*ROHO YAKE INADAI -- 50*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
Akiwa anaendelea kutazama, mara akaanza kuona kioo hicho kikichipua ufa! Akakoroma akitaka kusema jambo lakini hakuwa anaweza. Kioo kikaendelea kuchipua ufa zaidi na zaidi. Na mmoja wa mwili uliokuwemo ndani ukaanza kujigusa. Ukachezesha kidole!
Ukafuatiwa na mwingine, ukachezesha jicho!
ENDELEA
Baba yake Wayde akatamani kunyanyuka azuie anachokiona, ila hakuwa anaweza. Hata kusogeza tu mwili wake ulikuwa ni mtihani, angewezaje kunyanyuka? Akabaki akigugumia, macho yakimtoka machozi zaidi na zaidi kutengeneza mto. Ni punde, kioo kikavunjika na wale walio wafu wakawa wazima!
Wakasimama kwa miguu yao. Wakatazama kwa macho yao! Ajabu ni kwamba viumbe hivi havikuwa vikipumua, wala mapigo yao ya moyo hayakuwa yanaita. Miili yao ilikuwa ya baridi na macho yao yalitingwa na mboni zenye rangi ya maziwa yaliyoharibika.
Wakamtazama yule mzee pale chini, wasiwe na habari naye, wakajiendea isijulikane wapi wanaelekea.
**
Wakiwa wameshikana mikono, kwa pamoja wakamalizia kusoma kifungu cha mwisho ambacho Wisconsin alielekezea. Wakiwa wanasoma kifungu hicho, mshumaa ukaanza kufifia, mapazia yakapeperuka kwa upepo, na milango ikaanza kucheza yenyewe.
Hawakukoma, wakamaliza kusoma kabisa, kisha Wisconsin akamchanja Brian kidole gumba na kuchuruzia damu kwenye ukurasa ule waliokuwa wameusoma. Ajabu pakaanza kufuka moshi mweusi karatasi likijifinya kuwa jivu.
Moshi huo Brian alipoutazama kwa sekunde kadhaa, akahisi anapoteza akili yake. Akahisi anapotelea moshini. Hata mwili wake ukaanza kupungukiwa nguvu. Alijishangaa kichwa chake kikidondoka kwa uzito na kujikuta chini!
Akiwa anapata fahamu, akasikia sauti za wadudu, na ngozi yake ikahisi kukalia majani. Akafungua kope zake nzito na kuangaza. Alikuwa kizani, na zaidi alikuwa msituni!
Akanyanyuka upesi na kutupa macho yake huku na kule. Akavuta pumzi ndefu na kujikuna kwa kuwashwa na majani, kisha akaanza kusonga kufuata mwanga anaouona kwa mbali.
Alipotembea kwa dakika tatu, akahisi kuna mtu nyuma yake, upesi akageuka kuangaza. Hakuona mtu! Ni miti ilikuwa imesimama tuli, miti meusi!
Akavuta pumzi ndefu na kusonga na safari. Akatembea tena kwa takribani dakika mbili, akahisi mtu akikatiza kwa mara nyingine! Alipogeuka na kuangaza, hakuona mtu. Akaokota gongo la kuminyia mkononi kwa tahadhari.
Kisha akaendelea kutembea.
**
"Atakuwa sawa?" Mama aliuliza akimtazama Wisconsin. Mikono yake ilikuwa imemshika Brian ambaye alikuwa amelazwa kwenye kochi akiwa hana fahamu.
"Usijali," Wisconsin akamtoa mashaka. "Atakuwa sawa tu. Yeye ni mpambanaji, najua atashinda vita hii."
Mama akamtazama mwanaye na kutikisa kichwa kwa huruma. Alitamani amwamshe na kumkumbatia, ila alikuwa ulimwengu mwingine. Alikuwa yupo kwenye ulimwengu wa wafu.
Mama Brian akauliza, "na vipi kama akiuawa huko?" Wisconsin akamtazama kwa imani na kumwambia, "Halitatokea hilo."
