WANAWAKE NI WAUAJI..!? (65)
BY - MTOTO WA BECKER (The Special Thinker)
__________________________
________________
"Hussein mwanangu, usiwe mnyonge hivyo. Ndugu yako nipo hapa si nishakwambia...? mimi ndio ndugu yako babaa"
ilikuwa ni sauti ya mwanaume mtu mzima iliyosikika nyuma ya mlango alipokaa mtoto Zungu ambae jina lake halisi alikuwa anaitwa Hussein.
Sauti ile ilimfanya Hussein ageuke huku machozi yaliyojazana machoni muda mrefu alipokuwa anawaangalia kina Kinoge wakihama bila kupepesa macho, yalianza sasa kutiririka mashavuni mwake na kumtazama kwa uchungu yule mtu aliyemsemesha.
"baba, babaa unajua inauma sana. sasa wewe umewezaje kukaa mwenyewe na kuvumilia bila kulia pindi mama alipoondoka?"
aliuliza mtoto Hussein na kumfanya yule mtu ambae alikuwa ni babaake mzazi amnyanyue pale na kumkumbatia kwa nguvu huku akimsihi atulize kwanza moyo kwa kumshikashika kichwa akizichezea nyele zake ndogo za kipilipili huku mkono mwengine akimpigapiga mgongoni.
"Mwanangu Hussein, mbona ni rahisi sana baba...! ni rahisi mwanangu twende ndani nikakuhadithie"
aliongea babaake Hussein na kumchukua mwanae mpaka chumbani kuwapisha wapangaji wengine waendelee na shughuli zao mida ile pale ukumbini waliposimama jilani na mlango wa kutokea.
"Mwanangu mamaako amekuacha ungali una miaka mitano lakini japo nilimkumbuka ila haikuwa sababu ya kunifanya niwe mnyonge na kukosa kabisa furaha. Unajua kwanini?"
alianzisha maongezi babaake Hussein pindi walipokua wamekaa kitandani pale chumbani kwao.
"hapana baba, sijui"
"Kwa sababu wewe ulikuwepo, unajua kwanini uwepo wako ulikuwa sababu ya mimi kukosa huzuni na kuwa na furaha mbali ya kuwa mamaako hakuwepo tena?"
"Hapana baba sijui."
"Kwa sababu wewe ndie ndugu yangu na yule alikuwa mke wangu na ndio maana ameolewa tena na mwanaume mwengine na hata huko anaweza kuondoka tena na kuolewa pengine."
"aaah, sasa baba na mimi mama sio ndugu yangu?"
"Hapana mwanangu, wewe ni zaidi ya ndugu yako kwa sababu wewe ni mwanae na yeye ni mamaako unapaswa kumuheshimu na kumtembelea mara kwa mara."
"sawa baba, kwa hiyo Kinoge sipaswi kumlilia kwa kua sio ndogo yangu na huko aendako anaweza kupata rafiki kama mimi na wakihama tena atamuacha na kwenda kupata rafiki mwengine ikawa hivyohivyo eeeh.."
"Ni kweli kabisa mwanangu, hutakiwi kumuweka sana moyoni mwanamke mwengine zaidi ya mamaako mzazi ambae hawezi kuondoka na kukuacha moja kwa moja hata uwe uweje, ila hawa wengine mwanangu usiwaamini kabisa na kuwaeka sana moyoni kwani wataweza kukusababishia maumivu na mateso makubwa pindi watapogeuka na kwenda kwengine."
"sawa baba"
"Ndio hivyo mwanangu hupaswi kuumia mimi nipo na hata kama nisipokuwepo amini wa kukusaidia kweli ni mwanaume mwenzako japo wanawake ndio wanaoonekana kuwa na mioyo mepesi ya kusaidia lakini bado msaada wa ukweli upo kwa mwanaume baba. haya nyamaza wewe ni mmwanaume shika hela hii kanunue chapati uje tunywe chai"
"Asante baba nimeelewa, nami nakuahidi sitoumia tena kwa sababu ya Kinoge"
aliongea Hussein na kufuta machozi baada ya kuchukua pesa kwenda kununua hivyo vitafunwa huku akimuacha na tabasamu zito babaake.
* * * * *
Safari yao iliwachukua masaa mengi garini siku hiyo tokea asubuhi ile walipoliacha jiji la Dar na kuingia jijini Arusha majira ya saa moja usiku ambapo safari bado iliendelea mpaka kwenye vijiji vya mbali na Arusha mjini na huko ndiko kulikokuwa na makazi mapya ambayo walihamia familia ya bwana na bibi Juma pamoja na mtoto wao kipenzi aliyeitwa Kinoge.
"haaa! mamaa ndio tumefika hapaa!!?"
aliuliza kwa mshtuko Kinoge pindi alipoyaangalia mazingira waliyofikia kwa nje ambapo muda huo wale vijana waliopakia vitu kule jijini walikuwa wanavishusha wakipewa maelekezo pa kuviingiza na bibi mmoja ambae ndie alikuwa mwenyeji wao aliyewapokea.
"Kinoge kwani wee unapaonaje si pazuri tuu.. tena huku kuna maembe na machungwa kibaoo unayopenda furaaaahi basii."
mama alijaribu kumliwaza mwanae ambae sasa alikuwa tayari kakunja uso kutokana na kuchukizwa na mazingira yale ya kijijini.
Aliangalia kwanza hakukuwa na umeme, hakukuwa na barabara nzuri, nyumba zilikuwa zipo mbalimbali hali iliyomuumiza Kinoge na kuona ni afadhali wangemuacha jijini Dar na rafiki ake Zungu asingekuwa mpweke kuliko kuletwa pale ambapo aliamini hata marafiki wa kucheza nao kama Zungu hawakuwepo.
"iiihhhhhhyyaaaaaaaaaa.. sipaaatakiii mimiiii... Nirudiisheeeni kwa Zunguuuuu"
alianza kulia kwa sauti Kinoge na mamaake kujitahidi kumnyamazisha wakati huo babaake alikuwa anasombelea vitu na kuvipanga kwenye ile nyumba pamoja na wale vijana.
Baada ya shuguli zote za uhamiaji kukamilika na ile gari waliyokuja nayo kuanza safari kuelekea mjini na hatimae sasa Kinoge aliamini kuwa kweli wamefika na hasa pale alipokuja babaake na kumwambia.
"Mwanangu Kinoge, maisha ni mlima leo unapanda kesho unashuka harafu maisha ni popote usiangalie mazingira kwanza ukayakimbia unafikiri hata kule mjini kulikuwa vile? kule napo kulikuwa kama huku.. Watu wakahamia na kupasafisha wakaishi na kupatengeneza hadi leo umepaona vile. Basi hata huku napo kutakuwa kama vile endapo tutakaa na kupatengeneza. Haya twende ndani ukasalimiane na bibi eeeh"
Maneno ya babaake ndio yaliyompa nguvu Kinoge na kupiga moyo konde kuwa tayari kuanza maisha mapya.
Bwana Juma ambae ni baba mzazi wa Kinoge yeye alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi na wakati huo alikuwa amepata uhamisho wa huko Arusha ambapo aliuomba yeye mwenyewe ili apate nafasi ya kurudi nyumbani kwa mamaake ambae alikuwa mzee na alihitaji uangalizi wake na kwa kuwa miaka mingi aliipoteza Dar mpaka anazaliwa Kinoge na kufikia umri ule alikuwa hajawahi kufika pale kijijini lakini sasa hawakuwa na budi wote kwa pamoja walihamishia makazi kijijini kabisa.
Na huo ndio ukawa mwanzo wa Kinoge kupotezana na Zungu.
ITAENDELEA