Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

Simulizi ya kipelelezi: Idaiwe maiti yangu

STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA THEMANINI NA SABA
SONGA NAYO................


Wenzake waligeuka kumwangalia kwa muda, hali yake haikuwa njema japo alijikaza kusimama, zile hasira zake ndizo ambazo zilimfanya awe kwa kwanza tena kurudi kwa mwanaume yule, kurudi kwake ikawa safari yake ya mapema kwenda kuzimu. Alienda bila balansi ya kueleweka, aligeuka na mateke mawili mfululizo, aliishia kupiga hewa, aliinama na kujigeuza kwa kujiviringisha lakini alikuta kapiga hewa, hakumuona mhusika, kasi ambayo Gavin alikuwa anatembea nayo haikuwa inaendana naye, alibaki ameduwa mpaka alipohisi kuna mtu nyuma yake.

Aligeuka kwa pupa, bahati ikawa mbaya zaidi kwake, alikamatwa kwenye eneo lake la koromeo ambalo lilinyofolewa kikatili kiasi kwamba hata wenzake walianza kuingiwa na woga. Slyvanos alikufa akiwa hana msaada wowote ule, Dayana aliitoa bastola yake na kuruhusu risasi nyingi sana kuweza kupiga lakini alifanya kosa kwa sababu ziliishia kwa mwenzo na kummalizia kabisa. Jambo hilo liliwafanya wapaniki, siku zote vitani ukipaniki basi umeshapoteza, risasi hazikufaa kwa sababu waliona wangezidi kuuana wenyewe hivyo njia bora zaidi kwa hapo ikawa ni kutumia mikono tu kuweza kupambana na huyo bwana mbele yao japo ilionekana kuwa zoezi lenye utata mkubwa.

Dayana alitangulia mbele, alirusha ngumi yake ilitua kwenye tumbo la Gavin wala hakumkwepa, alirusha nyingine ilidakwa akavutwa kwa nguvu na kupigwa kichwa ambacho alihisi kwamba kinapasuka. Alirudishwa nyuma kidogo, ngumi ambayo ilizama kwenye eneo lake la moyo ilimfanya kushindwa kupumua vizuri, alikuwa anahema juu juu tena kwa nguvu kubwa kiasi kwamba alishindwa kuhimili kuendelea kusimama ikamlazimu aweze kukaa.
Jaden alikuwa anaichanganya miguu yake kwa kasi ila kwa bahati mbaya hakufanikiwa hata kumfikia bwana huyo, alisimama akiwa anakakamaa. Upanga ulizama kwenye shingo yake vibaya kiasi kwamba ulitokezea mpaka nyuma, ulipokuja kuvutwa, hakuwa hai tena, hayo yote Dayana alikuwa anayashuhudia kwa macho yake akiwa amekaa hana jambo anaweza kulifanya. Tigan aliichomoa bastola yake ili ashambulie kwa risasi, Tigana alijirusha juu na kurudi chini kwa kasi ya ajabu, risasi zilipiga hewa.
Mkono wake wenye bastola ulikutanishwa na mguu bastola ilimponyoka, Gavin aliurusha upanga wake juu kwa nguvu kubwa huku macho yake yakiwa makali isivyokuwa kawaida. Tigan alikuwa ameurusha mguu wake, mguu ulikutanishwa na ngumi nzito na kuufanya kupinda kiasi, alipiga kelele ambazo hazikudumu zikabadilika baada ya mkono kuzama kwenye mbavu yake ambayo ilivunjwa wakati anashtuka alikuwa anaelekea chini. Gavin alizunguka kwa sarakasi na kutua juu ya Tigan kwenye kifua, alitapika damu nyingi akiwa anahema kwa mbali mno lakini wakati huo ule upanga ulikuwa unatua kwenye mikono ya mwanaume huyo.

Aliudaka na kuuzamisha kwenye moyo wa Tigan, wanaume hao walikuwa wanakufa kama utani ila ndio ulikuwa uhalisia wa mambo hayo. Wanaume watatu mpaka wakati huo walikuwa kwenye hali mbaya, ni Crepin na Bariki Dumba ambao walikuwa wamesimama japo nao walikuwa hawako sawa kwani alikuwa amewapitia mara ya kwanza. Bariki alikuwa na uchungu ambao alitakiwa kuulipa, Tigan kwake alikuwa zaidi ya kaka.
Alipiga makelele akiwa anatukana na kumfuata Gavin kwani hakuwa mbali, kisu kilirushwa huku naye akiwa anakuja, lakini wakati anafanya hayo Gavin naye alikuwa ameutuma upanga wake ambao uliikatisha safari ya Bariki. Ulizama kwenye paja lake, mwanaume huyo alitua karibu na alipokuwa Bariki, alimtisha, hakuwa anaweza kwenda popote pale, aliutua mguu wake kwenye goti likapinda, aliuvuta upanga wake kwa nguvu na kuitua ngumi yake kwenye shingo. Bariki alishuka chini akiwa anagugumia lakini muda huo huo alikaa kimya, ni Crepin ambaye alikuwa anajishauri kama ashambulie au aondoke eneo hilo kwani alikuwa amebaki mwenyewe lakini misingi ya kazi yake haikuwa ikimtaka kabisa yeye kuweza kukimbia kwenye eneo la tukio.

Akiwa anajishauri alishangaa upanga unakuja upande wake, ulitua kwenye kifua bahati nzuri ulikuja kwenye kishikio, alipata maumivu makali kwani upanga huo ulikuwa mzito. Mwanaume huyo mbele yake Gavin alimfikia mara moja, wakati anarusha ngumi yake alipigwa na kitu kizito kwenye tumbo, ulikuwa mkono. Zilifuata ngumi tatu kwenye kifua akadondoka na kupoteza fahamu muda huo huo. Dayana alikuwa anajivuta chini alipokuwa akiwa hana hata ujasiri wa kuweza kunyanyuka ili apambane na bwana huyo ambaye alikuwa mbele yake.

Alikuwa amepoa tayari lakini hiyo nguvu ya kusimama ndiyo haikuwepo, alikuwa anahema na kumeza mate kama kibaka ambaye amefikishwa jela kwa mara ya kwanza kwenye maisha yake. Mambo ambayo aliyaona hapo kwa muda mfupi yalikuwa yanataka sana moyo kuweza kuyavumilia na kujifanya haujaona halafu usimame kupambana na bwana huyo. Alikuwa anajivuta kwenda nyuma mpaka pale ambapo alikita kwenye jiwe kubwa, alijua kabisa hana sehemu nyingine ya kuweza kwenda.

Ujivuni wake na maamuzi yake ya kujigamba ndiyo ambayo yalimfanya wakati huo kuishia sehemu mbaya kama hiyo, maamuzi yake yalikuwa ya kipuuzi na kwa wakati huo yalikuwa yanamtokea puani. Angefuata ule ushauri ambao alipewa mara ya kwanza asingekuwa kwenye majuto, mpaka wakati huo alikuwa mewapoteza vijana wake watatu na wawili hali zao hazikuwa zikieleweka vizuri huku yeye pekee ndiye ambaye alionekana kuwa mzima wa afya kabisa kiasi kwamba alikuwa anaweza hata kusimama na kuondoka eneo hilo. Gavin alimsogelea pale alipokuwepo.
“Nimekwambia mapema kuhusu hili bibie, haya maisha muda mwingine huwa yanawapa watu somo muda ukiwa umeenda ndiyo kama hivi. Ni dakika kadhaa tu nyuma nimetoka kukupa ushauri wa jambo gani la mhimu wewe kuweza kulifanya ila umedharau na kuleta ujuaji, maamuzi yako ya kipumbavu kama kiongozi yameyaponza maisha ya vijana wako. Sijui utakuwa na lipi la kujitetea kuhusu hilo.
Ukiwa na uwezo wa kufanya jambo fulani ogopa sana kutangaza hadharani kwa sababu kuna watu huwa wanamchukulia kila mtu kama mshindani kwao hivyo kama wakikujua wewe basi watakutafuta wakumalize. Ndilo kosa ambalo umelifanya kuanza kunitambia. Nikiwa China, kuna jamaa niliwahi kukutana naye, yeye alikuwa anajiamini kwamba anaweza kupiga mtu yeyote yule duniani hivyo alikuwa anazunguka kila sehemu akimkuta mtu mwenye uwezo wa mapigano basi anamhesabia kama ni mshindani ambaye ni hatari kwake hivyo akawa anawaua mpaka siku alipokuja kukutana na mimi.
Nilimuua kizembe tu kwa sababu alinidharau, lile ni kosa ambalo mpaka sasa nina uhakika huko aliko huwa analijutia. Ile dharau yake ndiyo ambayo iliondoka na maisha yake kama wewe ambavyo umewafanyia vijana wako. Haya mauaji hapa ni wewe ndiye sababu, wewe ndiye umewaua vijana wako kwa sababu ya ujuaji wako”
Ile ni shule zaidi ya kitabu alipewa lakini alianza kuielewa vizuri muda ukiwa umeenda. Alikuwa na nafasi ya kufanya hivyo mapema lakini alidharau, muda haukuwa rafiki kwake ndipo alilikumbuka hilo. Gavin alitoweka eneo hilo akimuacha Dayana mzima wa afya kabisa, alijua ile hatia ambayo angejikuta nayo ndiyo ilikuwa adhabu ya ubishi wake, jambo lile lingemtafuta maisha yake yote.

Dayana aliibeba miili ya wenzake na wale majeruhi na kuondoka nao huku akiwa anawaza sababu ya msingi ya kumjibu bosi wake. Kwa kosa ambalo alikuwa amelifanya, hasara ya kuliteketeza kundi lake kwa mkono wake mwenyewe? Hakuwa na uhakika kama kiongozi wake angemuacha hai hivyo hakupata hata tone la usingizi, alijitahidi tu kuihifadhi miili ya wenzake na kuwatibia wale ambao hawakuwa kwenye hali mbaya kisha akawa amezongwa na mawazo ya sababu za kumpa bosi wake.
Akiwa kwenye hayo mawazo ndipo alipokea ujumbe mwingine mzito na wa kutisha, alihisi huo ulikuwa mbaya kuliko hata ambalo lilimkuta na wenzake. Mkurugenzi Othman Micho alikutwa ameuawa na mwili wake ulipatikana kwenye bwana lake la kuogelea nyumbani, habari hiyo iliupasua moyo wake, alihisi jambo hilo haliwezekani alikuwa anaota ila hakuwa na uwezo wa kubadilisha lolote lile kwa sababu kama picha alitumiwa. Nani alikuwa amemuua mkurugenzi? Ni swali ambalo hata yeye hakuwa na uwezo wa kulijibu, alijihisi kuchanganyikiwa, kichwa kilikuwa kizito akakaa sehemu na kuanza kushusha kilio kwa hisia na uchungu mkubwa.
Ndiyo maana wakati huo alikuwa amekaa na kuujutia uamuzi wake, kushindwa kwake kuweza kufanya mahesabu na maamuzi sahihi. Dayana alijiona kwamba hana maana tena, alijiona kuwa yeye ndiye sababu ya yote hayo kutokea. Angeweza vipi kupambana na ulimwengu mwanamke huyo na kuibeba hatia ya hayo yote ambayo aliyasababisha? Moyo wake ulikuwa mdogo, mambo hayo yalikuwa makubwa asingewezekana nayo. Dayana alitoa bastola ambayo ilikuwa kwenye droo ya meza ambayo alikuwa ameegamia, alitazama kwenye simu yake ambako kulikuwa na picha za familia yake pamoja na hao wenzake wa THE INVISIBLE, kisha akajipiga risasi. Dayana aliamua kuyabeba maisha yake mwenyewe kwa kujiua kwa sababu ya hatia moyoni.

87 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA THEMANINI NA NANE
SONGA NAYO................



***********
Hussein Damoga, aliyekuwa mlinzi wa raisi alishtuka kutoka kwenye usingizi wa kifo, alikuwa anajihisi uchovu kwenye mwili wake na maumivu makali yalikuwa yanamuelemea. Hakuelewa yuko wapi kwa wakati huo mpaka akili yake inarudi lakini alielewa kabisa kwamba hali yake haikuwa nzuri hata kidogo, asingeweza kulidharau jambo hilo.
Aliyafumbua macho yake taratibu na kuanza kuangaza kila kona, alihisi uwepo wa mtu na alipo geukia upande wake wa kulia alishtuka na kujisikia vibaya. Raisi alikuwa ameketi eneo hilo akiwa anamwangalia kijana wake huyo, alijisikia vibaya kwa sababu yeye ndiye ambaye alikuwa anatakiwa kumlinda kiongozi huyo mpaka wakati huo ila kwa bahati mbaya sana hakuwa na huo uwezo kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya kitandani. Alimuangusha mheshimiwa.
“Kiongozi naomba unisamehe kwa sababu nilikungusha kutekeleza ile kazi, nilifanya kila ambalo ninaliweza lakini nakiri wazi kwamba yule mtu alikuwa ni hatari zaidi kwa upande wetu, sikuwa na uwezo wa kushindana naye kwa namna yoyote ile. Ni mtu mwenye uwezo mkubwa ambao sijawahi kuuona kabisa tangu siku nazaliwa”
“Najua uliniangusha na ndiyo maana nipo hapa, nipo hapa ili mimi mwenyewe niweze kulitatua tatizo hilo Hussein. Leo ni siku ya mazishi ya mke wangu, wauaji bado wapo wanazurura tu hawajakamatwa kwa sababu yako, mke wangu hawezi kurudi tena sijui kama unalielewa hilo”
“Nalielewa mheshimiwa, nakumbuka mtu yule alinipa onyo, alidai ananiacha hai ili nifikishe ujumbe kwako wa kukupa onyo. Alinitaka nikwambie kwamba omba Mungu usiwe umehusika kwenye jambo lolote na pindi akiwa na uhakika kwa asilimia zote mia moja basi hatakuacha hai tena”
“Mhhhhhh Hussein tangu lini umefundishwa uoga namna hii, tangu lini ukawa dhaifu kiasi kwamba unakubali hata kumtisha bosi wako? Unamtisha mtu ambaye ameyabadilisha maisha yako mpaka ukaanza kuonekana mtu mbele ya watu? Sikutegemea hata siku moja hili kutoka kwenye kinywa chako, umekuwa miongoni mwa wanadamu ambao bado wanaendelea kunishangaza hapa duniani”
“Mheshimiwa siongei hapa kwa sababu nakutisha, unajua kabisa mimi nakuheshimu kwa kila jambo ambalo umenifanyia kwenye maisha yangu, wewe ni raisi wangu ambaye nimeapa kuyatoa hata maisha yangu kwa ajili yako na….”
“Kwahiyo hapo kitandani ulipo ndipo uliapa kwamba utanilinda?”
“Hapana mheshimiwa”
“Sasa hivyo viapo vinatoka wapi?”
“Nisamehe kiongozi”
“Nikusamehe baada ya mabalaa kunitokea mimi, unaweza ukanirudishia mke wangu, unaweza ukairudisha ile furaha ambayo nilikuwa nayo mwanzo? Jibu ni kwamba hauwezi na wewe ndiye ambaye nilikuamini kwamba ungeifanya kazi hii kwa weledi mkubwa”
“Nilijaribu kadri ya uwezo wangu mheshimiwa”
“Haukujaribu, kwa sababu kama ungejaribu basi usingekuwa hapa muda huu na kuanza kusifia sifia kila ambaye unakutana naye”
“Sikutaka kuonekana muongo kwako ndiyo maana nimekwambia ukweli mheshimiwa”
“Ukweli kwamba?”
“Gavin Luca huenda muda wowote atafika kwako”
“Kwahiyo una imani raisi wa nchi anaweza kuvamiwa?”
“Nina imani na ulinzi wako ila sina imani kama kuna mtu anaweza kumzuia yule mtu”
“Ana nini cha ziada ambacho kimekutoa imani na ule ujasiri wako Hussein?”
“Ni kwa sababu huenda hujamuona mheshimiwa, kuna binadamu ambao wanaweza kuhimilika hata akiwa mbele yako lakini sio yule mtu, sina uhakika kama naye ana moyo wa kawaida kama sisi”
“Ulifanya kosa kubwa ambalo hukutakiwa kusamehewa kabisa, mara ya kwanza nilikuwa napanga nikupe msamaha na nafasi ya mwisho lakini sidhani kama unastahili hata kuweza kupewa nafasi yenyewe”
“Mheshimiwa najua nimekukosea pakubwa na kukukwaza lakini sio sababu ya mimi kukwambia uongo kwa sababu kufanya hivyo nitakuwa nayahatarisha maisha yako jambo ambalo sitaki litokee”
“Kwahiyo kwako ujasiri ni kukaa hapa na kuanza kumtisha raisi wako?”
“Sina maana hiyo mheshimiwa”
“Lakini mimi ndo naona hivyo”
“Kama kuna sehemu nimeongea vibaya naomba unisamehe na nipo tayari kubeba adhabu yoyote ambayo utanipa kwa makosa yangu ya kushindwa kumleta mama yule kwenye mikono yako”
“Una uhakika na ulicho kizungumza?”
“Ndiyo mheshimiwa, hii ni sehemu ya kazi yangu hivyo najua sheria inasema kama nikifanya kosa basi inatakiwa pia niwe tayari kukumbana na matokeo yoyote yale ambayo yatakuja mbele yangu”
“Unajua kabisa kwamba una familia Hussein!”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Vipi kama mkeo akilipa kwa niaba yako?”
“Mheshimiwa sijakuelewa”
“Umesema upo tayari kubeba adhabu yoyote kutoka kwangu ndiyo maana nimekuuliza kama mkeo anaweza kuilipa kwa niaba yako”
“Hapana kiongozi naomba usifanye hivyo”
“Hakuna sehemu nimesema jambo lolote, mimi nimekuuliza wewe swali hivyo ni jukumu lako kuweza kunijibu kwa usahihi zaidi”
“Kosa nimefanya mimi mheshimiwa, sio mke wangu”
“Basi utachagua wewe kama mkeo alipe au wanao”
“Mheshimiwa, tafadhali fanya lolote haya uyabebe maisha yangu ila familia yangu haihusiki kwa lolote kwenye hili”
“Lakini unakumbuka kabisa Hussein niliwahi kukufunza kuhusu jambo hili, kuna wakati familia zetu huwa zinalipia gharama kubwa tena kwa makosa ambayo tunayafanya sisi hata kama wao hawana hatia. Wewe ndiye ambaye umefanya kazi za kuyabeba maisha ya watu wengi sana na familia zao ambazo ziliwahi kunikosea mimi tena ulikuwa unafanya kazi hiyo bila hata kuuliza kwa sababu ulijua ni amri na ulikuwa ni wajibu wako kufanya hivyo, unataka kuniambia kwamba haukuwahi kuwaza kama zile familia hazikuwa zimehusika kwa madhambi ambayo waliyalipa?”
“Kiongozi najua hilo, naomba uyachukue maisha yangu lakini usiiguse familia yangu tafadhali”

“Hussein kama ingekuwa rahisi namna hiyo basi mpaka sasa mke wangu pia angekuwa salama. Kuna watu inatakiwa walipe madhambi ya watu wengine ili maisha yaweze kwenda, kama kila mtu atakaa sehemu kwa kutia huruma basi niamini mimi hii dunia haifiki popote, kuna muda haijalishi kwamba una hatia au hauna hatia ila utahukumiwa tu na utalipa kwa ajili ya watu wengine. Taifa kubwa tu kama Marekani asilimia sabini ya watu wake wapo jela na hawana makosa, sasa kwanini wapo jela? Walishindwa kulipa gharama za kuachiwa huru wakawa hawana namna zaidi ya kuingia huko.

Halijaishia huko tu hata hapa kwetu ipo hivyo, kuna watu wengi sana wapo magerezani na hawana hatia yoyote, kuna watu wapo kule kwa sababu waliwakosea watu wenye nguvu, kuna watu wapo kule kwa sababu wamezibeba kesi za watu wenye pesa, kuna watu wapo kule kwa sababu ya maamuzi mabovu ya mahakama, kuna watu wapo kule kwa sababu tu mwanasheria anaijua vizuri sheria aliamua kumfunga mnyonge ambaye haelewi lolote kuhusu sheria hivyo asingeweza kushindana naye mahakamani.
Unahisi mamlaka hatujui hayo yote? Lakini kwanini hao watu wanaendelea kuwepo huko wakati hawana hatia? Umenivua nguo Hussein, umenifanya nijihisi raisi dhaifu kwa sababu nilikupa kila rasilimali ambayo uliihitaji halafu taarifa ambayo unaniletea hapa ni kwamba haukumpata yule mama? Tena haujaishia hapo unaanza kunitisha kabisa bila uoga tena mbele yangu kwa kumsifia huyo mtu wako halafu wakati huo huo unategemea mimi nifanye vile unataka wewe?

88 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
Mkuu hivi vipande vya mwisho viko Sawa kweli mbona kama kuna kimoja hakipo?
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA THEMANINI NA TISA
SONGA NAYO................


Kuna maana kubwa ya mtu kuwa kiongozi, kuna wakati yanahitajika maamuzi magumu ili kutoa elimu na funzo, ni wakati sasa wa kulitoa hilo funzo ambapo nina imani hata wenzako hawatafanya kosa kama ambalo umelifanya wewe, litakuwa somo na kwa watu wengine. Bila kufanya hivi kila mtu atahisi anaweza kufanya kile anajisikia kisha atatokomea anako kujua yeye kirahisi au atakuja kunitongoza hapa kirahisi tu nitamuelewa. Wewe ndiye ambaye unatakiwa kuwa funzo kwa wengine kwa sababu ni mtu ambaye nilikuweka karibu na kukuamini sana”

Hussein alijua kwenye maisha kutumika kama funzo kwa watu wengine ni moja kati ya vitu vya hatari mno tena isivyokuwa kawaida hivyo alielewa jambo ambalo lilikuwa linaenda kutokea wakati huo. Mwanaume huyo alitakiwa kutumika kama mfano ili kuhakikisha wengine hawafanyi makosa kama hayo.
“Unaweza kuniahidi kwamba angalau utawaonea huruma hata wanangu?” aliongea akiwa anashusha machozi pale kitandani ambapo alikuwepo.
“Kiuhalisia ni kwamba sina mpango wa kumuua yeyote kwenye familia yako zaidi yako. Lakini mkeo lazima alipe na jambo hilo unatakiwa ulishuhudie kwa macho yako kisha baada ya hapo ambaye atakufa ni wewe tu Hussein na kama huwezi kulishuhudia jambo hilo basi hapo sitakuwa na namna zaidi ya kuua familia yako yote”
Ni maneno mazito ambayo raisi aliyazungumza wakati huo, Hussein alimuelewa kiongozi huyo alichokuwa anakimaanisha, moyo wake ulianza kwenda mbio isivyokuwa kawaida, siku hiyo aliona hasara za kuoa mwanamke mrembo mbele za watu. Maana ya mheshimiwa ni kwamba bwana huyo alitakiwa kumshuhudia mkewe wa ndoa akiwa anafanya mapenzi na mwanaume mwingine, jambo ambalo hakuwa na uhakika kama angeweza kulihimili lakini alipewa chaguo kwamba akifanya hivyo basi mkewe na wanae wangeachwa hai lakini kama angegoma basi wote wangekufa naye.

