SEHEMU YA 48
Siku hiyo sikuwa na furaha kabisa, si siku hiyo tu bali katika wiki hiyo nilikuwa na huzuni tele, moyo wangu ulikosa furaha kwa sababu ya Scaila tu.
Nilimpenda mno, huo ndiyo ukweli kutoka moyoni mwangu. Unaweza kuniona mjinga, sina akili lakini omba sana mambo haya yasikukute, kwani yakikukuta, unaweza hata kuchukua uamuzi mgumu.
Kuna watu wengi kama mimi, tena wengine ni zaidi yangu. Hebu fikiria, sikuwahi kumfuma Scaila akiwa chumbani na mwanaume, ni maneno tu, yaani maandishi ya kwenye simu ndiyo yaliyokuwa yakinipagawisha.
Sasa hebu fikiria, kuna mwanaume anamfumania mke wake ndani, chumbani akiwa na mwanaume mwingine, uchi wa mnyama lakini bado anamsamehe, mimi ni nani? Je, nimuache Scaila kwa sababu ya meseji? Yaani nikienda kwa mama yake, nimwambie nimeachana na Scaila kwa sababu ya meseji za bando la shilingi mia tano, ni upuuzi ulioje!
Kama binadamu mwenye uvumilivu, nilitakiwa kumpa nafasi msichana ya kubadilika basi hiyo hiyo nafasi alitakiwa kuipata Scaila, ila kwanza nilitakiwa kumwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea.
Nilijipanga na kuelekea kazini, nilipanga siku hiyo ndiyo ya kumwambia msichana huyo ukweli kabisa, yaani kama alikuwa akiyafanya mambo hayo basi aachane nayo, atulie na mimi na tujenge maisha.
Nilifika kazini na kutulia, hali haikubadilika, ilikuwa kama siku nyingine tu, nilikuwa na mawazo tele mpaka majira ya saa tatu asubuhi, simu yangu ikaanza kuita, nilipoangalia jina, alikuwa Scaila, nikashusha pumzi ndefu, kidogo mwili wangu ukachangamka na akili kukaa sawa, nikapokea.
“Halo bebi!” niliisikia sauti yake nyororo.
Kuna vitu vingi vya kuzoeleka lakini si sauti ya Scaila, kila nilipokuwa nikiisikia, ilinipagawisha mno.
Nilichanganyikiwa kupita kawaida na kila siku nilikuwa nikimuona kuwa mpya na ndiyo maana ninasema wazi kumuacha msichana huyu lilikuwa jambo gumu sana kufanyika.
“Halo mchumba...” niliita huku nikitoa tabasamu pana.
“Nimekumiss sana mpenzi!” aliniambia kwa sauti ya kudeka.
“Nimekumiss pia! Mama anaendeleaje?” nilimuuliza.