*ROHO YAKE INADAI --- 42*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
“Sasa tunafanyaje na ameondoka na vitu vile?” Dada Magdalena akauliza akiwa na shaka. Padri Alfonso akatabasamu, “tunafanyaje? Yani unauliza tunafanyaje? Kwani hujui huwa tunafanyaje?”
Dada Magdalena naye akatabasamu.
Hawakutia tena neno lingine.
ENDELEA
Basi afisa Randall akaenda kuonana na familia ya wakina Brian na kuwapa mrejesho wa kilichotokea, nao akawaambia wafike kituo cha polisi kesho asubuhi na mapema, alafu akaenda zake kupumzika.
Afisa Williamson alimshushia nyumbani na kutokomea kwenda kulaza usafiri wa polisi. Randall alikuwa amechoka sana kutokana na kazi za siku nzima. Baada ya kuingia nyumbani kwake, akala na kutulia kidogo sebuleni pamoja na mkewe, alafu muda si mrefu akaenda kupumzika kwa kujimwaga kitandani.
Hata hakuoga. Na muda si muda, akasombwa na usingizi kwa mkupuo. Hakusikia hata mkewe alipozima kila kitu na kuja kulala. Alikuwa usingizini haswa akikoroma na kuachama kinywa.
Kwa mujibu wa saa yake ya sebuleni, mshale ukasonga na kujongea kwenye kituo cha nane usiku. Ulipofika hapo, Afisa Randall akajikuta anaamka toka usingizini asijue nini kimemwamsha kwani bado alikuwa na usingizi mzito.
Akatazama kushoto kwake, akamwona mkewe akiwa amejilalia. Taa ilikuwa imezimwa na hali ilikuwa imetulia tuli kabisa. Hakusikia sauti ya kingine chochote kile zaidi ya pumzi ya mkewe ambaye aliyekuwa anahema kwa uzito.
Akarudisha kichwa chake kitandani na kufumba macho aendelee kulala, usingizi haukuja. Akajitahidi kuyafumba macho kwanguvu, lakini bado hakukuwa na kitu. Macho yaligoma kudaka usingizi abadani,
Muda si mrefu, akasikia harufu fulani ambayo ilimfanya afungue macho na kutazamatazama chumbani. Ni kama kitu kinaungua ila kinanukia. Akanusanusa kama paka jikoni apate kutambua kitu hicho ni nini lakini hakufanikiwa.
Na kadiri muda ulivyokuwa unasonga, akajikuta anahisi harufu hiyo zaidi na zaidi. Akamuita mkewe, “Hey, hey.” akimsukuma bega kistaarabu, ndo’ kwanza mwanamke akageukia kando na kuendelea kulala.
Akataka kuendelea kumwamsha ila akasita. Acha apumzike, akajisemea, kisha akaweka shuka kando na kushuka toka kitandani. Akasikia dirisha linatetemeka, haraka akatazama. Ulikuwa ni upepo. Akapuuzia na kuuendea mlango, akafungua na kutoka chumbani.
Ila punde akarejea na kutwaa bunduki yake kwa dharura ya kiusalama. Akaikoki vema, ndaniye kulikuwa na risasi tatu. Zinatosha kabisa. Akaanza kufuata harufu kwa kudaka korido aende sebuleni na kisha jikoni.
Alipofika sebuleni, akawasha taa. Akatazama kwa kurusha macho yake huku na huko, hakuona jambo. Basi akaelekea kule jikoni. Napo akawasha taa. Akakaguakagua, hakukuwa na kitu. Sasa harufu inatoka wapi?
Dirisha la jikoni likatetemeka, akarusha macho yake kutazama. Ulikuwa ni upepo. Pazia lilichezacheza na mwishowe upepo ulipopita, likatulia. Afisa Randall akafungua droo zote za jikoni na kutazama ndani kama kuna kitu kimeoza, hakuona kitu. Hapo ndipo pua yake ikamwambia harufu ilikuwa inatokea nje.
Akahisi na kuamini kabisa itakuwa inatokea nje. Basi akaona asijisumbue kwenda huko. Kama haipo ndani, basi hana haja ya kujisumbua. Ila kabla hajajirudisha chumbani, akaona haitachukua nguvu sana kutazama nje kwa kupitia dirisha. Huenda akaona wapi harufu inatokea.
Alipotupa macho yake, upande wa mashariki mwa jiko, bustanini, akaona mbwa wawili wakiwa wakiwa wanatafuna. Kwakuwa alikuwa mbali, hakuona mbwa hao wanatafuna nini, ila walichokuwa wanakula kilikuwa kinatoka kwenye mfuko wa nailoni. Si kwamba aliuuona, bali alisikia sauti yake.
Akatazama kwa umakini aone ni nini kile ambacho mbwa hula, hakuweza kuona. Akajiuliza na kustaajabu, ni hicho ndicho hutoa harufu aliyoisikia mpaka kule chumbani?
Dirisha la sebuleni likatikisika. Akatupa macho yake upesi kutazama, hakuona kitu. Ulikuwa ni upepo. Pazia lilicheza na kisha kutulia. Aliporudisha macho yake kule nje, hakuona tena wale mbwa! Wameenda wapi? Akarusha macho yake kutazama na kuwatafuta, hakuwaona.
Akiwa hapo anabung’aa, akasikia sauti za mbwa hao wakiwa wananguruma na kugombana. Walibweka na kunguruma kwa fujo kana kwamba wanagombea kitu, sauti zao zikawa kero na bughudha.
Afisa Randall alipotaka kuachana nazo, zikaendelea pasipo kukoma. Hapo akaona hana budi kuwafukuza mbwa hao kabla watoto wake hawajaamka. Akafungua mlango, akiwa ameshikilia bunduki yake vema mkono wa kuume, akatoka na kurusha macho yake kuwatafuta wale mbwa.
Hakuwaona. Akasonga hatua nane mbele na kisha akatazama tena, hakuwaona! Sasa kulikuwa kimya, ni sauti ya upepo tu wa taratibu ndiyo ambao ulikuwa unasikika.
Wale mbwa wameenda wapi?
Basi kwakuwa aliwakosa na tayari ameshatoka nje, akaona ni kheri akatazame pale bustanini kuona kitu gani ambacho wale mbwa walikuwa wanakula.
Akasonga na kutazama, hakukuta kitu. Ule mfuko haukuwepo, na mbali na hilo, hata alama za miguu ya mbwa, haikuwapo ardhini! Akiwa hapo, bado anaperuzi, kwa nyuma yake mlango aliotokea ukarudi taratibu na kujifunga iiiiiiiiiiiipp .. kisha, tas-tas! Sauti ya komeo ikaita na kumshtua!
Haraka akatoka pale alipo na kukimbilia mlangoni, akagonga na kusema, “Hey, nipo nje! Hey nipo nje!” mlango haukufunguka. Akagonga tena na tena akiita, mlango haukufunguliwa. Akajaribu kuuvuta pasipo mafanikio, mlango ulikuwa umefungwa!
Mlango huu wa jikoni ulikuwa umesanifiwa kwa chuma kizito na kioo kigumu kinachohakisi ndani kwa uhafifu. Na kwakuwa jikoni taa ilikuwa inawaka, kioo hiki kilionekana cheupe kana kwamba mwezi angani.
Basi Afisa alipoona juhudi zake za kugonga mlango hazikuzaa matunda, akatengeneza mduara kiooni kwa kutumia bapa za viganja vyake ili apate kutazama ndani kama kuna mtu ama mlango umejifungwa kwa makosa.
Alipofanya hivyo, akaona kuna mtu ndani, lakini hakuweza kumtambua mtu huyo kwani kioo kile cha mlango hakikuwa chepesi kuonyesha hivyo mtu huyo alikuwa anaonekana kana kwamba kivuli tu.
Randall akabamiza tena mlango na kuita. Akastaajabu, mbona mtu yule hakuwa anamfungulia? Hapa akapata shaka. Huenda ni jambazi! Basi haraka akatoka hapo mlangoni na kwenda kwenye madirisha ya sebuleni, akatupa macho yake ndani.
Hakumwona mtu. Ila kabla hajatoka hapo akiwa amelenga kwenda kwenye mlango wa sebule kujaribu kufungua, akaona kitu fulani koridoni. Kilikuwa ni kitu cheusi kirefu chenye umbo la binadamu, ila hakina sura. Afisa akadhani ni macho yake. Punde taa ya sebuleni ikazima!
Akashtuka.
Ikabakia taa moja tu ya kule jikoni ambayo mwanga wake ukawa unajimwayamwaya kwa uhafifu mpaka huku sebuleni. Hapo ndipo Afisa Randall akaona kile kitu ambacho kipo koridoni, kikiwa na umbo kama la binadamu, kikiwa kinawaka macho mithili ya paka. Moyo wake ukapata mshtuko sana. Akakodoa na kuachama akiwa haelewi kile anachokiona. Alitamani awe ndotoni, ila hapana, ilikuwa ni uhalisia!
Kabla hajavuta hata pumzi tatu, katika ule mwanga ambao ulikuwa unatokea jikoni kufika sebuleni, akaona kivuli cha mtu. Alikuwa ni mwanamke amevalia gauni. Mwanamke huyo alikuwa anacheza mienendo ya bluzi akinyanyua pindo la gauni lake na kusonga kusonga kushoto, kulia.
Akayarudisha macho yake kule koridoni, ajabu hakumwona tena yule kiumbe aliyekuwa anawaka macho kama taa. Akiwa anaangaza ajue yupo wapi, akastaajabu ameshikwa bega na mkono wa baridi kana kwamba barafu. Alipotazama, uso kwa uso akakutana ni kiumbe yule mwenye macho ya taa. Kiumbe mweusi na mrefu!
Akahisi moyo wake umeongeza makasia. Akapatwa na baridi kavu mwilini wake. Alijawa na kihoro haswa, upesi akanyanyua bunduki yake na kutupa risasi zote tatu kwa mkupuo, mara kiumbe yule akapotea!
Afisa akiwa amekodoa, anahema kama aliyekimbizwa, punde kidogo akaguswa tena begani na mkono wa baridi zaidi. Alipogeuka kutazama, akakutana na mwanamke aliyevalia gauni jeusi. Alikuwa amefunga kiremba kichwani kilichoziba mpaka uso wake.
Afisa akajaribu tena kufyatua risasi, hazikuwapo, ziliisha. Basi akawehuka na kuanza kukimbia akipiga makelele kuomba msaada.
**
Saa tatu asubuhi …
Kulikuwa na magari matatu ya polisi na nyumba ya afisa Randall ilikuwa imezungushiwa utepe wa rangi ya manjano na nyeusi kukataza watu wasiohusika kukatiza hapo.
Mbali na hivyo, watu kadhaa, haswa majirani, walikuwa wametoka nje ya makazi yao wakitazama eneo la tukio kwa macho ya maulizo na nyuso za mashaka. Kulikuwa na zogo fulani midomoni mwao.
Muda si mrefu gari ya wagonjwa ikawasili eneoni na kujitengenezea vema. Kutoka ndani ya nyumba, ikatolewa miili mitatu ambayo imefunikwa gubigubi, ikatiwa ndani ya gari la wagonjwa na kisha gari hilo kutimka.
**