Simulizi: Penzi ama kaburi?

Simulizi: Penzi ama kaburi?

Sehemu ya 60.

Shadya, msichana aliyekuwa na sura ya kipole, mrembo, mwenye moyo uliokuwa na upendo mwingi hakujua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia chuoni hapo.
Alimpenda sana Alex, alikuwa mwanaume wake aliyehisi ni wa kufa na kuzikana kumbe upande wa pili mwanaume huyo alikuwa akifanya mambo ya ajabu, ya kumdhalilisha na kumfanya kuonekana mtu asiyekuwa na thamani yoyote ile.

Alimpenda kijana huyo, alifanya kila kitu alichokitaka, hakuwa mnywaji wa pombe, ila kwa sababu yake akajikuta akiingia kwenye unywaji.

Dunia ilimchukua, ikaanza kumpoteza pasipo kugundua hilo. Alijiona msichana wa kawaida aliyewahi kufanya mapenzi na wanaume watatu tu kumbe haikuwa hivyo, zaidi ya wanaume kumi walikuwa wamelala naye, walimfaidi, waliujua utamu wake, sauti yake ya kimahaba kitandani waliijua vilivyo.

Baada ya manyanyaso ya kingono aliyofanyiwa bila kugundua akaanza kuyaona mabadiliko chuoni hapo, alishangaa, kila alipokuwa akipita watu walikuwa wakimwangalia kwa kumnyali, ni kama walishangaa ni kwa namna gani alifanya kitendo fulani cha aibu kwa mtu kama yeye.

Alitamani kujua hilo lakini hakuligundua kwa sababu tu alikuwa msichana mkimya ambaye hakuwa na mazoea na watu wengi.

Wale wachache ambao aliwazoea, waliogopa kumwambia, hawakujua angejisikiaje, waliumia mioyoni mwao, walimuonea huruma mno lakini bado midomo yao ilikuwa kimya, kama ilipigwa kufuli.

“Shadya!” alisikia akiitwa na mwanaume mmoja, alikuwa amekaa pembeni ya uwanja wa mpira wa kikapu chuoni hapo.
Shadya alimwangalia mwanaume huyo, alihisi alikuwa akitakwa kama wasichana wengine walivyokuwa wakihisi kila walipoitwa na wanaume fulani.
Alimwangalia mara moja halafu akampuuzia.
“Shadya!” mwanaume huyo akaita tena, mara hii akasimama na kuanza kumsogelea.

Shadya hakutaka usumbufu wala kuonekana malaya, kwa akili zake alizotoka nazo Zanzibar zilimwambia kuongea na wanaume wengi ni umalaya, mwanamke anayejiheshimu hatakiwi kuzungumza na mwanaume yeyote yule zaidi ya ndugu zake na watu wa karibu.
 
Sehemu ya 61.

“Nimekuita lakini!” alisema mwanaume huyo kwa sauti ya upole, Shadya akasimama, alisubiri kusikia akiambiwa nini, japokuwa hakupenda sana kusimama kama alivyofanya.

“Unasemaje?” aliuliza huku akiangalia huku na kule, aliwaogopa watu ila mtu aliyemuogopa zaidi alikuwa Alex kwani alidhani angehisi jamaa huyo alikuwa mtu wake.

“U msichana mzuri sana!” alisema jamaa huyo kwa sauti ya chini, sauti ambayo ilibeba ujumbe mzito ndani yake.
“Ndilo unalotaka kuniambia?” aliuliza huku akionekana kubadilika.

“Ninakupenda sana na ndiyo maana ninataka kukwambia ninalokwambia, upendo wangu kwako ni wa matendo na si maneno. Kama hao unaodhani wanakupenda ingekuwa kweli, basi wangekwambia mapema hili ninalotaka kukwambia,” alisema, Shadya akaanza kupiga hatua, jamaa akamshika mkono.
“Nisikilize kwanza!” alisema kwa upole huku akijaribu kumvuta.

“Nimesema niache! Nitapiga kelele!” alisema msichana huyo kwa hasira.
“Shadya! Si kila mwanaume anayekusimamisha anataka kukutongoza, jaribu kunisikiliza,” alisema, kidogo maneno hayo yakamfanya msichana huyo atulie na kuanza kumwangalia.

“Unataka kuniambia nini?”
“Unajua kitu gani kinaendelea chuoni kuhusu wewe?” aliuliza jamaa huyo.
“Kitu gani?”
“Unahisi umezungukwa na watu sahihi?” aliuliza swali lililomfanya Shadya kumkazia macho.

“Unamaanisha nini?”
“Pole sana!”
“Pole ya nini?”
Kabla jamaa hajajibu, simu ya Shadya ikaanza kuita, akashukuru Mungu, haraka haraka akaitoa na kuangalia jina, alikuwa Alex.

Akasogea pembeni na kuanza kuongea naye, hakuridhika, akatumia njia hiyo kama kumkimbia mwanaume yule, akaanza kupiga hatua kukatiza uwanjani kuelekea katika mabweni ya Magufuli.
“Shadyaaaa...” aliita jamaa, msichana huyo akawa anapiga hatua kusonga mbele.

Hiyo ilikuwa nafasi yake, hakutaka kumuacha msichana huyo, alikuwa na mengi ya kumwambia, akaanza kumfuata lakini naye baada ya kuona anafuatwa, akaanza kupiga hatua zaidi.
“Shadya! Alex anakuharibu!” alisema jamaa huyo baada ya kumfikia, kusikia hivyo, Shadya akasimama.

“Hebu subiri baby nitakupigia,” alisema Shadya kwa sauti nyororo kabisa, akakata simu na kumwangalia mwanaume huyo.

“Shadya! Kitu nitakachokwambia kisikushtue, usichukue uamuzi wowote ule mbaya,” alisema
 
Sehemu ya 62.

“Kitu gani?”
“Nitakalokwambia na kukuonyesha ni kwa sababu nakupenda, sikupendi kimapenzi bali nakupenda kama ndugu yangu, dada yangu wa damu,” alisema huku akimwangalia Shadya.

“Unanichelewesha, niambie unataka kusema nini! Mara Alex, mara ndugu yako wa damu, hebu niambie!” alisema Shadya, sasa akabadilika, alitamani kuondoka lakini alishangaa kuona akiendelea kusimama.

“Picha zako zimesambaa!” alisema mwanaume huyo.
“Picha zangu! Picha gani?”
“Za utupu, ukiwa na mwanaume chumbani! Shadya hivi unajua unaonekana kama malaya chuoni hapa?” alisema jamaa huyo.

Shadya alimsikiliza, kwanza akapuuzia, alihisi kama jamaa huyo alikuwa akitumia njia hiyo kumpata kimapenzi, badala ya kuuliza zaidi, ndiyo kwanza akatoa tabasamu.

“Hii njia yako ya kumtongoza mwanamke nimeipenda...eti picha zangu...” alisema Shadya kwani alikuwa na uhakika hapakuwa na picha zake zozote zile za utupu.

Alichokifanya jamaa huyo ni kutoa simu yake, akafungua sehemu ya picha na kumuonyesha msichana huyo. Shadya akachukua simu ile na kuanza kuangalia.
Macho yake yalipotua kwenye picha zile, alishtuka, hakuamini alichokuwa akikiangalia. Moyo wake ukapiga paaa! Akahisi kama waya uliokuwa na umeme ukipita mwilini mwake.

Pale aliposimama alihisi kupigwa ganzi, kulikuwa na upepo uliokuwa ukivuma kutoka kwenye miti lakini cha ajabu, ni ndani ya sekunde chache tu, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Mara ya kwanza alihisi ni picha zilizoeditiwa, akaanza kuangalia sura, ilikuwa yake, akaja kifuani, alikuwa yeye na alipoangalia pajani, aliliona doa lake, alikuwa yeye kabisa, hazikuwa picha za kueditiwa.

“Ma...ma...ma...ma...ma...” alitaka kuzungumza maneno fulani lakini alishindwa, mdomo wake ukawa mzito kufunguka, alihisi kama kulikuwa na mtu aliyekuwa akimzuia kusema kitu fulani.
Machozi yakaanza kutoka machoni mwake na kutiririka mashavuni, hakuamini alichokiona na wakati mwingine alitamani kile kilichokuwa kikionekana kwenye simu ile kiwe ndoto fulani.

Miguu ikaanza kulegea na kujikuta akikaa chini na kuanza kulia kwa sauti ndogo. Haikuwa picha moja, zilikuwa nyingi, zilizokuwa na aibu mpaka mwenyewe akaanza kuogopa.
“Alex...”
 
Sehemu ya 63.

Hilo ndilo jina lililomjia kichwani mwake. Alichanganyikiwa, alimpenda mwanaume huyo lakini kitu cha ajabu alimfanyia jambo la kinyama sana.

Hakujua kwa sababu gani mwanaume huyo alifanya uamuzi wa kupiga picha hizo na kuzisambaza, alikumbuka kila kitu kwamba alikuwa akilewa mara kwa mara kumbe mwanaume huyo alichukua nafasi hiyo kupiga picha hizo.

“Shadya! Huyu si Alex...” alisema mwanaume huyo, hapo Shadya akashtuka tena, akasimama.
“Ni mwanaume mwingine. Umekuwa ukifanya ngono na wanaume tofautitofauti bila kujua.

Alex aliamua kukutumia kingono, kuna wanaume zaidi ya kumi umefanya nao mapenzi! Pole sana Shadya, hakuna mtu anayetaka ulijue hili na ndiyo maana nimekwambia marafiki uliokuwanao si sahihi katika maisha yako!” alisema jamaa huyo.
“Alex amenifanyia hivi mimi?” aliuliza Shadya huku akilia.

“Pole sana! Pombe zilikufanya kutokug...” alisema jamaa huyo, hata kabla hajamaliza sentensi yake Shadya akatoka mahali hapo, akaanza kukimbia.
Hakutaka kubaki chuoni, ilikuwa ni aibu kubwa, alikimbia kama mtu aliyechanganyikiwa, moyo wake ulichoma, uliuma kupita kawaida.

Jamaa alijaribu kumuita ila hakuitikia zaidi ya kuendelea kukimbia kwa kasi kubwa. Alipofika getini, akatoka mpaka nje, mguuni alikuwa na kiatu kimoja, na hakulijua hilo.

Wakati akikimbia akaanza kumkumbuka Alex, chuki dhidi ya mwanaume huyo ikaanza kujijenga moyoni mwake, hakuamini kilichokuwa kimetokea.

Alipomaliza kwa Alex akaja kwa Gibson kisha Ngwali. Alijiona mjinga mno, aliikumbuka siku ambayo aliondoka Zanzibar na kuelekea Dar es Salaam, aliyakumbuka maneno ya mpenzi wake huyo aliyomwambia kuhusu jiji hilo.

Kulikuwa na wanawake wapole, washamba waliokuwa wakiingia humo kutoka sehemu mbalimbali, wanawake ambao hawakujua kitu chochote kile ila baada ya kuishi humo, wakajikuta wakianza kubadilika.

Wengine wakafakamia pombe, starehe zikawapata, wakaanza kufanya ngono na wanaume wengi na mwisho wa siku kupata mimba, na kama walichoma sindano za kuzuia mimba, wakajikuta wakipata UKIMWI.
 
Sehemu ya 64.

Hilo likamtisha mno, na mbio zake hizo alikuwa akikimbia kuelekea hospitalini, na hospitali ya karibu kutoka hapo alipokuwa ilikuwa ni Megra.

Huku akiwa amechoka, akafika hospitalini hapo na kuingia ndani. Ilikuwa ni majira ya saa 12:49 jioni, hapakuwa na watu wengi, hivyo akaunganisha mpaka mapokezi.

“Karibu dada...” alimkaribisha nesi aliyekuwa ampokeze.
“Nimek....uja kump...ima...” alisema huku akihema, jasho lilikuwa likimtoka, kila mtu aliyekuwa akimwangalia, alimshangaa.
“Kupima malaria?” aliuliza nesi huyo.
“UKI..MWI...” alijibu.

Japokuwa kilikuwa kitu cha kushangaza sana kutokana na muonekano wake lakini nesi hakushangaa, akamwambia chumba alichotakiwa kwenda hivyo kufanya hivyo.
Alipofika huko, akaelezea shida yake na kufanya kila alichotakiwa kufanya na kuelekea katika chumba husika na kutolewa damu yake.

Alikuwa na mambo mengi ya kufanya lakini hilo lilikuwa muhimu kwake. Maneno ya mwanaume aliyekutana naye na zile picha alizomuonyesha zilimtisha mno, moyo wake haukuweza kumsahau Alex, alionekana kuwa mwanaume mwenye moyo wa kinyama kupita kawaida.
“Alikuwa akiniuza kila nilipolewa?” alijiuliza huku akianza kulia pale kwenye benchi.

Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa nguvu, hofu ikamtanda, moyo wake ukagawanyika, upande mmoja ulimtia nguvu kwa kumwambia asihofu yupo salama lakini upande mwingine ulimwambia asijisumbue kwani tayari aliathirika.
“Allah naomba unisaidie!” aliomba kimya kimya.

Baada ya dakika arobaini na tano akaitwa, akainuka na kuanza kuelekea kwenye chumba alichohitajika. Akafuta machozi yake lakini macho hayakuacha kuwa mekundu kwa sababu ya kulia sana.
Alipofika, akakaa, alikuwa akitetemeka. Mbele yake alikuwa mwanamke mtu mzima, alionekana kuwa na hekima kuliko watu wote ndani ya dunia hii.
 
Sehemu ya 65.

Alivalia miwani na mikononi mwake alishika karatasi iliyokuwa na majibu ya damu ya msichana huyo. Kabla ya kumwambia kuhusu majibu hayo akaanza kumuuliza maswali mengi na kumshauri pia.

“Mara yako ya mwisho kufanya mapenzi ilikuwa lini?” alimuuliza mwanamke yule.
“Wiki mbili zilizopita!” akadanganya.
“Ulitumia kondomu?”
Akakaa kimya kwa sekunde chache.
“Ndiyo nilitumia.

“Una wapenzi wangapi?”
“Mmoja!”
“Ulishawahi kuja kupima naye?” “Hapana!”
“Kwa sababu gani?”
“Anaogopa!”
“Na wewe ni mara ya ngapi umekuja kupima?”

“Mara ya tatu!”
“Mara ya mwisho ilikuwa lini?”
“Miezi mitatu iliyopita!”
“Ukikuta hujaathirika, utachukua uamuzi gani?” aliuliza mwanamke huyo.

“Nitawalinda watu wote wanaonizunguka!” alijibu, alikuwa akitetemeka mno.
“Na ukikuta umeathirika?” Napo akakaa kimya kwa sekunde chache.
“Nitawalinda wote kwa kutumia kondomu, kula vizuri na kudumisha afya yangu,” alijibu.

Muda wote huo alikuwa na hofu, hakujiamini hata kidogo, aliona kabisa mwanamama huyo alikuwa akijichelewsha na matokeo yalikuwa wazi kwamba aliathirika. Lawama zote zikawa kwa Alex.

“Hivi Alex alishawahi kupima?” alijiuliza.
Baada ya maongezi ya nusu saa huku akifarijiwa kwa maneno matamu na ushauri wa hali ya juu, akapatiwa majibu ya damu yake, na kitu alichokiona zaidi ni neno HIV/ POSITIVE.

Hapohapo akajikuta akinyong’onyea, akaanguka chini kama mzigo.
Puuuu!
.
.
.

Itaendelea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom