Simulizi ya kusisimua

Simulizi ya kusisimua

Hili jamaa fix ,hadith gani haiendelei tangia juzi??Bali na li hadithi lako huko
 
maelezo katika hadithi hiyo inaonekana maimuna ni yule binti aliyekuwa anaishi na yule bibi aliyepekuliwa nyumba yake
 
SIMULIZI : YALIYONIKUTA TANGA
MSIMULIAJI : MARTIN MEKU
MAHALI : TANGA
SEHEMU YA 07

ILIPOISHIA

Nikairudisha ile simu mfukoni.
Wakati nairudisha ilikuwa kama
ninaizima akili yangu kwani hapo
hapo sikujielewa tena. Sikujua
kama nilipotewa na fahamu au
nilipitiwa na usingizi wa ghafla.
Sikuweza kujua.
Nilipozinduka nilijiona nimechoka,
kitu ambacho kilinipa dalili kuwa
nililala kwa muda mrefu pale
kwenye kochi. Nikatazama saa
yangu na kuona ilikuwa saa tisa
usiku. Nikataharuki. Mwenyeji
wangu hakuwepo. Nilikuwa bado
niko peke yangu.
Nikajiuliza Maimuna alikuwa
amekwenda wapi tangu muda ule.
Nikanyanyuka na kuanza
kumtafuta mwenyeji wangu.
Niliingia ukumbini nikaita
“Maimuna!”
Lakini sikupata jibu. Nikasukuma
mlango wa chumba cha kwanza
ambao ulikuwa wazi.
Nikachungulia ndani. Chumba
kilikuwa kitupu lakini kulikuwa na
boksi kubwa lililowekwa nyuma ya
mlango.
Nilichungulia ndani ya lile boksi
nikaona kitu kilichonishitua.
Nikaingia mle chumbani na
kutazama vizuri. Ndani ya lile boksi
niliona kichwa cha binaadamu,
tena kilikuwa kichwa cha Sajenti
Erick!
SASA ENDELEA
Kwa kweli nilipatwa na mshituko
mkubwa. Vile ambavyo nilitoka
usingizini nilijihisi kama nilikuwa
kwenye ndoto ya kutisha. Kwa
kutoamini macho yangu
nilikitazama kile kichwa tena na
tena. Akili yangu ilinithibitishia
kuwa sikuwa kwenye ndoto na
nilichokiona ni kichwa cha
binaadamu na ni cha Sajenti Erick!
Nikawa najiuliza Sajenti Erick
alichinjwa muda gani na alichinjwa
na nani na kwanini kichwa chake
kipo pale? Nikakumbuka kwamba
nilipigiwa simu na kachero
mwenzangu aliyenieleza kuhusu
kutoonekana kazini kwa Sajenti
Erick mchana kutwa wa siku ile.
Kile kichwa kwa jinsi
kilivyoonekana hakikuchinjwa
muda mrefu. Jeraha lake lilikuwa
bado bichi na lilikuwa linavuja
damu. Macho ya Sajenti Erick
yalikuwa wazi kuonesha kuwa
wakati anachinjwa alikuwa
ameshituka.
Akili ya kupelelezi ikaanza kunijia.
Nikazungusha macho yangu
kwenye kile chumba. Sikuona
mahali popote palipokuwa na
damu, hali iliyoonesha kuwa
Sajenti Erick hakuchunjwa mle
chumbani.
Wakati nayarudisha macho yangu
kwenye lile boksi nikaona magazeti
kwenye pembe moja ya kile
chumba. Nikaenda kuyatazama.
Yalikuwa magazeti mawili
yaliyowekwa pamoja. Juu ya
magazeti hayo kulikuwa na kete
tatu ambazo nilishuku zilikuwa
kete za kokeni.
Nilizishika na kuzinusa. Kwa vile
nilikuwa na uzoefu na unga huo
haramu niligundua harufu yake.
Ilikuwa ni kokeni. Nikaziweka
kando. Sasa nilishika yale magazeti.
Nilianza kuangalia mojawapo.
Kwenye ukurasa wa mbele
kulikuwa na habari ya ajuza
(kikongwe) aliyekamatwa Tanga na
kete za madawa ya kulevya.
Picha yake ilikuwa imechapwa.
Nilipoitazama nikagundua ilikuwa
ni ya yule mwanamke
tuliyemkamata siku ile mimi na
Sajenti Erick. Kumbe habari zake
zilichapwa kwenye gazeti.
Nikatazama tarehe ya lile gazeti
nikaona ni la siku za nyuma.
Nikashika lile gazeti jingine. Katika
ukurasa wake wa mbele kulikuwa
na habari iliyohusu kifo cha yule
kikongwe ambacho kilitokea katika
mahabusi ya polisi.
Mpaka muda ule nilikuwa sijaelewa
kitu. Nilikuwa nikijiuliza mengi
ambayo hayakuwa na majibu.
Wakati naliweka lile gazeti nikaona
kitone cha damu kikidondoka
kwenye kiganja changu.
Nikashituka na kutazama juu.
