PostGE2025 SMS moja iliwanyamazisha Wanahabari wengi wa Iringa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025

PostGE2025 SMS moja iliwanyamazisha Wanahabari wengi wa Iringa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2025

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections

Nchachali

New Member
Joined
Nov 29, 2025
Posts
3
Reaction score
2
Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Mwaka 2025 umeacha kovu ambalo halitafutika kirahisi si tu kwa sisi walaji wa habari, bali kwa Wanahabari wenyewe ambao wamejikuta wakivunjwa moyo, wakinyimwa nafasi ya kutumia kalamu zao, na wakidhalilishwa hadharani katika taaluma waliyoiamini.

Katika kipindi ambacho Taifa lilihitaji sauti za kuaminika, simulizi za Wanahabari zilififishwa kimyakimya, kulitanda ukimya mzito usioitwa kwa jina lolote ukimya usiotokana na kukosekana kwa habari, bali ule uliosababishwa na hofu iliyowazunguka kama wingu jeusi juu ya vichwa vyao.

Siku ya pili tu baada ya Uchaguzi (Oktoba 30, 2025), baadhi ya wamiliki wa Vyombo vya Habari walipokea simu kutoka “Mamlaka Inayosimamia Media hizo”, haikuwa ushauri, wala maelekezo ya kiufundi, ilikuwa ni kauli ya moja kwa moja:

“Msiongee chochote kuhusu uchaguzi. Msishirikiane na Vyombo vya Habari vya Kimataifa.”

Katika nchi inayotaka kuheshimu uhuru wa habari, maneno kama haya yanakata kama upanga unaovunja uhalisia wa taaluma.
IMG_3920.jpg
Wanahabari walibaki wameduwazwa, wengine waliniambia waziwazi kuwa kwa mara ya kwanza, vifaa vyao vya kazi kamera, kalamu, maikrofoni vilihisi kama mzigo unaoweza kuwasukumia matatani sekunde yoyote ile, kila sentensi waliyotaka kuiandika iliwalazimu kuangalia nyuma mara mbili.

Kila swali walilojaribu kuuliza, walilazimika kuvuta pumzi kwanza, hawakuwa wajinga wa taaluma, walikuwa tu wamefungwa na mipaka isiyoonekana ambayo iliwapokonya pumzi ya uandishi.
IMG_3917.jpg
Na hali haikuishia hapo
Kuna ndugu yangu mmoja aliyeniambia kuwa kipindi cha mchakato wa kusaka wagombea, kulikuwa na taarifa za baadhi ya Wanasiasa kujihusisha na vitendo vya rushwa, baadhi ya waandishi walijitahidi kuzifikisha taarifa hizo kwa mamlaka husika kwa nia njema ya kulinda maadili ya uchaguzi, lakini badala ya kuungwa mkono, walijikuta wakipokea ujumbe mfupi wa vitisho kutoka kwa haohao waliotajwa.

“Mwandishi fulani, nina taarifa zako.” Ujumbe mfupi, lakini wenye uzito wa kutosha kuwatetemesha, vitisho hivi vilizua hofu, vikawavunja nguvu na kuwafanya wengi wajiulize kama uaminifu katika kazi yao unawapeleka mbele au unawazika taratibu.

Nilipoongea na mmiliki mmoja wa chombo cha habari, sauti yake ilikatika tamaa:

“Siyo kwamba hatuna habari tunazo, Lakini tukizionyesha tu, kesho tunaweza kuwa tumefungiwa.”

Neno “kufungiwa” linaweza kuonekana jepesi kwa wengine, lakini katika ulimwengu wa Vyombo vya Habari, ni sawa na kufilisika, kuanguka, na kuporomoka kwa maisha ya Watu waliopo chini ya mwavuli wa ajira na taaluma hiyo.

Matokeo yake? Vipindi muhimu vikakatwa ghafla, habari zenye maswali mazito zikasitishwa bila hata neno la ufafanuzi, Maudhui ya digitali hayakupandishwa makusudi, Wananchi tukabaki gizani, tukitangatanga kutafuta majibu kama vipofu wanaogusa ukuta wakitafuta mlango.

Hapo ndipo maumivu ya kweli yanapoanzia, sisi walaji wa habari tulinyang’anywa haki yetu ya msingi ya kupata taarifa, tulitegemea Wanahabari watupatie mwanga, lakini nao walikuwa katika giza zito kuliko sisi.

Je, tumewahi kuona chombo chochote kikisimama hadharani kutuambia kilichoendelea? Hapana.

Je, ni kwamba hawakujali? La hasha.

Ni kwa sababu walinyimwa pumzi ya kusema walizuiwa, wakafungwa, wakatishwa.

Je, hili ni tatizo la Iringa pekee au ni sura pana ya nchi nzima? Hilo linabaki kuwa fumbo, lakini ukweli mmoja haujifichi

Taaluma ya habari imetupiwa mawe, na walio ndani ya tasnia hiyo wameumia kimwili, kiakili.

Leo tunajiuliza swali moja la msingi, ni lini Wanahabari watafanya kazi zao bila kuishi kwa hofu?

Kwa sababu kama taifa lisipowalinda, nani atawabeba, nani atawatetea, na nani atahakikisha kalamu haifi Tanzania?
IMG_3918.jpg
 
Back
Top Bottom