Alipewa mtihani mzito ambao hakuwa na uwezo wa kuukataa, bwana huyo alibebwa hapo na kupelekwa ndani ya chumba kingine, ndani ya hicho chumba kikubwa alishtuka baada ya kumuona mkewe amelazwa kitandani akiwa uchi bila nguo yoyote. Alipiga kelele kuweza kuwaasa wasifanye jambo hilo ila hata nguvu hizo hakuwa nazo, mwili wake ulikuwa na makovu mengi na majeraha ya kutosha hata kusimama tu alikuwa hawezi. Alijirusha kutoka kwenye mikono ya wale wanaume na kudondokea chini akiwa hajiwezi kwa lolote, mkewe alikuwa hawezi hata kumuangalia mumewe, naye alikuwa anafanya hivyo kwa ajili ya watoto wao.

Hussein alimuona mwanaume mmoja akiufungua mkanda wake taratibu akiwa anamsanifu, alikuwa anaenda kula mali ya bure kabisa bila kuitolea jasho. Bwana huyo alivua nguo zote na kupanda kitandani akaanza kujilia tunda kiulaini tu, Hussein alikuwa anashuhudia ukatili huo kwa mtu ambaye aliyatoa maisha yake kwa ajili yake ila sasa angefanyaje na bwana huyo ndiye mwenye nchi? Alilazimika kukubali amumivu hayo kuwalinda watoto wake.

Mwanaume huyo alimaliza nusu saa nzima akiwa anamfanya mwanamke huyo kutoa miguno, bila shaka hata yeye alinogewa akasahau kama alikuwa anabakwa kwa nguvu. Jambo hilo lilikuwa linampa maumivu makali mno Hussein ambaye bila kutarajia alipigwa risasi nyingi sana. Zoezi hilo lilifanywa na raisi mwenyewe kwa sababu hakuwa na imani tena na kijana wake, alihisi alimfanyia usaliti na kosa kubwa kusifia watu wengine wakati yeye mwenyewe yupo. Baada ya kuhakikisha amemaliza zoezi hilo, alitoka sasa kwenda kujiandaa kwa ajili ya kumpumzisha mkewe.

Jambo moja ambalo raisi alifanya kosa ni kuingia kwenye hiyo nyumba bila kufanya ukaguzi, eneo hilo mkuu wa majeshi alimhakikishia kwamba ndilo alikuwa amemhifadhi kijana wake baada ya kumkuta akiwa kwenye hali mbaya. Eneo hilo lilikuwa na kamera za siri kila sehemu ambazo zilikuwa ni taa za mwanga ambao ulikuwa unamulika humo ndani. Raisi kwa sababu alikuwa na jazba na mihemko, alisahau kabisa kuangalia yote hayo hivyo alinasa kwenye mtego maana yake kila ambalo alilifanya humo ndani lilirekodiwa. Haikuwa hali nzuri kwake.

Lengo la mkuu wa majeshi kufanya hivyo, alikuwa hana uhakika na mambo yake kwa wakati huo, alianza kuiona hatari kila kona ikimzunguka hivyo alianza kujitengenezea usalama wake mapema, alijua kuna siku raisi huyo angekuja kuujua ushenzi ambao aliufanya hususani baada ya kuanza kuwa na mashaka naye baada ya kuonekana kwamba alirudi ndani ya lile eneo ambalo walienda wote kwa mara ya kwanza hivyo alikuwa anajipanga ili kama kulikuwa na hatari yoyote ila baadae azitumie video hizo kama kinga kwani alitambua raisi akija kumzingua basi angetishia kumlipua nazo basi angejua hatua zingine ambazo zingefuata baadae.

Ilikuwa siku ya msiba wa mke wa mheshimiwa, ni siku ambayo kama taifa lilikuwa na harakati nyingi mno kwa ajili ya kumpumzisha first lady. Ni siku hiyo hiyo ambayo mheshimiwa alikuwa ametoka kuufanya ushenzi, alitoka kumuua mlinzi wake mwenyewe tena kwa udhalilishaji mkubwa yeye akidai kwamba alikuwa anatoa somo na kwa wengine ambao wa walikuwa wanatazama.

Raisi huyo aliifanya hotuba yake kwa masikitiko makubwa mno, masikitiko yake yalikuwa juu ya kumpoteze kipenzi wa maisha yake, alidai kwamba hana nguvu ya kufanya jambo lolote lakini ilimbidi kufanya hayo yote kwa ajili ya watanzania, alidai kwamba yeye ni mtu ambaye alilipenda taifa lake ndiyo sababu licha ya mkewe kuweza kufariki bado alikesha kwenye ofisi kuweza kulipigania taifa lake. Siasa ulikuwa ni mchezo mchafu na raisi George alikuwa miongoni mwa wachezaji wa hiyo michezo.

“Mabibi na mabwana! Ndugu zangu watanzania! Na wageni waalikwa kutoka pande zote za dunia! Leo ni siku ya simanzi kwangu, kwa familia yangu lakini pia kwa watanzania wenzangu. Mimi nimempoteza mke wangu, watanzania wamempoteza first lady wao lakini dunia imempoteza ndugu, rafiki na mpendwa wao ndiyo maana wote tupo hapa kuweza kumuaga kwa mara ya mwisho.
Msiba sio kupoteza wala sababu ya kilio, msiba ni ishara ya ushindi kwa watu werevu na watu imara, msiba upo kwa ajili ya kuhakikisha watu wanayakumbuka maisha baada ya kifo, kifo kinatukumbusha umuhimu wa watu kipindi walipokuwa hai, kifo kinatupatia somo la kuweza kuyafurahia maisha lakini kifo kinatoa pumziko la milele kwa mtu baada ya kuzongwa na maswaibu ya ulimwengu, yale ambayo kila siku yanawachosha watu, sasa kwanini mtu akifa ionekane kama ni mateso? Hii haiwezi kuwa sawa, mtu kufa ni ishara ya ushindi.
Mke wangu mpendwa amenitoka lakini kwa sababu ya uzalendo wangu ulio tukuta, kwa sababu nalipenda taifa langu kuliko jambo lolote bado nimekesha ofisini nikifanya kazi. Nimefanya hivyo kwa uzalendo lakini pia kumkumbuka mke wangu enzi za uhai wake, alikuwa mkono wangu wa kulia kwenye kazi, ni yeye ambaye alinitaka kila siku niweze kuwapambania na kuwapigania watanzania kwa namna yoyote ile, hivyo kama ulikuwa unaona raisi wako anafanya vizuri kila siku basi ujue kwamba nyuma yake alikuwepo mkewe ambaye alikuwa anamfanya yeye kuwa bora kila siku.
Najua kwamba kuna bazazi ndiye amehusika kuyafupisha maisha ya mke wangu, sikatai kwamba kifo ni ushindi ila ni ushindi mzuri pindi mtu akifa kwa mapenzi ya Mungu, binadamu hatakiwi kabisa kuyafupisha maisha ya mwenzake kwa sababu kuna siku hata yeye pia atakuja kufa kwahiyo rasmi natangaza zawadi ya shilingi bilioni moja za kitanzania kwa atakaye fanikisha kumpata Sarah Martin ambaye ndiye alihusika na tukio la kumuua mke wangu tena kwa kumdhalilidha hadharani.
Hakujali kama huyu ni mke wa raisi, yeye alitimiza adhma yake lakini hakuishia hapo tu bali alifanikiwa kuwaua na wenzake wa karibu akiwemo mwanajeshi ambaye alidaiwa kuwa mpenzi wake Nickson hivyo mwanamke huyu ni hatari na hafai kabisa kuwepo kwenye jamii yetu. Najua jeshi la polisi na jeshi la nchi wapo kumtafuta jambazi huyu muuaji ambaye nina imani watampata lakini nimetoa zawadi hiyo kwa ambaye atamuona mara moja na kutoa taarifa haraka mahali husika ili apatikane haraka zaidi kabla hajaua watu wengine. Mkumbuke tu kumficha mtu huyu ni kuikaribisha hatari kubwa kwenye jamii kwa sababu anaweza kuua watu wengine tena. Kama amemuua mke wa raisi hashindwi kumuua mtu wa kawaida mtaani hivyo ni hatari popote pale alipo, mnatakiwa kumripoti mapema sana.
89 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA TISINI
SONGA NAYO................


Kupitia msiba wa mke wangu nataka niwape somo dogo la maisha. Miaka zaidi ya mia moja iliyopita kuna hadithi ya kijana mmoja ambaye alirudi nyumbani akamkuta mama yake analia. Alipo muuliza mama yake sababu ya kulia kwake, alimpa taarifa mtoto wake kwamba mume wangu amefariki yaani baba wa yule mtoto.
Kijana yule mdogo hakushtuka wala habari ile haikuonekana kuwa mbaya kwake, alitabasamu kiasi kwamba alimshtua mpaka mama yake. Hata ungekuwa wewe lazima ungeshtuka, unamwambia mwanao kwamba baba yake amekufa yeye anafurahi lakini kijana yule hakuwa mjinga kufanya vile kuna sababu kuu mbili ambazo zilimfanya kuwa mtulivu na kutoa lile tabasamu. Baada ya pale ndipo alimtaka mama yake ampeleke ulipokuwepo mwili wa baba yake, mama huku akiwa na maswali mengi kichwani, alisimama kishingo upande na kumuongoza bwana mdogo huyo mpaka chumbani mahali ambapo ulikuwepo mwili wa baba yake ukiwa hauna uhai.

Baada ya kufika, aliubusu mwili wa baba yake kwenye paji la uso kisha akamgeukia mama yake akiwa anabubujikwa na machozi kwa wingi na kumuuliza;
“Mama unajua kwanini kifo cha baba hakijanishtua zaidi ya kutabasamu?” mama akiwa na kwikwi kwa kilio cha muda mrefu akajibu kwa sauti ya chini
“Sijui ila nimebaki tu nashangaa juu ya jambo hili mwanangu”
“Kuna sababu kubwa mbili mama. Sababu ya kwanza; baba yangu aliwahi kunipa elimu kubwa kuhusu kifo akiwa hai, aliniambia kwamba mtu wangu wa mhimu anapokufa sitakiwi kuonyesha udhaifu mbele yangu, sitakiwi kabisa kuwa mnyonge kwa sababu ni wakati ambao mimi natakiwa kuwa imara kuliko wakati wowote ule. Ni muda ambao najua mimi nimekua sasa, natakiwa kuanza kuzivaa changamoto kwahiyo kama na mimi nikianza kujiliza basi nitakuwa dhaifu kwenye maisha yangu yote na hilo ni kosa kwa mtoto wa kiume kuwa dhaifu” mama huyo alishangazwa na jibu la mtoto wake ambaye umri wake haukuwa unaendana na kile ambacho alikuwa anakitoa kwenye mdomo wake.

“Sababu ya pili mama ni kwamba unapokuwa mwanaume tambua kabisa matatizo yote ya ulimwengu yanakuwa kwenye mgongo wako hivyo ukilala kidogo tu yanakuelemea na kukupoteza. Kuwa mwanaume ina maana ya kuwa jasiri, ina maana kubwa ya kuwa faraja kwa wengine kwa sababu kuna watu ambao hawawezi kuwa imara pekeyao, wanahitaji bega la kuweza kushushia machozi yao. Sasa kama mimi nikiwa dhaifu ni nani ambaye atakupa wewe bega la kuegamia wakati wa kulia mama? Ni mimi mwanao ambaye nina jukumu la kufanya hivyo”
Niamini mimi mpaka kijana yule anamaliza kuongea yule mama alizidisha mara mbili yake kulia, alikuwa ni mtoto mdogo ila baba yake alimfunza mengi mema na kumkuza kwenye misingi sahihi ya kiume. Wakati anaongea hata yeye machozi yalikuwa yanamshuka ila alijifunza kusimama kwa ajili ya wengine pindi wakiwa hawana uwezo wa kufanya hivyo kwa uwezo wao wenyewe.
Ni funzo gani umelipata kwenye hadithi hii ya kijana huyu na mama yake? Ni kwamba mtu anapokufa, usitumie muda mwingi kulia bali utumie muda mwingi kujifunza yale mema ambayo ameuachia ulimwengu, yale mema yake ambayo anakuwa ameyaacha ndiyo maisha yake ya duniani na ile ndiyo alama yake hivyo badala ya kulia tunatakiwa kusherehekea maisha yake ambayo alipata kuyaishi.
Hili ndilo jambo ambalo nalihitaji hata kwa mke wangu, najua ubora wake akiwa hai, najua alikuwa ni mwanamke shupavu mbele ya wengi lakini kumbukumbu hiyo bora sitaienzi kwa ukubwa kama nitatumia muda wangu mwingi kuweza kulia au kusikitika badala ya kuyafurahia mema yake. Nina uhakika hata yeye huko aliko atakuwa na furaha zaidi akijua kwamba maisha ambayo aliyaacha hapa duniani nimeyaishi na kwa pamoja tumeyaenzi vizuri kiasi kwamba atajihisi hakuna deni hata moja ambalo ameliacha na hiyo ndiyo maana halisi ya maisha na kifo”

Bingwa la propaganda, raisi wa Tanzania Mr George alikuwa mtaalamu wa kucheza na mdomo wake, ni moja ya sababu kubwa ambayo ilimfanya kila siku bwana huyo azidi kua na ushawishi mkubwa kwa watu. Alitoa hotuba ambayo haikuwa ndefu sana ila ilikuwa na elimu na ujumbe mkubwa mno ndani yake, ujumbe ambao aliutoa hususani wakati anasimulia simulizi ya yule kijana na mama yake mbele ya mwili wa baba yake iliwafanya wengi kutoa machozi.
Watu walishusha machozi kwa sababu ujumbe ulikuwa unagusa, ujumbe ulikuwa unaeleza kwa mapana namna watu wanavyokutana na matatizo mengi lakini wanachagua kuwa imara wakati wanayapitia matatizo ya namna hiyo. Watu walikuwa wanampigia makofi mheshimiwa, kwa kweli aliwakosha na hotuba yake, kuna watu hawakutamani kabisa amalize kuongea walimtaka aendelee kutoa ujumbe wa namna hiyo kwani kuna watu wangepona zaidi ya pale.
Maisha muda mwingine huwa yanawapa watu machaguo magumu, kuna wakati watu wanakuwa wanapitia mambo mengi magumu lakini hawana sehemu pa kuyasimulia, hawana mtu wa kuwasikiliza hivyo wanapopata nafasi kama hiyo kumsikia mtu akiongea hadharani yale maumivu ambayo wanayo moyoni, huwa wanahisi kabisa kwamba ni mahali sahihi pa wao kumwaga chozi kupunguza uchungu na maumivu na ndiyo sababu ilikuwa moja kati ya hotuba bora ambazo ziliwahi kutolewa duniani usingeweza kuiacha hotuba ya raisi George siku hiyo, ndiyo maana watu walibaki wanalia lakini kilio ambacho kiliwapa tumaini la ushindi kwenye mioyo yao.

Raisi George baada ya kumaliza hotuba hiyo ulikuwa ni wakati wa kumuaga mkewe hivyo alitaka kushuka hapo alipokuwepo lakini wakati anaanza kuzitupa hatua zake kuna kitu alikiona, hakuamini kama ilikuwa ni bahati mbaya. Ilimlazimu kuyageuza macho yake kugeukia ule upande ambao alihisi kwamba ameona vibaya, hakuona vibaya bali ulikuwa ni ukweli wenyewe, alimuona mtu ambaye kwa mahesabu yake hakuamini kama angekuwa hapo siku hiyo na kama angekuwepo basi isingekuwa kirahisi namna hiyo tena hadharani. Moyo wake ulishtuka na kupiga kwa nguvu, alihisi kuchanganyikiwa huku wageni ambao walikuwepo kwenye jumba jeupe hapo wakiwa wanamshangilia kiongozi huyo kwa hotuba yake bora kabisa. Unahisi alimuona nani?

“Kiongozi!!” Alitamka kwa sauti yeye mwenyewe akiwa haamini, kama sio kelele za watu waliokuwa wanamshangilia basi wangemsikia wakati anamuita mtu mwingine kiongozi wakati yeye ndiye bosi wa nchi. Natron Vinza ndiye mtu ambaye alikuwa hapo wakati huo akiwa kwenye suti yake, huyo ndiye alikuwa kiongozi mkuu wa kundi la THE IMMORTALS, mwanaume huyo aliishi gizani kwa miaka mingi ila siku hiyo aliamua kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tena akiwa hajajifunika kitu chochote kwenye mwili wake maana yake alikuwa tayari hata kuonekana kwa watu.

Eneo hilo la Ikulu alikuwa analijua kila kona kwa sababu aliwahi kuwa raisi wa Tanzania, sasa alifuata nini ndani ya eneo hilo? Raisi alibaki ametahayari asijue kipi anatakiwa kukifanya wakati huo. Bwana huyo alikuwa amemtolea tabasamu raisi huyo lakini ambalo halikuwa la kirafiki sana, hakuwa na amani hivyo akataka kusogea upande ule ili akaongee na bwana yule kwa sababu ndiye ambaye alimuweka kwenye hiyo nafasi na kama angeamua kumuondoa basi lilikuwa ni swala la muda mfupi tu. Haukuwa umepita muda mrefu tangu akutane naye kwa mara ya kwanza na kumjua kama ndiye alikuwa bosi wao lakini wakati anawaza hayo yote alielewa kamba haikuwa imemzuia mtu huyo kufika hapo Ikulu.

Hakujua bwana huyo aliingiaje bila mwaliko ila alijua pia hawezi kushindwa kufika ndani ya hilo eneo huenda kila kona alikuwa na watu ambao walikuwa wanaangalia kile ambacho raisi huyo alikuwa anakifanya. Kama alikuwa anaufanya ushenzi basi ilikuwa inaenda kula kwake muda mfupi ambao ulikuwa unafuata. Raisi alikuwa anatembea haraka haraka akiwa na walinzi wake kuelekea lile eneo lakini alipofika pale, hakumuona yule bwana, zaidi watu wengi walikuwa wakimsogelea na kumpa pongezi kwa kutoa moja ya hotuba bora mno.
Alibaki amehamaki asijue afanye nini, alibaki anayashangaa mawingu na watu ambao walikuwa wanampongeza, kwake alihisi kama watu hao walikuwa wakimpigia makelele tu kwenye masikio yake, hakuona kama walikuwa na la maana lolote lile. Aliomba taratibu za msiba zipelekwe haraka ili mambo mengine yaweze kuendelea, hakuona kama kulikuwa na usalama wa kutosha kwa wakati huo, alitakiwa kuingia kazini haraka.

90 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA TISINI NA MOJA
SONGA NAYO................



***********
Muda ulikuwa unakwenda, mambo mengi yalikuwa yanaendelea kutokea, Tanzania ilikuwa inazidi kuingia gizani na mkombozi hakuonekana alipokuwa, watu walikuwa wanaendelea kuhamaki namna mitaa ilivyokuwa kimya huku wakiwa hawaelewi ni nani alikuwa na kete ya huo mchezo mkononi ila kama ungekuwa mchezo wa kubashiri basi wengi wangempatia Gavin Luca kuwa bingwa. Bwana huyo aliaminika na kukubalika kwa watu wengi japo serikali ilikuwa inajaribu kumchafua ila huo haukuwa muda wake Gavin.

Yalikuwa majira ya usiku pembezoni mwa ufukwe wa bahari, kulikuwa na msafara wa gari tatu aina ya V8 nyeusi. Eneo hilo walikuwepo wanawake wawili ambao ndio walikuwa wanahudhuria nyakati hizo za usiku. Alikuwepo mama mlezi wa Gavin Luca pamoja na mke wa Luca, Norah Hassan, Luca kilikuwa ni kifupisho cha jina la baba yake mzazi ambaye alikuwa anaitwa Lucas Antony, aliitoa herufi S kama ambavyo Dayana aliwaleza wenzake ili hata wakati wanamtafuta wasije kuwa na uwezo wa kuunganisha tukio hilo na jina lake lote kwa ujumla, jambo hilo lilikuwa moja kwa moja linamuweka yeye kwenye sehemu salama kabisa hivyo ingechukua muda mrefu watu kuweza kuling’ua hilo.

Norah alielezewa historia ya kutisha ya familia hiyo, kwa mara ya kwanza alianza kuwaogopa watu hao mpaka alipopewa sababu ya watu hao kuishia sehemu kama hiyo hususani mumewe wa ndoa Gavin mwenyewe. Hakuwa binadamu wa kawaida kama wengine, kwenye mwili wake alikuwa na kitu cha ziada ambacho kilikuwa kinampa utofauti huo ila mwisho wa siku hakuwa na namna ya kuupinga ukweli, hiyo ilikuwa ni familia yake na alikuwa ana binti yao tayari hivyo wasingemruhusu aende popote kwani alikuwa anaenda kuhatarisha maisha ya familia nzima.

Usiku huo alikuwa amemsindikiza mama mkwe wake kwenye fukwe ye bahari hiyo majira ya usiku, eneo hilo alikuwa akienda kila siku kwa miaka kadhaa tangu ajue mwanae na mumewe waliuliwa kwenye hilo eneo. Alikuwa anaenda kwa ajili ya kupata kumbukumbu bora ya maisha ya wapendwa wake, hali ilikuwa mbaya kwa wakati huo hivyo hakuwa anaenda mara kwa mara ila siku hiyo aliona ni wakati bora zaidi wa kwenda kupata kumbukumbu hizo ambazo zilikuwa zinamfanya ajihisi kuwa karibu na wapendwa wake. Alikuwa sawa ila pengine wakati haukuwa sawa ama haukuwa rafiki kwake kwani hakujua dunia imejiandaa nini.

Walikuwa na ulinzi mkali kwa sababu ilikuwa ni familia ya tajiri mwenyewe, lakini walinzi ambao walikuwa wanauongoza msafara huo walikuwa ni wawili. Mama huyo alikuwa na mlinzi wake binafsi mmoja lakini hata mke wa Gavin aliambiwa kwamba akulikuwa na mlinzi ambaye alikuwa akimlinda yeye kwa siri wakati wote na mlinzi huyo kwa wakati huo hakuwa wa siri tena bali alikuwa akionekana waziwazi.
Wote walikuwa wameshuka kwenye gari wakisubiri mama huyo na mkwewe wafanya ibada ndani ya eneo hilo ambapo ingewachukua kama dakika thelathini tu kisha wangeweza kuondoka. Wakiwa hilo eneo walishangaa baada ya kuona kuna mlinzi moja anadondoka chini. Risasi ilikuwa imeusambaratisha ubongo wake damu ikawarukia mpaka waliokuwa pembeni yake, wakati wanajiuliza ni nani aliwavamia na alikuwa wapi mlinzi mwingine alidondoka tena ikawalazimu ambao walikuwa karibu kwenda kumzunguka mama na mkwewe ili wasidhurike kwani bosi wao asingewaelewa.
Walinzi walikuwa wanadondoshwa lakini walinzi wale wakiongozwa na wale wawili walifanikiwa kuwaingiza kwenye gari moja ambalo liliwashwa na kuondolewa kwa kasi eneo hilo hata hivyo hawakufika mbali, gari hiyo iliyumba yumba almanusura lipate ajali. Tairi lake moja lilikuwa limepasuliwa vibaya kwa risasi ya mdunguaji ambaye hawakujua mpaka wakati huo alikuwa wapi. Walinzi walikuwa wanapiga simu kuomba msaada, upande wa pili ulitoa taarifa ya kufika eneo hilo kwa muda mfupi ila wao walitakiwa kuhakikisha kwa gharama yoyote ile mama na mke wa bosi wanakuwa salama hata kama wao watapoteza maisha.

Risasi hizo zilikuwa zinatokea kwenye mti mmoja ambao ulikuwa mita mia tatu kutoka eneo hilo, mti huo nao ulikuwa ufukweni mwa bahari lakini upande mwingine. Kuna mwanaume mmoja alikuwa juu ya tawi la mti akiwa amejikunja vyema kama nyoka na silaha yake nzito ndiye alikuwa analileta balaa hilo. Ile gari ilikuwa imesimama pale pale, hakuna mtu hata mmoja ambaye alikuwa ametoka, wakati huo walikuwa wamebaki walinzi watano tu kwa ujumla wao.
Karibu na hiyo gari ilipokuwa walionekana watu sita wakiwa wanakuja, watano walikuwa kwenye suti nyeusi lakini mmoja tu alikuwa amejifunika shuka jeupe pee sura yake ikiwa inaonekana kwa mbali kwa sababu pia uso wake haukuwa ukionekana. Wanaume hao walisogea eneo hilo lilipokuwepo gari hilo, walisimama baada ya kubakisha hatua kadhaa kisha mwanaume mmoja akasogea mpaka ulipokuwa mlango wa gari, aliufungua kwa nguvu lakini alirudi nyuma akiwa anatetemeka, alipigwa risasi nyingi kwenye mwili wake akaishia kudondoka.

Wale wenzake hawakuwa na wasiwasi kabisa, hapo ndipo mlinzi mmoja wa wanawake hao akashuka akiwa ameshika bastola mbili kwenye mkono wake.
“Hizo bastola zako kwa sasa hazina msaada wowote ule kwa sababu kosa moja tu litapelekea wote ambao wapo kwenye hilo gari kufa. Ningekuwa nawataka wote mkiwa mmekufa basi mpaka sasa hiyo gari ingekuwa imelipuka mpaka saivi ila hawa wanawake nawahitaji wakiwa hai ndiyo maana sijafanya hivyo lakini kama utaleta jeuri mimi sina hasara yoyote kuweza kuwaua kwa sababu hawanihusu” aliongea mwanaume huyo kwa sauti nzito isiyo na mashaka, alisogea kidogo lakini mlinzi ambaye alikuwa na bastola kwenye mikono yake hakumpa hiyo ruhusa, bado alikuwa anayatafakari maneno ya bwana huyo na mpaka kuja hapo akiwa hana silaha kwenye mkono wake maana yake alikuwa na plani yake nyingine ndiyo maana hata yeye hakukurupuka kushambulia, watu werevu huwa wanaelewa hali kama hizo na ni mwiko kukurupuka.

“Eneo hili lina mdunguaji ambaye nina uhakika utatumia sio chini ya dakika kumi kujua ni wapi alipo, mdunguaji huyo anajua vizuri kazi yake ndiyo maana amewaua walinzi wengi ndani ya muda mfupi. Kuanzia sasa nahesabu mpaka tatu hao watu ndani ya gari wanatakiwa kutoka vinginevyo atapiga risasi kwenye tenki la mafuta na unajua kabisa gari lilikuwa limeshika moto wakati wa kuondoka hilo kwahiyo unajua kama akifanya hivyo kitatokea nini” mlinzi huyo alianza kuhema kwa nguvu jasho likiwa linamtoka.

Uamuzi ulikuwa ni wake, kuamua kushambulia kisha gari ilipuliwe ama akubali analo ambiwa ili waangalie namna nyingine ya kufanya, wazo la pili lilikuwa sahihi aliwataka watu hao watoke kwa sababu hakukuwa na njia ya kukimbilia. Walitoka wanawake hao wawili wakiwa na walinzi wengine wanne ndani ambao wote walikuwa na silaha zao mkononi kuhakikisha wanawalinda vyema. Mwanaume huyo ambaye alikuwa anafoka ndani ya shuka lake jeupe baada ya kuwaona wanawake hao alilivua na kulitupia pembeni.

Mwanga wa taa ya gari ulikuwa unammlika vizuri mwanaume huyo, baada ya kutoa shuka hilo mwili ulikuwa unaonekana vizuri kwa sababu alikuwa kifua wazi na suruali, miguuni alivaa sendo za kawaida tu, hakuwa na papara. Mwili wake ulikuwa unatisha kwa mtu wa kawaida kuweza kuutazama kwa sababu ulikuwa na makovu mengi isivyo kawaida. Hata uso ulikuwa na alama kubwa ya kisu kupita lakini jambo la kushangaza zaidi ni kwamba kwenye kifua alikuwa na jina ambalo liliandikwa kwa herufi kubwa GAVIN LucA.

Hawakuwa wakimjua hivyo walibaki wanamshangaa namna alivyokuwa anatisha, hawakuelewa alitokea wapi na alikuwa anataka nini kwao.
“Nina imani wote mtakuwa mmeshangazwa na ujio wangu usio wa kirafiki hapa, najua wote mnashangazwa na michoro yangu kwenye huu mwili wangu! Nina uhakika mtayapata majibu yangu hivi karibuni ila kabla ya hilo nahitaji hao walinzi wote waje wapigane na mimi, kama wakishinda basi nitawaacha wote muende bila tatizo ila kama mkishindwa basi nitaamua mimi nini cha kufanya baada ya hapo” alikuwa anaongea kama anatania ila hakuonekana kuwa mtu wa utani alikuwa anamaanisha anacho kihitaji.
“Wewe ni nani hasa ambaye unaonekana kuwa mgeni kwenye macho yangu na una tattoo ya mwanangu mwilini?”
91 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 
STORY: IDAIWE MAITI YANGU
MWANDISHI: FEBIANI BABUYA
STORYTELLER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP: 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+

********************
SEHEMU YA TISINI NA MBILI
SONGA NAYO................


“Umeuliza swali zuri sana mama yangu ila muda sio rafiki wa kujibiwa hilo swali. Nimewaelekeza wenzako kwamba kuna mdunguaji umbali kadhaa kutoka hapa ambaye anaweza kuua watu kumi ndani ya dakika moja hivyo nina uhakika hata kama vijana wako watahitaji kunishambulia na hizo bastola bado hawawezi kufanikiwa kukuokoa wewe na huyo mwanamke ambaye natamani kujua ni nani mpaka awepo kwenye hii familia yako”
“Unataka nini kwangu?”
“Namtaka mwanao”
“Una uhakika utampata?”
“Ndiyo maana nimekuja kwako kwa sababu najua nitampata”
“Unafanya kosa kubwa kuhitaji kunishika mimi”
“Ndicho ambacho mimi binafsi nakihitaji” mama huyo hakuwa na namna, walikuwa kwenye hali ambayo haikuwa nzuri kutaka mashindano hivyo ikamlazimu vijana hao kutumia mikono kumfunga bwana huyo mdomo. Vijana wa kutegemewa walikuwa wawili hapo ndiyo maana hakuwa na wasiwasi japo hakujua aina ya mtu ambaye alikuwa mbele yake, mtu ambaye alionekana kuwa na usongo mkubwa na mwanae.

Davoc Mavambo, ndiye ambaye alikuwa hapo muda huo, ni yule mwanaume ambaye kama kumbukumbu zako ziko sawa basi utakumbuka kwamba mkuu wa majeshi alifanikiwa kwenda Mlandazi kwa ajili ya kuomba msaada na ushauri, yule mtu ambaye yeye alienda kwake kwa ajili ya kumuomba msaada ndiye alikuwa huyo bwana mwenyewe. Bwana huyo alidai kwamba aliwahi kukutana na Gavin Luca ambaye alimfanyia kitu kibaya mno na kuacha kumbukumbu mbaya kwenye maisha yake kiasi kwamba hakuwa na uwezo wa kumsahau tena.

Kwa taarifa yake ni kwamba huenda Gavin alikuwa alisha msahau muda mrefu, kwa sababu mara ya mwisho alipokutana naye alimuacha kwenye hali mbaya, alikuwa ana uwezo wa kumuua lakini bwana huyo aliomba kupewa nafasi ya mwisho ya maisha, aliapa kwamba asingekuja kuonekana tena mbele ya macho ya Gavin. Alikubali kumpa nafasi hiyo lakini kwa kumpa alama ambazo kila atakapo ziona asije kumsahau abadani na ndilo jambo ambalo lilikuwa linafanyika mpaka wakati huo. Kwenye mwili wake alikuwa na alama nyingi za makovu, hayakutokea kwa bahati mbaya bali yalisababishwa na huyo mtu ambaye alikuwa anamtaka kwa wakati huo.

Alikuwa na vita na uhasama binafsi na mtu huyo, mwanaume huyo alikuwa ameishi gizani kwa muda mrefu ila aliamua kujionyesha hadharani kwa ajili ya kumpata Gavin, kuna biashara ambayo alihisi wao walikuwa hawajaimaliza vizuri. Kosa la Gavin lilikuwa ni kumpa nafasi adui yake aishi tena wakati alijua kabisa watu wa namna hiyo mara nyingi huwa wanaishi na visasi moyoni hata kama itachukua muda gani bado kisasi hakiwezi kupotea hata siku moja. Alikuwa anajiponza mwenyewe Gavin, makosa ya kutohakikisha anaikamilisha kazi yake, yalikuwa yanamtokea puani.

Walinzi walienda wawili kwa kasi, walitaka kumuonyesha mwanaume huyo kwamba hawakupewa kazi hiyo kwa bahati mbaya, bwana Mavambo alizunguka kwa nguvu akiwa anaikaza mikono yake, walinzi hao walionekana kama watoto wadogo, wakati anajizungusha walipishana naye, ile wanageuka walidakwa kwenye shingo zao, zilidakwa akiwa anawanyanyua juu, alizitupa zile maiti mbili. Wote walishangaa, alikuwa na nguvu za ajabu mtu huyo ikamlazimu mlinzi wa mke wa Gavin kuingilia kati.

Kijana huyo alikuwa mwepesi mno, miguu na mikono ilikuwa inafanya kazi ipasavyo, alizunguka kwa sarakasi nyingi ambapo alitua na mguu wake kwenye kifua cha Mavambo, alirudi nyuma kidogo na kuinua uso wake, alipishana na kisu kikija shingoni, aliinama kikambaraza kifuani. Aliudaka mkono wa kijana huyo na kuuvunja, kile kisu kilimponyoka akakidaka, alikizamisha kwenye kifua cha kijana huyo isha akakipitisha shingoni kwa nguvu. Alidondoka akiwa anahangaika, mwanaume huyo alivua zile sendo zake na kubaki peku, aliunyanyua mguu na kuushusha kwenye kifua cha kijana huyo. Kilivunjika vibaya mpaka eneo la kifua likabaki kuwa bapa.

Walibaki wawili yule mmoja hata hakupewa nafasi ya kujianza alikutana na kisu cha shingo ambacho kilipenya mpaka nyuma kwenye gari baada ya kutoboa shingo na kupitiliza kulingana na nguvu ambazo zilitumika kukirusha. Kilikita karibu na sehemu ambayo alikuwepo mke wa Gavin ambaye aliishia kupiga kelele kwa uoga. Mavambo alikuwa anaangaliana na mlinzi mmoja wa mama yake Gavin, vijana hao walikuwa ni hatari mno lakini kwa Mavambo walionekana kuwa watoto, hawakuwa saizi yake.

Kijana huyo alijifunga kitambaa cheusi kichwani akiwa amekiweka kisu kwenye mdomo wake, ni yeye pekee ambaye alibaki na alijua kabisa kwa mtu ambaye alikuwa mbele yake asingeweza kupambana naye hivyo njia pekee ilikuwa ni kumsubiri Othman afike hapo kuwapa msaada ndiye mtu ambaye alimpa taarifa kwamba walivamiwa na mama alikuwa hatarini pamoja na mke wa bosi. Lengo lake alihitaji kupoteza muda ili hata akifa, afe msaada ukiwa umefika tayari. Kitambaa ambacho alikuwa amejifunga ulikuwa ni utambulisho wao hivyo alikivaa kwa heshima ya mama huyo ambaye kwa miaka mingi yeye ndiye alikuwa anahakikisha anakuwa salama hivyo hata kama angekufa basi angehesabika kama shujaa aliyefia vitani. Hakuweza kutumia risasi kwa sababu alijua kosa hilo lilikuwa linaondoka na maisha ya wawili ambao alipaswa kuwalinda, alielewa kazi ya wadunguaji vizuri ndiyo maana hakujaribu kufanya kosa lolote lile zaidi ya kununua muda hapo uzidi kwenda.

Kijana huyo alisogea kwa mahesabu makali kumfuata Mavambo, alitimua vumbi wakati ananyanyuka pale alipokuwepo. Huyo uwezo wake ulikuwa ni tofauti na wengine kabisa, buti lake lilitua kwenye tumbo la Mavambo ambaye alirudi nyuma lakini wakati akiwa amezubaa kisu kilitua kwenye tumbo lake ila hakikuzama ndani, kilitoboa sehemu ndogo sana ya tumbo lake kiasi kwamba mpaka kijana huyo alipigwa na butwaa, hakuelewa mwanaume huyo alikuwa na uwezo upi kiasi kwamba kisu kisiwe na uwezo wa kupenya kirahisi anapo likaza tumbo lake.

Alitua chini akiwa amebeba pointi zake zote tatu, alikishika vyema kile kisu akiwa anahema, shughuli ilikuwa mbichi kabisa, alisogea kwa hesabu kali, alidunda na kugeuka kwa sarakasi, mguu wake haukufika kwenye mwili wa mtu huyo ila ni yeye ambaye alirudi alikotoka. Alijibamiza kwenye gari akiwa anatoa damu kwenye mdomo wake, hakupenda kujibamiza bali ni nguvu ya ngumi ambayo alipigwa ndiyo ilimrudisha kule alikokuwa ametoka, asingeweza kabisa kushindana nayo, iliuzidi uwezo wa mwili wake.

Alikirusha kisu chake kwa nguvu kwa Mavambo, alikidaka kwa vidole viwili tu kisha akakirudisha kwa kijana yule ambaye alikuwa anakimbilia alipo, kilizama vibaya kwenye kifua kiasi kwamba hata ile kasi yake ilipungua hivyo akafika tofauti na mahesabu yake yalivyokuwa. Alipewa mtama mzito akakosa kabisa balansi, alipigwa na goti la kifua akatapika damu huku akidondokea kwa wale wanaume ambao walikuja na mavambo eneo hilo nao walimrudisha tena hewani. Ilisikika tu sauti ya mwanamama Valaeria akisema;
“Noooooooooooo” ni wakati ambao aliona kijana huyo shingo yake inatenganishwa kikatili. Wakati anarudishwa Mavambo aliipitisha mikono yake kiunoni akatoa mabapa mawili na kwa sababu kijana huyo hakuwa na balansi vizuri vilizama kwenye pande zote za shingo yake kisha vikazungushwa na kukutanishwa katikati, shingo ilikuwa haifai. Vilichomolewa kwa nguvu na kusokomezwa kwenye mdomo wake. Habari yake iliishia hapo, walinzi wote wakawa wamepotea kwenye mkono wa bwana huyo ambaye alikuwa na nguvu na mafunzo ya ajabu kwenye mwili wake.
“Ni zamu yake sasa kuweza kulipa” aliongea Mavambo akiwataka vijana wake waweze kuwabeba wanawake hao ili waondoke.
“Sijui ni aina gani ya kifo ambacho atakuua” aliongea mwanamama yule akiwa anabebwa kwa nguvu.
“Nitasubiri nione” Mavambo aliongea kwa jeuri wakati huo alikuwa anaondoka hapo.
92 inafika mwisho.

FEBIANI BABUYA.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom