SIMULIZI : YALIYONIKUTA TANGA
MSIMULIAJI : MARTIN MEKU
MAHALI : TANGA
SEHEMU YA 24
ILIPOISHIA
Usiku ule ulikuwa balaa!
Hatukulala. Mke wangu alikuwa
akipiga kelele usiku kucha akidai kuwa kila
alipofumba macho
alikuwa akiona msichana anampiga
bakora akimwambia avue zile
dhahabu alizovaa.
Mwisho wake ilibidi mke wangu
atii na kavua zile dhahabu nilizokuwa
nimempa na hapo
ndipo alipopata usingizi.
Kulipokucha asubuhi nilikichukua
kile kisanduku nikakitia kwenye
begi na kumpa polisi aliyekuwa
jirani yangu. “Tafadhali nihifadhie hili begi
langu
nitalichukua kesho” nikamwambia.
Kwa vile yule polisi alikuwa rafiki
yangu akalichukua begi hilo na
kunihifadhia chumbani kwake.
Nikaenda zangu kazini. Niliporudi kutoka
kazini mke
wangu akaniuliza maswali mengi
kuhusu zile dhahabu nilizokuwa
nimempa ambazo zilikuwa
zimemtia wasiwasi mkubwa.
Nikamdanganya kwamba dhahabu hizo
nilizinunua kwa sonara na
kwamba nilishazirudish a.
“Sasa kwanini nilikuwa naota ile
ndoto ya kuchapwa?” akaniuliza.
“Sijajua lakini nimemueleza sonara
huyo ameniambia alikosea akaniuzia
dhahabu za majini lakini
kwa vile nimezirudisha
hakutakuwa na tatizo.”
Nikaendelea kumdanganya ili
kumtoa wasiwasi.
SASA ENDELEA Nilidhani kwa kuhamisha kile
kisanduku kwa mwenzangu ndio
ningemaliza yale matatizo ya
majini lakini nilikuwa
nimejidanganya.
Yapata saa nane usiku wakati nimelala, yule
polisi niliyempa lile
begi lenye kisanduku anihifadhie
alinibishia mlango.
Nilipofungua mlango nilimuona
amesimama mbele ya mlango
akiwa na lile begi mkononi. “Chukua hili
begi lako, linaniletea
miujiza chumbani kwangu”
akaniambia huku uso wake ukiwa
umetaharuki.
“Miujiza gani tena?”
“Kuna joka linatoka ndani ya hili begi halafu
linazunguka chumbani
kwangu”
Nikajifanya nashangaa.
“Joka?”
“Ndio joka. Tena joka kubwa sana.
Linazunguka chummbani kisha linarudi
kwenye hili begi linapotea”
“Mh! Unanieleza habari ya ajabu
sana”
“Kwani umeweka nini humu ndani”
“Sijui kilichomo humo ndani. Hilo
begi alilisahau mtu mmoja aliyekuja hapa
nyumba kuomba
maji ya kunywa” nikamdanganya.
“Mh! Basi lichukue. Siwezi kuliweka
kwangu”
Nikalichukua lile begi. Yule polisi
akarudi nyumbani kwake. Na mimi
nikapatwa na kizungumkuti.
Nilikuwa sijui nikaliweke wapi. Yale
maelezo ya polisi mwenzangu
yalinitisha.
Nilipoona nimekosa pa kuliweka
nililiweka chini ya meza pale sebuleni.
Nikafunga mlango wa
chumbani ili kama kuna joka
linalotoka lisiingie chumbani
mwetu.
Wakati ule mke wangu alikuwa
amelala. Hakuwa akijua kilichokuwa
kinaendelea.
Nilishukuru kwa hilo. Laiti
angekuwa macho akasikia yale
niliyokuwa nikiyazungumza na
yule polisi, ingekuwa taabu.
Wakati nimejilaza kitandani nikiwaza,
nilijiambia kuwa ule
uganga niliofanyiwa na yule
mganga wa kijijini kwetu haukufaa
kitu, sasa vituko vilikuwa vinanijia
nyumbani kiasi kwamba mimi
mwenyewe nilikuwa nimeshapata uoga na
nilikuwa sijui la kufanya.
Nikajiambia tamaa yangu ya
kumiliki zile dhahabu sasa
inaniponza.
Wakati niko kwenye lindi la
mawazo nikapitiwa na usingizi ghafla,
nikaota nimeamka saa kumi
na mbili asubuhi, nikatoka na lile
begi na kwenda kule magomeni
kwenye yale mkaburi. Nilipofika
nikakitoa kile kisanduku na
kukiweka juu ya kaburi mojawapo. Hapo
hapo nikaona kinatitia chini
na kupotea kabisa.
Baada ya hapo nilizinduka
usingizini nikatazama saa na kuona
ilikuwa saa kumi na mbili
kasorobo, nikavaa nguo na kutoka
chumbani. Nilikwenda kuosha uso
na kusukutua maji. Nikalichukua
lile begi na kutoka nalo bila hata
kumuaga mke wangu.
Nilikwenda kupanda daladala
nikaenda Magomeni. Nilifika kule
makaburini nikakitoa kile
kisanduku na kukiweka juu ya
kaburi kama vile nilivyoota usiku.
Hapo hapo nikaona kile kisanduku
kinazama chini.
Kilizama hadi kikapotea kabisa. Nilitishika
sana lakini kwa vile tukio
lenyewe nilishaliota nilijikaza.
Kile kisanduku kilipopotea, nikajua
kimerudi kwa wenyewe.
Nikaondoka na kurudi nyumbani.
Nilipofika nilimkuta mke wangu bado
amelala. Nikaenda kuoga.
Wakati narudi kutoka kuoga
nikamkuta ameshaamka.
Sikumwambia chochote.
Baada ya siku ile sikuona tena vile
vituko vya majini. Tukio hilo licha ya kunitesa
lilinipa fundisho
ambalo sitalisahau. Nikawa polisi
muadilifu sana niliyefanya kazi
yangu kwa misingi ya haki na
sheria na sio kama nilivyokuwa
hapo mwanzo. Hayo ndiyo yaliyonikuta
tanga’
usiache kunitumia maoni yako