Sehemu ya 68.
Moyo wake kwa wakati huo uligawanyika mara mbili, kuna upande ulimwambia hakutakiwa kujiua kwa sababu bado angeweza kuishi miaka mingi lakini upande mwingine ulimwambia ni lazima ajiue kwa sababu tu kusingekuwa na maisha zaidi, mbaya kuliko yote, watu wangekuwa wanamcheka tu.
“Yaani watu wakijua umeathirika, hutokaa kwa amani, utachekwa, utanyapaliwa, yaani hutokuwa na maisha ya raha hata kidogo,” aliisikia sauti moyoni mwake.
Hiyo ndiyo ilimtia hofu na kuwa na msimamo wa kutaka kujimaliza tu. Hapo bweni hakukaa sana, akaondoka na kuelekea mtaani ambapo akanunua sumu ya panya na kurudi tena na kukaa kitandani mwake.
“Allah naomba unisamehe!” Hakutaka kusubiri, moyo wake ulikuwa na maumivu makali mno, kila alichokuwa amekipanga alihisi kama kingevurugika kwa kuwa tu aliathirika alipokuwa chuoni.
Akachukua glasi ya maji na sumu ile, akachanganya na kunywa, akajifunika na shuka lake, tumbo likaanza kumkata na hakuchukua dakika nyingi, akatulia, mapovu yakamtoka mdomoni na kufariki dunia.
Hakuna mtu aliyejua kama msichana huyo alifariki dunia, alionekana kama amelala, baada ya masaa matatu ndipo watu walipokuja kugundua.
Kila mmoja alishangaa, taarifa zikaanza kusambaa kwamba Shadya amejiua kwa kunywa sumu akiwa bwenini. Taarifa zilipofika kwa Rahim, hakuamini, alilia mno, hapakuwa na mtu aliyejua sababu zaidi yake, na hakutaka kumwambia mtu yeyote zaidi ya ndugu zake tu.
Mwili wake ukachukuliwa na kupelekwa hospitalini, ukahifadhiwa mochwali baada ya kugundulika alikuwa amefariki dunia.
Wazazi, ndugu, jamaa na marafiki walilia kwa ajili yake, kila mmoja alijaribu kujiuliza sababu ya msichana huyo kuuchukua uamuzi mkubwa namna hiyo lakini hakuna aliyejua lolote lile zaidi ya Rahim ambaye aliamua kuwa kimya kwa sababu maalumu.
Siku iliyofuata mwili ukasafirishwa mpaka Zanzibar. Wazazi wake walihuzunika mno, walijitahidi kutafuta pesa kwa ajili ya binti yao, waliishi maisha ya shida kwa sababu yake na kaka yake, ili wasome tu.