SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya...........42
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA....
"Felix, hadi hapa nilipofikia nimepambana na watu wazito na wakubwa kuliko hata wewe, mwisho wa siku wote niliwasweka gerezani. Acha tuone nani atakuwa na mchezo mzuri kati yangu mimi na wewe." Brandina alijisemea mwenyewe na baada ya hapo akapiga hatua kurudi ofisini kwake.
SASA ENDELEA...
"Afande Afande"
Mara Inspekta Brandina alisikia sauti ya kike ikimuita kutokea nyuma yake, akageuka kutazama. Alikuwa ni mwanadada mrembo Tesha.
"Tesha..!!" Aliita Inspekta Brandina
"Ndiyo ni mimi afande, yuko wapi Felix? Nini kinaendelea?" Alijibu Tesha kisha akauliza maswali mfululizo, wakati huo alikuwa akihema kwa nguvu sana
"Vipi mbona hivyo ulikuwa unakimbia?"
"Ndiyo nimekimbia kuanzia hapo sheri, kuna vijana wamenisababishia ajali kizembe kabisa" Alieleza Tesha asijue kuwa huu ulikuwa ni mpango wa makusudi uliofanywa na MG Family ili kumzuia asifike kituo cha polisi hadi pale watakapo maliza jambo lao.
"Kwa hiyo gari umeliacha wapi..?"
"Nimemwita kijana wangu mmoja anashughulikia taratibu nyingine muhimu, afande mbona hunijibu kuhusu Felix?"
"Felix hayupo hapa, mmepishana sekunde tu. Tumeshamuachia huru"
"Mmemuachia? Vipi kuhusu ile taarifa uliyonipa pale airport, kwa maana hiyo sio kweli Felix hana kosa si ndiyo hivyo afande?"
Brandina alitulia kwa muda kisha akatikisa kichwa chake kukubali.
"Nilijua tu Felix hawazi kufanya hivyo. Ameondoka mda mrefu, unaweza kujua alipoelekea?"
"Hauna namba yake?"
Lilikuwa ni swali gumu kwa Tesha kulijibu kwa sababu baada ya kutengana na Felix hata mawasiliano yalikufa. Ni kweli namba yake ya simu alikuwa nayo lakini Felix hakuwa akipatikana kwa muda mrefu hivyo Tesha akaamini Felix amebadilisha namba ya simu.
"Hauna namba yake?" Brandina alirudia Tena swali lake.
"Aah! Ipo lakini hapatikani , labda kama amewasha simu sasa hivi" Tesha alidanganya huku akizuga na kuchukua simu yake akafanya kama anataka kumpigia Felix
"Teshaa.." Brandina aliita, Tesha akainua uso wake kumtazama
"Usihangaike kumpigia mfuate nyumbani, kaondoka hapa na mama yake"
"Mama yake? yupi?"
"Huwafahamu wazazi wa Felix?" Aliuliza Inspekta Brandina. Hili lilikuwa ni swali la mtego akataka kujua kama watu hawa ni wapenzi basi huenda Tesha akamueleza kitu chochote kitakacho msaidia katika upelelezi wake kuhusu ukweli wa familia ya Felix.
"Mmh! Ukweli siwajui. Afande mimi na Felix hatuna muda mrefu sana kwenye mahusiano, sijui vitu vingi kuhusu yeye" Tesha alijibu akitoa kauli ambayo ilimfanya Brandina asiulize maswali mengine zaidi ni kama alimshtukia.
"Sawa, Felix kaondoka hapa na mama yake, yule mama David ndio mama yake Felix pia"
"Whaat!!"
"Yes! Iko hivyo, walipotezana kwa muda mrefu na leo ndio wamekutana hapa hapa kituoni" Alieleza Brandina.
Hizi zilikuwa ni taarifa ngeni zilizomuacha Tesha kinywa wazi. Eti mama yake David ni mama yake Felix pia .


Safari kurudi nyumbani kwa mama David ilikuwa ikiendelea. Garini walikuwepo watu watatu yaani Haron, Felix na mama David. Kulikuwa na hali ya ukimya wa muda mrefu ndani ya gari hilo, kila mmoja alionekana kuwaza lake huku Haron akiwa ndiye dereva.
Hatimaye mama David alivunja ukimya huo.
"Mwanangu yuko wapi...?"
Kimya...
"Hamjanisikia? Nawauliza mwanangu yuko wapi? Tayari nimeshaifanya kazi yenu.." Mama David aliuliza tena safari hii kwa ukali kidogo.
"Mama mwanao yuko salama kuwa mtulivu, subiri tufike nyumbani" Alijibu Haron.
Wakati huo Felix alikuwa kimya kabisa huku akionekana kuwa mbali sana kimawazo. Bado mwanamke mrembo Tesha alikuwa ameganda kwenye ufahamu wa ubongo wake, kila sekunde alikuwa akilikumbuka lile tukio la uwanja wa ndege alipokutana na Tesha kwa mara nyingine baada ya kipindi kirefu kupita.
"No, lazima nimuone Tesha, lazima nimuweke karibu yangu. Nitamlinda mwenyewe dhidi ya baba" Aliwaza Felix
Dakika chache baada walifika nyumbani kwa mama David. Wakakuta tayari Madam Husnata na timu yake walishafika na kusimama nje ya nyumba hiyo wakiwasubiri.
Mara baada ya gari kusimama mama David alikuwa ni wa kwanza kushuka, akawa anapiga hatua ndefu ndefu kuelekea pale aliposimama Husnata.
"Kazi yako imeisha mwanangu yuko wapi?" Mama David aliuliza akiwa na jazba sana. Madam Husnata hakujibu kitu badala yake sauti ya Tatu ilisikika akiita jina la mama kutokea ndani ya nyumba ya Mama David.
Mama David alikimbia haraka kumuwahi binti yake ambaye naye alitoka akikimbia wakakutana katikati na kukumbatiana kwa upendo mkubwa sana. Mama David alishindwa kuyazuia machozi yaliyoanza kumtoka kwa wingi.
"Hi"
"Hi" Felix na Madam Husnata walisalimiana.
"Habari za muda mrefu Felix.."
"Ni nzuri sana"
"Karibu tena Tanzania"
"Asante nimekaribia.."
"Sikujua kama unampenzi anaitwa Tesha, by the way nimekumiss sana" Alisema Husnata, Felix hakijibu kitu akaishia kumtazama tu, ilionekana wazi wawili hawa kuna kitu kinaendelea katikati yao. Ndio sababu Husnata alishtuka akiwa pale ghorofani baada ya Kareem kuzungumza habari za mahusiano ya Felix na Tesha.
Macho na akili ya Felix vyote alikuwa amevielekeza waliko mama David na mwanae Tatu namna walivyokuwa wamekumbatiana kwa upendo mkubwa. Felix alijikuta akili yake inahama na kwenda mbali sana. Siku zote alikuwa akitamani kuishi maisha ya amani na upendo kama wanavyofanya binadamu hawa. Hakuna kitu alikuwa anakichukia kwenye maisha yake kama kuambiwa yeye si binadamu wa kawaida.
Felix alijisahau kabisa, akawa amekaza macho yake kuwatazama Mama David na mwanae Tatu. Husnata naye akawa anamtazama Felix asielewe amepatwa na nini.
"Mmeshaweka kila kitu sawa?" Haron alimuuliza Husnata.
"Yap! Kila kitu kiko vizuri bado tu kuongea na huyu mama aendelee kutunza siri maana nahisi askari wataendelea kuja kumuhoji, hasa yule wanamwita Brandina"
"Sawa, hongereni mmecheza mchezo mzuri sana. Hata mzee Magnus ninaimani atawapongeza sana akisikia"
"Ni kawaida yetu, hakuna kitu kinaweza kuishinda MG Family"
"Nakubali..." Alisema Haron kisha akapiga hatua akasogea karibu na Felix.
"Felix sasa tunaweza kwenda kisiwani kwa Mzee, bila shaka anatusubiri kwa hamu kubwa" Alisema Haron lakini Felix akawa kimya, hakujibu chochote.
"Felix..."
"Hapana siendi kisiwani" Alisema Felix uso wake ukionekana kumaanisha alichokisema. Haron na Husnata wakatoa macho kwa mshangao.
"Unamaana gani Felix"
"Haron, nenda kamwambie baba asante kwa kunitafutia familia, nafikiri ni wakati wangu sasa wa kuishi maisha yangu nikiwa huru, na hii ndio itakuwa familia yangu kuanzia leo" Felix alifafanua huku akiwatazama Mama David na Tatu ambao sasa walikuwa wakipiga hatua kuingia ndani, Felix akaanza kuwafuata nyuma.
"Mnataka nini tena kwangu?" Mama David alifoka mara baada ya Felix kufika pale walipo.
"Nina ombi moja kwako Mama yangu..."
"Nini? Ombi gani?" Aliuliza Mama David, mara Felix akasogea karibu yake na kupiga magoti mbele yake.
Lilikuwa ni tukio lililowaacha kinywa wazi si Haron, si Husnata na hata mama David mwenyewe alishangaa.
"Kwanza kabisa kwa niaba ya wenzangu naomba utusamehe kwa hiki tulichokifanya kwako mama yangu. Lakini pia naomba uniruhusu niwe mwanafamilia wako mama, naomba niichukue nafasi ya marehemu mwanao Feisal. Najua sio rahisi kunielewa lakini tafadhali kwa ruksa yako mama naomba nifanye mwanao niko chini ya miguu yako" Felix aliongea kwa hisia kali.
Ni kweli kabisa alikuwa anamaanisha kile anachokisema. Kwa aina ya maisha aliyokuwa akiishi kijana huyu akifuata sheria kali za baba yake Magnus ambaye alidiriki kumtenga hadi na watu anaowapenda kama vile Tesha, ni kweli kabisa Felix alikuwa na haki ya kuongea maneno kama yale.
"We kijana... Hivi haijatosha tu kwa yote mliyoyafanya kwangu. Mnanitakia nini tena ondokeni...nimesema siwataki...ondoka..ondokaaa" Mama David alipaza sauti huku akivua kandambili yake akaanza kumtandika nayo kijana Felix.
Haraka Haron aliwahi na kwenda kumzuia Mama David aache kufanya kile anachokifanya, ilikuwa ni hatari sana kama Magnus baba wa Felix atazipata habari hizi.
"Sogeaa... " Felix alipaza sauti akainuka ghafula na kusimama katikati ya Haron na mama David. Akawa anamtazama Haron kwa macho makali sana.
"Katu usithubutu tena kuinua mkono wako kumgusa huyu mama, iwe mwanzo na mwisho, nasema iwe mwanzo na mwisho" Felix aliongea kwa jazba huku mdomo wake ukitetemeka, macho yake yakawa yanabadilika na kuwa ya kijani kisha yakarudi tena kwenye hali yake.
Ilikuwa ni kwa mara ya kwanza Haron anamshuhudia Felix akiwa katika hali hiyo, hapo akaamini ni kweli Felix ameamua.
"Felix..." Mara kuna sauti ya kike ilisikika ikiita. Felix na wengine wote wakaelekeza macho yao mahali sauti hiyo imetoka.
Uso kwa uso Felix anagonganisha macho yake na macho ya Tesha.
Je, nini kitafuata?
ITAENDELEA...