68.
Moyo wake ulimuuma lakini hakuwa na cha kufanya, hakuruhusiwa kuhuzunika hivyo maumivu yale aliyoyapata, yalikuwa moyoni mwake tu.
Alipopokonywa kisu kile, wakaambiwa waende katika mlango mmoja wa chumba, huo ulikuwa na jina kubwa lililosomeka Lusifa mlangoni.
Walipofika, mlango ukajifungua na kisha kuingia ndani. Sehemu hiyo ilionekana kuwa tofauti na vyumba vingine, pale kulikuwa na uwanja mkubwa zaidi ya wa mpira wa miguu, mbele kabisa kulikuwa na jumba moja kubwa na la kifahari.
Sehemu hiyo ilikuwa na msisimko wa ajabu, hawakuona kitu chochote kile cha kutisha lakini kila walipokuwa wakilisogelea jumba lile, walikuwa wakisisimka mno.
Mbele kabisa wakakutana na watu wengi warefu, urefu wao unaweza kufikia ule wa twiga, walikuwa na mapembe kama ya ng’ombe, chini walikuwa na kwato za kondoo.
Walikuwa wakitisha sana, walipowaangalia vizuri wakagundua kwamba hao walikuwa majini, yale yaliyokuwa yakija duniani huku wakiwa na maumbo hayo na kuwatisha watu.
Hawakuonekana kujali, wakazidi kupiga hatua kuelekea mbele zaidi, huko, wakakutana na sehemu iliyokuwa na bwawa kubwa kama haya yaliyokuwepo duniani (swimming pool), bwawa lile halikuwa la maji bali lilikuwa ni la damu tu.
Pembeni ya bwana hilo kulikuwa na mabomba makubwa kadhaa, mabomba hayo yalikuwa na kazi ya kumimina damu ndani ya bwawa lile.
Katika mabomba yale kulikuwa na maneno yaliyokuwa yameandikwa, moja liliandikwa magari, hilo lilikuwa bomba pekee lililokuwa na kazi ya kukusanya damu kutoka kwa watu waliopata ajali za magari duniani.
Huku duniani watu wanapopata ajali, na kama ile ajali ni ya kishetani, basi zile damu zao zinakwenda katika bwana lile kupitia bomba lile. Mbali na bomba hilo, pia kulikuwa na bomba jingine lililoandikwa ndege, hilo nalo lilikuwa na kazi hiyohiyo.
Haikuishia hapo, kulikuwa na megine yameandikwa treni, meli na pikipiki, yote hayo yalikuwa yakipitisha damu kuelekea katika bwana hilo. Mbali na mabomba yote hayo, kulikuwa na bomba jingine ambalo liliandikwa mhanga.