Simulizi: Scaila Michael

Simulizi: Scaila Michael

SEHEMU YA 50

Wakati huo alikuwa jikoni akiendelea kuandaa chakula. Niseme ukweli tu, ninakubali Scaila hakuwa na tabia nzuri, hasa ya uaminifu lakini kwenye majukumu ya ndani alikuwa akiyafanya kama mwanamke aliyekamilika.

Hakuwa akimruhusu Grace kufua nguo zangu, alizifua mwenyewe, alipenda sana kupika chakula kila alipokuwa nyumbani, alipenda sana kufanya usafi chumbani, yaani ninadiriki kusema alikuwa mwanamke aliyekamilika kwa majukumu mengine kuliko hata wale ambao walikuwa waaminifu katika ndoa zao.

Baada ya kuandaa chakula, nikakaribishwa na kwenda kula. Tulikaa mezani huku kila mmoja akifurahi na kutaniana hapa na pale.

Kuonekana na furaha kama nilivyokuwa ilikuwa kazi ngumu mno, nina uhakika kulikuwa na wanaume wengi ambao wasingeweza kuwa kama mimi kwani wangeanzisha ugomvi na hata kununanuna, haikuwa hivyo kwangu.
“Hebu vuta picha kuhusu harusi yetu,” nilimwambia Scaila.

“Yaani sipati picha itakuwaje!” aliniambia huku akionekana kuwa na furaha.
“Ungependa tukaifungie wapi? Ninataka siku hiyo mpaka marafiki zangu washangae,” nilimwambia huku nikitoa tabasamu.

“Wewe utataka tukafungie wapi?”
“Popote pale. Ila kwenye fungate ninataka twende katika Visiwa vya Comoro, yaani tukakae hata wiki tatu,” nilimwambia.

“Oh! Itakuwa si mchezo mume wangu!”
“Nitakununulia bonge moja la zawadi siku ya harusi yetu, nitafungua akaunti za watoto wetu kabla ya kuzaliwa, nakwambia nitafanya mambo mengi sana kwako, ni kwa sababu utakuwa mke wangu nitakayekupenda mpaka mwisho wa maisha yangu,” nilimwambia.

Scaila akaniangalia huku akionekana kuwa na furaha tele, aliamini kila kitu kingekwenda kufanyika kama kilivyopangwa, kuna siku angekuwa mke wangu wa ndoa.

Nilikuwa na akili zangu, za peke yangu, nilitaka kama ingetokea siku tukaachana basi majuto yake yawe makubwa kwa kumpoteza mwanaume aliyekuwa na mipango madhubuti na maisha yake.

Tulizungumza mengi mno, nilimwambia mambo ambayo nadiriki kusema sikuwahi kumwambia mwanamke yeyote yule, nilimpa ahadi nyingi ambazo ningezifanya baada ya kumuoa na kuwa mke wangu wa ndoa.
 
SEHEMU YA 51

Baada ya kuzungumza mengi huku Grace akiwa pembeni, nikamchukua na kuelekea naye chumbani, tukakaa kitandani huku akiwa ameniegemea kwenye kifua changu.

Hapo nikawa najiuliza kama lingekuwa suala sahihi kumwambia kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea ama nilitakiwa kuwa kimya kama mwanaume aliyekamilika.

Nilijiuliza mambo mengi, swali la kwanza lililokuja kichwani mwangu, ingekuwaje kama angekasirika? Angeumia, na mimi sikutaka kumuumiza msichana niliyekuwa nampenda kama yeye, sasa nifanyeje?
“Scaila...” nilimuita kwa sauti ndogo.
“Abee mume wangu,” aliitikia.

Nikashusha pumzi, nilitamani sana kumwambia kila kitu lakini kwenye kuliwakilisha suala kama hili lilihitaji hekima ya hali ya juumno.

“Nikuulize swali?” nilimuuliza.
“Uliza tu!” aliniambia kwa sauti ya chini.
“Hivi ikatokea ukagundua ninakusaliti! Utafanya nini?” nilimuuliza.

Akashtuka kumuuliza swali hilo, alikuwa ameegemea kifua changu, nikamuona akitoka na kuniangalia machoni, alionekana kama kubadilika hivi.

Nilijua alichokuwa akijiuliza juu ya swali langu, halikuwa la kawaida hata kidogo, lilimfanya kuwa na hofu na mimi na kuhisi inawezekana nilianza kumsaliti.
Ngoja nikwambie kitu, hakuna kitu anachokichukia msaliti kama kusalitiwa.

Huwa wanajua wanawaumiza wengine lakini kamwe hawataki kuona na wao wakiumizwa na ndiyo maana Scaila alionekana kama kuumizwa na swali lile.
“Unamaanisha unanisaliti?” aliniuliza huku akiniangalia.

“Hapana! Nimekuuliza ili kujua?”
“Una mpango wa kunisaliti?”
“Sitoweza, ila ninataka kusikia jibu lako mpenzi,” nilimwambia, nikaachia tabasamu.

“Mh! Sijui nitafanya nini! Naomba tu hilo suala lisitokee, nitaumia sana,” alinijibu.
“Kwa sababu gani uumie?”
“Kwa kuwa nakupenda!”
“Unaweza kumsaliti mtu unayempenda?” nilimuuliza huku nikimwangalia kwa umakini kabisa.

Kwanza akanyanyamaza, tayari alihisi kulikuwa na kitu nilichokuwa namaanisha. Akanikazia jicho halafu akawa kama mtu aliyekuwa akifikiria kitu fulani cha kunijibu.

“Kwa nini umeuliza hivyo?”
“Ulishawahi kunisaliti?” nilimtupia swali jingine.

“Nyemo! Leo una nini?” aliniuliza, wakati akionekana kutokuyapenda maswali yangu, mimi nilikuwa natabasamu tu.
“Ninahitaji kufahamu! Ushawahi kunisaliti?” nilimuuliza
 
SEHEMU YA 52

“Don’t dare to lie to someone who knows the truth,” (usijaribu kumdanganya mtu anayejua ukweli) nilimwambia, akashtuka.
“Unamaanisha nini?”
“Ni msemo ulioandikwa na mtu fulani hivi, unamjua Boniphace Ngumije?” nilimjibu na kumuuliza.

“Yule mwandishi wa vitabu? Rafiki yako?”
“Ndiyo!”
“Ila maana yako nini?”
“Ni maneno tu! Naomba nikaoge kwanza,” nilimwambia, nikapotezea mambo hayo kwani tayari niliona alianza kubadilika na kuwa na hofu.

Nikavua nguo zangu, nikachukua taulo na kuelekea bafuni kuoga. Sikufichi, hakuna siku ambayo nilimuona Scaila akiwa amebadilika kama siku hiyo.

Alinywea, alikuwa akiniangalia huku akiwa na maswali mengi mno. Scaila ameniumiza sana, nadhani umeyasoma mambo yote ambayo yalitokea kati yangu na yeye, hivyo na mimi nikataka nianze kumuumiza nafsi yake, awe na maumivu, ateseke kila siku kwa kujiuliza juu ya nilichokuwa nikimwambia.

Nilichukua dakika kadhaa bafuni, nikatoka na kumfuata kitandani, alionekana kuwa mpole sana, wakati mwingine alikuwa akitoa tabasamu lakini nilijua kabisa halikuwa kutoka moyoni, lilikuwa tabasamu lenye maswali mengi nyuma yake.
“Unaifahamu muvi ya Acrimony?” nilimuuliza.

“Hapana! Inahusu nini?”
“Ni filamu ya maisha tu. Kulikuwa na jamaa alimpenda sana msichana, akamuahidi mambo mengi atakayoyafanya baada ya kumuoa, bahati mbaya wakaachana kwa talaka kabla mwanaume hajafikia ndoto zake za kuwa tajiri, hivyo yale yote aliyokuwa ameahidiwa, akapewa mwanamke mwingine,” nilimwambia, maneno hayo yakazidi kumtia hofu.

“Unanitia hofu!”
Nikatabasamu.
“Usijali! Ni muvi tu. Wakati mwingine unapopata nafasi ya kuaminika, kuahidiwa mambo mengi baada ya kuoana, usijali kuyaacha mambo hayo akafanyiwa mwanamke mwingine,” niliendelea kumwambia huku nikijifuta maji.

“Mh!”
“Scaila! Kuna wanawake wengi wanatamani kuolewa, wengine wanasaka ndoa mpaka kwa waganda, wanajichubua kwa kuamini wanaume wanapenda wanawake weupe, wengine wanatumia mpaka dawa za kichina kuongeza makalio....wanafanya hivyo kwa sababu wanahitaji ndoa. Unapofanikiwa kupata mwanaume anayekuahidi kukuoa, anakufanyia mambo mengi, achana na watu wengine,” nilimwambia, niliamua kumpa kadarasa kidogo.
 
SEHEMU YA 53

Unapofanikiwa kupata mwanaume anayekuahidi kukuoa, anakufanyia mambo mengi, achana na watu wengine,” nilimwambia, niliamua kumpa kadarasa kidogo.

“Ila leo nahisi una kitu. Unadhani nimeanza kukusaliti?” aliniuliza.
“Hapana! Scaila, hebu simama,” nilimwambia, akasimama na kusogea karibu yangu. Tukakumbatiana.
“Jaribu kubadilika! Nataka uwe mke bora!” nilimwambia kwa kumnong’oneza sikioni, nikawa nayasikilizia mapigo ya moyo wake makusudi.

“Sawa! Nitabadilika.”
“Klabu hakuwezi kukupatia mume bora! Marafiki hawawezi kukuombea upate mume bora kwa sababu wanajua utabadilika na kuwaacha. Unapoamua kutafuta mume wa kuoa, kubali kubadilika hata kama itakugharimu sana,” nilimwambia.

“Sawa mpenzi! Nimekuelewa!”
“Unapoona umeshindwa, mshirikishe hata Mungu, ila lengo kamili ni kubadilika. Usijaribu kunidanganya,” nilimwambia.
“Sawa. Nitabadilika.”

“Ahsante!” nilimwambia, nikamuachia, nikamwangalia usoni na kutoa tabasamu, niliyaona macho yake jinsi yalivyokuwa, alikuwa na hofu tele.
|
|

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne.
 
SEHEMU YA 54.

Kuna vitu ningependa kukufundisha msomaji, mara nyingi unapotaka kufanya kitu simama kwa nafasi yako, kama upo kwenye mapenzi, huyo mtu uliyekuwanaye, mpende kama hutokuja kupenda tena.

Yaani wajibu wako ndiyo ambao unatakiwa kufanywa. Ni kama shuleni, mwanafunzi ana wajibu wa kujifunza, hakuna kitu kingine zaidi ya hicho, na kwenye mapenzi ipo hivyo, unapotakiwa kuwa na wajibu wa kumpenda mtu, kumjali, kumsikiliza na kumuheshimu, fanya hivyo.

Kuna mambo mengi yanatokea nje ya uwanja, sisi binadamu huwa hatujakamilika hata kidogo lakini jitahidi unapofanya madudu basi mwenzako asijue. Mwili wa binadamu umejazwa matamanio, akipita dada na kisketi kifupi umeona mapaja, unatamani, unapomuona kaka kapita kifua wazi na garden love kuonekana, unatamani.

Kutamani kupo, tamaa tumeumbiwa binadamu na ni vigumu kuzuilika ila inapotokea ukanasa kwenye mtego, jitahidi sana kumuheshimu huyo uliyekuwanaye, kama ulikuwa unampiga mabusu kila asubuhi, mpige, usisahau kufanya hivyo kwa sababu nje kuna mtu anakupagawisha kwa maneno matamu ya uongo.

Nilitamani sana somo hili nimpe Scaila, wakati mwingine nilitamani hata kuchukua simu ya jamaa na nimtumie meseji, ili ajifiche kufanya mambo hayo lakini nilishindwa kufanya hivyo.

Pamoja na kumlaumu Scaila ila wakati mwingine mimi ndiye nilionekana kuwa na makosa. Inawezekana mtoto wa watu alikuwa akifanya siri sana, tena kwa kujificha lakini upekuzi wangu ndiyo ulinifanya nikutane na haya ninayokutana nayo.

Kwa Scaila nilikuwa mvumilivu kwa sababu nilimpenda kutoka moyoni. Nisikilize! Kama unampenda mtu kutoka moyoni na unahisi utakuwa umepata pigo sana akiondoka kwenye maisha yako, naomba usimfuatilie kabisa.

Huwa tunasema simu ya mpenzi wako ni kama bomu la machozi, ukiichukua tu, ni lazima ulie, kama huna moyo wa uvumilivu, ule wa kupambana na hayo utakayokutana nayo huko, potezea na uishi kwa amani kabisa.
 
SEHEMU Y 55.

Kuna ndoa nyingi zimeharibika kwa sababu ya simu tu, kuna ndoa ambazo sasa hivi unaposoma simulizi hii zinayumba kwa sababu ya simu, kama unaona simu ni kitu kidogo ambacho kinaweza kuitetemesha ndoa yako ama uhusiano wako, achana nayo, ipotezee kwani utakapogundua yale utakayokutana humo, uhusiano utavunjika ama kuchukua uamuzi mbaya. Yaani simu ya laki mbili unavunja uhusiano uliodumu kwa miaka mitano au ndoa iliyodumu kwa miaka kumi.

Nilikuwa na uwezo wa kumuacha Scaila muda wowote ule, nilikuwa na sababu lukuki lakini nilihitaji kumuona akibadilika na kuwa mtu mwingine. Nilihitaji kumpa nafasi ya pili nione kama atanielewa ama vipi.

Usiku huo alikuwa na mawazo tele, nilimuharibia siku yake na kuhisi nilijua kila kitu. Nilichokifanya ni kumuacha akiwa na mawazo yake na mimi kulala.

Asubuhi niliamka mapema sana na kujiandaa kwenda kazini, wakati amekwenda kuandaa chai, haraka sana nikawasha kompyuta yangu kwa ajili ya kuangalia mawasiliano yake ya usiku uliopita.

Niliamini aliwasiliana na marafiki zake, inawezekana waliniongelea kwa kile kilichotokea. Nikafungua humo, niliamini ningepata picha ya mabadiliko yake ama kuwa vilevile.

Nikakuta amewasiliana na marafiki zake wawili, wa kwanza alikuwa Janeth na mwingine alimsevu kwa jina la Mariamu. Nilichokifanya ni kuanza kumfungua huyo Janeth na kuanza kusoma.
Scaila: Janeth! Nahisi Nyemo amejua kila kitu.

Janeth: Kujua kila kitu kuhusu nini?
Scaila: Kwenda klabu! Yaani ameniambia mambo hayo mpaka siamini kabisa.

Janeth: Mh! Mambo gani tena shoga?
Scaila: Yaani ni kuhusu klabu, amenihusia mambo makubwa, ya msingi lakini moyo wangu umegawanyika, upande mwingine unaniambia ni mambo ya kipumbavu.
Janeth: Mh! Shoga kazi unayo! Kwani alikwambia nini?

Scaila: Ishu za klabu, sijui mume bora hapatikani klabu, yaani amenichanganya! Sijui kajuaje!

Janeth: Achana naye! Nahisi ameanza kuhisi! Kwani mama si ulimseti vizuri ama alitoa boko?

Scaila: Nilimseti.
Janeth: Sasa atakuwa amejuaje? Au anakutega?
Scaila: Sijajua!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom