliana nacho maana kama Madame Pamela na wale makomandoo wangetaka kunidhuru au kuniua wasingeshindwa, kwani uhai wangu ulikuwa mikononi mwao.

Hatimaye nikameza funda kubwa la mate nikijitahidi kuyachuja mawazo yale kichwani mwangu na wakati huo zile dawa za kutuliza maumivu nilizomeza zikifanya kazi yake mwilini mwangu.

Na muda ule ule nikashuhudia tena kitasa cha mlango wa kile chumba kikizungushwa taratibu kisha ule mlango ukasukumwa ndani na kufunguka.

Nilimuona mwanamke mmoja mnene ambaye niliweza kumtambua kwa mavazi yake kuwa ni muuguzi akiingia mle ndani huku akiwa amebeba kikapu kilichokuwa na hotpot dogo la chakula, mabakuli mawili yaliyokuwa na mfuniko, sahani, kijiko kikubwa cha kupakulia na kingine cha kulia chakula.

Nyuma ya yule muuguzi alifuatia yule daktari aliyetoka mle chumbani dakika kadhaa zilizokuwa zimepita akiwa amebeba bilauri pamoja na chupa kubwa ya maji ya kunywa.

Waliingia na kuviweka vile vyombo juu ya meza ndogo kando ya kile kitanda. Moyo wangu ulilipuka kwa furaha baada ya kuona kile chakula nikajua sasa nipo salama, lakini furaha yangu ikayeyuka ghafla baada ya kumuona Madame Pamela akiingia huku ameongozana na walinzi wawili.

Itaendelea...
 
HEKAHEKA! 27

Na Bishop Hiluka

Nyuma ya yule muuguzi alifuatia yule daktari aliyetoka mle chumbani dakika kadhaa zilizokuwa zimepita akiwa amebeba bilauri pamoja na chupa kubwa ya maji ya kunywa.

Waliingia na kuviweka vile vyombo juu ya meza ndogo kando ya kile kitanda. Moyo wangu ulilipuka kwa furaha baada ya kuona kile chakula nikajua sasa nipo salama, lakini furaha yangu ikayeyuka ghafla baada ya kumuona Madame Pamela akiingia huku ameongozana na walinzi wawili.

Endelea...

Madame Pamela alikuwa amevaa suti nadhifu ya kike ya rangi ya kijivu ya ‘single button’ iliyokuwa imemkaa vyema na kumpendeza sana, wale walinzi wake pia walikuwa wamevaa suti nyeusi na miwani myeusi.

Moyo wangu ukapiga kite kwa sekunde kadhaa huku nikihisi mwili wangu ukifa ganzi na mara ubaridi fulani wa aina yake ukaanza kunitambaa mwilini huku mapigo ya moyo wangu yakibadili mwendo wake na kuanza kwenda mbio isivyo kawaida!

Nikabaki nimemtumbulia macho Madame Pamela kana kwamba nilikuwa nimemuona zaraili mtoa roho. Mwanzoni sikuona tashwishwi yoyote kwenye uso wake, bali alisimama akawa akinitazama kwa makini.

Wasiwasi mwingi ukanijaa, nikaanza kuhisi kuwa nilikuwa nimefuatwa kwa ajili ya mahojiano kwa mara nyingine na ikiwezekana nipate mateso makali kuliko niliyopata mwanzo hadi nicheue taarifa walizokuwa wakizihitaji.

Nilifungua mdomo wangu kutaka kusema lakini nikajikuta nikibaki mdomo wazi huku donge la fadhaa likinikaba kooni.

Hata hivyo, tabasamu jepesi la upendo nililoliona usoni kwa Madame Pamela na macho yake makubwa yaliyonitazama kwa upole tofauti na siku ile ya kwanza alipokuwa akinihoji kwenye kwenye chumba cha mateso makali, vikaufanya moyo wangu utulie kidogo.

“Unaendeleaje, Bwana Maximilian?” Madame Pamela akaniuliza kwa sauti ya upole huku akitabasamu.

Swali lake likanishtuka sana, mwanzoni nilidhani kuwa labda nilikuwa sijasikia vizuri aliponiita kwa jina la Maximilian badala ya jina la Brown Senga walilokuwa wakiniita mwanzo!

Nikafungua mdomo wangu kutaka kujibu lakini nilijikuta nikishindwa kusema chochote kwa kuwa nilikuwa njia panda. Kwa kweli sikumwelewa kabisa huyu mwanamke!

Wazo la kwamba labda nilikuwa ndotoni likanijia tena lakini akili yangu ikakataa, hivyo mara hii milango yangu ya fahamu ikawa makini zaidi huku nikiishirikisha akili yangu kikamilifu katika kuniletea taarifa sahihi za kuaminika kama nilichokisikia kutoka katika kinywa cha Madame Pamela kilikuwa sahihi au lah!

“Usihofu, najua una maswali mengi sana akilini mwako na pengine unadhani labda uko ndotoni,” alisema Madame Pamela akiniangalia kwa uyanikifu huku akionekana kuyasoma mawazo yangu.

“Pole sana,” alisema tena kwa sauti ya upole baada ya kuniona nikiwa bado nipo kimya huku nikimkodolea macho. Na hapo akaufanya moyo wangu ulipuke kwa furaha isiyopimika.

“Ahsante,” nikamjibu huku nikijaribu kuyasoma mawazo yake kuona kama uso wake ulimaanisha kile alichokuwa akikisema au lah!

Kuna wakati nilidhani labda alikuwa akinitega ili kujua kama nimepata nafuu ili nirudishwe tena katika chumba cha mateso makali kuhojiwa.

“Pole kwa yote yaliyotokea, nilipopata taarifa kuwa unaendelea vizuri nikashukuru sana, na nilipoambiwa kuwa umeamka nikaona vema nije mwenyewe kukuona na kuongea na wewe mambo fulani…” alisita kidogo na kugeuza shingo yake kuwatazama wale watu wengine waliokuwemo mle ndani ya kile chumba.

“Nahitaji nafasi kidogo ya kuongea na Maximilian, kama hamtojali,” alisema Madame Pamela akiwaambia wale watu huku akisogea na kuketi kwenye kiti kilichokuwa kando ya kile kitanda.

Niliwaona yule daktari, muuguzi na wale walinzi wake wawili wakitoka ndani ya kile chumba na kutuacha peke yetu, hapo nikajikuta nikianza kufarijika zaidi na tukio lile la kuondoka kwa wale walinzi wa bosi wa usalama wa taifa na kutuacha peke yetu.

Kisha Madame Pamela aligeuka kunitazama kwa makini akionekana kama aliyekuwa akiwaza mbali sana au akijishauri jambo kama aniambie au la.

Hata hivyo, sikuthubutu kufungua mdomo wangu kuongea chochote bali nilibaki kimya nikimtumbulia macho bila kusema chochote. Kikapita kitambo kifupi cha ukimya kisha kama aliyegutuka alitaka kusema neno lakini akasita na kuvitazama vile vyombo vya chakula vilivyokuwa juu ya meza.

“Samahani, unapaswa kula kwanza ili upate nguvu kisha tutaongea, maana niliambiwa una njaa sana,” alisema Madame Pamela huku akiinuka na kulifunua lile hotpot.

Nilipotupa jicho langu kuangalia ndani ya lile hotpot nikagundua kuwa kulikuwa na mchemsho wa ndizi na samaki aina ya sato. Pia aliyafunua yale mabakuli mawili yaliyokuwa na mifuniko, bakuli moja lilikuwa na mboga za majani na saladi na jingine lilikuwa na matunda mchanganyiko.

Kwa msaada wa Madame Pamela nilifanikiwa kunyanyuka kidogo na kukiegemeza kichwa changu kwenye mto niliokuwa nimeugemezea ukutani pembeni ya kitanda. Wakati huu nilisikia kichwa changu kikipwita kwa maumivu kana kwamba nilikuwa nimebebeshwa mzigo mzito sana.

Madame Pamela akachukua sahani na kijiko kikubwa na kuanza kunipakulia chakula kisha akaonja kidogo na kunipa huku akionekana kukifurahia sana kile chakula.

Nami sikujivunga, nikakipokea kile chakula na kwa kuwa nilikuwa nina njaa sana, nilikifakamia bila kujali maumivu ya mwili niliyokuwa nayo wakati huo.

Wakati nakula kile chakula Madame Pamela alikuwa akiniangalia kwa uyakinifu sana katika namna ambayo sikuweza kuielewa na sikujua alitaka kuongea nami kuhusu nini. Hata hivyo, sikutaka kuisumbua tena akili yangu kuwaza, yote niliamua kumwachia Mungu.

Nilimaliza kula kile chakula ambacho kiukweli kilikuwa kitamu sana, kisha Madame Pamela akavitoa vile vyombo na kuvisogeza kando.

Kikapita tena kitambo kirefu cha ukimya, hakuna aliyesema neno kati yetu. Na baada ya muda mrefu nikamuona akivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu huku akikohoa kusafisha koo lake. Hapo nikajua sasa mahojiano yameanza.

“Maximilian… ni kwamba tangu tulipokukamata pale uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere hatukuridhika bali tuliendelea kuchunguza, hivyo ilibidi nitume watu wangu kufuatilia kwa umakini mkubwa taarifa zako kwenye ubalozi wetu huko Amsterdam na kwingineko, kwa mujibu wa taarifa za kiintelijensia zilizokuwa zimetufikia…” hatimaye alivunja ukimya Madame Pamela.

“Hadi wakati ule nakuja pale CMI kwenye chumba cha mateso bado taarifa tulizokuwa tukizipata kuhusu wewe zilikuwa zikitukanganya kidogo, kiasi kwamba ilinishangaza sana kuona uliwezaje kuwepo katika maeneo zaidi ya moja kwa wakati mmoja! Nikahisi huenda wewe si binadamu wa kawaida!

“Muda ule nilipokuwa nakuadhibu mle kwenye lile tangi la maji waliingia maofisa wetu wawili wa usalama waliokuja na taarifa fulani za kiitelijensia zilizonifanya kusitisha yale mateso, ingawa tayari ulikuwa umepoteza fahamu baada ya kupigwa na shoti ya umeme na hali yako ilikuwa mbaya sana,” alisema Madame Pamela kwa huzuni.

“Kwa kifupi tu, taarifa hizo zilihusu kugunduliwa kwa eneo ambalo zilikuwa zimefichwa silaha ambazo ndizo zilizokuwa zimeibwa kule kwenye bohari ya silaha na zilikuwa zitumike kufanyia ugaidi, hivyo nikawaamuru wale makomandoo wakuwahishe hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya matibabu lakini wakihakikisha unawekewa ulinzi ili usiweze kutoroka hadi pale tutakapojiridhisha na zile taarifa kisha tukufungulie mashtaka ya ugaidi,” alipofika hapo aliweka kituo na kuangalia kando huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kuwaza mbali kidogo.

Kauli hiyo ikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, hofu ikiwa imeanza kuniingia moyoni nikamtazama Madame Pamela kwa wasiwasi huku nikianza kuhisi hali ya hatari iliyokuwa ikinikabili.

Itaendelea...
 
HEKAHEKA! 28

Na Bishop Hiluka

“Kwa kifupi tu, taarifa hizo zilihusu kugunduliwa kwa eneo ambalo zilikuwa zimefichwa silaha ambazo ndizo zilizokuwa zimeibwa kule kwenye bohari ya silaha na zilikuwa zitumike kufanyia ugaidi, hivyo nikawaamuru wale makomandoo wakuwahishe hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo kwa ajili ya matibabu lakini wakihakikisha unawekewa ulinzi ili usiweze kutoroka hadi pale tutakapojiridhisha na zile taarifa kisha tukufungulie mashtaka ya ugaidi,” alipofika hapo aliweka kituo na kuangalia kando huku akivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu akionekana kuwaza mbali kidogo.

Kauli hiyo ikaufanya moyo wangu upige kite kwa nguvu huku kijasho chembamba kikianza kunitoka, hofu ikiwa imeanza kuniingia moyoni nikamtazama Madame Pamela kwa wasiwasi huku nikianza kuhisi hali ya hatari iliyokuwa ikinikabili.

Endelea...

Nilimkodolea macho kwa wasiwasi kama vile nimeona guruneti lililokuwa limetelekezwa mle chumbani na magaidi wa kundi la al-Shabab na wakati wowote lilitaka kulipuka. Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu la kirafiki ili kunitoa hofu.

“Mchana wa siku ile kuna vijana wadogo walikuwa wanachunga mifugo yao katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani, eneo ambalo ni karibu na kijijini kwao! Wakati wakiwa ndani ya huo msitu wa Kazimzumbwi wakaokota bomba la PVC lililokuwa limefichwa, na baada ya kulifungua ndani walikuta lilikuwa na bastola na vitu vingine kadhaa vilivyowatia shaka.

“Wale vijana wakawataarifu wazazi wao ambao nao wakautaarifu uongozi wa serikali ya kijiji, ndipo ikashauriwa vitu vile vipelekwe polisi! Baada ya vitu hivyo kupelekwa polisi, vikachunguzwa na kukakutwa ramani ambayo polisi waliitilia shaka.

“Haraka sana polisi waliifuatilia ile ramani ndipo ikawapeleka moja kwa moja kwenye handaki dogo ndani ya ule msitu wa Kazimzumbwi. Kutokana na vitu vilivyokutwa ndani ya lile handaki polisi wakapata wasiwasi kuwa inawezekana walikuwa wanashughulika na jambo kubwa na nyeti zaidi kuliko uwezo wao, kwani kiliwachostaajabisha ni kuwa handaki lile lilichimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo na lilikuwa lina mpangilio wa hali ya juu wa kiwango cha kijeshi. Na hapo ndipo idara yetu ilipotaarifiwa kuhusu jambo hili,” alinyamaza Madame Pamela na kuinuka kisha akaanza kupiga hatua akizunguka zunguka mle ndani.

Nilibaki kimya nikimtazama Madame Pamela kwa wasiwasi, sikujua kwanini alikuwa akinieleza yale yote, na sikujua kama bado walikuwa wakidhani kuwa nilikuwa nahusika na uhalifu ule, hivyo alikuja ili nimpe taarifa nyingine zaidi! Muda huo huo nikahisi tena ubaridi wa woga wa aina yake ukinitambaa taratibu mwilini.

Niliendelea kumtazama Madame Pamela wakati akizunguka zunguka kwa muda mle chumbani kisha akageuka kunitazama huku akilamba midomo yake iliyoanza kukauka.

“Tulipopewa taarifa zile haraka sana niliwatuma watu wangu huko na walipowasili iliwachukua saa kadhaa tu kung’amua kuwa vitu walivyovikuta ndani ya lile handaki dogo vilikuwa vinahusiana moja kwa moja na mtu anayeitwa Brown Senga au Godwin Sengerema, vitu ambavyo imetuchukua muda mrefu tukihangaika kutafuta taarifa zake. Kisha watu wangu wakachunguza alama za vidole walizozikuta kwenye lile handaki na zilionekana kutofautiana sana na alama zako za vidole jambo lililozidi kutuchanganya, lakini alama zile zilifanana sana na alama za vidole kwenye nyaraka za Brown Senga.

“Ndipo tulipoanza kuhisi kuwa ninyi ni watu wawili tofauti ingawa mnafanana sana kwa karibu kila kitu. Mle ndani ya lile handaki pia tulikuta kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini, pia taarifa za uwepo wa mahandaki mengine mawili ya aina ile, moja likiwa katika pori la Hifadhi ya Moyowosi mkoani Kigoma na jingine likiwa wilayani Kongwa katika mkoa wa Dodoma, yote yalifanana kwa jinsi yalivyochimbwa kiustadi na kujengewa kwa ndani kwa vitofali vidogo vidogo kama lile lililokutwa katika msitu wa Kazimzumbwi mkoani Pwani…” alinyamaza na kumeza mate.

Nilibaki hoi kwa taarifa zile za kiintelijensia ambazo zilisababisha nywele zangu zisisimke kichwani.

Madame Pamela alinitazama kwa makini na kuachia tabasamu pana la kunifariji kisha akasogea pale kwenye kiti na kuketi tena.

“Nimekueleza yote haya ili ufahamu ni kwa namna gani hatulali kuhakikisha nchi hii inakuwa salama lakini wakati mwingine tunakuwa katika mazingira tata yenye mkanganyiko wa taarifa, hasa kwa mambo makubwa kama haya yanayohusu usalama wa nchi na wananchi wake,” alisema Madame Pamela na kuweka tena kituo.

“Kwa kutumia taarifa zilizokuwa ndani ya kile kijarida kidogo kinachohusu kituo cha siri cha mafunzo ya karate na ujasusi nchini tukaanza kumfuatilia Brown Senga mpaka tukafanikiwa kumpata na kumkamata akiwa kajichimbia mafichoni Dodoma kwenye maktaba yake ya siri iliyosheheni nyaraka mbalimbali za kijasusi, na ndani ya maktaba hiyo kulikuwa na kila kitu ambacho angekihitaji, silaha, nyaraka za kijasusi, kifurushi cha kujikimu, dawa za dharura za huduma ya kwanza, fedha nyingi za kigeni na za Tanzania nadhani ni zile zilizoporwa katika Benki ya Wananchi…

“Pia kulikuwa na majarida ya mazoezi ya kawaida na ya kijeshi na vitu vingine vingi ikiwemo mtambo maalumu wa udukuzi wa mawasiliano wa Satellite GPS and Traces wenye mvuto wa hatari uliotengezwa kwa madini ya Uranium ambao ulikuwa umefungwa kwenye kompyuta maalumu ukifanya kazi ya kufuatilia taarifa na mawasiliano yote ya simu, kompyuta na vifaa vyote vya kielektroniki viwezavyo kutumia Intaneti…

“Tulimkamata wakati akiandaa mkakati wa mwisho wa namna ya kutekeleza tukio kubwa la mauaji ambayo angeyafanya kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wiki ijayo katika siku ya Mei Mosi, kwani walitega mabomu mawili yenye nguvu kubwa karibu na jukwaa kuu na alikuwa na saa ambayo akiibonyeza tu yanaanza kujihesabu na ikifika kumi yangelipuka na kuifanya nchi hii iingie kwenye taharuki isiyoelezeka… kama hufahamu siku ya Mei Mosi ni siku kubwa sana ya wafanyakazi ambayo inakusanya wafanyakazi na viongozi mbalimbali wa serikali kwa ajili ya kusherehekea, na mwaka huu imepangwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye atakayekuwa mgeni rasmi siku hiyo.

“Mpango huo wa mauaji ulikuwa umepewa jina la ‘Operation Underground Elimination’ na ndani ya huo mpango kulikuwa na orodha ya washirika wote katika mtandao wa kigaidi aliouongoza, baadhi yao ni wanasiasa, maofisa wa jeshi, vigogo waliowahi kutumbuliwa serikalini kwa tuhuma mbalimbali, wafanyabiashara wakubwa na watu kutoka nje ya nchi waliopewa jina la ‘wafadhili’. Wengi wao hasa waliopo hapa nchini tayari tumekwisha wakamata na wengine bado tunawasaka kwa udi na uvumba popote walipo duniani, tutawakamata na kuwafikisha katika mahakama ya ugaidi.”

Kauli ile ya Madame Pamela ikawa imeamsha nguvu mpya kwenye mwili wangu na hapo hapo nikajihisi kupona.

“Kwa kuwa wewe umeingia kwenye matatizo haya makubwa yaliyokaribia kuyagharimu maisha yako kutokana na kufanana sana na Brown Senga, Rais amenituma nije kukuomba radhi na kukueleza kuwa serikali inaomba radhi na itakupa dola laki moja za Marekani kama fidia,” alisema Madame Pamela na kusimama.

Nilijikuta nikiyasahau machungu yote kutokana na furaha kubwa niliyokuwa nayo, kisha kitambo kifupi cha ukimya kikapita tena mle ndani huku wote tukizama kwenye tafakuri. Madame Pamela alinitazama jinsi nilivyokuwa nikionesha furaha isiyoelezeka.

Nilifungua mdomo nikataka kusema lakini sauti ikagoma, nilikosa kabisa neno la kusema na hivyo nikajikuta nikiwa nimeganda kama sanamu nikimkodolea macho yule bosi wa usalama wa taifa utadhani nilikuwa nimegeuka sanamu!

Mara kikohozi kidogo kikanitoka, na nyuma yake wimbi la machozi ya furaha lilikuja mbio, machozi ya furaha yakamwagika na kuanza kulowesha mto niliokuwa nimeegemeza kichwa changu utadhani milizamu iliyopasuka.

Nilijaribu kuyazuia machozi lakini nikashindwa, sikuwa na namna nyingine yoyote ya kuyazuia yasitoke, hivyo niliyaacha yamwagike huku nikiendelea kumtumbulia macho yule bosi wa usalama wa taifa bila kusema chochote.

Muda wote Madame Pamela alikuwa akinitazama kwa tabasamu kisha akatoa simu ya mkononi kutoka kwenye mkoba wake na kunipa. Nilipoitazama vizuri ile simu nikagundua kuwa ilikuwa ni simu yangu iliyochukuliwa pale uwanja wa ndege na watu wa usalama nilipokuwa nahojiwa.

“Kwa sasa unaweza kuwasiliana na yeyote utakaye, tumekwisha wasiliana na familia yako na kuwaeleza kuwa ulipofika Dar es Salaam ulipata matatizo ya kuvamiwa yaliyosababisha ulazwe hospitali, hatukutaka kuwaeleza jinsi tukio lilivyotokea kwani haya mengine yatabaki kuwa siri kati ya serikali na wewe,” alisema.

Nikashusha pumzi za ndani kwa ndani huku nikiachia tabasamu.

“Halafu huwezi kuamini, kumbe wewe ni kaka binamu, babu yako mzaa mama na babu yangu mzaa baba walizaliwa kwa baba mmoja na mama mmoja! Mungu akuponye haraka, mdogo wangu, na nimeambiwa kuwa huenda ukaruhusiwa kutoka hospitali baada ya siku tatu au nne kama hali haitabadilika. Nitarudi tena baada ya siku mbili kukuona,” alisema Madame Pamela na kunipapasa kwenye paji langu la uso katika namna ya upendo.

Kisha alipiga hatua zake taratibu kuufuata mlango na alipoufikia alishika kitasa cha ule mlango na kukinyonga taratibu, mlango ukafunguka, akachungulia nje na kugeuka kunitazama kwa tabasamu.

“Nilisahau kukwambia, Susan na Pamela wapo hapa kukuona,” alisema na kutoka nje akiuacha mlango wazi, na muda huohuo nikamuona mchumba wangu Susan na binti yetu Pamela wakiingia. Nilipata mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha isiyoelezeka.

“Asante Mungu,” nilijikuta nikisema kwa furaha huku nikiwatazama kwa makini na kushusha pumzi ndefu za ndani kwa ndani. Machozi ya furaha yakaanza tena kunitoka na kuulowesha mto niliolalia.

MWISHO.

0685666964 au bjhiluka@yahoo.com
 
Sawa
HEKAHEKA!

Na Bishop Hiluka
0685666964


Dondoo:

Wanamwita “Gaidi Mstaarabu” kwa kuwa ni mpole, mcheshi na mstaarabu sana! Mafunzo ya kijajusi aliyoyapata katika nchi za Israel na Libya yamemfanya kuwa mwanamkakati mzuri sana wa matukio ya kihalifu na kuidhihirishia dunia kuwa hakujapata kuwepo mhalifu kama yeye…

Je, nini kipo nyuma ya masimulizi haya? Ni nani huyu gaidi mstaarabu? Fuatilia simulizi hii mwanzo hadi mwisho...

Angalizo: Inawezekana ukakuta baadhi ya matukio katika masimulizi haya yanafanana na mambo uliyowahi kuyasikia au kuyashuhudia, hii ni kwa sababu wazo la hadithi hii limetokana na baadhi ya mambo ya kweli yaliyowahi kutokea sehemu fulani. Majina yaliyotumika katika hadithi hii ni ya kubuni, na kama itatokea yamefanana na mtu yeyote mahali popote au kwa namna yoyote matukio katika hadithi hii yakatokea kumgusa yeyote basi itakuwa ni kwa bahati mbaya tu, wala halikuwa kusudio langu...

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom