Imeandikwa na Basil Msongo, Dodoma; Tarehe: 13th April 2011
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, leo amepata wakati mgumu kuongoza kikao cha uchaguzi wa wajumbe kwenye taasisi mbalimbali za kibunge kwa kuwa wabunge walikuwa wanajibishana na kusababisha vurugu bungeni.
Msitumie wingi wenu kutuburuza, mmezoea kutuburuza, tufunge mlango tupigane walisema wabunge na kusababisha vurugu bungeni kwa takribani dakika kumi.
Mabishano hayo yalisababisha Spika akasirike na kuwaeleza wabunge kuwa walikuwa wanafanya mambo ya kijinga.
Vurugu hizo zilianza baada ya Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), kusema bungeni kuwa, mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi hizo ulifanywa kwenye dark market.
Wabunge wanaoaminika kuwa ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walishinikiza Mbunge huyo afute kauli yake, Makinda akamtaka Wenje afute kauli yake.
Wenje alisimama lakini hakufuta kauli yake, baadhi ya wabunge wakawa wanapiga kelele kushinikiza afukuzwe wakitumia maneno out out out, atoke nje .
Wabunge hao walimtaka Mbunge huyo atoke, akanywe kikombe cha Babu, Loliondo.
Mara kwa mara Spika alilazimika kuwatuliza wabunge kwa kuwataka wamsikilize Mbunge aliyekuwa anazungumza.
Makinda aliwaeleza wabunge kuwa wanapaswa kutambua kuwa wananchi wamewachagua, na walikuwa wanawaangalia.
Kwa nini mnafanya fujo isiyokuwa na akili
waheshimiwa wabunge tunafanya mambo ya kijinga alisema Makinda lakini wabunge waliendelea kurushiana maneno.
Kwa mara nyingine Spika alimtaka Wenje afute kauli yake kwa kumweleza kuwa alikuwa amemtukana yeye Makinda na wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi ya Bunge.
Alimweleza Wenje kuwa wao wote ni watu wazima na ni jambo la kawaida kwa Mbunge kufuta kauli bungeni.
Alimuuliza Wenje kwamba ingemgharimu shilingi ngapi kufuta kauli yake, na akamuuliza Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kama Mbunge huyo angefanya hivyo, ingemgharimu kiasi gani.
Baadhi ya wabunge waliendelea kushinikiza Wenje afukuzwe, na kelele hizo zilizidi baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, kumweleza Spika kuwa ulikuwa wakati mwafaka kwake kumuamuru Wenje atoke nje ya Bunge.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, alisema ni kweli Kamati ya Uongozi ya Bunge ilikutana kuzungumzia suala hilo, lakini hazikutolewa fomu ili wagombea wajaze.
Zitto alisema, kamati hiyo si dark market lakini haikuwa sahihi kuitafsiri visivyo kauli ya Wenje, wao (wabunge) wote ni wanasiasa, wawe na ngozi ngumu.
Baadhi ya wabunge waliendelea kusisitiza kuwa Wenje atoke, Zitto akawajibu kuwa hatoki, na wabunge wengine wakasema hatoki mtu, tutatoka wote
Makinda alimpa Wenje fursa nyingine ya kufuta kauli yake, Mbunge huyo akasema, hakusema Kamati ya Uongozi ni dark market, ila alimaanisha mchakato uliotumika, ma mwishoni akasema, anafuta maneno dark market, anaweka white market.