Huko juu niliona kitu cha
kushitusha. Niliuona mwili wa
Sajenti Erick usio na kichwa ukiwa
umening’inizwa kwenye miti
iliyopaulia nyumba! Lile jeraha la
kwenye shingo ndilo lililotonesha
tone la damu lililotua kwenye
kiganja changu.
Mwili ule uliunda picha ya kutisha
sana hasa kwa vile mtu mwenyewe
nilikuwa namfahamu. Ujasiri wa
kipolisi niliokuwa nimebaki nao
uliniishia pale pale. Kama
nisingekuwa makini
ningekurupuka na kutoka mbio
kwani hisia zangu zilishanusa hali
ya hatari.
Nilijua kuwa hata mimi maisha
yangu yalikuwa hatarini. Mahali
nilipoingia palikuwa sipo!. Nikainua
hatua ili nitoke katika kile chumba.
Baada ya kupiga hatua mbili
nilikanyaga mahali palipotitia!
Nikajiona natumbukia chini.
Lilikuwa shimo la urefu wa kama
futi nne. Miguu yangu ilipotua chini
nikaona kitu kinanizongazonga
kwenye miguu kikinipandia juu.
Nikajaribu kukishika. Nikaona
nimeshika kichwa cha nyoka!
“Yesu wangu!” nilishituka na
kukivuta juu. Haikuvutika kwani
sehemu yake ya mkia ilikuwa
imenizonga kwenye mguu. Nilitaka
kuwania kupanda juu ya lile shimo
nitoke lakini nilijiambia nikikiacha
kile kichwa nyoka yule atanigonga.
Nikakipeleka kichwa hicho chini ya
mguu mwingine kisha
nikakikanyaga kwa kupiga mguu
wangu chini. Kile kichwa kilipasuka.
Ndipo nilipoweza kutoka kwenye
lile shimo. Nilikuwa nahema kama
niliyekuwa nafukuzwa.
Nilipotoka tu kwenye shimo hilo
nilikwenda ukumbini nikaelekea
kwenye mlango wa nje.
Nilipoushika ili niufungue nikaona
ulifungwa kwa nje. Mlango
haukufunguka!
Nikasikia sauti za watu waliokuwa
wakizungumza huko nje. Sauti ya
mwanaume na mwanamke.
Zilikuwa zikisikika kwa mbali lakini
zilikuwa zikikaribia kwenye ule
mlango. Nikajua ni watu
wanakuja.
Nikatega masikio kuwasikiliza.
“Sasa mama yuko wapi?” Ilikuwa
sauti ya kiume iliyouliza.
“Mama yuko uani, anachimba
kaburi kabisa” Sauti iliyojibu
niliitambua, ilikuwa ni ya yule
msichana aliyenikaribisha mle
ndani.
“Na huyo polisi mwingine
aliyewabambikia kesi yuko wapi?”
Ile sauti ya kiume ikauliza tena.
“Nilimuacha ukumbini amelala, sijui
kama atakuwa ameamka”
“Sasa acha tumshughulikie na yeye
kama mwenzake”
“Mama yangu, nimekwisha!”
nikajiambia niliposikia maneno
hayo. Kumbe tatizo lilikuwa ni ile
kesi tuliyombambikia yule
mwanamke.
Sasa akili yangu ilitanzuka.
Nilimkumbuka yule msichana.
Alikuwa ndiye yule aliyekuwa na
yule mwanamke kwenye ile
nyumba tulipokwenda
kuwakamata. Yule msichana
alikimbia, tukamshikilia mama
yake peke yake.
Kwa hofu kwamba ningeuawa
kama alivyouawa Sajenti Erick,
nilikimbilia kwenye mlango wa
uani. Niliukuta mlango upo wazi,
nikatoka uani ambako kulikuwa
kiza lakini kulikuwa na
mbalamwezi.
Kwenye pembe moja ya ua huo
nilimuona bibi mmoja ameshika
shepe akichimba shimo.
Nilipomuona tu nikakumbuka yale
maneno ya yule msichana
niliyemsikia akisema “Mama yuko
uani, anachimba kaburi kabisa”
Nikajiuliza lilikuwa kaburi langu au
ni la Sajenti Erick? Wakati
namtazama yule bibi
nikamkumbuka. Alikuwa ni yule
mwanamke tuliyemkamata na
kumbambikia kesi ya kumkuta na
madawa ya kulevya.
Jambo ambalo lilinishangaza ni
kuwa mwanamke huyo alikufa
akiwa mahabusi lakini muda ule
nilimuona akiwa hai tena
akionekana akiwa na nguvu za
kutosha.
Kitu ambacho kilikuwa cha ajabu
zaidi ni kuwa bibi huyo alikuwa
uchi wa mnyama na mwili wake
ulikuwa umejaa manyoya meupe
marefu. Nikaiona miguu yake,
ilikuwa na kwato kama miguu ya
punda!
Je nini kitatokea? Usikose
kuendelea na hadithi hii kesho.
 
SIMULIZI : YALIYONIKUTA TANGA
MSIMULIAJI : MARTIN MEKU
MAHALI : TANGA
SEHEMU YA 08

ILIPOISHIA

“Leo nimekwisha!” nikajiambia.
Nilikuwa sina pa kukimbilia. Lakini
nilikwishatambua kila kitu.
Sikujua niliwezaje kuwasiliana na
yule msichana hadi nikafika katika
nyumba ile ya mauti! Kusema kweli
nilijipeleka mwenyewe!
Kwa vyovyote vile, nilijiambia,
nyumba ile haikuwa ya binaadamu
wa kawaida. Yule bibi alikuwa jini!
Na kama alikuwa jini, niliendelea
kujiambia, sitaweza kunusurika mle
ndani.
Licha ya kutoka pale uani, yule bibi
hakushituka. Aliendelea kuchimba
lile shimo kwa bidii.
Hakuna binaadamu yeyote
anayekubali kufa kirahisi,
nikageuka haraka na kurudi
nilikotoka. Wakati nafika kwenye
mlango wa mbele, mlango huo
ulikuwa unafunguliwa. Nilijificha
nyuma ya mlango. Akaingia yule
msichana.
Na yeye alikuwa uchi na alikuwa na
umbile sawa na lile la mama yake.
Alikuwa amejaa manyoya mwili
mzima na miguu yake ilikuwa ya
kwato nyeusi. Mkononi alikuwa
ameshika upanga.
Mwenzake alikuwa mwanaume. Na
yeye alikuwa kama walivyokuwa
wenzake. Hapo nikagundua kuwa
yule mama na binti yake
waliokuwa wakiuza vitu vya
dhahabu, walikuwa ni majini lakini
watu hawakuwa wakijua.
SASA ENDELEA
Ule upanga aliokuwa ameushika
Maimuna ulikuwa wa nini?
Nikajiuliza.
Lakini jibu lilikuwa wazi kuwa
upanga huo ulikuwa ni kwa ajili ya
kuchinja kichwa changu. Bila shaka
ndio uliotumika kumchinja Sajenti
Erick.
Usiku huo ulikuwa wa balaa
kwangu. Nilijuta kulaimisha
mawasiliano na yule msichana hadi
yakanikuta yaliyonikuta. Lakini
nilihisi kukutana tena na majini hao
ilikuwa ni mipango yao ya
kutukomoa kama walivyomkomoa
Sajenti Erick kutokana na ile
dhambi tuliyowafanyia.
Kosa langu ni kuwa nilijiingiza
kichwa kichwa mara tu Maimuna
aliponitumia meseji aliyodai kuwa
haikuwa yangu bali alikosea
namba. Ilikuwa tamaa yangu ya
wasichana iliyopelekea nifike
mahali hapo pa mauti.
Maimuna na mwenzake
walipoingia hawakuufunga ule
mlango wa nje. Kama
wangeufunga wangeniona.
“Yuko wapi?” Maimuna akauliza
alipoona sikuwepo mahali ambapo
nilikuwa nimelala. Akakimbilia
uani. Mwenzake aliyekuwa naye
akamfuata.
Hapo ndipo nilipopata upenyo wa
kutoka. Nilipotoka nje nilianza
kukimbia. Jambo lililonishangaza ni
kuwa nilijiona niko kwenye msitu
wa kutisha. Nilikuwa najikimbilia
ovyo bila kujua nilikuwa
ninakwenda wapi.
Nikatoa simu yangu mfukoni na
kuwapigia polisi wenzangu ili
nipate msaada. Wakati napiga simu
nilikuwa nakimbia. Simu
ilipokelewa. Aliyepokea alikuwa
mwanamke. Nikamwambia.
“Mimi ni Martin Lazaro wa CID
nimepatwa na matatizo, naomba
msaada wenu”
“Mimi ni Maimuna. Uko wapi
Martin, nakutafuta?” Sauti
ikaniuliza kutoka simu ya upande
wa pili. Mara moja niliitambua sauti
ya Maimuna.
Nikaikata simu haraka kwa kuona
nilikuwa nimekosea namba na
kumpigia yule msichana muuaji
niliyekuwa namkimbia.
Nikasimama na kuiangalia kwa
makini namba ya polisi kisha
nikaipiga. Nilikuwa nimesimama.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio na
nilikuwa nahema kama niliyekuwa
nafukuzwa.
Simu ikapokelewa tena. Kabla ya
kusema chochote nikaisikia tena
sauti ya Maimuna ikiniuliza.
“Uko wapi?”
Moyo ukanilipuka kwa hofu.
Nikaitazama ile namba. Nikaona ni
namba ya polisi lakini aliyepokea
alikuwa Maimuna. Nikaamini kuwa
wale walikuwa majini kweli.
Nikakata simu na kuendelea
kukimbia. Simu ikawa inapigwa.
Nikasimama na kutazama namba
iliyokuwa inapiga, nikaona namba
ya polisi.
Nikaipokea haraka.
“Jamani nina matatizo, nikipiga
simu inakwenda kwingine…”
“Inakwenda wapi?” Sauti
iliyoniuliza ilikuwa ya Maimuna.
“Wewe nani?” nikamuuliza kwa
kutaharuki.
“Mimi Maimuna umenisahau mara
moja hii, wakati tulikuwa wote
hapa nyumbani…”
Nikakata ile simu na kuendelea
kukimbia. Kutahamaki nikajiona
nimetokea mbele ya ile nyumba ya
Maimuna.
Nilikuwa nakimbia lakini nilipiga
breki ya ghafla, nikaitazama ile
nyumba iliyokuwa mbele yangu.
Nilihakikisha kuwa ilikuwa ndio ile
ile nyumba ya Maimuna na mahali
palikuwa pale pale. Kwa maneno
mengine ni kwamba nilikuwa
nimerudi hapo hapo.
Mlango ulikuwa umefungwa,
nikaona unafunguliwa. Sikujua nani
angetoka, nikageuka na kuanza
tena kukimbia. Sasa nilikuwa kama
mwendawazimu niliyekuwa
nikijikimbilia ovyo.
Wakati ninakuja katika eneo lile
hakukuwa na msitu. Kulikuwa na
vichaka tu na miti michache ya
mikoroshi. Sasa niliona ajabu kuona
msitu wa kutisha. Sikuweza kujua
jinsi msitu huo ulivyotokea.
Simu yangu ilkuwa inaita lakini
sikushughulika nayo tena,
niliendelea kukimbia tu. Nia yangu
ilkuwa kutokea katika barabara au
njia ya watembea kwa miguu lakini
sikuona njia wala barabara.
Ghafla niliona nyumba kwa mbali.
Ilikuwa inawaka taa kwa nje,
nikakimbilia kwenye nyumba hiyo
ili kuomba msaada. Nilipofika
niligonga mlango.
“Jamani naomba msaada…jamani
naomba msaada” nikasema huku
nikiendelea kugonga.
Baada ya muda kidogo mlango
ukafunguliwa.
“Karibu” Bibi mmoja aliyekuwa
amejitanda shuka nyeupe
akanikaribisha.
Nikamueleza ule mkasa ulionifika.
Nilipomaliza kumueleza
akapandisha juu gauni lake na
kuniuliza.
“Hao watu unaosema wana kwato,
kwato zao ni kama hizi?”
alinionesha miguu yake.
Nilipoitazama nikaiona ina kwato
kama zile za kina Maimuna!
Nikashituka na kumtazama yule
bibi usoni. Sasa nikamuona vizuri.
Alikuwa ndiye yule aliyekuwa
akichimba kaburi kule uani kwa
Maimuna.
“Eh! Amefikaje huku!” nikajiuliza
kabla ya kugeuka nyuma na
kuanza tena kukimbia.
“Mbona unakimbia?” akaniuliza.
Sikumjibu, niliendelea kukimbia.
“We kijana hebu njoo…” Yule bibi
alinipigia kelele.
Nikageka na kumtazama. Alikuwa
ametoka nje akiniangalia.
Nikajipoteza kwenye msitu.
Nilikuwa nimechoka na moyo
ulikuwa ukinienda mbio sana.
Nilijua kuwa wakati wowote
ningeweza kuanguka na kuzimia.
Kitisho nilichokipata kilikuwa
kikubwa na kiliutikisa moyo wangu
hasa. Sikuwa mtu wa kuamini
mashetani lakini siku ile niliamini
kuwa mashetani wapo na
wanatisha. Licha ya kujitahidi
kukimbia muda wote nilijua kuwa
nitakufa kwani sikuwa na ujanja
wa kutoka kwenye msitu huo. Ile
hofu peke yake ingweza kuniua.
Hapo nikaanza kumlaumu Sajenti
Erick kwani yeye ndiye aliuleta
mpango ule wa kwenda
kumkamata yule bibi na
kumbambikia kesi ya madawa ya
kulevya.
Je nini kitatokea?
 
SIMULIZI : YALIYONIKUTA TANGA
MSIMULIAJI : MARTIN MEKU
MAHALI : TANGA
SEHEMU YA 09

ILIPOISHIA

Nikajiambia yeye ndiye aliyestahili
adhabu aliyoipata lakini mimi
nilikuwa naonewa tu. Nikaapa
kimoyomoyo kama nitasalimika
sitarudia tena kushirikiana na polisi
wasio waaminifu.
Kwa vile nilikuwa hoi, nikaanguka
chini na kupotewa na fahamu.
Nikiwa sijielewi niliota nainuliwa
na mtu aliyenikuta nimeanguka.
“Mbona umelala hapa?” akaniuliza.
“Nlinguka nilikuwa nakimbia”
nikamjibu.
“Oh pole sana. Ulikuwa unakimbia
nini?”
Nikamueleza ule mkasa
ulionitokea.
“Kwani wewe ulikuwa hujui kama
yule bibi na mwanawe Maimuna ni
majini?”
“Nilikuwa sijui. Kumbe majini
wanaishi na binaadamu?”
“Ndio, wanaishi na binaadamu na
wanafanya biashara kama
binaadamu lakini hawapendi
dhuluma”
SASA ENDLEA
“Lakini mimi sijawadhulumu kitu”
“Nani aliyewadhulumu?”
“Aliyewadhulumu wameshamuua”
“Si alikuwa pamoja na wewe?’
“Hapana. Yule alikuwa mkuu
wangu wa kazi. Kila anachoniambia
mimi nafuatisha”
“Sasa mimi nitakusaidia uweze
kurudi nyumbani kwako kwa
sababu mama yake Maimuna
sielewani naye ingawa trunajuana
sana. Kama atakasirika, wewe
utakuwa umeshasalimika”
“Nitashukuru baba kama
utanisaidia kwa hilo, kwa maana
nimekuwa nikihangaika sana
kwenye huu msitu bila kupata njia
ya kutokea”
“Usiniite baba, mimi si baba yako,
umenielewa?”
“Nimekuelewa. Nakushukuru sana
kwa msaad wako”
“Umekosea tena. Usinishukuru
kabla sijakusaidia. Ngoja nikusaidie
ndipo unishukuru”
“Sawa”
“Haya, amka uende zako. Njia ile
pale”
Hapo hapo nikajiona nazinduka.
Nilipofumbua macho nikajiona
nimelala chini ya mbuyu. Mbuyu
wenyewe ulikuwa ni ule Mbuyu
Kenda, mahali niliposhushwa na
pikipiki wakati nakuja kwenye
eneo lile.
Sasa njia nikawa nimeijua.
Niliangukia mahali pengine
nimezindukia mahali pengine.
Kusema kweli nilishukuru kutokea
mahali hapo. Nikatoa simu na
kumpigia yule mwenye bodaboda.
Simu yake ikawa haipatikani.
Nikapiga polisi lakini kwa uoga.
Nilichohofia ni kuwa simu yangu
isije ikapokelewa na Maimuna.
Baada ya simu kuita kwa sekunde
chache ikapokelewa.
“Kituo kikuu cha polisi hapa,
unahitaji msaada gani?” Sauti
iliyosikika ilikuwa ya kiume.
Nikajua sasa simu ilikuwa imefika
polisi.
Nikajitambulisha na kujieleza huku
nikisisitiza kupata msaada wa
usafiri haraka.
Polisi niliyekuwa nikizungumza
naye alikuwa ni Inspekta Benenza.
Nilipompa yale maelezo alishituka
na kutaharuki, akaniuliza.
“Uko sehemu gani?”
Nikamtajia sehemu niliyokuwa.
“Subiri hapo hapo, polisi watafika
sasa hivi. Kwa muda huu jitahidi
kujilinda mwenyewe”
“Sawa afande”
Nikakata simu. Ubaridi uliokuwa
ukipepea ulinidhihirishia kuwa
ilikuwa ni alfajiri. Nilijifuta
michanga kwenye nguo zangu
kasha nikasogea kwenye kiza ili
nisionekane. Macho yangu
yalikuwa yakiangaza kila upande
nikiwahofia Maimuna na mama
yake kunifuata mahali hapo.
Kulikuwa kimya. Sauti zilizokuwa
zikisikika zilikuwa za vidudu
vilivyokuwa vikipigwa na baridi
kwenye vichaka. Ukimya huo
badala ya kunipa matumaini
ulinisababishia hofu. Ulikuwa
ukimya unaotisha.
Nikajiambia kama Maimuna na
mama yake watatokea itabidi
nikimbie kwa miguu kurudi mjini.
Kutokana na hofu hiyo macho
yangu yalizidi kugeuka kila upande
kuhakikisha kuwa hakukuwa na
chochote kinachokuja.
Nilikuwa nikihesabu dakika kwa
wasiwasi. Nilikuwa nikiona polisi
wenzangu walikuwa wanachelewa
kufika mahali hapo. Kuchelewa
kwao kungeweza kuhatarisha
maisha yangu kwani mahali
nilipokuwa usalama wangu
ulikuwa mdogo sana.
Tangu kuzaliwa kwangu sikuwa
nimewahi kufikwa na mkasa wa
kutisha kama ule. Sikuwahi
kuushuhudia mwili wa mtu
ninayemfahamu ukiwa hauna
kichwa wala sijawahi kushuhudia
kichwa cha mtu ninayemfahamu
kikiwa peke yake.
Pia sijawahi kuona majini. Nilikuwa
nawasikia tu na nilikuwa siamini
habari zao. Kadhalika sijawahi
kuona eneo likibadilika na kuwa
msitu tena msitu wa kutisha kama
ule niliouona…
Mwanga wa taa za gari uliotokea
kwa mbali ulikatiza mawazo
yangu. Nikahisi lilikuwa gari la
polisi linalonifuata mimi. Mwanga
huo ulisogea kwa kasi, nikaweza
kuusikia muungurumo wa gari hilo.
Nikajitokeza barabarani ili waweze
kuniona.
Gari hilo likanipita lakini lilikuwa
gari la polisi. Haraka nikatoa simu
yangu na kupiga kiyuo cha polisi.
Alipokea Inspekta Beneza.
“Mimi Martin…”
Kabla sijamwambia nilichotaka
kumwambia alinikatisha.
“Nimeshatuma gari…”
“Gari la polisi limenipita…”
“Limekupita mahali ulipo…
hawakukuona?”
“Nafikiri hawakuniona,
wamekwenda mbali zaidi”
“Ngoja niwapigie, simama kando
ya barabara. Ukiliona gari hilo
linakuja wapungie mkono”
“Sawa afande”
Nikakata simu.
Nilisogea kabisa kando ya barabara
macho yangu yakiangalia upande
ulioelekea lile gari. Gari lenyewe
lilikuwa limeshafika mbali na
sikuweza kuliona tena.
Ghafla nikasikia sauti za watu
wanaozungumza. Nikageuza
macho haraka kuelekea ule upande
niliosikia sauti. Ulikuwa ni upande
ule wa kuelekea kwenye nyumba
ya Maimuna na mama yake.
Nikawaona watu wawili wanakuja.
Nikawagundua. Walikuwa
Maimuna na yule mwanaume wa
kijini aliyekuwa naye. Nilishituka
sana na sikuwa na pa kukimbilia.
Nikajua sasa ninakufa.
“Lazima atakuwa amefika huku”
Sauti ya Maimuna ikasikika.
“Kama amekuja huku tutamuona”
Sauti ya kiume ikamjibu.
“Wewe ndio umekosea, yule
alikuwa amejificha nyuma ya
mlango”
“Tutampata tu, hana ujanja”
Je nini kitatokea? Usikose
kuendelea na hadithi hii
 
SIMULIZI : YALIYONIKUTA TANGA
MSIMULIAJI : MARTIN MEKU
MAHALI : TANGA
SEHEMU YA 10

ILIPOISHIA

Maimuna alikuwa ameshika ule
upanga wake akiangaza macho
yake huku na huku. Sikuweza tena
kusubiri, nikatoka mbio. Nilielekea
upande ule lilikoelekea gari la
polisi.
Wakaniona!
“Si yule!” niliisikia sauti ya
Maimuna.
“Twende tumfuate” Sauti ya kiume
nayo ikasikika.
Niliendelea kukimbia. Kila
nilipopiga hatua tatu nilitazama
nyuma. Niliwaona wananifuata.
Hawakuwa wakikimbia lakini
walikuwa wanakuja kwa haraka.
Kwa mbali nikaona mwanga wa
gari linalokuja. Nikazidi kukimbia.
Niliona nikimbie nikiwa katikati ya
barabara ili watu waliomo ndani ya
gari hilo waweze kuniona.
Nikajitokeza katikati ya barabara
huku taa za gari zikinimulika.
Haikutosha kujitokeza katikati ya
barabara. Niliinua mikono yangu
miwili nikawa nalipungia gari hilo
ili kulisimamisha. Niliomba gari hilo
liwe la polisi lililonipita. Kama
halitakuwa gari la polisi
halitasimama. Litanikwepa na
kuendelea na safari yake.
“Jamani simameni, nakufa.. jamani
simameni nakufa!” nilikuwa
nikipiga kelele.
Nyuma yangu Maimuna na
mwenzake walikuwa wakiendelea
kunifuata bila kujali kama kulikuwa
na gari linakuja.
Sikuwa na hakika kama gari hilo
lilikuwa la polisi. Na kama lilikuwa
na polisi sikuwa na hakika kama
wangeweza kupambana na majini
hao waliokuwa na hasira na mimi.
SASA ENDELEA
Gari hilo lilipunguza mwendo na
kusimama katikati ya barabara.
Kama lingeendelea kuja
lingenigonga kwa vile na mimi
nilikuwa katikati ya barabara.
Taa za gari hilo zilikuwa
zikinimulika. Mpaka muda huo
sikujua gari hilo lilikuwa la nani.
Mara tu liliposimama, niliona polisi
wakishuka haraka haraka.
Walikuwa polisi sita waliokuwa na
bunduki. Hapo nikajua kuwa
lilikuwa gari la polisi ambalo
lilinipita mara ya kwanza.
Walikuwa wameshanitambua
wakanifuata haraka haraka.
“Kitu gani Martin?” Polisi mmoja
aliyekuwa na cheo cha Koplo
akaniuliza.
“Nikageuka nyuma ili niwaoneshe
wale majini. Nilishaanza kuwambia.
“Wale majini bado wananifuata…”
Lakini nilisita nilipoona wale majini
hawapo. Walitoweka ghfla nyuma
yangu.
“Kitu gani Martin?” Polisi huyo
aliniuliza tena baada ya
kutonielewa.
Sasa nikawaeleza kwa utulivu
mkasa mzima.
“Sasa wako wapi hao majini?”
Polisi mwingine akaniuliza.
“Wametoweka sasa hivi”
“Una hakika kwamba Sajenti Erick
amechinjwa na umekiona kichwa
chake kiko mbali na mwili wake?”
yule koplo wa polisi akaniuliza.
“Nimekiona kichwa chake kiko
ndani ya boksi na mwili wake
unaning’inia juu”
“Ni sehemu gani?”
“Sehemu yenyewe mmeipita, ni
pale mbele kwenye mbuyu”
Niliwaonesha kwa kidole.
“Ingia kwenye gari twende”
Nilikuwa wa kwanza kujipakia
kwenye gari. Nilikaa kwenye siti
iliyokuwa kando ya dereva. Mwili
wote ulikuwa umenijaa baridi ya
hofu. Baada ya polisi hao kujipakia,
gari likaondoka. Tulipokuwa
tunaukaribia ule mbuyu, polisi
aliyekuwa akiendesha aliniuliza.
“Ni mbuyu ule pale?”
“Ndio ule pale. Kuna njia upande
wa kushoto”
Tulipofika katika eneo lililokuwa na
mbuyu huo, dereva alikata
kushoto. Tukaingia kwenye
vichaka.
“Ni kwa upande gani?”
“Twende tu. Huko mbele kuna njia
inaelekea kulia”
Tulipoifikia njia hiyo inayoelekea
kulia, dereva akaniuliza.
“Njia yenyewe ndio hii?”
“Ndiyo hii, sasa kata kulia. Tutaiona
hiyo nyumba”
Dereva akakata kulia.
“Huku ulifikaje wewe?” Dereva
huyo akaniuliza.
“Ni ushawishi tu wa yule msichana”
nikamjibu.
“Huoni kama kunatisha?”
Nikaguna na kunyamaza kimya.
Muda ule ndio niliona kunatisha.
Wakati ule namfuata yule msichana
sikuona kama kunatisha kiasi kile.
“Yaani sajenti Erick ni marehemu?”
polisi aliyekuwa akiendesha gari
hilo alikuwa bado haamini
niliyowaeleza.
“We twende, utakwenda ona
mwenyewe”
Baada ya mwendo mfupi tukaiona
ile nyumba mbele yetu.
“Nyumba yenyewe ni ile pale”
nikamwambia polisi aliyekuwa
akiendesha.
Akalisimamisha gari mbele ya
nyumba hiyo. Tukashuka. Koplo wa
polisi aliishika vyema bunduki yake
akaenda kubisha mlango. LIcha ya
kubisha kwa sekunde kadhaa
hakukuwa na majibu. Akaupiga
teke mlango huo ambao
ulifunguka.
Mlango ulipofunguka aliwaashiria
polisi wengine wamfuate. Sote
tukaingia ndani. Kila polisi alikuwa
ameielekeza mbele bunduki yake
tayari kukabiliana na tukio lolote
litakalotokea.
Kwa kutumia mwanga ule wa
fanusi ambayo bado ilikuwa
inawaka tuliangaza macho kila
upande. Ile sebule ilikuwa tupu.
Tukaingia ndani zaidi.
Nilimuonesha koplo wa polisi kile
chumba kilichokuwa na kichwa cha
Sajenti Erick pamoja na mwili wake.
Kabla ya kuingia koplo huyo
aliwaashiria polisi wawili kwenda
uani na kumuweka chini ya ulinzi
yeyote watakayemuona.
Aliwambia polisi wengine waingie
katika vumba vingine kwa wakati
mmoja. Ndipo mimi na yeye
tulipoingia katika kile chumba.
Polisi mmoja alikuwa amebaki
ukumbini kmwa ajili ya kuweka
ulinzi.
Tulipoingia humo chumbani
niliutazama ule mwili uliokuwa
ukining’inia, haukuwepo.
Nikalisogelea lile boksi lililokuwa
nyuma ya mlango na kulitazama
ndani. Kile kichwa hakikuwemo
isipokuwa damu iliyokuwa ikivuja
kutoka kwenye kichwa hicho ndio
iliyosambaa ndani ya boksi.
“Kichwa chenyewe kilikuwa humu
lakini kimeondolewa”
nikamwambia koplo huyo.
“Una maana hii damu ilitoka
kwenye kichwa hicho”
“Ndiyo. Kilikuwa kinavuja damu”
“Na ule mwili uliosema ulikuwa
unaning’inia uko wapi?”
“Ulikuwa uking’inia hapa”
Nikamuonesha pale mahali
ambapo chini yake palikuwa na
matone ya damu.
“Ulikuwa unadoda damu, hii hapa
chini”
“Ina maana wameuondoa?” Koplo
akaniuliza. Uso wake ulikuwa
umeshabadilika rangi kwa taharuki.
“Wameuondoa au wameuzika, kwa
sababu yule bibi alikuwa akichimba
kaburi uani”
“Hebu twende na huko”
Koplo alitangulia kutoka. Mimi
niliyachukua yale magazeti
yaliyokuwa yamewekwa pembeni
mwa chumba kisha nikatoka.
Polisi wote tukakutana tena hapo
ukumbini.
“Mmekuta nini?” Polisi mmoja
aktuuliza.
“Kuna damu tu” Koplo alimjibu.
Je nini kitatokea?
 
khaaaaa hiyo ndo faida ya dhuluma,na iwe fundisho kwa wengine c kwa police tu bali kwa watu wengine pia,hayaa tunasubiri sehemu ya 11
 
Dah hii stori hii, inanikumbusha kitu, ila kama hii ni simulizi tuu, sawa ila haya mambo yapo na wengine yashatukuta japo c kwa dhulma, ila huyu polisi safar hii aliingia cha kike, am waiting
 
Hahahahaha hii inafaa iwe movie ya Hollywood coz bongo movie watatuletea madudu
 
Kwa kuwa aliyeianzisha hii stori yupo kimyaa na hataki kuiendeleza ngojea mimi niwe nijifanye kimbele mbele niendelezee
 
Back
Top Bottom