Simulizi ya Kijasusi: Hakuna aliye Salama

Simulizi ya Kijasusi: Hakuna aliye Salama

HAKUNA ALIYE SALAMA
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 12


Giza lilikuwa limetanda nje ya jumba hilo lililotengwa, ambapo damu ilikuwa bado haijakauka sakafuni. Kinu alimsitiri Mama Lutu kwa blanketi dogo alilolitoa chumbani, akaiweka picha ya Benedicto na Rosemary juu ya kifua chake kilichonyamaza kabisa. Kifo chake hakikuwa cha kisiasa tu, bali kilikuwa kifo cha kishujaa, kipande kingine cha ukombozi kilichoanguka kabla ya kuandikwa kikamilifu.

Lakini Kinu hakuwa na muda wa kuomboleza. Saa yake ya mkononi ililia kwa mdundo maalum, ishara ya hatari ya juu: DEKA wanalikuwa wanakaribia eneo hilo.

Alikusanya haraka karatasi zilizokuwa bado zimesalia mezani. Ile barua ya Benedicto, baadhi ya kurasa za DIRA KUU ambazo alikuwa amefanikisha kuzichukua. Hakuwa na picha tena, ile iliiacha na Mama Lutu. Lakini alikuwa na jina. Jina moja tu lililoanguka kutoka kinywani mwa Mama Lutu kabla hajakata roho:
“Max.”
Alilitafakari jina hilo akiwa njiani kutoroka. Max alikuwa nani? Jina hilo halikuwa kwenye faili lolote, halikuandikwa popote, lakini sauti ya Mama Lutu ililitamka kwa uzito wa siri kuu.

Kinu alitoka kwenye eneo hilo kwa kutumia mlango wa nyuma wa bunker ya maficho, akapanda gari dogo la hatchback ambalo waliliweka wiki mbili zilizopita kama sehemu ya mpango wa tahadhari. Hakuwasha taa, alitembea kimya kwenye barabara za vumbi za nje ya jiji, akielekea kwenye eneo jipya la maficho ambalo alikuwa amelibuni pamoja na Andrew kabla ya operesheni ya kuingia Ikulu.

Ndani ya saa moja, alikuwa amefika kwenye ghorofa moja lililo karibu na uwanja wa ndege usiotumika, eneo ambalo lilitumika miaka mingi iliyopita kama jengo la wachora ramani wa Jeshi. Sasa lilikuwa ni kama pagale tu.

Alipofika ndani, alikuta Andrew akiwa tayari ameshafika, akiwa amevaa jaketi nzito jeusi, macho yake yakiwa na weusi wa mtu ambaye hakulala kwa siku mbili. Moreen alikuwa amejeruhiwa kidogo begani, alikuwa akijipaka dawa ya antibayotiki, macho yake yakiwa makavu, hayakuwa na machozi, yalikuwa na maamuzi.

Kinu hakuongea. Alimtazama Andrew tu, kisha akasema, “Mama Lutu ameondoka. Aliniokoa. Wamejua nilikuwa na DIRA. Walijaribu kuichukua ikashindikana, wakachana baadhi ya karatasi, Nilibakiza baadhi ya kurasa. Na alinipa jina… Max.”

Andrew alijisogeza, macho yake yakivutwa ghafla na jina hilo. “Umesema nani?”
“Max,” Kinu alirudia. “Alitamka jina hilo kabla hajafa. Kama hitaji. Kama maagizo.”

Andrew alifunga mikono yake, akanyamaza kwa sekunde chache, kisha akasema kwa sauti ya chini, “Hilo jina… limenikumbusha mtu mmoja. Lakini si mtu wa kawaida.”

Moreen akamtazama, “Unamjua?”

Andrew akaanza kutembea pembeni mwa meza, akatoa kijifaili kutoka kwenye begi dogo la ngozi. Alikifungua taratibu.

“Miaka tisa iliyopita, tulikuwa na jasusi mmoja wa ndani ambaye aliitwa kwa jina la kiutendaji ‘Maxwell R.’ Alifanya kazi ndani ya DEKA kwa miaka mitatu, lakini baadaye alitoweka baada ya kujaribu kuwasilisha ushahidi wa rushwa kwa Idara ya Kimataifa ya Upelelezi ya Afrika Mashariki. Hakuwahi kurudi. Taarifa zake zilifutwa. Mtu pekee aliyewahi kuniambia kuhusu Max, alikuwa Benedicto. Na aliapa kuwa Max alikuwa amejua mambo yote kuhusu chanzo halisi cha DEKA, pamoja na namna mifumo ya nje, Ulaya na mashirika ya biashara, ilivyokuwa ikiendesha DEKA kama mradi wa kiuchumi.”

Kinu akapumua kwa nguvu. “Ina maana… Mama Lutu alimjua Max ni nani?”

Andrew akatikisa kichwa. “Alimficha. Labda hata kumtumia. Lakini Max alikuwa silaha ya dharura. Hadi leo sikuwahi kumwona. Picha yake haikuwahi kuwekwa mahali popote. Alikuwa kama kivuli tu.”


Moreen akasimama, akajifunga bandeji begani, kisha akasema, “Tunahitaji kumtafuta Max. Hicho ndicho Mama Lutu alitaka. Hiyo ndiyo zawadi ya mwisho aliyotuachia"

Andrew akawaza kwa dakika kadhaa. Kisha akasema, “Kuna mtu mmoja anayeweza kusaidia. Alikuwa mshirika wangu zamani. Alifungwa miaka mitano kwa kosa la kutengenezewa. Lakini aliachiwa kimya kimya mwaka jana. Huyo ni mtu pekee aliyewahi kuwasiliana na Max kwa njia ya barua pepe ya VPN ya ujasusi. Na sasa… huenda anatuhitaji sisi zaidi ya sisi tunavyomhitaji.”

Kisha akafungua laptop iliyokuwa imefungwa na kuingiza password ndefu. Alituma ujumbe mfupi kwa anwani iliyosimbwa: cosmasProtocolZero@cyphernet.bz

Saa moja baadaye, walikuwa wamejificha kwenye basement ya chumba cha kuhifadhi vinasa sauti vilivyoharibika. Mlango wa chuma ulifunguliwa taratibu, miguu ya buti nzito ikasikika kwenye ngazi.

Ndipo alipoingia, Cosmas
Alikuwa amebadilika. Sura yake ilikuwa imezeeka kwa miaka ya mateso, lakini macho yake bado yalikuwa na ule wepesi wa kijanja. Alikuwa na uso wa mtu aliyeshinda vifo vingi bila kuliona kaburi. Alikuwa amevaa koti la kijeshi la ngozi, na mikononi akiwa na flash mbili na begi dogo
Aliposimama mbele ya Kinu, Andrew na Moreen, hakusema “habari.” Badala yake, alitoa kijifurushi kidogo cha sigara, alafu akawasha moja, kisha akauliza:

"Nini nani kawaagiza kuniita kwa jina la nililokwisha kulisahau"

Andrew akajibu, “Tulipoteza mtu muhimu. Alituambia tukutafute. Na alitutaja jina moja. Max.”

Cosmas akakaa kimya kwa muda. Akavuta sigara yake kwa nguvu, kisha akasema kwa sauti ya mtu aliyekuwa amebeba siri kwa muda mrefu sana:

“Max… hajafa. Lakini kama mnamtafuta, basi mjue, mnaamsha moto ambao hata DEKA hawajui namna ya kuuzima.”

Kisha akachomoa flash kutoka kwenye koti lake, akaielekeza kwa Andrew.
“Hiki ni kipande cha mawasiliano ya mwisho kati yangu na Max. Nilitunza tu kwa siku ya mwisho. Labda hiyo siku ndiyo Leo"
******

Andrew alichukua flash ile kwa mikono miwili, kana kwamba alikuwa amekabidhiwa nyuklia. Akaikagua kwa macho kabla hajaiunganisha kwenye laptop iliyolindwa kwa encryption ya kiwango cha kijeshi. Moreen alijisogeza pembeni, macho yake yakielekea
pembeni ya dirisha dogo lililokuwa juu ya ukuta.

Kinu alikaa kimya, lakini ndani ya akili yake kulikuwa na milipuko ya maswali. Max ni nani hasa? Ni mtu wa upande wa DEKA aliyesaliti? Au ni silaha ya dharura iliyosahauliwa makusudi?

Andrew alipowasha flash, skrini ilionyesha faili moja tu:
MAX_COMM_FINAL.mp4

Aliibonyeza. Video ikaanza kuchezwa.
Ilianza na picha ya maji mengi kama ziwa au bahari hivi. Kamera ilikuwa imesimama juu ya mwamba wa kaskazini mwa Ziwa Tanganyika. Kulikuwa na upepo mkali, na nyuma yake, sauti ya mtu mmoja ilisikika, ikiwa wazi lakini yenye hila ya mtu aliyeficha mengi.
“Kama video hii imekufikia mikononi mwako, basi DEKA wapo ukingoni. Na mtu pekee ninayemwamini ataisoma ni Rosemary Lutulia… au mtu aliyechaguliwa naye.”

Kamera ikageuka kidogo, na sura ya mwanaume ikaonekana.
Alikuwa ni mweusi wa kawaida, lakini macho yake yalikuwa na ukali wa mtu aliyekutana na usiku zaidi ya mara elfu. Mdomo wake ulikuwa umezeeka kuliko uso wake. Alikuwa na kovu dogo kwenye taya la kushoto. Haiba yake ilitosha kueleza jinsi alivyotumia nusu ya maisha yake kufanya kazi gizani, usiku wengine wakiwa wamelala.

"Jina langu si muhimu. Lakini ninyi mmeniita Max. Nilikuwa ndani ya DEKA kabla ya jina hilo halijazaliwa. Niliona uovu ukianza kama cheche. Nilijaribu kuuzima. Wakanifuta kazi na kutaka kuniua, Lakini niliishi.”

“DIRA halisi haipo kwenye faili la karatasi. Ipo ndani ya akili zetu, tulioshuhudia, tulioishi, tuliosalitiwa. Na sasa ni muda wa kuitoa hadharani.”

Sauti ikakatika kwa sekunde chache, kisha picha ya mji wa zamani ikaanza kuoneshwa, barabara ya changarawe, minara ya redio ya kale, na sehemu ya ghorofa iliyobomoka.

“Nipo Kalambo. Sehemu ambayo haijulikani kwenye ramani za sasa za kidigitali. Nilijificha hapa kwa sababu huku hakuna kioo. Hakuna simu. Hakuna DEKA. Kuna watu wachache tu wanaoamini kuwa haki bado inaishi, itaishi milele.”

Kamera ikamwonesha akiwa ameketi kwenye meza ya mbao, mkono wake ukiwa umeweka flash nyingine. Kisha akasema:
“Kuna sehemu ya mwisho ya ushahidi. Faili za mawasiliano ya DEKA na taasisi za kifedha, picha za utesaji, video za mikataba ya siri. Zipo kwenye flash hii. Na flash hii… haifunguki bila retina yangu. Au retina ya mtu mmoja tu: mtoto wa damu ya Benedicto.”

Kinu alishtuka. Alimtazama Andrew. Andrew alitazama chini, akavuta pumzi ndefu. Moreen aliketi taratibu.
“Max alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Benedicto,” Andrew alitoa, sauti yake ikiwa nyembamba. “Lakini sikuwahi kujua kuhusu mtoto…”

Kinu akamkatisha. “Hivi inawezekana? Benedicto alikuwa na mtoto aliyeishi kwa siri? Na Mama Lutu?”
Moreen akasema kwa haraka, “Aliwahi kunitajia mtu… aitwaye Dalia. Msichana aliyewahi kulelewa kwenye taasisi ya kidini, akapelekwa Kenya baada ya vurugu ya kisiasa. Lakini alikataa kusema ni mtoto wa nani. Labda... ni yeye.”

Andrew alitikisa kichwa. “Inawezekana. Huu ndio mwisho wa kitendawili. Tukiweza kumpata Dalia, tunaweza kufungua flash ya Max. Na hiyo flash... ndiyo pigo la mwisho. La ushindi.”

Balongo, maarufu kama Cosmas, alikuwa kimya muda wote huo. Kisha alitazama saa yake ya mkononi, akasema:

“Nina mawasiliano na watu wa ndani wanaoweza kusaidia kumtafuta huyo msichana. Lakini tunahitaji kwenda Kalambo. Haraka. Maana baada ya ujumbe huu kufunguliwa, Max atakuwa anasubiri. Na kama DEKA wamevujisha habari hizi, basi hata Max hayuko salama tena.”
“Ni lazima tuende usiku huu,” Kinu alisema. “Tutagawanyika. Mmoja aende Kalambo. Wengine watumie mtandao wa mtaani kumtafuta huyu Dalia.”

Balongo akainuka. “Mimi na Andrew tutaenda Kalambo. Wewe Kinu na Moreen mtafuteni Dalia. Tumieni taarifa yoyote ambayo Mama Lutu au Benedicto waliwahi kuiacha nyuma. Huyu mtoto anaweza kuwa mlango pekee wa kuwasha shambulio la mwisho.”

Moreen akanyanyuka. “Tutaanzia kwenye makanisa ya zamani ya Masista eneo la Bukoba na maeneo ya Nakuru, Kenya. Nitawasiliana na rafiki yangu mmoja wa zamani aliyewahi kufanya kazi za kijamii huko.”

Andrew akaweka flash ya Max kwenye kifaa cha siri. “Hii IPO mkononi mwangu sasa. Tukiipoteza… tumepoteza kila kitu.”

Walitazamana kwa ukimya. Watu wanne, kila mmoja akiwa na jeraha lake, lakini wote wakibeba mzigo wa taifa.
Kinu alisogea karibu na dirisha dogo, akatazama usiku.
“Kwa mara ya kwanza, tumeona nuru. Tumekuwa na ramani. Na sasa, tunahitaji mshale wa mwisho. Tutamtafuta Max. Tutampata Dalia. Na DEKA… mwisho wao utakuwa umefika”

Balongo akachomoa bastola yake, akasema kwa tabasamu la kijanja:
“Wamezoea vita vya risasi. Sasa tuwape wanachotaka"

---
Itaendelea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom