STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL:
thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
********************
SEHEMU YA TISINI NA NNE
SONGA NAYO................
Bashir ni kweli alikuwa karibu na kwa mheshimiwa, nyumbani kwake kabisa Bunju na ndiko ambako walikuwa wamepanga kukutania, alikuwa amenyoosha barabara kuu lakini alichepuka kuanza kuifuata njia ambayo ilikuwa inaenda moja kwa moja kwa mkuu wa majeshi, alikuwa amebakiza mita elfu moja kuweza kufika nyumbani kwa mheshimiwa ndipo aligundua kwamba kuna mtu alisimama barabarani akiwa amempa mgongo.
Mtu huyo hakujali honi ya gari ambayo alikuwa anaipiga bwana huyo, huenda alimsikia ila akamdharau, hapendi dharau bwana huyo, kwanini adharauliwe kirahisi namna hiyo? Alighafilika Bashir kiasi kwamba alishuka ndani ya hiyo gari akiwa na hasira mno baada ya kubakisha hatua kadhaa ili aweze kumfikia mtu wake huyo.
Taratibu alianza kupunguza mwendo wake, ni baada ya viashiria kadhaa ambavyo vilimpa uhakika kwamba hakuwa salama ama mazingira yote kwa ujumla hayakuwa salama kabisa hilo eneo. Namna mtu huyo alivyokuwa amesimama hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, hakuwa akiyumba wala kutikisika, alisimama kama mti ambao ulikuwa umekufa. Bashir aliangaza kila pembe lakini hakuona jambo lolote la maana wala dalili za uwepo wa watu wengine jambo ambalo kidogo lilimpa amani.
“Wewe ni nan….” ile kasi ambayo aligeuka nayo Gavin hata yeye hakutegemea, aliona kitu kinakuja upande wake jambo ambalo lilimfanya arudi nyuma kwa nguvu ili kujihami. Alifanikiwa kukipangua akagundua kwamba ni upanga ulikuwa unakuja kwenye kifundo maana yake mhusika hakuwa anahitaji kumuua haraka. Licha ya kufanikiwa kupangua lakini bastola haikuwa kwenye mkono wake, mkono ambao ulikuwa na bastola ndio ambao aliutumia kuweza kupangua upanga huo hivyo hata bastola yenyewe ilidondokea mbali.
Alimwangangalia mwanaume huyo lakini kwa bahati iliyokuwa mbaya hakufanikiwa kabisa kuweza kuiona sura yake, ilikuwa imefunikwa na kitambaa usoni. Spidi ambayo alikuwa anatembea nayo mwanaume huyo haikuwa ya kawaida wala hakuwa na uwezo wa kwenda nayo sawa, alirudi nyuma baada ya kuona bwana huyo anakuja kwa spidi ya kimbunga, ngumi zilikuwa zinakuja nzito mno upande wake.
Alikoswa na mguu ambao ulikita kwenye gari mpaka sehemu hiyo ikabonyea na kuweza kuharibika vibaya mno. Alirudi nyuma akiwa anaipimia bastola yake lakini ilikuwa mbali, alistaajabu aliyokuwa anayaona, hali iliyo mfanya kutamka kwa sauti kubwa
“GAVIN LucA” alikuwa sahihi kabisa, bwana huyo ndiye mwenyewe kabisa ambaye alikuwa hapo muda huo. Ni mtu ambaye walikuwa wakimtafuta sana ila siku hiyo tena akiwa mwenyewe alipata bahati ya kukutana naye ana kwa ana, alikuwa anazijua vizuri sifa za bwana huyo walikufa makomando kadhaa msituni tena kama watoto wadogo, hata yeye alikuwa na hayo mafunzo lakini hakuwa na imani kama atafanikiwa kupona, jambo la mhimu kwake ilikuwa ni kupata msaada ambao hakuujua unakuja muda gani.
Alikuwa akizielewa sheria za mapigano, ukikubali kushambuliwa basi mara zote lazima itakula kwako hivyo alitakiwa yeye ndiye ashambulie zaidi ya anavyo shambulia na hapo ndipo alifanya maamuzi ya kumfuta bwana huyo kwa spidi na nguvu zote. Alitoa visu kwenye buti zake, hakuwa anaviacha mahali hivyo vilikuwa ni mhimu kwake, alimkosa bwana huyo kwenye mguu wake wa kulia, aliinuka na kuzamisha kisu lakini hakikuingia, kilidakwa kabla hakijafika mbali kikaishia kwenye nguo.
Gavin alijizungusha kwa nguvu kubwa akiwa anarusha ngumi nzito ambapo nne zilitua kwenye taya ya Bashir, alitoa muungurumo akiwa anamwaga meno. Alirudi nyuma ila alihisi kama anaona kivuli, hakikuwa kivuli bali sarakasi za Gavin na zile nguo nyeusi ambapo aliishia kwenye kifua cha Bashir, alipigwa mateke matano akatua chini akiwa anavuja damu ambayo aliitema.
Akiwa pale chini alizunguka kwenda upande upande, alipishana na goti ambalo lilitua chini kiasi kwamba mpaka ardhi ilitikisika kabisa akawa anahema kwa nguvu akiwa mwingi wa wasiwasi. Aliinuka kuhitaji kuirukia bastola, alikutana na teke la uso ambalo liliirarua vibaya sura yake akarudi nyuma akiwa anagalagala huku uso wake ameufumba kwa sababu alikuwa anaona kiza mbele. Alijikaza kusimama ila aliinama tena, teke lilitua kwenye goti, mlio wa kuvunjika kwa goti ilikuwa ni kama kelele za mtu akiwa anavunja kuni.
Gavin aliiokota bastola ambayo ilikuwa imedondokea pembeni ambayo alikuwa nayo Bashir kwa mara ya kwanza. Alimsogelea bwana huyo taratibu na kumwangalia akiwa analalamika kwa maumivu ambayo alikuwa anayapitia. Kwa namna ambavyo alikuwa anajifanya hana hatia basi usinge amini kabisa kwamba ndiye yule ambaye alikuwa anaua wenzake kama kuku bila kujali hali ambayo walikuwa wanaipitia.
“Haukupaswa kuwa miongoni mwa hawa watu Bashir”
“Naiomba nafasi nyingine tafadhali mimi kuanzia sasa nitakuwa mtu mwema na nitafanya kila ambalo ni jema mbele ya jamii, nakuomba” Bashir siku hiyo alikuwa anaomba nafasi ya kuweza kuishi kwa mara nyingine, nafasi ambayo hata yeye hakuwahi kumpatia mtu yeyote yule, kifo kilimtia mbavuni bwana huyo akawa hana namna nyingine zaidi ya kufanya hivyo ili aweze kuishi kwa mara nyingine tena.
“Kuna kosa ambalo mpaka sasa najiuliza nilikosea wapi ila nahisi limekuja kuleta matatizo makubwa kwangu na kwa watu wangu wa karibu. Sina kumbukumbu kwamba ni nani ila nahisi miaka kadhaa ambayo imepita kuna mtu niliwahi kumsamehe hivi hivi kama unavyo omba wewe japo yeye aliomba kwa kumaanisha akiwa anatia sana huruma, nahisi kumpa nafasi nyingine ni moja kati ya makosa makubwa zaidi mimi kuwahi kuyafanya kwenye maisha yangu mpaka leo kwa sababu bila kufanya vile nahisi mpaka sasa kuna matatizo yasingetokea hivyo kukusamehe wewe ni sawa na kurudia ko……” Gavin kabla hajamalizia taarifa hiyo simu yake ilianza kuita mfukoni, aliitoa na kuipokea.
Haikuonekana kuwa simu nzuri kwa sababu ilimbadilisha, bila shaka alipokea tarifa mbaya wakati huo ndiyo maana sura yake ilikuwa tofauti ghafla. Simu hiyo ilibadilisha upepo wake na kumfanya aruhusu risasi zote ambazo zilikuwa kwenye bastola kwenda kwenye kichwa cha Bashir. Mwanaume huyo alikufa vibaya sana akiwa anaendelea kuomba msamaha ili aweze kuachwa.
Ulipita muda kidogo tu ndipo msafara wa mkuu wa majeshi ukawa unakuja kupitia eneo hilo. Msafara huo ulikuwa kwenye mwendo wa kawaida lakini wenye tahadhari kwa sababu mheshimiwa huyo alikuwa ameitangaza vita mpaka na raisi wa nchi hivyo alitakiwa kuwa makini kwa masaa yote ishirini na manne. Msafara huo uliweza kusimama hususani baada ya kugundua kwamba kwa mbele kulikuwa na gari ambayo ilisimama barabarani.
Alishuka akiwa na tahadhari kali, makomando wake walikuwa makini kuhakikisha kwamba mheshimiwa anakuwa salama muda wote. Gari ambayo aliiona mbele haikuwa mpya kwake, alikuwa akiijua vyema kabisa kwa sababu ilikuwa ni ya kijana wake Bashir hapo akahisi hali ya hatari mbele yake. Haikuwa kawaida kabisa kwa kijana wake kuweza kufanya makosa ya namna hiyo na hata siku moja asingeweza kufanya jambo la namna hiyo hivyo ikamlazimu kusogea zaidi ili aweze kuona kilichokuwa kimetokea ndipo akahamaki aliyokuwa anayaona. Kijana wake huyo alikuwa amekufa na sio kufa tu alikuwa amekufa kikatili isivyokuwa kawaida. Alionekana kabisa kwamba aliteseka kabla hajafa, mwanaume mmoja aliinama na kuugusa mwili wake;
“Bado ni wa moto sana, kwa maana hiyo huyu amekufa sio zaidi ya dakika kumi ambazo zimepita. Maana yake muuaji bado yupo karibu na eneo hili” walishtukia jambo hilo lakini walikuwa wamepoteza muda mwingi kufikiria, ni wakati ambao walihisi mmoja wao anashuka taratibu kuelekea chini.
Komando huyo alishuka taratibu baada ya upanga ambao ulikuwa na makali ya kutisha kutoboa vibaya shingo yake ukatokezea mpaka mbele. Alibaki amelishika koo lake wakati wenzake wanahamaki akiwemo mkuu wa majeshi kwani lilikuwa tukio la ghafla ambalo hawakujiandaa nalo kwa muda huo. Wakiwa wanaangaza huku na huko waliona kivuli juu, nguvu ambayo mtu aliyekuwa juu alikuwa anakuja nayo ilikuwa ni kubwa mno, mtu huyo alitua kwenye kifua cha mkuu wa majeshi ambaye alibebwa mpaka kwenye gari, alijibamiza vibaya mgongoni kiasi kwamba hakuwa na uwezo wa kusimama tena. Alibaki anahema kwa maumivu akiwa analalamika na kutukana ila muda haukuwa muda rafiki kwa ajili ya kufanya jambo hilo.
Gavin aligeuka kwa sarakasi zingine akiwa anamkimbia bwana ambaye alikuwa ametoa bastola na kuanza kupiga risasi ovyo.
94 inafika mwisho.
FEBIANI BABUYA.