muyakb24
JF-Expert Member
- Jul 31, 2018
- 412
- 275
31SEHEMU YA 31
Maisha baina yangu na Scaila yalikuwa matamu sana, tulipendana kwa dhati na muda mwingi tulikuwa pamoja.
Sikuyaona madhaifu yake kwa wakati huo, kila nilipokuwa nikirudi nyumbani nilipokelewa kwa mbwembwe nyingi na mahaba tele.
Kiukweli hapo ndipo niligundua unapokuwa kwenye mapenzi mazito una nguvu ya kufanya kitu chochote kile.
Scaila aliuteka moyo wangu, alilifahamu hilo na alihakikisha kila siku ninakuwa mtu wa furaha katika maisha yangu yote.
Kwa kweli sikutaka kumfuatilia kabisa hasa kwenye simu yake, nilihitaji awe huru, afanye lolote analolitaka lakini aniheshimu na kujua kwamba mimi ni mume wake mtarajiwa.
Mambo yalikuwa mazuri mpaka pale ambapo niliona anakuwa bize sana na simu. Kama ni kuchati, basi kwa Scaila ilikuwa si mchezo, kila wakati aliishikilia simu yake na kuandika meseji kwenda kwa watu wengine.
Kwa sababu nilimpenda, sikutaka kabisa kumfuatilia, sikutaka kuona akikasirika kwani yeye ndiye alikuwa furaha yangu katika maisha yangu kipindi hicho.
Nilianza kuingiwa na shaka kuhusu simu yake, ila wakati mwingine nilijiambia sikutakiwa kuwa hivyo kwa sababu nilipenda, na mtu ukimpenda, jambo la kwanza kabisa unatakiwa kumwamini.
Hivyo ilikuwa ni hivyo, hata alipokuwa akiiacha simu yake hapo, iwe inaita au ujumbe wa maneno kuingia wala sikujishughulisha nao hata kidogo.
Nakumbuka kuna siku nilirudi nyumbani majira ya saa kumi, siku hiyo niliwahi kwa sababu nilimaliza biashara zangu mapema sana hasa kwenye kukusanya mahesabu na hivyo nilihitaji muda mwingi wa kupumzika.
Nilipofika nyumbani, nilimkuta Grace lakini Scaila hakuwepo nyumbani. Sikutaka kuwa na wasiwasi naye kwa sababu nilimwamini sana.
Nilikaa sebuleni huku nikiendelea kufanya mambo yangu kwenye kompyuta yangu ya mapajani.
Muda ulikwenda lakini hakurudi nyumbani, nilianza kuingiwa na wasiwasi, ikanibidi nifanye maamuzi ya kumpigia simu na kumuuliza alipokuwa. Kabla ya kufanya hivyo, kitu cha kwanza nikaona lingekuwa jambo jema nijue mahali alipokuwa, nikamuita Grace na kumuuliza.
“Wifi yako yupo wapi?” nilimuuliza.
“Alikwenda kwa mama!” alinijibu.