"Vipi kama likitokea?" Mama akasisitiza. "Kama akiuawa huko na huku itakuwaje? ... atakufa pia?"
Wisconsin akatikisa kichwa kuafiki, "ndio, atakufa pia. Hatoamka katika usingizi wake huu."
Mama akajawa na hofu. Akaketi na kumlaza mwanaye mapajani mwake. Mwanaye wa pekee. Naye Wayde akaweka kiganja chake kwenye paji la uso la Brian na kusema, "Tafadhali, kuwa salama."
Kidogo mshumaa ukazimika na ndani kukawa totoro.
"Nini kinatokea?" Mama akapaza sauti. Wisconsin akafanya jitihada za kuwasha mshumaa, ulipowaka, wakamwona mtu akiwa amesimama mlangoni. Mtu mpana mweusi. Wote wakashtuka!
Wasipate muda wa kujiuliza, mtu huyo akamvamia Wisconsin, akamkaba na kumnyanyua juu, kisha akamtupia kwanguvu ukutani!! Alafu, kwa kasi kali ya shingo yake, akamgeukia Mama yake Brian na kumnyooshea kidole chake kirefu. Akasema, "Wewe na mwanao, wote mtakufa!"
Akamnyaka Mama Brian, ila kabla hajafanya kitu, Wayde akamrukia mgongoni na kujaribu kumng'ata shingoni. Haraka akamdaka binti huyo na kumtupia kwenye meza ya runinga. Meza na runinga yake vikavunjikavunjika! Wayde akalalama sana kwa maumivu.
Bwana yule, mweusi kwa rangi, uso wake ukiwa haujulikani ni wa nani, akamgeukia sana Mama Brian aliyekuwa amemkumbatia mwanaye, akamtazama kwa kupindisha shingo, kisha akayarudia maneno yake, "wewe na mwanao, wote mtakufa" akamnyaka Mama Brian na kumnyanyua juu kama unyoya, alafu naye akamtupia mbali, akajibamiza na kudondoka chini akiwa hoi bin taabani.
Sasa dubwana likawa limebaki na mwili wa Brian pekee. Brian ambaye yupo hapo kimwili tu. Akamtazama na kumnyanyua juu akiwa amemkaba, akasema, "sasa na mwisho wako umefika!"
Akanyanyua mkono wake wa kushoto juu, ukachomoza kucha ndefu kama koleo, akamzamishia nazo Brian tumboni, Mama akapiga kelele kwa maumivu ya mwanaye! Mwili wa Brian ukaanza kumimina damu lukuki na yule Dubwana akafurahi haswa.
Akautupia mwili huo kochini alafu akanyonya vidole vyake vyenye makombo ya damu kisha akajilamba kana kwamba ametoka kula chakula kitamu.
"Tafadhali, mwache mwanangu!" Mama akalia. "Kaa mbali na mwanangu wewe shetani!"
Dubwana lile likaangua kicheko na kusema, "nishamwacha ajifie. Bado wewe!"
Likaanza kupiga hatua zake nzito kumfuata Mama Brian, alipomkaribia akamdaka shingo yake na kumnyanyua juu alafu akamkandamizia ukutani. Mama Brian akapapatika kutetea uhai wake. Miguu yake ikaogelea hewani akiwa anaelekea kufa.
Ila kheri, na ni ghafla tu, hilo dubwana likaanza kupoteza nguvu zake kwa upesi! Likastajaabu. Likamwachia Mama Brian akadondoka chini na yeye akaangaza huku na huko akitafuta kinachomtafuna.
Kule kingoni, dirishani, akamwona Wisconsin akiwa amefungua pazia sehemu ndogo na mkononi mwake ameshikilia kitabu anasoma. Basi dubwana hilo likakasirika likinguruma, haraka likaanza kusonga kumfuata Wisconsin akammalize mara moja!
Akiwa amebakiza hatua moja kumkabili mtu wake, Wayde akamrukia na kumganda mgongoni. Kabla hajamwondoa binti huyo, akastaajabu akichomwa na vioo usoni, tena mara nyingi asizoweza kuhesabu. Kumbe Wayde alikuwa ameteka baadhi ya vipande vya runinga. Na japo naye vilikuwa vinamkata kiganjani, hakuwa anajali!
Alimtofoatofoa yule dubwana na kumfanya alalamike kwa kunguruma. Macho yake ambayo hayakuwa yanaonekana, yakavuja damu akihangaika huku na kule kumtoa Wayde mgongoni. Mithili ya chombo kilichokumbwa na dhoruba, akawa anapepesuka, anajigonga na kutaka kuanguka.
Alipofanikiwa kumtia Wayde mkononi, akamvuta kwanguvu kisha akamminya shingo yake akitaka kumvunja na kummaliza moja kwa moja, ila hakuwa na nguvu hizo tena. Sasa alijihisi mdhaifu kuliko hata mara ya kwanza. Magoti yalishindwa kumbeba kabisa akaangukia chini kama mtu anayesujudu.
Mikono yake ikamwachia Wayde, ambaye naye alidondoka akiwa amechoka, amejeruhiwa. Haraka Wisconsin akaenda kumjulia hali binti huyo, na asipoteze muda, akamwagiza aweke presha kwenye jeraha la Brian ingali yeye akienda kutafuta huduma ya kwanza.
Kidogo akarejea akiwa na mkoba wa huduma hiyo, akatoa bandeji na dawa, upesi akamtia dawa Brian na kumfunga kisha akamwendea Mama. "Upo sawa?"
Mama akatikisa kichwa kuafiki. Wisconsin akamnyanyua ampeleke kumlaza kochini, lakini kabla hajasonga, akamwona dubwana lile likiwa limeamka! Tayari alishakusanya nguvu zake kama hapo awali!
"Mungu wangu!" Mama Brian akanong'ona. Upesi Wisconsin akapaza sauti, "Wayde, zima mshumaa!" Haraka Wayde akapuliza mshumaa na kuzimika.
Kidogo Wisconsin, akauwasha tena, na mara hii ulipowaka, mlangoni wakawa wamesimama watu watatu! Kutokana na mwanga hafifu, hawakuwa wanaonekana vema ila Wisconsim aliwatambua. Ni wale watoto wafu wa Helo.
Basi akasema maneno ya ajabu, na mara wale wafu wakamvamia dubwana yule na kumteketeza wakihodhi haki yao kama watoto wa Hernandez Lorenzo. Haki ambayo watoto hawa wa kuasili; Alfonso, Brewster na Olivia waliiteka kwa muda!
**
"Brian, amka! Brian, Brian, amka!" Sauti hiyo ya kike ilikuwa inanong'ona kwenye masikio ya Brian. Hakuwa anajitambua yupo wapi. Alikuwa gizani. Tangu, dubwana lile lilipomkita tumboni kule kwenye ulimwengu wa waliohai, alipoteza nguvu na fahamu.
Sasa anaanza kurejea kwenye hali yake. Bado akiwa kwenye ulimwengu wa kiza! Ule wa waliokufa. Na mtu yule aliyekuwa anamhisi yupo nyuma yake, ameshamteka! Mguu wake wa kuume umedakwa na anaburuzwa.
Akafungua macho yake na kuangaza, alikuwa hajui anapelekwa wapi. Alichokiona ni mwanaume jabali akimburuza kana kwamba kiroba.
Akaangaza kushoto na kulia kwake, bahati akajigongoa kwenye jiwe. Akalibeba jiwe hilo pasipo kulalamika kwa maumivu. Alivumilia. Alipoweka vema mkononi akalirusha kumbamiza yule aliyemshika, naye akageuka na kumtazama.
Alikuwa ni Helo!
Alimdaka Brian kwanguvu, na mara kule kwenye ulimwengu wa waliohai, mwili wa Brian ukaanza kuchuruza damu puani!
Puh! Brian akatupwa chini. Kabla hajakaa sawa, akazabwa teke kali la kichwa. Akahisi kupoteza fahamu. Akiwa ameshajua ameshakwisha, hajui tena alipo, akasikia tena sauti ya kike ikimwambia, "amka! Brian, amka!"
Akafungua macho yake kuangaza, akaona akiwa ameshakaribia kwenye makazi yale yaliyokuwa na mwanga hafifu aliouona kwa mbali. Akajikakamua. Kidogo, bwana yule akamshtukia. Akamwapua na kumbeba kuzama naye ndani. Akiwa amebebwa, Brian akasikia sauti za funguo mfukoni mwa Helo.
Walipofika kwenye chumba fulani, Brian akatupiwa humo na kisha Helo akasimama akimuuliza ni nini amekuja kufanya huko kwenye ardhi ya wafu.
"Kwanini waja huku na hutaki kusikia?" Na akahitimisha, ".. yanipasa nikuue ile uje kutuama huku kabisa maana unapapenda!"
Akamsogelea Brian amnyake, ila ghafla akasikia sauti za watu wakiwa wanagongagonga mlango. Akanguruma kuguna na kutoka humo ndani kwenda huko aliposikia sauti. Ilikuwa ni kwenye chumba ambacho amewafungia mateka wake. Mateka wa kiroho anaowatumikisha. Humo ndani alikuwapo pia na Kecie.
Akafoka, "mnataka nini? Kufa mara ya pili!"
Wote wakatulia. Akajipapasa mfukoni, hakuhisi ufunguo. Akastaajabu! Upesi akakimbilia kule alipomwacha Brian, kufika hakukuta mtu. Akaangaza akishangaa.
Kidogo, akahisi vishindo vya watu. Alipotoka ndani, koridoni akakuta roho zile ambazo alikuwa amezifungia. Zilikuwa tayari huru!
Akafoka, "kabla sijawaangamiza, rejeeni zizini!" Uso wake ulikuwa umeghafirika kwa hasira. Kecie akamjongea na kumwambia, "hauwezi kutufanya chochote hivi sasa, Helo. Hauna nguvu hiyo tena!"
Helo akatazama mikono yake akiwa amekodoa. Akajaribu kumkamata Kecie, akashindwa, mkono ulivuka kama kivuli. Akastaajabu na kuhofia.
Kecie akamwambia, "muda wako umekwisha, Helo. Ni wakati wako wa kuangamia."
Mara, "hapana!" Sauti ya kiume ikasikika. Kutoka nyuma ya wakina Kecie akatokea Brian aliyesonga mbele kabisa. Mkononi alikuwa ameshikilia funguo, ni yeye ndiye aliyewafungua huru wakina Kecie.
Akamtazama Helo na kumwambia, "familia yako iko hapa. Nadhani hauna haja tena ya kuusumbua ulimwengu wa walio hai."
Helo alipotazama nyuma akawaona watoto wake watatu. Akawakimbilia na kuwakumbatia kwanguvu macho yake yakiwa yanalenga machozi.
Kecie naye akamshukuru Brian kisha akamuaga kwa kumfumba macho na kumwambia"rudi sasa duniani. Umemaliza kazi yako Brian."
**
Brian akakohoa.
"Ameamka!" Mama akalipuka kwa furaha. Akamkumbatia mwanaye kwanguvu na kumbusu kwenye paji la uso. Wayde naye akamkumbatia na kisha Wisconsin. Walikuwa wamemaliza na kufaulu mtihani!
Walijawa na furaha tele. Punde Karen akajiunga nao, wakafanya tafrija fupi. Kesho yake Wayde akarejea kwao na kupewa taarifa kuwa baba yake alikuwa hospitalini akiendelea vema
.
Alipomweleza baba yake kilichotukia akiwa kitandani amelazwa, baba yake akamshika mkono kwanguvu na kumwambia, "umefanya kile ambacho sisi tulishindwa." Kisha akatabasamu na kumbusu, "hauna haja ya kuomba msamaha. Najivunia kuwa nawe."
**
.
.
MWISHO