Hakuna Aliye Salama
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 07
Usiku uliofuata, Kinu na Moreen walikuwa wamejificha ndani ya nyumba ndogo ya mbao pembezoni mwa milima ya Bagamoyo. Walikuwa wakimsubiri mtu kwa jina la Jaji, aliyewahi kuwa mmoja wa waratibu wa DEKA miaka kumi nyuma, kabla hajajitoa kwa siri.
Mtu huyo alifika saa mbili usiku, akiwa amevaa koti la kuukuu na suruali ya kitambaa. Alikuwa na ndevu ndefu, nywele nyeupe zilizojificha ndani ya kofia.
“Naelewa nini mnachopitia,” alitamka kwa sauti nzito ya kizamani. “Niliwahi kuwa ndani ya jumba hilo. Niliona uovu ukizaliwa na kulelewa kama mtoto wa kifalme.”
Kinu alimsikiliza kwa makini.
“Nawapa jina moja,” Jaji aliongeza. “Jina la mtu aliye ndani ya DEKA, lakini moyo wake haupo nao. Amefungwa kwa hofu ya familia yake kuuawa. Anaitwa Profesa Daudi Luhanga. Alikuwa mtaalamu wa mawasiliano ya serikali. Sasa anafanya kazi kwa kulazimishwa. Anaweza kuwasaidia… lakini mkimpa tumaini na uhakika wa kushinda. Nilisikia habari za wale watu mliowafuata Tabora na Singida walivyouawa. Hii inanambia hata Mimi nipo mbioni'
Wakati huohuo, kwenye jumba la kifahari lililojaa mapazia ya damu za wazalendo, kikao cha siri kilikuwa kinaendelea.
Wahusika sita walikuwa wameketi kwenye meza ya mbao nyeusi. Wawili kati yao walikuwa wazee, mmoja akiwa na miwani yenye kioo cha rangi ya samawati na mwenzake akiwa na fimbo ya ndimu. Watatu walikuwa watu wazima waliovaa suti nyeusi. Na mmoja kijana, mwenye simu tatu na macho ya tahadhari.
Kiongozi wa DEKA, akiwa ameketi katikati, alisoma karatasi ndefu na kusema:
“Kinu na Moreen wamevuka mipaka. Wanapaswa kufunguliwa mashtaka. Kesi ya uhaini, uharamia wa mtandao, uchochezi wa kitaifa, na uhalifu wa kiusalama.”
Akainua mkono, akasema:
“Amri hii ipelekwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa Mwanasheria Mkuu, na kwa IGP. Hakuna kuchelewa. Wafunguliwe mashtaka mara moja.”
Na kweli…
Kesho yake, taarifa ilitoka kwa njia ya televisheni, redio na mitandao ya kijamii:
“Watu wawili wanaotuhumiwa kwa kupanga uasi dhidi ya taifa, uchochezi na uhalifu wa mtandao wamefunguliwa mashtaka. Wanajulikana kwa majina ya Kinu na Moreen. Serikali imeunda timu maalumu ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.”
Moreen alikuwa akichota maji kisimani wakati aliposikia sauti ya redio hiyo. Alidondosha ndoo. Kinu alipokea ujumbe wa WhatsApp uliojaa viunga vya video zao wakitoa ushahidi. Sura zao zilitapakaa kila kona.
“Tumebambikiwa,” Kinu alisema, sauti yake ikiwa ya maumivu na hasira.
Usiku huohuo, polisi walivamia nyumba yao. Walifanikiwa kukimbia. Waliishi vichakani, kwenye miji ya watu masikini, wakibadilisha mavazi na mitindo Yao ya Maisha ya kila siku. Lakini DEKA na Polisi haikuacha kuwatafuta.
Kwa muda huo, harakati zilitulia. Watu waliokuwa wakisambaza ujumbe wa haki walinyamaza. Watumiaji wa mitandao walijificha Kwa kuogopa. Hofu ilimvaa Kila mtu.
Lakini Morris, jasusi wa zamani na Marcus, mwanaharakati kutoka Geneva, waliungana kwa simu ya siri na kumuandikia barua ya kuaminika Kiongozi wa Mabadiliko, aliyekuwa mafichoni Dodoma.
Barua yao ilikuwa na ujumbe mmoja:
“Siku ya Wanawake Duniani, tunaomba ruhusa ya maandamano ya kutetea Haki. Tutavaa vazi jeusi kama kiashiria Cha maombolezo Kwa waliokuwa, kupotezwa na kwaajili ya Kinu na Moreen. Hatutasema neno. Lakini miguu yetu itasema yote.”
Na kweli, tarehe hiyo ilipofika, maelfu ya wanawake walijitokeza barabarani wakiwa wamevaa nguo nyeusi na kubeba mabango ya upendo, amani, na uhuru. Hakuna aliyesema neno. Walitembea.
Lakini Polisi walikuja na mabomu ya machozi. Walikamata baadhi yao. Waliwatia watu hofu. Lakini picha za maandamano hayo zilisambaa ulimwenguni. Vyombo vya kimataifa viliripoti:
“Nchi inayoogopa wanawake wasiozungumza, ni nchi iliyokufa moyo.”
Maisha ya Mahabusu
Kinu alikamatwa kwenye stendi ya basi la mikoani alipokuwa akijaribu kutoroka kwenda Iringa. Alifungwa pingu kama jambazi hatari akiwa chini ya Ulinzi Mkali. Alipigwa. Akaingizwa ndani ya gari la polisi. Moreen alikamatwa baadaye, akiwa kwenye nyumba ya mwanamke mmoja aliyekuwa akimhifadhi.
Walipelekwa jela ya Keko. Vyumba vyao vilikuwa vya giza, na sakafu ya saruji iliyokuwa baridi kama moyo wa amphibia.
Kinu alipangiwa kazi ya kusafisha choo cha gereza. Moreen alipewa kazi ya kufua nguo za askari.
Kila walipopewa karatasi hata kama ni kipande cha gazeti waliandika ndani yake ujumbe:
“Usikubali kupotea. Ukipotea, dunia haina tumaini. Yashikilie Maisha Kwa nguvu zote. Tumaini la Taifa ni letu"
Walijua gereza halikuwa mwisho wa mapambano Yao. Isipokuwa ni hatua Moja inayosubiriwa na hatua nyingi zinazofuata.
*******
Mahabusu kulijaa mbu na kiza kilichojaa mipango mibaya kama mawingu ya radi yanavyolikaribia jangwa. Ndani ya gereza hilo lenye kuta nene za huzuni, mwanga wa bulb moja dhaifu uligawanya giza kwenye seli ya Kinu, ukilenga moja kwa moja kwenye uso wake uliokonda kwa mawazo.
Kinu alikuwa amelala kifudi fudi juu ya godoro lililofifia, lakini usingizi ulikuwa mgeni mwenye adabu mbaya ulikuja na kuondoka kabla hajamkaribisha.
Mlango wa chuma ulilia kama mtu anayeomboleza. Walinzi wawili waliingia. Mmoja alichukua ndoo, mwingine alimtazama kwa jicho la nyoka mwenye sumu.
“Kuna amri, umetumwa kusafisha korido ya ghorofa ya chini,” mmoja alisema.
Kinu hakusema neno. Alijua. Mara moja alijua. Ghorofa ya chini? Usiku wa saa saba? Hakuna choo kule, wala wafungwa.
Alivaa viatu vyake vya plastiki na kuchukua ndoo na beseni. Alitembea kimya kama kivuli na kibwengo. Wakampeleka kwenye korido ya mwisho, yenye taa iliyokuwa inatikisa kama mshumaa kwenye upepo wa ufukweni.
Alipofika, mlango wa nyuma ulifungwa kwa kishindo. Kabla hajageuka, kivuli kilimtokea nyuma. Mwanaume mrefu, mwenye sura iliyofichwa na barakoa nyeusi alimsogelea taratibu, akachomoa kitu kilichometameta kwenye mwanga hafifu.
“Kifo chako kimepitishwa,” sauti ya kiume ilisema kwa ukatili wa msumeno.
Lakini Kinu hakuwa mtoto wa jana. Aliruka ghafla, akamgonga adui kwa beseni kichwani. Kelele ya chuma na maumivu ilijaza korido hiyo. Wakati mwingine, uhai huja kwa sekunde chache za ujasiri usiopimika.
Kinu alikimbia akapita kwenye njia nyembamba, akateleza kwenye mapovu ya sabuni ya chooni, akaanguka. Lakini kabla hajainuka, Mwanaume mwingine alikuwa tayari nyuma yake.
Walimzingira. Wanne. Mikono yao ilikuwa na nyundo, kamba, na baruti ndogo ya umeme wa ganzi.
Walimshika, wakamvuta kwenye chumba kidogo, chumba kisichotumiwa, kilichojaa fangasi ukutani na harufu ya uozo. Wakamfunga kamba mikononi, wakampiga mfululizo tumboni, mgongoni, na kichwani.
Lakini wakati mmoja alipoinama kumpiga tena, Kinu alitumia kichwa chake kumpiga pua Mwanaume aliyembele yake. Damu ikamwagika. Alijirusha kwa nguvu, akakata kamba upande mmoja, akampiga mwingine teke la mbavu. Sasa ilikuwa vita ya kujitetea.
Ulikuwa ni vita ya mtu anayepigania haki, hata akiwa kifungoni. Walipopata nafasi ya kumpiga na bastola ya ganzi mlio wa filimbi ukasikika kutoka nje. Mlango wa nje ukafunguliwa kwa nguvu.
“kuna Nini hapa!” sauti ya askari wa kawaida ilisikika.
Watu waliokuwa wamemzunguka Kinu walitawanyika kama panya waliomwagiwa maji ya moto. Askari waliingia, wakamkuta Kinu akiwa amejaa damu usoni, jicho moja likiwa limevimba.
Hakusema kitu. Hakuwalaumu. Hakulia. Aliinua kichwa chake, akatazama juu kama mtu aliyemaliza maombi ya mwisho.
“Wataniua,” alisema kimoyomoyo. “Lakini si kabla sijasema ukweli.”
Usiku huo, upande wa wanawake
Moreen alipata ujumbe wa karatasi ulioingizwa kupitia chini ya mlango. Ulikuwa umeandikwa kwa kalamu ya wino mweusi:
“Kinu amejaribiwa kuuawa. Anaishi, baada ya kukabiliana vilivyo. Hiyo haimaanishi hawatarudi. Watajariby wawezavyo. DEKA imeingia gerezani. Hata ukuta hauna masikio tena sasa una macho.”
Aliweka karatasi hiyo kwenye shimo dogo alilolifukia kwa kijiti nyuma ya ndoo ya maji. Alilia kimya, machozi yakimulika historia ya upendo, ujasiri, na mateso. Alikumbuka tangu siku ya kwanza alipokutana na Kinu. Kutoka kuwa Mwanamke mpaka Make-up mpaka kuwa mwanaharakati mwenye kuahughulikia mambo ya hatari na magumu.
Alijua. Walikuwa wanawamaliza mmoja baada ya mwingine. Lakini pia alijua mtu hufa mara moja tu. Lakini sauti ya haki haiwezi kuzikwa na udongo wa gereza.
*****"""
Morris alikuwa ameketi ndani ya chumba kidogo cha kioo jijini Geneva, Uswisi, mbele ya kamati ya kimataifa ya haki za binadamu. Alikuwa amevaa suti ya buluu, tai isiyo na alama, lakini macho yake yalikuwa na uzito wa kilio cha mataifa yenye ukandamizaji wa haki za binadamu.
“Mimi ndiye shahidi wa kwanza wa mateso haya. Wako gerezani si kwa uhalifu, bali kwa kusema ukweli,” alisema kwa Kiswahili kizito kilichotafsiriwa papo hapo kupitia headphones za wajumbe kumi na wawili waliomkodolea macho.
Marcus alikuwa nyuma yake, akigawa nakala za picha, nyaraka, na rekodi za sauti za mateso na ukiukwaji wa haki. Ilikuwa ni mwanzo wa presha kubwa ya kidiplomasia, ripoti zilianza kusambazwa, barua zikaandikwa kwa wakuu wa mashirika ya haki duniani, na redio za kimataifa zikaanza kuuliza maswali kuhusu hatma ya Kinu na haki za waliopotezwa na kuuawa.
Lakini wakati dunia inaanza kusikia kilio cha gerezani, ndani ya kuta za gereza la wanawake, kisasi kilikuwa kinachanua kama sumu kwenye mti wa miiba.
Moreen alipata chai ya jioni, kama kawaida. Lakini ladha ya siku hiyo ilikuwa tofauti ilikuwa na utamu wa bandia na harufu ya unga wa viwandani. Dakika thelathini baadaye, alianza kutapika, macho yakawa mekundu, na ngozi yake ikaanza kutoa jasho la baridi.
Wafungwa wenzake walipiga kelele akapelekwa hospitali ya gereza kwa haraka. Daktari mmoja alipokuwa akimpa huduma ya dharura, alimnong’oneza,
“Hii ilikuwa sumu ya polepole, lakini unabahati kwani una allergy na kahawa. Wala usingejua umewekea Sumu. Ungekufa polepole ndani ya siku hizi thelasini.”
Wakati huo, katika kona ya giza ya jiji la Dar es Salaam, Mama Lutu alikuwa kwenye gari la abiria, akivua mavazi ya kawaida na kuvaa vazi la kininja. Alikuwa anatoroka,, tena baada ya mapambano ya hatari na Andrew Kamage kwenye ranchi ya ng’ombe.
Siku moja nyuma, Andrew alikuwa amemuita Mama Lutu ofisini mwake baada ya kugundua nyendo zake kupitia mfumo mpya wa ufuatiliaji alioujenga kwa siri. Walipokutana, kulikuwa na mazungumzo mafupi ya kistaarabu, kisha Andrew akafunga mlango kwa rimoti.
“Umechagua upande wa giza, upande wa udhalimu,” Andrew alisema.
“Na wewe umebaki kwenye ndoto za mabadiliko yasiyoishi, ndoto za alinacha ambazo haziwezi kutokea" Mama Lutu akajibu.
Kisha mapambano yakaanza, meza ziligonga ukuta, vioo vilipasuka, risasi zikaelekezwa kwenye dari. Mama Lutu alikuwa na kisu kidogo cha mfukoni; Andrew alikuwa na bastola ya risasi za ganzi.
Kwa zaidi ya dakika thelathini, walizunguka kila kona ya ranchi hiyo, wakipigana kama Simba wawili waliowekewa uzio mmoja. Hatimaye, Mama Lutu alifanikiwa kumchoma Andrew kisu begani na kukimbilia msituni kupitia sehemu ya nyuma ya shamba, lakini bila kujua Andrew alikuwa amepata mkoba wake wa siri uliokuwa na documents nyeti, majina ya mawasiliano ya DEKA, ratiba zao na ramani ya mikutano ya ndani ya mfumo.
Andrew, akiwa na jeraha, alishika mkoba huo kwa mikono yenye damu na kusema taratibu,
“Umenitoroka lakini umeniachia ushahidi WA Siri"
Usiku huo, Andrew alituma baadhi ya nyaraka kwa Marcus na Morris kwa njia salama ya kimtandao. Ulimwengu ukawa na ushahidi wa kwanza wa kielektroniki wa uwepo wa DEKA.
Moreen, akiwa katika kitanda cha chumba cha uangalizi maalum, alipokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa Marcus:
“Hujafa. Na sasa dunia inajua. Anza kupona. Vita inaanza.”
Kinu naye, gerezani, alipokea barua ya mkono, yenye maneno machache sana lakini yaliyokuwa na uzito kama ardhi:
“Tunakutoa nje. Uhai wako ni ujumbe wa dunia.”
*******
Mlango wa gereza kuu la Keko ulisikika ukilia kwa sauti ya ajabu majira ya usiku, sio mlio wa funguo, mashine maalumu ndizo zilizokuwa zinatumika. Kamera za uangalizi zilikuwa zimesimama zilikuwa zimedhibitiwa na kifaa kidogo cha kielektroniki kilichokuwa kimetundikwa kwenye dari la maktaba ya gereza.
Ndani ya seli, Kinu alikuwa amejilaza kama mfu aliyeishiwa matumaini. Lakini ndani yake kulikuwa na msisimko wa vita, vita ya mabadiliko. Alijua: usiku huo haukuwa wa kawaida.
Mlango wa chuma ulifunguliwa kwa sauti ya kuunguruma kama ya simba aliyejeruhiwa. Mtu aliyevaa sare ya mlinzi wa gereza, lakini mwenye mwendo wa jasusi, aliingia. Alitoa ishara, ishara ya wanajeshi wa zamani waliokuwa katika kikosi cha vipuli vya vifaru.
“Twende,” aliongea kwa sauti ya chini, macho yakiwa hayatembei kwenye uso wa Kinu, bali kwenye kuta na kona za chumba.
Safari ya kutoka ikaanza kupitia njia za chini ya ardhi katika mtaro wa maji taka uliosahaulika kwenye ramani ya matumizi. Harufu ya kutapika na mchanganyiko wa kinyesi na historia ya unyanyasaji ya wafungwa wa kisiasa, ilijaza mapafu yao.
Baada ya dakika thelathini, walifika kwenye mlango mdogo wa chuma uliokuwa umefichwa chini ya paa la karakana ya magari ya magereza. Mlango ulifunguliwa kwa alama ya kidole.
Gari aina ya Land Cruiser lilikuwa likisubiri nje. Kinu aliingizwa ndani, kofia ya sura bandia akavalishwa. Gari lilitokomea gizani.
********
Asubuhi ilipochomoza, taarifa zilianza kutiririka kama mto wa habari uliotokana na mvua zilizonyesha usiku mzima.
“Mfungwa wa kisiasa atoroka Gereza la Keko kwa njia isiyojulikana.”
“Wizara ya Mambo ya Ndani yatoa tamko la kuunda tume ya uchunguzi.”
Lakini kilichoanza kama uchunguzi wa kawaida kiligeuka kuwa karaha ya ndani ya mfumo wa usalama. Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Benedicto Mlauzi, alipokea ripoti ya siri iliyokuwa na jina moja lisilosomeka kwa watu wa kawaida, DEKA-6.
“Ni nini hiki?” aliuliza.
Afisa wa kitengo cha uchunguzi alitoa faili lenye majina, ramani, na mawasiliano ya kikundi cha ndani kilichojipenyeza kwenye taasisi za dola.
Benedicto alijua DEKA haikuwa hadithi ya mtaani. Ilikuwa kichaka kilichojengewa kasri ndani ya moyo wa taifa... Ndani ya mihimili inayoshililia nchi.
Lakini hakukubaliana na uozo huo. Akaitisha kikao cha siri. Wajumbe wanne waliingia. Wengine wawili walikuja kwa kuchelewa. Waliketi kimya, kila mmoja akiwa na ajenda tofauti mioyoni mwao.
“Nina uhakika kuna watu humu wanafanya kazi na DEKA,” Benedicto alisema. “Lakini hiyo haijalishi. Tumeanza vita sio kwa mabomu, bali ya ukweli. Kupambana kulinda Taifa, wote tunakumbuka tuliapa. Sasa kama sisi walinzi wa taifa hili ndio tumegeuka Mbwa mwitu wa kulirarua Taifa hili. Unafikiri Nini hatma ya kizazi chetu"
Wengine walinyamaza. Mmoja alitabasamu, akajifuta jasho. Mwingine alitoa simu na kuandika kitu kwa haraka.
********
Katika kona ya Chuo cha Sayansi ya Habari, Profesa Daudi Luhanga alikuwa amekuwa kivuli chake. Mwanaume aliyejulikana kwa nadharia za uhuru wa mawasiliano, sasa alikuwa chini ya uangalizi wa DEKA, akilazimishwa kutumia akili yake kulinda uongo, Ufisadi, dhulma na mauaji kinyume na sheria na haki za binadamu.
Lakini alipopewa ujumbe wa mkono kutoka kwa Benedicto, moyo wake ulianza kuamka.
“Tunajua bado una nafsi,” uliandika ujumbe huo. “Tuonyeshe mlango wa ndani.”
Profesa Luhanga alijibu kwa kipande cha ramani na nukuu ya maneno:
“Mamlaka inayojificha ni mamlaka ya giza. Nuru huwa haina makazi ya kudumu, lakini huja kila inapohitajika.”
Usiku huo, kikao kilifanyika ndani ya nyumba ya kale yenye paa la bati lenye kutu na ukuta wa chokaa. Kinu, akiwa na kovu jipya usoni, Moreen aliyeponea kifo, Marcus, Morris, na Benedicto walikaa pamoja.
Profesa Luhanga alisimama.
“Acheni niwaonyeshe mtandao uliopo ndani ya mifupa ya taifa. Wako serikalini. Wako mahakamani. Wako ndani ya chombo cha habari. Na wako pia… hapa.”
Kimya kilitanda. Kila mtu alimkodolea macho, akiwa na swali moja kichwani:
"Je, tutavunjaje mfumo unaojua jinsi ya kuishi hata ndani ya damu yetu wenyewe? Mfumo unaotutazama na kutufuata kama kivuli Kila tuendako?"
*******
Hakuna kilicho bora duniani kama muungano wa watu wanaotoka pande tofauti, lakini wakakutana kwenye lengo moja. lengo la ukombozi. Hicho ndicho kilichotokea kati ya Benedicto Mlauzi, Kinu, na Moreen. Kila mmoja alikuwa na majeraha yake, historia yake, na maumivu yake, lakini wote walikuwa na ndoto moja: kuvunja minyororo ya DEKA, kulikomboa taifa liwe mikononi mwa wananchi wote. Na sio kikundi Cha watu wachache wanaotumia siasa na Dola kujinufaisha wenyewe huku wakiacha mamilioni ya wananchi wakiumia na kutesaka katika Lindi la umaskini.
Mpango wa kuwatoa Kinu na Moreen kutoka mikononi mwa DEKA ulianza kimyakimya baada ya Benedicto kupata taarifa ya ndani kutoka kwa Afisa mmoja wa gereza aliyekuwa amekuwa na mashaka kwa muda kuhusu mizengwe ya ndani ya mfumo. Afisa huyo, kwa jina la Aaron, alikuwa na kumbukumbu za mateso aliyoyaona gerezani, lakini alikuwa akinyamaza kwa kuhofia maisha yake.
Lakini ilipofika siku ya jaribio la kumuua Kinu, Aaron alituma ujumbe wa siri kwa Benedicto kupitia laini ya kielektroniki ya ndani ya usalama:
“Huyu mtu ni zaidi ya mfungwa. Ana ujumbe mkubwa. Tafuta njia ya kumtoa.”
Benedicto aliunda kikosi kidogo kisicho rasmi, akitumia vijana wa kitengo cha usalama wa data, walinzi waaminifu wachache na mtaalamu wa kielektroniki, kijana mwenye ujuzi mkubwa anayeitwa Titus. Kupitia njia ya chini ya ardhi, walimtoa Kinu na baadaye Moreen, na kuwapeleka kwenye eneo la siri la kupumzika, lililojengwa chini ya jengo la zamani la ukaguzi wa barabara lililoachwa miaka mingi nyuma, maeneo ya Upanga Magharibi.
Walikutana usiku mmoja wa jumatano, kwenye chumba kilichojaa ramani, vishikwambi, na taarifa nyingi za siri. Benedicto alitembea polepole, macho yake yakikazia kila picha ya uso wa DEKA iliyowekwa ukutani.
“Hamko peke yenu tena,” alisema kwa sauti iliyojaa ukomavu wa vita ya kiakili. “Tumeanzisha vita ya ndani ya mfumo. Na ninyi mko mstari wa mbele.”
Moreen aliketi kando ya Kinu. Alikuwa bado anapona taratibu baada ya sumu aliyopewa gerezani. Kinu alimtazama Benedicto, macho yake yakiwa na mchanganyiko wa shaka na matumaini.
“Je, tunaweza kuwaamini? Mfumo huu umewatupa wengi wetu,” Kinu alisema.
“Ndio maana nataka tufumue mfumo huo kutoka ndani,” Benedicto alijibu. “Na tunaanza na mtu ambaye anawajua wote.”
Mama Lutu
Wakati huo, Mama Lutu alikuwa amejificha katika nyumba ya kulala wageni eneo la Kunduchi, akitumia jina la bandia: Mariam Saidi. Hakujua kama taarifa zake tayari ziko mikononi mwa Andrew Kamage, wala hakujua kuwa kamera moja ya ndani ya hoteli ilimnasa akiwasiliana na mtu asiyejulikana usiku wa manane.
Aliendelea kutuma ujumbe kwa DEKA, akijifanya bado yuko ndani ya mpango wa Benedicto. Lakini moyo wake haukuwa na amani. Alihisi kama anayesogelea mdomo wa simba akiwa na ngozi ya nyati.
“Ulinzi wa ndani umevurugika,” aliandika kwa simu ya kisiri. “Lakini naendelea na kazi.”
Moreen alikuwa tayari amepata dondoo kutoka kwa Titus, mtaalamu wa data, kuwa simu moja inayohusishwa na Mama Lutu ilikuwa ikituma ishara kwenye mlingano mmoja na minara inayotumika na DEKA.
Kinu akasema, “Tunamjua. Ila tusimwambie. Tusiwanyime maadui nafasi ya kuamini wameshinda. Kufanya haraka sana kunaweza kusababisha makosa ya kimedani. Pia inaweza wapa DEKA nafasi ya kuwa na hofu jambo ambalo litawafanya watumie nguvu zaidi. Hii inaweza kuvuruga na kuumiza wasiohusika walionje ya mpango"
Profesa Luhanga alifika kwenye kikao kilichofanyika siku hiyo usiku. Alikuwa amevaa shati la mikono mirefu, suruali ya kaki, na sura ya uchovu ilionekana dhahiri. Aliweka kwenye meza ramani mpya ya mtandao wa DEKA, alama za mawasiliano, na namba za akaunti zinazotumiwa kufadhili mashambulizi ya kisiasa na mauaji ya siri.
“Kama tukiwa wakweli, tupo kwenye bomu la taifa ambalo linaweza kulipuka na kuangamiza nchi yetu. Tunapaswa tuwe waangalifu,” alisema. “Wengi walioko kwenye mfumo ni watu wakiwa wenye nguvu, lakini hawawezi kuzuia tunachokifanya. Kazi yetu ni kuwazindua.”
Benedicto akainuka. “Tutahitaji zaidi ya ushahidi, tunahitaji ushawishi, tunahitaji ushiriki wa wananchi. Propaganda za mitandaoni, vibonzo, memes ziendelee,” alisema. “Na hilo tutalipata kupitia nguvu ya watu. Tuanze sasa.”…
*******.
Mipango ya Siri hufanyika katika giza Nene. Usiku wa Manane. Mipango ya mafanikio hupangwa Kwa Siri. Gizani, usiku wakati watu wa kawaida wakiwa wamelala.
Ndivyo ilivyo Kwa kazi za kijasusi. Yadaiwa usiku hasa katikati ya usiku na asubuhi ndio muda ambao ufunuo wa roho hushuka katika ulimwengu wa watu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa.
Usiku ulijificha kwenye vichochoro vya jiji kama mtu aliyejeruhiwa anayejificha asipate kudhihirika. Dar es Salaam ilikuwa imevaa vazi la hofu, anga lake limetandikwa na wingu la kiza Cha tahadhari. Hakuna aliyekuwa salama, wala hakuna aliyethubutu kunyanyua mdomo. Wakati haukuwa umefika lakini haukuwa mbali.
Ndani ya pango la chuma lililojengwa chini ya ardhi, lililojificha chini ya kiwanda cha reli ya zamani ya Tanganyika, walikuwepo watu wachache waliokaa kimya. Miale ya chemli moja ya betri ilichora taswira za nyuso zao ukutani kama sanamu za mashujaa waliolala. Mashujaa wa kweli waliopigania uhuru. Uhuru ambao sasa ulikuwa umeporwa.
Benedicto Mlauzi alisimama mbele ya ramani kubwa ya taifa, iliyokuwa mbele kwenye ukuta, kwenye skrini ya kioo, akitazama kwa makini kama mchora ramani na mtaalamu wa GIS. Mikono yake miwili iliambatana na vishikwambi vitatu, kila kimoja kikionesha picha tofauti: maandiko ya upinzani, video ya askari akimnyanyasa kijana wa mtaani, na ramani ya njia za chini za mji.
“Wameifunga nchi kwa minyororo ya hofu, hawataki watu waseme maovu yao. Na Kila atakayesema humwinukia na kumuangamiza” alisema kwa sauti ya kuumauma midomo “lakini sisi tutatumia haki na kweli. Watatufunga miguu lakini si ndimi zetu. Wataua miwili yetu lakini sio dhamira na nia zetu"
Mioyo ya vijana wale ilijaa mshindo wa mapambano Maneno ya Benedicto yaliamaha hisia na shauku ya ukombozi. Kinu alikuwa ameketi upande wa kushoto wa chumba, macho yake makini, uso wake ukiwa umejaa makovu, makovu ya mateso gerezani, makovu ya usaliti, na Moreen alikuwa kando yake, sura yake ikiwa imetulia, lakini ndani ya nafsi yake kulikuwa na radi isiyosikika.
Benedicto aliinua kidole na kugusa picha ya msanii maarufu, Jay Razz, msanii wa muziki wa mitaani mwenye sauti ya utetezi wa watu wanyonge.
“Tutaanza na sauti. Tutamwomba aimbe nyimbo ya waliopotezwa. Tutampa majina na picha zao. Atazungumza kwa lugha ya mtaa, lugha ya watu wa kawaida.”
Halafu akawageukia Kinu na Moreen. “Mitandao ya kijamii ni jukwaa letu. Tumieni influencers. Wapewe hadithi za kweli. Wapewe takwimu. Wapewe nyuso za watu waliopotea. Na mjue, kila mfuasi mmoja ni risasi yetu ambayo itatufaa katika vita hii”
Moreen alikumbuka wimbo wa Jay Razz uliokuwa ukisambaa kama moto wa volcano, Sauti ya Mtaa. Ulikuwa na maneno kama sumu inayopenya mishipa ya ubongo
“Kama sauti yetu ni kosa, basi nchi hii imekosea… Kama kukosoa ni uhaini, basi uhuru huu ni mtego...”
Kwa mbali, kelele za mitaani zilianza kusikika, si za magari wala honi, bali za nyimbo na mikono ya waandamanaji waliovaa fulana nyeupe zenye maandishi makubwa: “Nimechoka Kuishi Kwa Hofu”.
Benedicto hakuishia hapo. Alitamka neno moja lililowafanya waliokuwepo wote kutikisa vichwa: “Tutawateka.”
“Tutamchukua kiongozi wa chama cha madereva. Tutamchukua yeye na familia yake. Tutamtuma ujumbe, si wa bastola, bali wa uhai. Tukishamtisha hatakuwa na chaguo. Ataitisha mgomo na wakati huohuo, chama cha upinzani kitapaza sauti mitaani.
Huu ndio ulikuwa mpango. Wakuitisha vuguvugu la maandamano na mgomo mkubwa wa kudai haki lakini zaidi kuipa serikali na kundi la DEKA wakati mgumu kuwafuatilia Kinu, Moreen, Andrew na Benedicto.
Siku ya Mgomo,
Siku hiyo ilifika kwa upesi. Saa moja asubuhi, magari ya abiria, mabasi, daladala, na boda boda vilisimama katikati ya jiji kana kwamba vilikuwa sanamu za Shaba
Kufumba na kufumbua, mabango yalijitokeza. Watu walivaa kofia nyeupe, wengine walivaa nguo za matambara zenye picha za waliopotea. Waliimba:
“Tutembee na sauti zetu, tupaze sauti zetu kudai haki zetu. Haki za ndugu zetu. ” “Mama yangu alilia, si kwa kuwa mimi muhalifu, bali kwa kuwa nilisema ukweli.”
Katika vurugu hizo, Serikali ilimkamata Ludovick Mchopa, kiongozi wa madereva. Lakini mgomo haukusimama. Kwa sababu tishio halikuwa tena kwa kiongozi, bali kwa moyo wa familia.
Viongozi wa madereva familia zao zilikuwa zimetishiwa kudhuriwa na kundi la Benedicto.
Abiria na wananchi walianza kulalamika na uvumilivu ulipoteza nafasi katika mioyo Yao.
Siku hiyohiyo, tangazo lilitolewa kutoka Ikulu: Benedicto Mlauzi atenguliwa na kuhamishiwa kama balozi nchini Guinea Bissau.
Lakini alikuwa tayari ameotesha mbegu ya mapinduzi. Alikuwa amewaachia kina Kinu ramani ya mioyo ya wananchi waliokuwa tayari kuamka. Na sasa alikuwa kivuli kinachotembea ndani ya maboresho ya historia ya nchi.
**********
Katika Ranchi ya Andrew Kamage, mwanga mmoja mdogo wa taa ya mafuta ulizunguka korido ya nyumba ya mbao, ukitengeneza kivuli cha mzee huyo aliyevaa miwani.
Andrew alifungua jalada lililoandikwa “Mama Lutu.” Ndani yake kulikuwa na ramani ya kila eneo alilowahi kuingia Mama Lutu, mawasiliano yake ya siri, na barua moja ya mkono isiyo na jina, yenye maneno:
“Yuko ndani lakini si wetu.”
“Tunamfuatilia,” Andrew alijisemea. “Lakini mwisho wake unakuja.”
*******
Kwa mbali, ndani ya chumba kimoja kilichojaa harufu ya chakula kilichoharibika. Mama Lutu alikuwa akizungumza na mtu kupitia redio ya kisasa ya digitali.
“Ndiyo. Benedicto ametoweka. Kinu na Moreen bado mafichoni. Lakini ramani yao ninayo.”
Akatabasamu. Tabasamu la mtu aliyeshinda kwa siri, lakini pia aliyejua anacheza na moto wa mionzi.
Mama Lutu alitazama skrini ya simu yake iliyokuwa inaonyesha ramani na kiduara chekundu kilichokuwa kinamwekua mwekua. Ilikuwa inaonyesha mahali walipokuwa Kinu na Moreen, mafichoni.
Mama Lutu alitabasamu huku kumbukumbu zake zikionyesha jinsi alivyoiweka chip ya GPS kwenye Saa ya mkononi ya Moreen.
Hiyo ndiyo ilikuwa inampa kujiamini kuwa Bado alikuwa na nafasi ndani ya DEKA.
Itaendelea