Simulizi: Safari Yangu Kuzimu

Simulizi: Safari Yangu Kuzimu

30

Watu walizidi kukusanyika mahali pale wakiwasikiliza watu hao waliokuwa wakipeana vitisho kwamba yeyote angeweza kumuua mwenzake.

Hakukuwa na mtu aliyeingilia, labda kwa sababu wengi waliyafahamu maisha ya huyu mzee huyu aliyeitwa Hamisi tena huku wengine wakimsonta kidole kijana yule aachane naye lakini hakutaka kuacha, aliendelea kumwambia kwamba angeweza kumuua.

“Kijana anatafuta balaa, huyu mgeni nini?” aliuliza mzee mmoja.
“Si mgeni, ni mwenyeji kabisa.”
“Sasa kwa nini anampiga mkwara huyu mzee, hamjui nini?”

“Anamjua sana, si unajua hivi visifa vya vijana wetu,” alisema mzee mwingine.
Mzee Hamisi hakutaka kuzungumza sana, akaondoka na kuingia ndani huku akiwa amefura kwa hasira.

Kijana yule hakuondoka, alijiona kuwa bingwa na kuona mpinzani wake ameshindwa.

Alitukana na kutukana huku mikwara ikiendelea kusikika mdomoni mwake lakini mzee Hamisi hakurudi nje, aliendelea kubaki mulemule ndani kwake. Nakumbuka kijana yule alichukua zaidi ya dakika tano zaidi kutukana na kisha kuondoka.

Usiku ulipoingia, nikaanza kumuona mzee Hamisi akiwa kwenye mti mmoja mkubwa uliokuwa katikati ya uwanja mmoja mkubwa wa mpira. Mahali hapo alisimama peke yake na baada ya dakika kadhaa, kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliofika uwanjani hapo.

Kila mtu alikuwa mtupu, haikujalisha kama ni mtu mzima, mtoto au kijana, uwe mwanaume au mwanamke, unapokuwa hapo ulitakiwa kuwa mtupu. Niliwaona wanawake wawili wakiwa wamebeba chungu kimoja kikubwa na kukipeleka mbele kabisa kisha mwanamke mmoja aliyeonekana kuwa mtu mzima kusogea karibu na kile chungu.

“Leo ni siku ya kuleta mahitaji yenu na kufanyiwa kazi,” alisema mwanamke yule, sauti yake ni kama ililazimishwa iwe ya kutisha.

Ngoja nikwambie kitu. Miongoni mwa mambo mengi niliyoambiwa na Yusnath ni kuhusu siku maalumu ambayo hutumika kwa ajili ya kupeleka mahitaji yao kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Wachawi hutenga siku maalumu kwa ajili ya kufanyia kazi matatizo yao.
 
31

Siku hiyo, kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akiwasumbua, labda kuna mtu ambaye hakuwa akirogeka kirahisi basi siku hiyo jina lake lingetumbukizwa ndani ya chungu kile na kufanyiwa kazi.

Kama mtu huyo hakuwa na nguvu zozote zile basi angepata kile walichotaka akipate, labda ugonjwa wa kudumu na mambo mengine mabaya ambayo mchawi anataka mtu huyo ayapate.

Baada ya kuambiwa hivyo, nikamuona mzee Hamisi akisogea karibu na chungu kile na kusimama huku akiwaangalia wachawi wengine waliokusanyika uwanjani hapo. Alikuwa na hasira kama mtu aliyepagawa hivi, kila mtu akabaki kimya akimsikiliza.

“Nimekasirishwa sana mkuu,” alisema mzee Hamisi huku akiwa ameyageuzia macho yake kwa mwanamke yule aliyeonekana kuwa kiongozi mahali hapo.
“Sema chochote kile, tutalifanyia kazi,” alisema kiongozi.

“Kuna kijana amenikera sana,” alisema mzee Hamisi.
“Unataka tumfanye nini?”
“Awe kichaa tu ili iwe fundisho kwa kila mtu mtaani,” alisema.

“Anaitwa nani?”
“Ramadhani.”
“Sawa. Ombi lako limekubaliwa. Weka jina lake katika chungu hicho.”
Alichokifanya mzee Hamisi ni kukiingiza kikaratasi kilichokuwa na jina la kijana yule, Ramadhani katika chungu kile kilichotoa moshi mkubwa na kwenda kusimama na wenzake.

Siku hiyo ilitumiwa vilivyo, kila mmoja alikuwa na kazi ya kuchukua kikaratasi kilichokuwa na jina la mtu aliyekuwa akitaka kumfanyia jambo na kukiweka katika chungu kile.

Ndugu yangu, asikwambie mtu kwamba unapokuwa mchawi basi utakuwa na maisha yenye uhakika kwamba kila kitu utakachokitaka basi kitafanikiwa.

Kuna wachawi wanakutana na vitu vya kutisha mno, kuna wengine kazi zao zinashindwa na hivyo kujikuta wakikamatwa. Mchawi yeyote yule anayekamatwa kwa uzembe wake basi ni lazima apewe adhabu kule kuzimu.
 
32

Hii ndiyo sababu inayowafanya wengi kupeleka majina ya wabaya wao. Kulikuwa na watu wagumu kurogeka, kuna wengine wana kinga kali, mchawi anaposhindwa kumroga, basi huenda kwenye uwanja wao wa makutanio na kueleza kile kilichotokea.

Anachokifanya mchawi mkuu ni kuchukua lile jina na kuliweka kwenye kile chungu kisha kumpa mtu huyo nguvu na kurudi.

Anaporudi, huwa na nguvu ya ziada, atakaposhindwa kwa mara nyingine, hapo ndipo wanapoongeza nguvu, yaani haendi mmoja, wanakwenda na wengine hata watano, wanaposhindwa hapo ndipo wanapotafuta njia nyingine.

Kuna wachawi wengine huwa wanakufa kazini, wengine wanapata misukosuko mingi, yote hiyo wanaita ajali kazini na mara nyingi hutokea kwani si kila mtu huwa rahisi kurogeka.

Mara baada ya mzee Hamisi kuliweka lile jina katika chungu kile, akawa na uhakika kwamba kile alichokitaka ni lazima kingefanyika tu kwani aliamini kijana yule hakuwa na nguvu kubwa, hata kama alijiamini kwa kumpiga mikwara, bado alijiona kuweza kumfanya kijana yule kuwa kichaa.
Uchawi ukatumwa!
.
.
Itaendelea.
 
Mbichi kabisa hii! Ngoja nitue hapa nijenge na kiota maana mziogo c wakipolepole
 
33

Niliuona uchawi ukianza safari kumfuata kijana Ramadhani ili uweze kumdhuru na kuwa kichaa. Katika upande wa pili nilimuona akiwa amekaa chumbani kwake, alikuwa na mawazo mno, alionekana kama mtu aliyekata tamaa kwa jambo fulani.

Nikauona ule uchawi unaingia ndani. Ndugu yangu, huwezi kuuona huu uchawi kama huna nguvu fulani. Sikuwa kwenye ulimwengu wa kibinadamu bali nilikuwa kwenye ulimwengu wa kijini. Ule uchawi ulipofika mlangoni, ukaingia ndani kwa ajili ya kumvaa kijana yule.

Sikujua nini kilitokea, nilimuona Ramadhani akishtuka, akasimama harakaharaka na kukunja ngumi, kitu cha kushangaza, uchawi ule nao ukasimama. Sijajua kama Ramadhani alikuwa akiuona au la, akafungua droo yake ndogo ya kitanda na kuchukua kikaratasi kimoja kilichoandikwa maneno mengi kwa Lugha ya Kiarabu na kuanza kukisoma kwa harakaharaka.

Ule uchawi ukamfuata na kumvamia, nikasikia sauti kubwa kama ya radi ikipiga, ule uchawi nikauona ukishindwa kumuingia na hapohapo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Mh!” nilijikuta nikiguna.
Usiku huohuo nikauona uchawi ule ukirudi mpaka kule ulipotumwa. Hakukuwa na hali ya kawaida, kila mtu alipouona ukija, akakimbia mahali pale na kusimama pembeni kabisa ya uwanja ule, ule uchawi, kutokana na nguvu kubwa iliyokuwa nao, ukakivunja kile chungu hivyo wachawi wote kujua kwamba ule uchawi ulishindwa huko ulipotoka.

“Ni lazima tuungane, mtu mmoja hawezi kututisha,” nilimsikia mzee mmoja akizungumza maneno hayo, alikuwa mbali kabisa na aliogopa kusogea kule kilipokuwa chungu kile.

Baada ya dakika tano tena walipoona hali imetulia, wakasogea mpaka pale kulipokuwa na chungu kile kilichovunjika na kuanza kuangalia kwa ndani, hakukuwa na kitu chochote zaidi ya manyoya ya kuku tu.

Kila mmoja akashangaa, japokuwa walijua kulikuwa na wakati wachawi walishindwa kufanya jambo fulani, lakini kwao hawakuwahi kushindwa, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza.

Mzee Hamisi alikosa la kuongea, kila wakati aliuachamisha mdomo wake, hakuamini juu ya kile kilichokuwa kimetokea. Ramadhani alikuwa na nguvu mno na hakuwa mtu wa kumchezea hata kidogo.
 
34

“Haiwezekani! Haiwezekani!” nilimsikia mzee Hamisi akisema kwa sauti kubwa.
“Huyu mtu ana kinga kubwa sana,” alisema kiongozi wao.

“Tufanye nini? Tuongeze nguvu kumfuata?” aliuliza mchawi mwingine.
“Hatuwezi kwenda kwa kukurupuka, ni lazima tujipange, vinginevyo tutaumbuka,” alisema kiongozi yule.

Hapohapo wakapangwa watu waliotakiwa kwenda kwa Ramadhani kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kijana yule anamalizwa haraka iwezekanavyo kwani waliamini hakukuwa na mtu aliyekuwa na uchawi mkubwa zaidi yao.

Wachawi wengine waliochaguliwa kwa ajili ya kwenda huko, walikuwa na hofu mno, hawakupenda kwenda kwa kuwa walijua kazi huwa ngumu, kuna kushindwa na hata mwisho wa siku kukamatwa.

“Nitawapeni maelekezo juu ya nini cha kufanya,” alisema kiongozi yule na kuanza kuwapa maelekezo.

Hakuchukua muda mrefu kuwaelekeza nini cha kufanya, baada ya kumaliza, akawapa unga fulani na kuwataka kujipaka nyusoni mwao na kupotea, ghafla nikawaona wakiwa juu ya nyungo zao huku kiongozi wao akiwa mbele kabisa akiwaelekeza nini cha kufanya.

Nilikuwa nikiyaona yote, mzee Hamisi alikuwa ametulia kwenye ungo wake uliojaa tunguli nyingi, mkononi alikuwa ameshika usinga mmoja mkubwa na alikuwa akiupepea kila ungo wake ulipokwenda kwa umbali fulani.

Hawakuchukua muda mrefu wakawa wamefika katika nyumba waliyotaka kuingia. Ilikuwa ni usiku sana, katika mtaa huo waliokuwepo, kulikuwa na watu wengine, hasa vijana ambao walikuwa wakinywa pombe na hata kucheza drafti lakini hakukuwa na yeyote aliyewaona mahali hapo.

“Nani anaanza kuingia?” aliuliza mchawi mmoja.
Kiongozi wao ndiye aliyekuwa akiamua ni nani wa kuingia na nani wa kubaki nje, alichokifanya ni kuwachagua wachawi wawili, walikuwa mabinti wadogo, kwa kuwaangalia kwa harakaharaka ungeweza kugundua walikuwa wakijifunza mambo ya kishirikina.

“Kwa nini waende wao?” aliuliza mwanamke mmoja, nilihisi alikuwa mzazi wa watoto hao.
“Ni lazima wajifunze mengi, bila hivyo, hawatokua,” alijibu kiongozi.
 
35

Ngoja nikwambie kitu kimoja, kwenye suala zima la kuingia ndani ya nyumba ya mtu aliyeshindikana kichawi huwa linaogopwa sana, hakuna mtu anayependa kuingia humo kwani wengi wanaoingia hunaswa na mwisho wa siku kukutwa mpaka asubuhi wakiwa hapohapo wamenasa na mbaya zaidi, wakati mwingine hufariki dunia.

Kila mmoja aliogopa hivyo kuwasakizia wale mabinti ili waingie ndani. Mama yao alijua kwamba hiyo ilikuwa ni moja ya hatua kubwa na ngumu sana na ndiyo maana alilazimisha sana mabinti zake wasiingie ndani.

“Lakini ndiyo wanajifunza,” alisema mama yao.
“Hata kama! Ndiyo wajifunze jinsi ya kuroga watu kama hawa,” alisema kiongozi

Mwanamke yule hakuwa na jinsi, japokuwa alikuwa na mapenzi makubwa kwa mabinti zake lakini akakubaliana na kiongozi wake kwamba awaache mabinti zake waingie ndani kwa ajili ya kumroga Ramadhani.

Kilichofanyika ni kuupuruzia dawa mlango wa nyumba ile na pembe zote kisha mabinti wale wakaambiwa waingie ndani. Ghafla wakapotea na kuwaona wakiwa kwenye pembe moja ya nyumba ile na kuanza kuingia ndani.

Nilibaki kimya, nilikuwa nikifuatilia kila ktu tena kwa ukaribu, nilitaka kuona ni kitu gani kingetokea mahali hapo. Pale nje walipobaki, wale wachawi walikuwa wakiendelea kufanya mambo yao, walicheza utupu huku wakiendelea kupulizia unga fulani katika nyumba ile.

Huku kila mmoja akiwa bize, ghafla ukasikika uyowe mmoja mkubwa kutoka ndani. Kila mmoja akashtuka! Hawakujua nini kilitokea ndani.
 
36

Mwanamke yule ambaye watoto wake walikuwa ndani ya nyumba ile akaanza kulia, alijua kile kilichotokea kwamba watoto wake walikuwa wamenasa na hivyo ilimaanisha wangekutwa asubuhi au wangekufa usiku huohuo.

Hilo likamkosesha amani, akajaribu kuwaambia wenzake walitakiwa kuelekea ndani kwa ajili ya kuwanasua lakini kila mmoja akaonekana kuogopa kwani Ramadhani hakuonekana kuwa mtu wa kutania.

Walijaribu kukaa pale huku wakifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya kwani nao muda haukuwasubiri, uliendelea kusonga mbele jambo lililowafanya kuwa na wasiwasi zaidi.

“Tuingieni....” alisema mwanamke yule mwenye watoto wake.
“Hapana! Hatuwezi kuingia, huyu mtu anaonekana kuwa hatari,” alijibu kiongozi.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, Ramadhani hakuwa mtu wa masihara, kila mmoja aliogopa kuingia.

Mwanamke yule alibaki akilia lakini kilio chake hakikubadilisha matokeo yoyote yale, watoto wake walinaswa ndani.
Siku iliyofuata, taarifa zikaanza kusambaa kulikuwa na watoto wa hawakuamka kitandani, walikuwa wamefariki dunia.

Kilikuwa kifo cha kushtukiza sana, hakukuwa na mtu aliyejua kama kulikuwa na ushirikina kati yao na ndiyo kitu kilichopelekea kufa kwani walikwenda kumroga mtu aliyekuwa na nguvu zaidi yao.

Watu wakaanza kukusanyika msibani pale, wachawi waliofika mahali hapo wakaanza kuangaliana kwa macho ya shaka kwani walijua kile kilichotokea, watoto hawakufa duniani bali walichukuliwa misukule na Ramadhani.

“Hivi watu wanaweza kugundua kweli?” aliuliza mzee mmoja, alikuwa na upara kichwani, alivalia msuli mrefu.

“Hawawezi kujua, tusubiri tukazike tu.”
Ingawa wale waliokuwa wakiosha maiti walijua zile zilikuwa maiti lakini ukweli hawakuwa wakiosha maiti kama walivyoona bali ilikuwa ni migomba.

Wakati jeneza likiwa limeletwa nje tayari kwa kuswaliwa na maziko, ghafla mwanaume mmoja akaanza kuja kwa kasi msibani pale, alionekana kuwa na jambo la muhimu sana alitaka kuwaambia, alipowafikia, akaanza kumwangalia kila mtu aliyekuwa mahali pale, mwanaume yule hakuwa mwingine bali alikuwa Ramadhani.
 
37

Macho yake yalikuwa ya chuki mno, kila alipowaangalia wachawi wale, alikunja uso wake huku akisonya kwa hasira kitendo kilichotafsiriwa kuwa dharau na hakikutakiwa kuonyeshwa msibani pale.
“Hebu nyie wachawi inukeni muwaambie wenzenu ukweli,” alisema Ramdahani kwa dharau kubwa.

Hakukuwa na mtu aliyesimama, hata mama yao na marehemu ambaye alijifanya kulia, akanyamaza na kuona kwamba tayari walikuwa wakienda kuumbuka. Mtu aliyekuwa akiongoza mazishi yale, shehe mmoja aliyeonekana kuwa na heshima kubwa mtaani akamwangalia Ramadhani na kumwambia aondoke.

“Shehe, hamuendi kuzika maiti, mnakwenda kuzika migomba,” alisema Ramadhani, watu wote wakashtuka.
“Unasemaje?” shehe aliuliza kwa mshtuko.

“Hao watoto wapo nyumbani, nimewahifadhi,” alisema Ramdhani maneno yaliyomshtua kila mtu mahali pale.

“Wewe kijana hebu tuondolee uchizi.”
“Kama mnaniona chizi, angalieni maiti hizo,” alisema Ramdhani.

Walichokifanya mashehe wawili ni kusimama na kuyafuata majeneza yale yaliyokuwa na maiti zilizofungwa mikekani kwa lengo za kuzifungua.

Kila mtu msibani pale alibaki kimya, alitaka kushuhudia kile kilichozungumzwa na kijana yule.
Wale watu walikuwa mbali, wakasogea karibu, walitaka kuona kama kweli mule hakukuwa na maiti kama walivyojua au Ramadhani alikuwa akiwadanganya.

Wachawi wale ambao walikwenda kuroga nyumbani kwake usiku uliopita wakaanza kuondoka kwa kujifichajificha kwani tayari walijua mambo yaliharibika.

Mashehe wale walipoyafikia majeneza yale, wakazitoa maiti zile kutoka ndani na kuziweka mkekani, watu wakakodoa macho zaidi kwa kutaka kushuhudia kile kilichokuwa ndani ya mikeka ile.

Kwa kuwa hawakuwa na uhakika na hawakutaka kumuamini sana Ramadhani, wakaanza kuchungulia wao wenyewe kuona kama kulikuwa na maiti au migomba kama alivyosema Ramadhani.

“Mtumeee! Migomba! “ alisema shehe mmoja na hivyo kufungua mikeka ile.
Watu wakapigwa na bumbuwazi, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, ndani ya mikeka ile hakukuwa na maiti yoyote ile zaidi ya migomba miwili ambayo wao ndiyo walitakiwa kwenda kuizika.

Mama wa marehemu akaanza kulia kwa uchungu, hakulia kwa kuwa watoto wake walikuwa wamefichwa ila alilia kwa kuwa alijua fika huo ulikuwa wakati wa kuumbuliwa.
 
38

“Hawa watoto walikuja kuroga nyumbani kwangu usiku,” alisema Ramadhani na kuendelea:

“Nilichokifanya ni kuwasimamisha na ndiyo maana mnaona wamekufa lakini ukweli ni kwamba hawajafa bali walikuja kuroga nyumbani kwangu,” alisema Ramdhani.

Minong’ono ikaanza kuibuka msibani hapo, kila mtu aliyeyasikia maneno yale alipigwa na butwaa, watu ambao hawakuamini kama uchawi ulikuwepo, hapo wakaamuni kwa asilimia mia moja.

“Huyu mama yao alikuja nao akiwa na wenzake, wakawaacha na kuwasakizia waingie ndani na wakati wanajua hawakuwa na uwezo wa kuroga,” alisema Ramadhani, watu wote wakamwangalia mwanamke yule, kilio cha unafiki kikakata, akainama chini kwa aibu.

“Sikutaka kuwaua mabinti hawa kwa kuwa hawajui chochote kile, waliingia kwa kushinikizwa tu. Twendeni mkawachukue,” alisema Ramadhni na kuanza kuondoka mahali hapo.

Hakukuwa na mtu aliyetaka kubaki, wote wakaanza kumfuata Ramdahani ambaye alikuwa akitembea kwa mikogo mikubwa. Mkononi alishika hirizi kubwa nyekundu, alitembea kwa hatua ndefundefu ila kwa mwendo wa taratibu.

Walipofika nyumbani, akawaambia watu wale wasubiri na kisha kupulizia dawa fulani na kuwaita wasichana wale ambapo mlango ukafunguliwa na wasichana hao kutoka wakiwa kama walivyozaliwa, huku wakiwa wanatisha kwani bado walikuwa kwenye hali ya kichawi. Watu waliotangulizana na Ramadhani walipowaona wasichana wale, wakaanza kukimbia kwa hofu.

Kwa muonekano, walitisha mno, hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kubaki mahali hapo na kuwaangalia mabinti wale, walikuwa na muonekano wa kichawi ambao ulizidi kuwaogopesha watu zaidi.

Alichokifanya Ramadhani ni kuwaweka chini na kuwapaka unga fulani, ulikuwa ni wa njano, aliyapaka macho yao na miguu yao, baada ya kufanya hivyo, akaanza kuiongea maneno yasiyoeleweka na hapohapo mabinti wale wakarudi katika hali ya kawaida.

Kwanza walishangaa walikuwa wapi, kwa mbali mbele yao kulikuwa na umati wa watu ukiwashangaa, walipojitazama, wakagundua walikuwa watupu jambo lililowafanya kuanza kuziziba sehemu zao za siri kwa kutumia viganja vya mikono yao.
.
.
Itaendelea.
 
39

Pasipo kutegemea, mabinti wale wakaanza kulia. Kwao iliwauma sana kuwa katika mazingira hayo, hawakuwa wakikumbuka kile kilichowafanya kuwa mahali hapo lakini baada ya kumuona Ramadhani, wakakumbuka kila kitu.

“Wachukueni muwapeleke kwao,” alisema Ramadhani, walichokifanya wanaume wenye moyo wa chuma ni kuwachukua na kuwapeleka nyumbani kwao huku kundi kubwa la watu likiwafuatilia kwa nyuma.

Walitembea kwa aibu mpaka walipofika nyumbani kwao na kuingia ndani, kwa kipindi cha wiki nzima, hawakutaka kutoka ndani kwani walikuwa wakijisikia aibu mno.

Nilimuona mzee Hamisi akiwa amechanganyikiwa, kile kilichotokea, kilimuuma sana. Alipagawa kwani aligundua Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo na ndiyo maana hata pale kwenye ugomvi, na yeye alikuwa na moyo wa kumpiga mikwara angeweza kumuua.

Hakutaka kukaa jijini Dar es Salaam, akaondoka kuelekea Bagamoyo. Hapa subiri nikwambie kitu kimoja, mchawi yeyote anapoona ameshindwa sehemu fulani, huwa hataki kukubali bali anachokifanya ni kutafuta hata msaada wa watu wengine kuhakikisha anafanikiwa mpaka kutimiza kile alichokuwa akikihitaji.

Huko Bagamoyo alikuwa akimfuata mzee mwingine ambaye alionekana kuwa nuksi sana, mzee aliyemuaminia kwa kuwa na uchawi wenye nguvu.

Alipofika huko, akaenda kuonana na mzee huyo na kuanza kuzungumza naye.
“Anatumia uchawi wa wapi?” aliuliza mzee huyo, aliitwa mzee Maliki, alijulikana Bagamoyo nzima kwa uchawi.

“Wa Kanda ya ziwa!”
“Kutoka Kigoma?”
“Ndiyo!”
“Daah! Hapo kuna kazi kubwa, ila tutafanikiwa.”

Wachawi walikuwa wamegawanyika, walikuwa wale kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi na Kanda nyingine nyingi. Kwenye kila kanda, kulikuwa na nguvu yake lakini wachawi wengi waliogopa uchawi kutoka Kanda ya Ziwa.

Huko Kigoma, asilimia kubwa ya uchawi wao ulikuwa ukichanganyikana na ule kutoka Kongo ambao ulijulikana kwa kuwa mkubwa na wenye nguvu kuliko ule wa Tanzania.

Watanzania wengi walikuwa wakiuogopa uchawi huo na ndiyo maana mzee Hamisi aliposema kwamba uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani ulitoka Kanda ya Magharibi, mzee Maliki akaogopa.
 
40

“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kwangu sidhani kama nitaweza ila kama utahitaji sana, kesho tuelekee Tanga, kuna mtu ambaye anaweza akatusaidia,” alisema mzee Maliki.

“Sawa hakuna tatizo.”
Mzee Hamisi hakutaka kurudi Dar es Salaam, alichokifanya ni kusubiri hukohuko Bagamoyo ili kujiandaa na safari ya kwenda Tanga kwa mtu mwingine ambaye aliambiwa kwamba alikuwa na nguvu kubwa mno.

Usiku hakulala kwa raha, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Ramadhani aliyeutetemesha ufalme wake. Alimchukia kijana huyo na alitaka kuhakikisha kwamba kila kitu atakachokifanya basi mwisho wa siku kijana huyo afe.

Asubuhi ilipofika, wakaamka na safari ya kuelekea Tanga kuanza. Kuna kitu huwa kinashangaza sana, unaweza kumkuta mchawi akiwa bize na mambo yake, tena ya msingi kabisa lakini linapokuja suala la kuroga, yaani yupo radhi aache mambo yake yote lakini mwisho wa siku afanye kile anachotakiwa kukipata.

Si kwamba mzee Maliki hakuwa bize na mambo yake, alikuwa bize mno lakini alipoambiwa suala la kutaka kumroga mtu fulani, mambo yake yote akayaacha pembeni na kutaka kufanya kile alichokuwa amewambiwa, yaani alikuwa akihusudu uchawi kuliko kitu chochote kile.

Baada ya saa moja wakawa ndani ya basi wakielekea Tanga. Walikuwa wakipiga stori tu njiani huku kila mmoja akionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. Basi lilipofika Segera, njia panda ya kwenda Moshi na Tanga, likasimama.
Kila mmoja akahisi kwamba inawezekana kuna abiria alikuwa akishuka au wengine wakiingia lakini kitu cha ajabu, basi likasimama kwa muda mrefu sana lakini dereva hakuliondoa jambo lililowakera abiria.

“Dereva unazingua, hakuna abiria anayepanda, sasa tunasubiri nini hapa? Au tunamsubiri mkeo?” aliuliza abiria mmoja, kwa muoenakano wake tu ulionyesha alikuwa kisirani.
“Gari haiondoki!” alijibu dereva.
“Haiondoki au haiwaki?”
“Kuwaka imewaka, wala sikuzima, ila kuondoka haiondoki, sijui tatizo nini,” alisema dereva yule.
 
41

Maneno ya dereva yule yalimshangaza kila mmoja, hakukuwa na aliyeamini kama kweli gari lilishindwa kuondoka na wakati ilikuwa imewaka.

Alichokifanya abiria mmoja aliyeonekana kuwa mtaalamu wa magari akasimama na kuelekea kule kwa dereva ambaye akampisha na yeye kukalia kiti, akajaribu kukanyaga mafuta ili waondoke, gari haikuondoka.

“Mmmh!”
“Imekuwaje?”
“Ndiyo kwanza naona leo, imekuwaje gari haiondoki?” aliuliza dereva.
Minonong’ono ikaanza kusikika ndani ya basi lile, hakukuwa na mtu aliyejua kwamba kile kilichokuwa kikiendelea kilikuwa katika utawala wa nguvu za giza hivyo kwa akili ya kibinadamu jambo hilo lisingewezekana kabisa.

Mzee Hamisi na Maliki hawakuelewa chochote kile, ila waliposikia kwamba hali hiyo haikuwa ya kawaida kutokea duniani kwamba gari liwake lakini lishindwe kuondoka, wakaanza kuelekea kwa dereva ambaye bado alikuwa kwenye sintofahamu.

“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Hata kabla dereva hajajibu swali hilo, ghafla wingu kubwa likaanza kujikusanya, ndani ya sekunde kumi tu, tayari jua halikuonekana, hapohapo mvua kubwa ikaanza kuinyesha huku ikiambatana na radi kali iliyowafanya watu wote kuogopa.
“Mmh!” aliguna mzee Maliki.

Ilikuwa ni mvua kubwa, ilishuka kwa kasi kiasi kwamba kila mmoja akadiriki kusema hakukuwa na mvua kubwa iliyowahi kunyesha kama ile. Radi ziliendelea kupiga, kila mmoja akazidi kuogopa.

Mzee Maliki alishtukia kitu, kila alipoiangalia mvua ile, haikuwa ya kawaida, ilionekana kuwa na chembechembe za uchawi hali iliyomfanya kugundua kwamba kazi ilikuwa imeanza hivyo hakutakiwa kupuuzia.

Abiria ndani ya basi waliogopa, wengine wakaanza kulalamika kwamba dereva alitakiwa kuliondoa gari mahali hapo haraka iwezekanavyo. Kwa mzee Hamisi, hakugundua kitu chochote kile, kwake, mvua ile ilionekana kuwa ya kawaida sana.

Mzee Maliki akarudi kule kulipokuwa na kiti chake na kisha kuchukua mkoba wake aliouacha, mzee Hamisi alishangaa, alijua vitu vilivyokuwa ndani ya mkoba ule vilikuwa nini, sasa kwa nini mzee huyo aliuchukua.

“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi.
“Unadhani hii mvua ni ya kweli?”
“Ndiyo!”
 
42

“Hapana! Nahisi huyo mtu kashaanza kufanya kazi.”
Aliposema hivyo tu ikawa kama mzee Hamisi amefunguliwa macho, mvua ile iliyokuwa ikinyesha, haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa, hivyo naye akajiandaa kwani tayari alijua kwamba muda wa mapambano ulikuwa umefika.

Mzee Hamisi akatoa tunguli zilizokuwa ndani ya mkoba wake, kila abiria akaogopa, hawakujua mzee huyo alitaka kufanya nini. Hakutoa tunguli tu bali pia alichukua na usinga kisha kushuka garini na kuanza kuchezacheza huku akizunguka kwa staili ya mduara.

Kila mtu alibaki akimshangaa lakini wala hakujali, alichokifanya ni kuendelea vilevile. Katika hali ambayo kila mtu aliishangaa, ni ndani ya dakika kama mbili hivi mvua ikakatika ghafla lakini cha ajabu ardhi ikiwa haijalowana hata kidogo. Watu wote wakapigwa na butwaa.

“Eeeeh!”
Huo ndiyo ulikuwa uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani, ulikuwa uchawi wa hali ya juu sana na uliotisha ambao ulihitaji nguvu ya ziada kuusimamisha. Baada ya hapo, akarudi ndani ya basi kwa ajili ya kuondoka lakini bado basi lile halikuweza kuondoka mahali hapo.

Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu walikuwa wamekwishafika Segera, wakateremka kwa ajili ya kuchukua basi jingine ambalo lilikuwa likielekea Tanga ili wasiweze kukwama njiani na wakati kutoka hapo mpaka Tanga wala hakukuwa mbali.

Walitulia kituoni wakisubiri basi. Ndugu yangu, uchawi upo na mtu anaweza akaroga sehemu yoyote unapokuwa. Kwa wale waliowahi kufika Segera watakuwa wanaelewa kwamba mahali hapo huwa hakukauki mabasi hata mara moja, kila siku na kila saa magari yanapita yakielekea Moshi, Dar au Tanga.

Lakini huwezi amini, siku hiyo watu hao walikaa zaidi ya masaa mawili, hakukuwa na basi lolote lile lililopita kuelekea Tanga.

Hiyo wala haikuwa hali ya kawaida, walijaribu kuangalia huku na kule lakini hakukuwa na basi lolote hali iliyowafanya kutoka pale kituoni na kuwafuata watu waliokuwa wamekaa pembeni na kuwauliza.

“Samahanini?” alisema mzee Maliki.
“Bila samahani.”
“Mbona leo magari hayapiti hapa?”
“Magari ya kwenda wapi?”
 
43

“Tanga!”
“Unamaanisha mabasi?”
“Ndiyo!”
“Mmefika muda gani?”
“Tangu masaa mawili yaliyopita.”

“Eeeh! Sasa mabasi hayo yote yanayopita hamuyaoni au mnatufanyia kusudi wazee wetu?” aliuliza kijana mmoja, wote wakabaki wakiwashangaa wazee wale.
“Mabasi yanapita?”

“Ndiyo! Tangu lini umeona Segera ikakaukiwa na mabasi?” alihoji kijana mmoja.

Mpaka hapo wakajua kwamba walichezewa mchezo hivyo mzee Maliki akaulizia choo kwani alisema alishikwa na haja.

Akaonyeshewa choo cha kulipia na kwenda huko. Mbele yake tayari aliona kulikuwa na kazi kubwa sana ya kufanya hivyo pasipo kufanya kitu wangeweza kukesha barabarani.

Alichokifanya mara baada ya kufika chooni ni kuchukua usinga wake na tunguli lake, akasimama wima kuelekea upande wa kusini na kuanza kuzungumza maneno fulani yaliyofanana na lugha ya Kiarabu, alipomaliza, akajipiga na ule usinga kifuani, miguno na mabegani kisha kujipulizia unga fulani.

Alipomaliza, akatoka ndani ya choo kile, kitu kilichompa uhakika kwamba kweli walikuwa wamerogwa alianza kuyaona mabasi yakiwa mengi kituoni huku mengine yakiitia abiria kwamba yalikuwa na safari ya kwenda Tanga.

Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, akamwambia mzee Hamisi kwamba walipaswa kuendelea na safari kwani bado hawakuwa wamefika. Garini, mzee Hamisi alibaki akiuliza tu, hakuamini kama mambo yote hayo yaliyokuwa yametokea yangetokea siku hiyo.

Hapo ndipo alipoamini zaidi kwamba Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo na alikuwa na uchawi uliokuwa na nguvu kuliko hata ule aliokuwa akimiliki yeye.

Safarini, hawakutaka kupiga stori, kila mtu alikuwa anawaza lake kichwani, kwa mzee Hamisi, alikuwa akijifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kummaliza Ramadhani ambaye alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.

Kadiri alivyojifikiria, ndivyo alivyoingiwa na hofu moyoni hata kuona kwamba huyo mzee waliyekuwa wakimfuata, hakuwa kitu mbele ya Ramadhani.
.
.
JE, nini kitaendelea?
 
44

Waliendelea na safari yao kuelekea Tanga, mioyo yao ilikuwa na hofu tele kwani vile vitu alivyokuwa akivifanya Ramadhani havikuwa vya kawaida hata kidogo, uchawi aliokuwa akiufanya ni ule uliozoeleka kuonekana Kongo na nchi zingine zilizopo Magharibi mwa nchi ya Tanzania.

Kutoka Segera mpaka Tanga hawakupata shida yoyote ile, walipofika njiani hata kabla ya kuingia mjini wakateremka na kuchukua magari ya kwenda Handeni alipokuwa akiishi mzee Majoka, mzee aliyekuwa akisifika kwa uchawi Handeni nzima.

Histori fupi ya mzee Majoka ambayo nilipewa na Yusnath ni kwamba alikuwa mzee mpole sana kwa kumwangalia, muda mwingi alionekana nadhifu kiasi kwamba watu wengi walivutiwa na maisha yake.

Alikuwa mtu wa swala tano, kila alipoonekana, kanzu kubwa ilikuwa mwilini mwake kitendo kilichowafanya watu wengi kumuita jina la ustadhi ila baada ya kwenda kuhiji Macca, akapewa jina la Alhaji Majoka.

Mzee huyu alifanikiwa kupata watoto watatu wa kike, Rehema, Micilia na Fatuma ambao alizaa na mkewe kipenzi mwenye asili ya Kiarabu aitwaye Salhia. Mzee Majoka alimpenda sana mke wake zaidi ya kitu chochote kile na alikuwa mtu mwenye wivu kupitiliza.

Kuna kipindi alipata taarifa kwamba kuna jamaa alikuwa akimmendea sana mkewe, alipata taarifa kwa kipindi kirefu sana na kuna kipindi aliambiwa kwamba tayari jamaa huyo aliyeishi kidogo Dar alifanikiwa kufanya mapenzi na mke wake huyo, hivyo alichokifanya ni kwenda kumuonya kutembea na mkewe.

Kutokana na upole wake, kijana yule alipingana naye, akamwambia kwamba hakuwa akitembea na mkewe, lakini kwa kuwa alimaanisha kile alichokisema, alimwambia kwamba asijaribu kufanya hivyo kwani yeye ndiye aliyemtolea mali na kumuoa.

Kijana yule aliyejiita Mtoto wa Town hakukoma, pamoja na kuambiwa na mzee Majoka, akawa anaendelea kutembea na mke wa mzee yule.

Mzee Majoka hakumlaumu mkewe, maisha aliyokuwa akijiweka kijana huyo, kwa pale kijijini ilikuwa ni lazima kwa mwanamke yeyote yule kuvutiwa naye, hivyo alichokifanya ni kumfuata tena na kumuonya.
 
45

“Mzee! Hivi kweli unavyoniona ninaweza kutembea na mkeo, bibi zima?” aliuliza Mtoto wa Town aliyependwa kuitwa kwa jina la Diamond kutokana na jinsi nywele alivyoziweka na nguo alizokuwa akizivaa.

“Najua mke wangu ni mzee, lakini nakuomba kama unatembea naye, acha mara moja, sipendi masihara kabisa,” alisema mzee huyo kwa sauti ya upole lakini kwa mbali ilijaa ukali.

Baada ya siku mbili, watu hawakujua kitu gani kilitokea lakini kuna siku taarifa zikasambazwa kwamba kijana yule amenasiana na mke wa mzee Majoka porini chumbani.

Siku hiyo ilikuwa balaa, taarifa zilisambazwa sana kijijini hapo na watu kuelekea kule kulipokuwa na chumba cha kijana yule, kweli wakawakuta wawili hao wakiwa wamenasiana.

“Hili tego, jamani hili tego,” alisema mwanakijiji mmoja.
Mtoto wa Town akawa analia tu, alijaribu kuomba msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia kwani mtu aliyeweka tego alikuwa mume wa mwanamke huyo, hivyo mzee Majoka akaenda kuitwa.

Alipofika na kuwakuta watu wale wakiwa kwenye hali ile, akashangaa sana kwani aliwahi kumfuata kijana huyo mara mbili na kumwambia kuhusu mke wake lakini alipinga kwamba hakuwa akitembea naye, sasa ilikuwaje leo hii wawe wamenaswa?

“Mzee naomba unisamehe!” alisema kijana yule huku akilia kama mtoto.
“Kwa kosa gani?”
“Kutembea na mkeo! Uwiiiiiii! Naomba unisamehe!”
“Wewe si ulisema hutembei naye, sasa imekuwaje?”
“Mzee naomba unisamehe!”

Mzee Majoka alikataa, akaondoka chumbani hapo huku akiwaacha watu wakiwaangalia watu wale, wengine walikuwa wakicheka lakini wengine walisikitika.

Wazee wa kijiji hicho wakaamua kumfuata mzee huyo na kumuombea msamaha kijana huyo, kwa shingo upande akakubali hivyo anawanasua kwa kutumia madawa yake, kuanzia siku hiyo kijana huyo akahama Handeni na kuhamia Tanga Mjini.

Ukiachana na hilo pia kulikuwa na kijana mwingine ambaye alikuwa akimmendea sana binti wa mzee huyo, Micilia, kila alipokuwa akienda kuchota maji, alikuwa akimfuata nyuma kama mkia, alimpenda sana na hivyo kujaribu kutupa ndoano yake.
 
46

Micilia akanasa na hivyo kuanzisha uhusiano na kijana yule aliyeitwa kwa jina la Saidi ila kijijini hapo aliamua kujiita Side Mnyamwezi.

Baada ya kufanya mapenzi na Micilia, hatimaye binti huyo akapata ujauzito, nyumbani walipomuuliza, akwaambia kwamba ilikuwa ni ya Side Mnyamwezi.
Kijana huyo akaitwa na kuulizwa juu ya mimba ile, akakataa katakata na kusema kwamba haikuwa yake kwani kama ingekuwa yake, ingekuwa tumboni mwake.

“Hiyo siyo yangu! Kama ni yangu anipe sasa,” alisema Side Mnyamwezi kwa nyodo sana, watu wote waliokuwa eneo hilo wakaanza kucheka, mzee Majoka aliumia sana.
“Kwa hiyo unataka akupe?”

“Ndiyo! Si umesema yangu! Nipeni,” alisema Side huku akipeana tano na marafiki zake waliokuwa kijiweni.
Mzee Majoka hakuongea sana, alichokifanya ni kwenda chumbani na kujifungia.

Hakutoka siku nzima, kesho asubuhi akasikia watu wakigonga hodi kuhitaji msaada, alipoufungua mlango, akaambiwa kwamba kijana yule, Side Mnyamwezi amevimba tumbo na alikuwa akilia huku akilitaja jina la mzee Majoka.
Alichowaambia ni kwamba alitaka kumuona huyo Side, wakaenda kumuita, Side alipomuona mzee huyo tu, akaanza kulia huku akimuomba msamaha.

“Nini tena?” aliuliza mzee Majoka.
“Naomba unisamehe mzee, ile mimba kweli ni yangu!”
“Ndiyo ni yako na ndiyo maana nimeileta kwako,” alisema mzee Majoka.
“Naomba unisamehe mzee, sitorudia tena.”

“Kwani umenikosea?”
“Mzee naomba unisamehe!”
Siku hiyo Side alilia sana, aliomba msamaha na mwisho wa siku mzee huyo akamsamehe na mimba kurudi kwa Micilia huku akimuonya kijana huyo kwamba kama hatoilea mimba ile, angemrudishia tena akae nayo.

Kuanzia siku hiyo, jina la mzee Majoka likavuma, akajulikana Handeni nzima kwamba alikuwa mzee nuksi ambaye hakukopesha, yeye alikupa keshi endapo tu ungemletea masihara. Kuna mambo mengi ambayo aliyafanya katika wilaya hiyo ya Handeni ambayo ilithibitisha kwamba alikuwa nuksi.

Uchawi wake huo ukamfanya kila siku usiku kwenda makaburini, kazi yake kubwa ilikuwa ni kufukua maiti na kuchukua viungo. Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba uchawi wa mzee Majoka ulikuwa mpaka ule wa kupaa usiku na ungo.

Mara kwa mara alikutana na wenzake katika vikao vyao hasa vya wachawi wa Ukanda wa Pwani ambapo huko walipanga mikakati yao jinsi ya kuwaroga watu mbalimbali na kusafuiri kwa ungo kuelekewa sehemu tofautitofauti.

Japokuwa kulikuwa na wachawi wengi, lakini katika ya wachawi wote wa Kanda ya Pwani, hasa Tanga, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uchawi zaidi ya mzee Majoka, mzee ambaye alikuwa akifuatwa na wazee wawili, Hamisi na Maliki kwa ajili ya kupambana na kijana aitwaye Ramadhani.
.
.
Je, nini kitaendelea?
 
47

Walipofika Handeni, wakapokelewa na mzee Majoka ambaye alikwishapewa taarifa juu ya ujio wa watu hao. Kwa muonekano aliokuwa nao mzee huyo, mzee Hamisi hakuamini kama angeweza kuifanya kazi yake kwani alionekana kuwa mpole mno.

Asilimia kubwa ya wachawi, huwa hawana sura za kipole, wengi wao wanakuwa kama watu wenye roho fulani chafu, unaweza kujua kwamba mzee fulani ni mchawi, unapomuona au kupishana naye, mara nyingi unashikwa na hofu.

Mchawi anajulikana hata kama atakuwa katika hali gani, wengi wanakuwa na muonekano wa tofauti na huwa watu wasiojali sana, ila kwa huyu mzee Majoka, alionekana kuwa tofauti kabisa.

“Ndiye huyu?” aliuliza mzee Hamisi.
“Ndiye mwenyewe. Unamuonaje?”
“Tumekuja kupoteza muda, anaonekana haiwezi kazi hii,” alisema mzee Hamisi, imani yake haikuwa kabisa kwa mzee huyo hata kidogo.

Wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa mzee Majoka, njiani, kila mtu alikuwa akizungumza kwa fuaraha tele, kitendo cha kupokea ugeni huo, mzee Majoka alihisi kuthaminiwa mno.

Kila mtu aliyekuwa akiwaangalia watu hao, alijua tu kwamba walikuwa wachawi kwani walitangulizana na mtu aliyekuwa balaa kwa kuroga mtaani hapo.

Hakukuwa na watu waliowasogelea, na hata wale ambao kwa bahati mbaya walijikuta wakiwa karibu yao, walitoa salama kiuoga na kuendelea na mambo yao.

Walipofika nyumbani, mzee Majoka akawakaribisha na kuingia ndani ambapo moja kwa moja mazungumzo yakaanza.
“Kuna shida gani? Maana ulinieleza juujuu tu,” alisema mzee Majoka.


“Unamuona huyu rafiki yangu?”
“Ndiyo.”
“Amekutana na maswahibu si mchezo,” alisema mzee Maliki.

“Maswahibu gani?”
“Kuna mtu anamsumbua sana, alikuja kwangu, nikataka kumsaidia ila nikachemka kabisa,” alisema mzee Maliki.

“Umechemkia nini?”
“Yule jamaa anatumia uchawi wa Magharibi.”
“Magharibi?” aliuliza mzee Majoka huku akishtuka.
“Ndiyo!”
“Ooppss...” alishusha pumzi mzee Majoka.

“Vipi tena? Na wewe unaushindwa?”
“Hahaha! Tangu lini umeona nimeshindwa kitu? Hakuna kitu kama hcho,” alisema mzee Majoka kwa kujiamini.
“Basi tufanye kazi.”
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom